Sunday, 12 June 2016

Zanzibar haiko shuwari kama Munavyofikiria

NI takribani miezi saba sasa tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Marudio Zanzibar ambao ulifanyika MaƧhi 20, mwaka huu.
Kumalizika kwa mchakato wa uchaguzi ni hatua moja kubwa ya kuanza hatua za ujenzi wa taifa kwa nguvu ya pamoja -lengo likiwa ni kuwatumikia wananchi.
Kwa asilimia kubwa upande wa pili wa Muungano (Tanzania Bara) wamemaliza siasa za uchaguzi mkuu na sasa ni kazi ya kuwatumika wananchi ikiwa ni jukumu la msingi kwa serikali iliyopewa ridhaa na wananchi kuwatumikia.
Kasi hiyo inaongozwa na kauli maarufu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, isemayo "Hapa Kazi Tu".
Upande mwengine wa Muungano (Zanzibar), hali ni tofauti sana. Naweza kusema ni afadhali ya siasa zilizokuwepo wakati Uchaguzi Mkuu kuliko kipindi ambacho Zanzibar inapita kwa sasa.
Ni wazi kwamba hivi sasa, Zanzibar inapita katika kipindi cha siasa za majitaka, chuki, uhasama, fitna na mfarakano mkubwa katika jamii.
Ni kipindi hiki ambacho shughuli za uchaguzi mkuu zimemalizika karibu siku 90 nyuma, matokeo yametolewa katika uchaguzi ambao ulikosa msisimko na haukuwa na cha kushangaza katika matokeo yake kufuatia kususiwa na vyama kadhaa vya upinzani kikiwemo chama kikuu cha upinzani Visiwani Zanzibar, CUF.


Matokeo yaliyotangazwa ya kukipa ushindi mkubwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye ngazi ya Madiwani na Wawakilishi hayakuwa ya kushangaza. Dalili zilionyesha mapema kuwa CCM watashinda nafasi hizo kwa asilimia mia moja huku ngazi ya Urais wakishinda kwa aslimia 91.4.
Hii ni kutokana na kuwa mshindani mkubwa wa CCM katika siasa za Zanzibar; chama cha CUF kilikuwa tayari kimetangaza kususia uchaguzi huo wa Machi 20.
Wakati tayari Dk. Ali Mohammed Shein akiwa tayari ametangazwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), ameapishwa na kuunda serikali, kuitisha Baraza la Wawakilishi na kuzindua Baraza la Wawakilishi mpaka katika hatua kubwa ya sasa ya kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17; bado Zanzibar inaishi katika siasa za uchaguzi - tena zikiwa mbaya zaidi kwa wakati huu.
Nasema ni mbaya zaidi kutokana na kuchagizwa na kauli na matukio ambayo hayaoneshi kamwe afya njema kwa ustawi kama taifa moja.
Tayari wananchi wa Zanzibar wamegawanyika kisiasa na wamekwenda mbali zaidi pengine kuliko wakati wowote wa siasa chafu za Zanzibar.
Kauli za viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa serikali zimekuwa zikitengeneza chuki na visasi kwa wananchi kila kukicha.
Leo Zanzibar watu hawasalimiani, wanachagua misikiti, usafiri, hawashirikiani katika misiba, harusi na shughuli nyengine za kijamii kwa kutofautiana itikadi za vyama vya siasa.
Haya hayakuja kwa bahati mbaya, yamelimwa na kupaliliwa huku yakiwekewa mbolea ya 'samadi' kuyarutubisha na sasa ndiyo tunayavuna.
Nasema tunayavuna kwa sbabu yamepandwa na tukaruhusu yakuwe na sasa tunayavuna. Baadhi ya wanasiasa Zanzibar wamepanda chuki ya U-CCM na U-CUF, U-Unguja na U-pemba huku akina sisi tukishangilia kauli zao chafu na za kupuuzwa matokeo yake ndiyo kugomeana katika shughuli za kijamii.
Athari ya migomo hiyo ni mbaya na kubwa na kwa bahati mbaya sana wanaoumia kwenye jamii ni wananchi ambao kwa kawaida ni wale wenye kipato kidogo.
Ingawa kwenye nchi yenye serikali makini lazima hatua, tena za busara sio za kibabe, zichukuwe nafasi yake kuhakikisha mshikamano unapatikana katika jamii, kuendelea kuongoza jamii yenye utengemano kwenye nchi ni hatari sana na katika hili hatua za haraka na thabiti kabisa zinapaswa zichukuliwe.
Tusiaminishane kuwa Zanzibar hakuna tatizo, itakuwa ni unafiki na uongo wa kiwango kikubwa kujiaminisha kuwa eti Zanzibar ni shwari.
Zanzibar kuna tatizo tena si dogo na abadan halipaswi kukaliwa kimya, lazima kitu kifanyike kuwatoa huko waliko Wazanzibari.
Najua hili lina uzito wake kwa sababu miongoni mwa viongozi wakubwa wa vyama vya siasa na viongozi wa ngazi za juu wa serikali miongoni mwao si waumini wa umoja wa kitaifa. Kwao, hali hii wanaifurahia sana kwa maslahi yao binafsi bila kujali athari inayobakia katika jamii.
Jamii ya Wazanzibari haihitaji utengano inahitaji umoja kama tunavyojulikana tangu enzi na dahari kuwa Wazanzibari ni watu wastaarabu, wakarimu, wapole na watu wanaoishi kwa kupendana sana.
Bahati mbaya hayo yote yanaweza kubakia katika vitabu vya historia kwa sababu tayari wanasiasa walishavuruga hiyo hali kwa maslahi yao huku wanachi wakitumika bila kujijua kuwa wanatumika kama ngazi tu.
Lazima kifanyike kitu kwa ajili ya Zanzibar, tuache kudanganyana kwenye majukwa ya kisiasa kuwa Zanzibar ni shwari, kuna tatizo Zanzibar.
Maridhiano hayaepukiki, swali ni aina gani ya maridhiano yanayohitajika kwa sasa? Kwa sababu huko nyuma tayari kuna miafaka karibu mitano imeshafanyika lakini haikuwa na matokeo chanya ya kuendelea matokeo yake mmoja kwa utashi wake anatumia nafasi aliyonayo kuonekana yeye ni bora zaidi.
Maridhiano yanayohitajika Zanzibar kwa sasa yawe tafauti kabisa na maridhiano yote yaliyopita. Lazima yawekewe misingi imara ya kuendelea na kuzuia mianya yote ambayo inaweza kutumiwa na wahafidhina kuwarejesha Wazanzibari kwenye siasa za chuki na visasi.
Wazanzibari hawahitaji kurejea kwenye chuki na uhasama. Zanzibar inahitaji kusonga mbele si kila uchao kuwe na siasa za majitaka tu huku mfumuko wa bei wa bidhaa muhimu kama chakula zikiendelea kupanda kwa kasi aya ajabu.
Lazima tuandae mazingira ya kufanyika maridhiano ya kweli sasa na katika hili kunahitajika kujitolea zaidi na kuweka pembeni kila aina ya maslahi binafsi tuongozwe na Uzalendo kwanza kwa maslahi makubwa ya Zanzibar ya sasa na Zanzibar ya miaka elfu mia moja ijayo.
Zanzibar inahitaji kusonga mbele, nafasi bado ipo kuitoa hapa na huko inapoelekea. Tutumie akili zetu kwa weledi zaidi kwa kuangalia maslahi mapana zaidi ya Zanzibar tunayoitaka.
Tuanzie hapa kujua chanzo na namna ya kutibu tatizo tena iwe tiba ya milele si hii ya 'nusu kaputi' –kupatana miaka miwili ya kinafiki baadae tunarudi tena kwenye siasa za ubaguzi na chuki.
Tuongozwe na uwazi, ukweli na uwajibikaji kwa kila mmoja wetu ili kuirudisha Zanzibar ya upendo, ukarimu na umoja.
Mwandishi wa makala Ali Mohammed ni mwanahabari mwenye makazi yake visiwani Zanzibar. Anapatikana kwa simu namba 0773 572592.


No comments: