Friday, 17 June 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MPANGO WA KATIBU MKUU WA CUF MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD WA KUTAFUTA SULUHU YA MGOGORO WA KISIASA WA ZANZIBAR ALIOUTANGAZA JUZI HUKO MAREKANI INAYOTOLEWA LEO JUNI 17, 2016 NA MNADHIMU WA KAMBI YA CUF KATIKA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA ALLY SALEH (MB)
Ndugu Waandishi wa Habari,

Hivi sasa Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye ni Rais wa Nyonyo za Wazanzibarialiyeshinda Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana huko Zanzibar yupo katika ziara ya kimataifa nchini Marekani na Canada.

Ziara hiyo imefanywa kwa makusudi ili chama chetu kipaze sauti katika juhudi yetu ya kupaza sauti mbele ya jumuia ya kimataifa kuwaelezea yaliojiri Zanzibar na yanayoendelea kujiri ikiwa ni sehemu ya kupigania haki yetu ambayo tunaamini inshallah itarudi mikononi mwetu.

Maalim Seif pamoja na sehemu nyengine mbali mbali na kuonana na viongozi wa kiserikali wa nchi hizo, basi pia amefika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini New York ili kupaza sauti yetu juu ya dhulma iliyofanyiwa CUF na kuishitaki Serikali ya Rais John Pombe Magufuli ambayo imepuuza kilio cha CUF.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete ndio iliyoiweka madarakani Serikali haramu ya Dk Ali Muhammed Shein na Dr. Magufuli ndie anayeilinda hivi sasa kwa kisingizio cha kufungwa mikono kikatiba.

Ndugu Waandishi
CUF inazidi kusisitiza kuwa dhulma inayoendelea hadi sasa kwa Polisi kukamata watu ovyo na kupiga mabomu ya machozi hata juzi usiku, kukamata watu ovyo, lawama yote ya haya anabeba Rais Magufuli na tunaunga mkono hatua ya Maalim Seif kuuelezea ulimwengu juu ya hilo pale alipohojiwa na kipindi cha Televisheni cha Voice of Americakupitia mtangazani Shaka Ssali.

Ndugu Waandishi

Wabunge wa CUF kwa kipekee kabisa wanaunga mkono tamko la Malaim Seif kuelekeza kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa ulipo Zanzibar hivi sasa ambapo CUF inaigomea Serikali ya Dr. Shein.

Wabunge wa CUF wanampongeza Maalim Seif kwa kufungua milango ya kuwezesha kuanzwa kwa mchakato wa kutufuta suluhu huko Zanzibar yote akiwa na mapenzi na nchi yake na tunataraji kuwa watawala wa Zanzibar na wa Serikali ya Muungano watapokea hatua hiyo ya Maalim Seif.

Maalim Seif ameelezea juu ya Mpango wa Hatua 6  (Six Point Plan) wa kuitoa Zanzibar katika jinamizi liloinamia hivi sasa ambao ni kama huu ufuatao:

1.    Kuundwa kwa Serikali ya pamoja ya muda

2.    Serikali hiyo kuwa ni ya kitambo cha miezi 6

3.    Serikali hiyo kuongozwa na Mzanzibari asiye na muelemeo wa kisiasa na anayekubali na pande kuu za kisiasa Zanzibar

4.    Kuandaliwa uchaguzi mwengine Zanzibar ndani ya kipindi hicho cha miezi 6

5.    Uchaguzi huo usimamiwe na jumuia za kimataifa

6.    Kuheshimika kwa matokeo ya Uchaguzi huo kwa mujibu wa sauti ya umma

Ndugu Waandishi

Hatua hii ya Maalim Seif inadhihirisha umahiri wake katika siasa, moyo wake wa kuipenda Zanzibar na ujasiri wake wa kufanya maamuzi magumu na ndio maana tukaona haja ya kumuunga mkono ili kuipaza sauti yake hiyo ya kusaka suluhu ya Zanzibar isikike na Watanzania wote.

Tunaamini kuwa Wazanzibari na Watanzania walikuwa wakisubiri kwa hamu hatua hii ya Maalim Seif  ya Chama cha CUF kutoa pendekezo la kuitisha mazungumzo ili kuanza kulikabili suala hilo la Zanzibar kwa maslahi ya Wazanzibari na amani na utulivu wa Watanzania.

Ni imani yetu kuwa karibuni tu tutasikia kauli ya Serikali ya Muungano na watawala wa Zanzibar juu ya pendekezo hili la Maalim Seif kwa sababu hakuna njia yoyote ya kupata suluhu ya Zanzibar bila mazungumzo ya kukaa mezani na CUF imefungua mlango kama ilivyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 1995 na pia baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2000 na kupatikana muwafaka kwa faida kubwa ya Wazanzibari.

ALLY SALEH  (MB)

MNADHIMU WA KAMBI YA CUF

Bunge la Jamhuri ya Muungano

No comments: