Saturday 13 February 2016

MAGUFULI AMETHIBITISHA HOJA YETU.


Inawezekana kuna sehemu ya Wazanzibari ambao wamevunjwa moyo sana na kauli ya Rais John Pombe Magufuli aliyoitoa leo juu ya dhima yake kwenye mkwamo uliosababishwa na ‘uhuni’ wa Chama chake cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha. Hiyo ni kwa sababu walikuwa wameweka matumaini yao kwake. Mimi niliwahi kuandika kuwanaweka dau langu kwa Magufuli ili kumpa muda wa kuonesha kile ambacho angeliweza kufanya kwa mkwamo uliotokana na uhuni huo, lakini hata kwenye makala hiyo niliweka neno la tahadhari kuwa dau lenyewe linakwendana na namna ambavyo kiongozi huyo aliyejipatia sifa ya ‘utumbuaji majipu’ angeliendea suala hili. Lakini bahati nzuri amethibitisha kuwa hana tafauti na wenzake, nami nathibitisha kuwa nitamchukulia kama nilivyowachukulia wenzake. 
Jambo ninalotaka kuwaambia Wazanzibari wenzangu hao ni moja: hakuna kipya ambacho Rais Magufuli amekisema cha kuwafanya wao kuvunjika moyo. Kama kuna chochote ambacho Amiri Jeshi Mkuu huyu ametusaidia kwenye hotuba yake hiyo kwa taifa mbele ya wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, basi ni kututhibitishia hoja yetu ya muda wote, kwamba Serikali ya Muungano wa Tanzania (ambayo ndiyo hiyo hiyo serikali ya Tanganyika) ina sera yake maalum kuelekea Zanzibar. Sera hiyo, kama nilivyoielezea kwenye makala zangu kadhaa, inaongozwa na akili ya mkaliaji kwa mkaliwaji.

Kwa kusema kwake kwamba hataingilia kile alichokiita ‘maamuzi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar’ kwa kuwa Tume hiyo ni huru kama ilivyo ya Muungano (NEC), lakini atawashughulikia watakaoleta ‘fyokofyoko’, Rais Magufuli alikuwa anaakisi mwangwi wa sauti za watangulizi – Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete – lakini kwa tuni ya ukweli zaidi na uhalisia zaidi. Ukweli wenyewe sio kuwa ZEC na NEC ni tume huru. Hapana. Kwa watu ambao kila siku wamekuwa wakisisitiza kuwa baba anakuwa sahihi kumkataa mtoto wake mmoja aliyezaliwa pacha wa yai moja na akamkubali pacha mwengine kwa kuwa ati mkewe alikuwa mzinzi, sasa wanajikanganya kwa kusema tume moja ikiwa huru na nyengine inakuwa huru.
Akiandika hivi majuzi, mwanasheria wa siku nyingi visiwani Zanzibar, Awadh Ali Said, anauliza: “Vipi utamuingilia kati mchezaji mwenzako wa Timu moja? Endapo wachezaji na muamuzi wote wanatoka Timu moja kuna haja ya muamuzi kuingiliwa? Si anajua kazi yake? Si atatimiza wajibu wake? Na hili hufanywa kwa usanifu na ubobezi wa hali ya juu. Halifanywi kiholela. Tumesahau? Si hivi karibuni tu tulimuona aliyekuwa Makamo Mwenyekiti wa Tume hiyo hiyo “iliyo huru” akiibuka hadharani na Kadi ya Chama Tawala akigombea uteuzi wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Tawala. Huyu pia aliwahi kuwa Makamo Mwenyekitu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC.) Aliwahi pia kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na Jaji Mkuu wa JMT. Nafasi ambazo kisheria na hata kimaadili hazimruhusu kuwa mwanachama wa Chama cha Siasa. Hivi huyu wakati huo akiwa madarakani alikuwa anategemewa kuingiliwa? Si anajielewa!!! Katika hali hii tuna uhakika gani kama na Mwenyekiti wa sasa wakati ukifika hatojaribu bahati yake naye?”
Majibu ya maswali haya sio tu yanayasuta majigambo ya Magufuli juu ya ‘uhuru wa Tume za Uchaguzi’, bali pia yanaeleza tatizo hasa lililopo na kuuharamisha hata ushindi wake mwenyewe uliomuweka madarakani. Wakati Rais Magufuli alipouliza kwa nini Tume ya Uchaguzi ya upande mmoja (akikusudia NEC) iwe huru na ya upande mwengine (akikusudia ZEC) isiwe huru katika kujijengea uzio wa hoja yake ya ‘kutokuingilia maamuzi ya ZEC’, alikuwa hapo hapo anajipiga risasi za miguu, kwani wenye akili wanamuuliza “sasa inakuwaje uchaguzi wa Tume moja (ZEC) uwe haramu na wa nyengine (NEC) uwe halali?”
Ukweli alioueleza kiuhalisia ni kuwa Tanganyika (soma Muungano) utaendelea kuhakikisha kuwa Zanzibar haitawawili na chama chengine kisichokuwa CCM, kwa kuwa CCM Zanzibar ndiyo inayohakikisha maslahi yake kwenye visiwa hiyo. Ukijumlisha kauli hii na ile ya Waziri William Lukuvikanisani, huwezi kukosa jawabu kamili.
Kauli za kulinda Mapinduzi na Muungano ndiyo kisingizio kikubwa kinachotolewa na watawala panapohusika uhusiano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa visingizio hivyo, mtawala anaweza kuenda maili nyingi za ziada – kando ya haki za binaadamu, uhuru na demokrasia – ili kulinda maslahi ya mkaliaji kwenye ardhi ya mkaliwaji. Amefanya hivyo kwenye chaguzi zote tangu kurudi tena kwa mfumo wa vyama vingi na atafanya hivyo milele madhali tu sera yake kuelekea Zanzibar haijabadilika.
Kwa hivyo, kama kuna chochote – narudia – ambacho Rais Magufuli amekifanya kwenye hotuba yake hii, basi ni kututhibitishia hoja yetu sisi ambao tunaamini kuwa kilichopo si Muungano bali ukoloni wa nchi moja ya Kiafrika dhidi ya nyengine. Alichofanya ni kuuthibitishia ulimwengu pia kuwa CCM – iwe Tanganyika, iwe Zanzibar – haiamini kwenye uchaguzi kama njia sahihi ya kusalia madarakani, bali inaamini katika kuutumia uchaguzi kama njia ya kuuonesha ulimwengu kuwa kuwapo kwake madarakani kunatokana na uchaguzi. Pana tafauti kubwa sana baina ya “kuuamini uchaguzi” na “kuamini kuutumia uchaguzi.”
Sasa nini kinaweza kufanyika baada ya ukweli kusemwa kwa uhalisia kutoka kinywa cha Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Ni kuifufua na kuipeleka mbele ya jumuiya ya kimataifa ile “Ajenda ya Zanzibar” kwa kutumia njia za sheria za kimataifa na za amani.

Ahsante Rais Magufuli kwa kutuonesha njia.Zanzibar Daima 

No comments: