Tuesday 1 March 2016

Mazombi walivyovamia uchaguzi wa Mayor wa Jiji la Dar

Mdee, Kubenea wakamatwa, Simbachawene atoa neno
HALIMAMDEE
NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema hakuna amri iliyotolewa kuzuia Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliotakiwa kufanyika Februari 26, mwaka huu.
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Waliarwande Lema, alisema hayo jana alipotakiwa kutoa ufafanuzi kuhusu amri hiyo aliyodaiwa kuito kuzuia uchaguzi huo.
“Hakuna amri ya kuzuia uchaguzi wa meya, aliyesema mahakama imetoa zuio ni muongo,” alisema Hakimu Lema.

HAKIMU MFAWIDHI KISUTU
Awali mapema asubuhi jana, waandishi wa habari za mahakama waliwasili ofisini kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi Cysprian Mkeha kutaka ufafanuzi kuhusu zuio linalodaiwa kutolewa na mahakama hiyo kuzuia uchaguzi huo wa meya.Hakimu Mkeha, alisema Februari 25, mwaka huu hadi anaondoka kazini hakukuwa na maombi yoyote yaliyowasilishwa kupinga Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam.Alisema aliyekuwa na zuio hilo linalodaiwa kutolewa mahakamani alipeleke, na kwamba nyaraka halali ya mahakama lazima inakuwa na sahihi ya hakimu aliyetoa pamoja na sahihi yake. Mkeha aliwataka waandishi wa habari kumtafutia zuio hilo ili aweze kulizungumzia zaidi.
WAANDISHI NA MAJADILIANO
Baada ya maelezo hayo, waandishi kwa pamoja walitoka nje ya ofisi ya mfawidhi na kuanza mjadala kuhusu utata wa zuio hilo.Mjadala huo ulikuwa ni juu ya namna ya kuipata amri hiyo kuona kama ilikuwa halali ilitolewa na mahakama ama la.Baada ya dakika kadhaa, Hakimu Mkeha alipita katika eneo hilo na kuwataka waandishi hao kumfuata, ambapo wote waliambatana na hakimu huyo hadi katika ofisi ya Hakimu Leman a kumuuliza kuhusu zuio hilo.Swali: Mheshimiwa tunaomba kujua kama ulitoa amri ya kuzuia Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliotakiwa kufanyika Februari 26, mwaka huu.
Jibu: Hapana…Hapana.
Swali: Kuna amri ya zuio la Februari 5, mwaka huu lilitumika kuzuia uchaguzi, lilionyesha limetolewa na wewe.
Jibu: Kulikuwa na maombi ya zuio yalifunguliwa Februari 5, mwaka huu na Susan Masawe na Saad Khimji dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wakiomba zuio la muda mrefu la uchaguzi uliotakiwa kufanyika Februari 8, mwaka huu.Hakimu Lema alisema maombi hayo yalikuwa ya upande mmoja, ambapo mahakama ilitoa zuio dogo na kutoa muda mfupi hadi Februari 15 maombi yasikilizwe kwa pande zote mbili kuwapo.“Februari 15, mwaka huu ilipofika, waleta maombi hawakutokea mahakamani, kesi ikaahirishwa hadi Februari 23, mwaka huu ambapo pia hakuna aliyetokea.“Kwa kuwa hakuna aliyefika, mahakama ililiondoa shauri hilo, hivyo na zuio dogo pia liliondoka kwa sababu maombi yaliondolewa mahakamani,” alisema.
Hakimu Lema alisisitiza kuwa hakuna zuio lililotolewa na mahakama na kwamba aliyesema kuna zuio ni muongo.Hata hivyo, nakala inayodaiwa kuzuia uchaguzi huo ni ya Februari 5, mwaka huu ambayo kisheria haipo mahakamani tangu Februari 23 shauri lilipoondolewa.Hakimu Mfawidhi Mkeha alipotakiwa kuthibitisha kama alipokea maombi Februari 25 ya kuzuia uchaguzi na kumpangia hakimu yoyote, alisema hakuna maombi yoyote yaliyowasilishwa mahakamani hadi muda wa kazi unamalizika.
UCHAGUZI FEBRUARI 26
Vurugu kubwa zilitokea katika Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliopangwa kufanyika Februari 26, mwaka huu mara baada ya kuahirishwa tena kwa mara ya nne.Katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Theresia Mmbando ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, alitangaza kuuahirisha kwa madai ya kuwekewa pingamizi mahakamani na wakazi wa jiji hilo, Susan Massawe na Saad Khimji.Madiwani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa katiba ya Wananchi (Ukawa), walidai kuwa hawajapata barua ya pingamizi hilo, hivyo wakataka waruhusiwe kufanya uchaguzi peke yao kwa kuwa akidi ya madiwani kufanya uchaguzi ilikuwa imetimia.Wakati Ukawa wakijiandaa kufanya uchaguzi huo wenyewe, polisi zaidi ya 15 walivamia ukumbini na kuwataka waondoke jambo lililowachukiza na kuibua patashika ndani ya ukumbi.
KAULI YA SIMBACHAWENE
MTANZANIA lilipomtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene kuhusu utata huo, alisema kwamba hajapata taarifa zozote hadi kufikia jana.“Nilitegemea leo (jana) nipate taarifa ya kilichotokea, lakini kwa bahati mbaya huyo aliyepaswa kunipa taarifa hiyo niliambiwa alipigwa yuko hospitali. Siwezi kusema chochote kwa sasa hadi nitakapopata taarifa rasmi ndiyo nitaeleza msimamo wa Serikali,” alisema Simbachawene.
MDEE, KUBENEA MBARONI
Wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na madiwani wawili wa chama hicho, wamehojiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutokana na vurugu zilizotokea kwenye uchaguzi huo mwishoni mwa wiki.Wabunge hao ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Saed Kubenea (Ubungo) ambaye aliunganishwa katika mkasa huo wakati alipokuwa akiwasilisha malalamiko yake kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lukas Mkondya kuhusu kusitishwa kwa uchaguzi huo.Wakati akiwasilisha malalamiko hayo, alielezwa kwamba na yeye ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa kwa ajili ya mahojiano, hivyo alitakiwa kutoa maelezo yake.Mdee akiwa ameambata na Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Kati saa 7:20 mchana akiwa kwenye gari aina ya Prado yenye namba T 781 ANU huku ikiongozana na gari ya polisi Land Cruiser yenye namba T 424 BZN.
Baada ya kufika kituoni hapo, alipelekwa katika chumba cha Mkuu wa Upelelezi Kanda Malaumu ya Dar es Salaam na kuhojiwa.Mbunge mwingine ambaye anatakiwa kufika katika kituo hicho kwa ajili ya kuhojiwa ni Mwita Waitara (Chadema) ambaye anatafutwa na polisi.Hata hivyo, ilipofika saa 11:50 jioni waandishi wa habari waliokuwapo katika eneo la Polisi Kituo Kikuu cha Kati, walielezwa kwamba dhamana ya Mdee imezuiwa huku Kubenea akiachiwa.Katika mahojiano hayo ya polisi, madiwani wa Hamphrey Sambo wa Mbezi na Efraim Kinyafu wa Saranga wote wa Chadema pamoja na kada wa chama hicho Kata ya Mabibo, Shafii Juma waliunganishwa katika kesi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, Kubenea alisema alifika kwa lengo la kutoa taarifa ya udanganyifu uliowasilishwa na Wakili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Elias Nawela kuhusu zuio la kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.
POLISI WATINGA KWA MEYA
Awali maofisa wawili wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamevaa kiraia kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Ilala, walifika katika Ofisi ya Meya wa Ilala iliyopo eneo la Mnazi Mmoja na kumtaka meya hiyo, Charles Kuyeko kuwapatia majina ya madiwani waliofanya vurugu katika uchaguzi huo.Maofisa hao walikuwa na magazeti mawili ya kila siku ambayo yalikuwa na picha zilizoonyesha madiwani hao wakilumbana na polisi ambapo meya huyo alijibu kwamba hawatambui kwakuwa mkutano huo ulikuwa na madiwani wengi.Alisema iwapo wanahitaji kuwakamata, aliwataka kusubiri kikao cha madiwani kitakachofanyika Machi 3, mwaka huu na hivyo wanaweza kuwapata ila akatoa angalizo kwamba wasubiri hadi kikao hicho kitakapomalizika.
PROFESA SAFARI
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema kosa alilokamatiwa Mdee ni kumfanyia vurufu msimamizi wa uchaguzi huo, Mmbando.
“Halima hakuhusika kabisa na vurugu zile, lakini tunajua hizi ni hila za CCM na kesho (leo) tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari katika Ukumbi wa Karimjee,” alisema Profesa Safari ambaye ni mwanasheria.
WANASHERIA WAKOSOA
Wanasheria mbalimbali wamesema kuwa waliosababisha Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam kuahirishwa wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuwa ni kosa la kijinai.Kauli hiyo ya wanasheria imekuja muda mchache baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutoa tamko juu ya amri iliyotolewa kuzuia uchaguzi huo kuwa si halali.Akizungumza na MTANZANIA kupitia simu yake ya kiganjani, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema kitendo kilichofanywa na chama tawala CCM ni cha kihuni na kwamba hakipaswi kufumbiwa macho.“Huu ni uhuni waliofanya CCM…wachukuliwe hatua za kisheria, na polisi ndio wafanye hivyo kwa sababu ni kosa la jinai. Wanaendaje kusema uongo na kuzuia shughuli halali kwa uongo?” alihoji Lissu.Kwa upande wake aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles Rwechungura, alieleza kushangazwa kwa kitendo hicho akisema waliohusika kufanya hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.“Nadhani nitoe maoni yangu binafsi, si ya TLS kwa sababu mimi nimemaliza muda wangu hivi karibuni…hilo jambo kama ni la kweli limenisikitisha sana na kunishangaza kwa chama tawala kughushi, kudanganya na uchaguzi halali kuahirishwa, kwanza imetia hasara. Hivyo wahusika wachukuliwe hatua kwa sababu ni kosa la jinai,” alisema Rwechungura.
Habari hii imeandaliwa na Kulwa Mzee, Elizabeth Hombo, Nora Damian na Asifiwe George (Dar es Salaam)

No comments: