Sunday 21 February 2016

Mpigania Demokrasia wa Zanzibarafariki dunia huko Dubai jana



Aman Thani Fairooz
(1929 - 2016)

‘’…ikiwa uhuru wa tarehe 10 Disemba 1963 ulikuwa ‘’uhuru bandia’’ nao ukaweza kukubalika katika Umoja wa Mataifa, ukapata na kiti chake katika Ukumbi wa Umoja wa Mataifa na ukapandisha na Bendera ya Zanzibar huru katika Kiwanja cha Umoja wa Mataifa na Waziri Mkuu wa serikali huru ya Zanzibar Sheikh Muhammad Shamte Hamad akaukhutubia Ukumbi wa Umoja wa Mataifa na Wajumbe wengine kama wa Japan akaukhutubia Ukumbi kwa kuipongeza Zanzibar, Ikiwa yote haya yalikuwa bandia, basi tupeni hayo yenu ya binadamu ya tarehe 12 Januari 1964 mnaoyaita mapinduzi ambayo mnayajua kwa hakika kuwa si ‘’mapinduzi,’’ bali ni mavamizi…’’

(Aman Thani kutoka kitabu chake kipya ambacho hakijachapwa)
Hayo hapo juu ni kutoka katika kalamu ya Aman Thani akiandika katika kitabu chake cha pili (hakijachapwa).

Hakika ni maneno mazito na yenye kufikirisha.Aman Thani amefariki leo alfajir Dubai ambako alikimbilia kiasi cha miaka 40 iliyopita baada ya kutoka jela alikofungwa Tanzania Bara. Aman Thani ameacha hazina kubwa ya kumbukumbu zake binafsi kuhusu vipi hali ikuwa wakati wa kupigania uhuru na wakati baada ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964 ambayo yeye kila alipozungumza aliyaita ‘’mavamizi.’’ Aman Thani ameandika vitabu viwili. Kitabu chake cha kwanza, ‘’Ukweli ni Huu’’ kitabu ambacho kama jina lake lilivyo Aman Thani alirekebisha mengi katika propaganda ambazo kwa hakika zimevuruga historia ya Zanzibar. Kitabu hiki kilichapwa mwaka wa 1995. Kitabu cha pili alikikabidhi kwa ajili ya uchapaji na kipo katika ngazi ya uhariri.Namshukuru Allah kuwa nillibahatika kukutana na Aman Thani Dubai mwaka wa 1999 nilipomtembelea nyumbani kwake Rashidiya na alinikabidhi nakala kadhaa za kitabu chake ''Ukweli ni Huu,'' akanambia niwape wenzangu wengine wasome wajue ukweli.

Katika blog hii majuma machache yaliyopita nimeweweka video tisa za Aman Thani mwenyewe akizungumza kuhusu historia ya Mapinduzi ya Zanzibar. video hizi zimevutia watazamaji wengi kiasi inaniwia shida kwa sasa na kwa hakika sina maneno yanayoweza kutosha kumueleza yeye na yale aliyoshuhudia na kutenda katika kupigania uhuru wa Zanzibar. Laiti Aman Thani asingetuachia hazina hii mengi ambayo sasa yamekuwa hadhir kwetu yangepotea. Nawaachia wasomaji wamsikilize Aman Thani mwenyewe akiirudisha hadhira yake nyuma miaka 50 iliyopita kuujua ukweli katika historia ya Zanzibar.Tafadhali msikilize marehemu Aman Thani akieleza yale yaliyopitika Zanzibar baada ya mapinduzi:

No comments: