Tuesday 19 April 2016

Magufuli na Style yake mpya ya kutumbua majipu.


Tuseme tena kwa kinywa kipana. Haki haisimami kwa maamuzi ya jukwaani. Kinachofanyika ni uongozi kwa msingi wa kuogopa mtu badala ya kuogopa sheria na ukali wake. Unapomsimamisha mtu kazi hadharani kwa kusikiliza kelele za Mkuu wa Mkoa na katika "mob justice" hii basi hujengi ila unatia viraka tu. Haya yalifanywa huko nyuma katika zama za Mao, na inafanana kabisa na kile kipindi cha giza cha watuhumiwa wa uchawi ulaya waliochomwa moto hadharani kwa sababu ya woga.

Tunaendeshwa katika siasa za kitoto kabisa, kwamba Rais wa nchi anauliza wananchi achomwe mtuhumiwa au aachwe, tunasahau kwamba kama mwajiri kuna matakwa ya kisheria na haki za pande zote mbili. Nitatoa mfano mdogo miaka kumi nyuma nilipokuwa kazini. Mmoja wa wakurugenzi alikuwa akiiba fedha za kampuni. Alichomewa na wafanyakazi wake, haraka akapewa barua inayoendana na haki yake na ya muajiri katika masuala ya nidhamu. Alisimamishwa kama mtuhumiwa na kuhakikishiwa haki na heshima yake kama mtuhumiwa. Haki haijengwi kwa kuvunja nyengine hata kwa ukubwa wa kosa.

Alisimamishwa kazi kupisha uchunguzi, na moja ya amri kutoka kwa mkuu wa "HR" ni kwamba tuhuma zile zibaki kwa wakuu pekee kuepuka madhara ya kimaslahi katika uchunguzi au kumuondoshea heshima mtuhumiwa kabla ya hukumu kutolewa. Kesi ilifika mahakamani na mtuhumiwa akapewa kifungo cha mwaka baada ya ushahidi kuwa wazi wa wizi na kuthibitishwa na mahakama. Haki ya muajiri na muajiriwa haikubaliani kabisa na hii "mob justice" ya Magufuli tena tu kwa tuhuma za Mkuu wa Mkoa. Si tumeona juzi jinsi mahakama ilivyomuachia Meneja wa Tanesco baada ya kutoridhika na ushahidi wa wanaoshitaki, kwani nini kuwe na kukutupuka katika majukwaa na maamuzi ya ajabu kabisa?

Sina dhumuni ya kumtetea mtuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi yake na dhamana aliopewa au kama napinga kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mtuhumiwa ikiwamo kusimamishwa kazi ila ninachokiona tunakosea ni kuhalalisha namna ya usimamishwaji haki unavyofanyika kwa ubabe mkubwa huku tukivunja na kudharau haki kwanza ya ajira kwa muajiri na muajiriwa. Pili ni namna tunavyojitia aibu na hizi "mob justice" za majukwaa za kudhalilishana na kuwekeza haki pana kwa msingi wa uoga kwa mtu mmoja mwenye nguvu badala ya woga kwa taasisi yenye dhamana ya hukumu na kusimamia haki.

Magufuli anachokosa ni kulichukuwa hili suala kama lake binafsi, na kutumia ubabe katika tafakur ya kusimama na haki. Laiti kama ataisimamisha vyema mahakama na taasisi zetu za usalama na sheria basi haitatokea siku kwa Rais kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa jiji. Na ubaya katika tamthilia kama hizi za "mob justice" na woga wa kuvunja sheria kwa sababu ya mtu ni kwamba anapoondoka na haki yake nayo humfuata. Mfano mdogo tu ni Mwalim na jinsi alivyochangia anguko la haki baada ya kuondoka kwake sababu ni woga ulijengwa kwake na si kwa taasisi ya kusimamia haki.

Siamini kwamba utajenga haki kwa misingi ya ubabe, haina faida ya muda mrefu na athari yake ni jamii kusubiri uondoke tu warudi katika mazoea. Lakini kama unataka kuisimamisha haki ya kudumu, fanya marekebisho katika "pyramid" nzima ya haki, kuipa utukufu wake unaostahili, kurudisha imani yake kwa wananchi pamoja na uhuru wake katika maamuzi bila ya upendeleo kwa yoyote. Bahati mbaya sana Magufuli ni miongoni mwa wana CCM walioridhia kupingwa kwa rasimu ya Warioba iliobeba zaidi umuhimu wa maadili, haki na miiko ya uongozi. Miongoni mwa waliokataa kuyapunguza mamlaka makubwa ya Rais kwa Mahakama, Bunge na vyombo vya utoaji nidhamu. Ni miongoni mwa walioridhia Rais kubaki na nguvu kubwa kiasi sasa zinatumika majukwaani kama miaka ya 60 wakati taifa likiwa changa baada ya uhuru na bila ya elimu kwa walio wengi.

Hakuna kosa kubwa au udogo linalokidhi haja ya uvunjwaji wa haki na heshima ya watuhumiwa. Mtuhumiwa hata kwa ushahidi wa aina gani atabaki na haki ya kutodhalilishwa, kilichofanyika leo ni anguko la haki na dhamana ya muajiri kwa muajiriwa. Sasa kesi ifike mahakamani na mtuhumiwa aweze kujitetea na mahakama ikamuacha huru tutaweza kutumia jukwaa na kumuomba radhi? Tutaweza kumlipa gharama za kumdhalilisha hadharani? Turudi nyuma katika kesi ya meli ya uvuvi ya wachina na namna ya amri holcelaby zilizokuja kutuathiri. Usistaajabu kama anaweza kuonekana hana hatia, kwani yule meneja wa Tanesco aliefutiwa kesi aliwezaje kujitetea akashinda?
Wapo wanaosema Mkuu Makonda aliunda timu ya mawakili kuchunguza kashfa hii ili haraka Meya wa Ukawa  asije kukitia aibu chama cha Mapinduzi ilibidi Chama kicheze movie hii kupunguza demage ya majipu ya CCM kwenye serikali na mabaraza mengi ya miji inayoongozwa na ukawa.

No comments: