Monday, 24 October 2016

PROF NDALICHAKO JIAMINISHE KWA WATANZANIA KAMA WAO WALIVYOKUAMINI.

NA,
MWL RAZAQ MTELE MALILO.

Mh Prof Ndalichako, waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi,
Watanzania wengi walifurahi kusikia uteuzi wako wa kuiendesha wizara hii ambayo ni msingi wa maendeleo Katika taifa lolote lile duniani  na Mimi pia nilikuwa na imani na wewe japo sijapoteza imani moja kwa moja ila unanikatisha tamaa juu ya utendaji wako Katika mambo mengi Sana unayoyafanya na huwa najiuliza ni wewe Ndalichako ambaye ni Profesa?
Maswali haya pia watanzania wengi hujiuliza na wengi hawaamini kuwa ni wewe na pengine wangesikia Ndalichako mwingine ameonekana Malawi wangeamini.
Watanzania wanaanza kupoteza imani na wewe japo bado hatujakata tamaa moja kwa moja ila tunashtushwa na utendaji wako kwani haendani na matarajio ya Watanzania.

NI WAPI UNATUANGUSHA?

1. TAMKO LA ULAZIMA WA KUSOMA MASOMO YA SAYANSI KWA SHULE ZA UPILI.

Mh Ndalichako na umma wote wa Watanzania nawajulisha kuwa hata Mimi nathamini na kutambua kuwa sayansi ni muhimu na hivyo lazima serikali na wadau wafanye juhudi kwenye suala hili.
Mataifa mbalimbali yaliyoendelea duniani yaliwekeza kwenye elimu sayansi.

Mh,  tamko lako hili ni la Nia njema ila Kama Profesa ulitakiwa kufanya uchunguzi na utafiti kabla ya kulitoa kwani muda uliotoa tamko hili sio muhafaka hasa ukizingatia bado Hakuna mazingira rafiki kwa masomo hayo.

Nikitegemea kabla ya tamko hili ungeandaa mazingira bora kwa masomo hayo Kama kutayarisha walimu wa kutosha wa masomo hayo na kuandaa mazingira ya kujifunza na kufundishia masomo hayo Kama kukamilisha ujenzi wa maabara za masomo ya sayansi kwa kila shule na kuwa na vitabu bora vya kiada na ziada vya masomo hayo.
Baada ya kukamilisha hayo kwa kila shule ndipo ilitosha kutoa tamko hilo kuliko ulivyofanya.

Zipo shule nyingi za upili zinazomilikiwa na serikali hasa zile za Kata hazina walimu wa sayansi hata mmoja na Leo unapowapa agizo hili unategemea watasoma kwa njia zipi....!!!...???.
Hapa nilishtushwa na hata watanzania wengi wanaofikiri kwa kuitumia ubongo wamepigwa na butwaa kuhusu agizo hili.
Mh,  nikupe mfano wa shule niliyosoma Mimi, Shule ya Upili Mipingo iliyopo mkoani Lindi. Ambayo tangu ianzishwe 2007 haina Mwalimu wa Hesaba hadi sasa na mwaka juzi imepata mwalimu mmoja wa Biolojia na kufanya kuwa na Mwalimu mmoja wa sayansi. Hiyo ni mfano ila zipo shule nyingi hazina maabara hata Mwalimu mmoja wa sayansi na zipo nyingine hazina walimu wakutosha hata Hao walimu wa sanaa.
Hivyo Mh,  Kama Prof ulitakiwa kuandaa mazingira kwanza au ungesema baada ya miaka Fulani masomo ya sanaa yatakuwa lazima.
Hapo tungekuunga mkono.

2. KUSHINDWA KUZISIMAMIA TCU NA HESLB.

Ni dhahiri waziri Prof Ndalichako umeshindwa kuzisimamia taasisi hizi zilizopo chini yako na hata Mh Rais Magufuli amekiri hili alipokuwa akizungumza na umma wa wanaudsm alisema kuwa hakukuwa na Coordination.

TCU inatoa selection za vyuo kwa wanafunzi huku baadhi ya  vyuo vikiwa vimebakiza wiki mbili hadi moja kabla ya kufunguliwa na majina hayo yanatakiwa yapelekwe bodi ya mikopo kwa ajiri ya kuyapitia ili kutoa mikopo kwa wenye sifa.
Utakuta muda unabana kwa bodi ya mikopo HESLB kufanya uchambuzi na kutoa majina Ya wanufaika.
Lakini pia TCU imekuja na utaratibu wa kutoa majina upya kwa wanafunzi wanaoendelea na wameshindwa kutoa majina hayo wakati vyuo vimefungwa na wameanza kutoa Huku tayari baadhi ya vyuo vikiwa vimefunguliawa Kama vile UDSM.
Uzembe wote huu TCU wanafanya Prof Ndalichako anaona na Hakuna aliyochukua.

Kwa upande wa HESLB  , Licha ya kufanyika mageuzi makubwa kwenye hii taasisi lakini bado hata viongozi wa sasa wameshindwa kujifunza na kurekebisha makosa ya viongozi wale waliotumbuliwa.

HESLB Licha ya kufungua mapema maombi ya mikopo kwa wanafunzi lakini uzembe uliofanyika ni kuchelewa kuyapitia majina hayo.
Imetoa majina waliokosea kuomba wakati muda umeenda mno na siku ya mwisho wa kufanya marekebisho kwa wanafunzi waliokosea kujaza fomu ilikuwa ni siku sita kabla ya UDSM kufunguliwa na vyuo vingine pia.
Mimi nilijiuliza hivi HESLB itachukua muda gani kuyapitia majina hayo na kutoa majina Ya wanufaika kabla ya vyuo kufunguliwa?
Mwishowe walishindwa au wameshindwa kutoa majina ya wanufaika kitu ambacho kimepelekea usumbufu kwa wanafunzi.
Hayo yote yasingejitokeza Kama Ndalichako ungekuwa makini kuzisimamaia taasisi hizi zilizopo chini yako ili kutekeleza Majukumu yake kwa wakati na kuepuka usumbufu kwa wanafunzi.
Yote yanafanyika wewe ukiwa unaona.


3. UTARATIBU WA UTOAJI WA MIKOPO.

Tumeona Prof Ndalichako umechemsha kwenye utoaji wa mikopo kitu kilichosababisha lawama kila Kona Licha ya kujitetea kwingi lakini Huwezi kukwepa ukweli kwamba wewe ndio chanzo cha haya yote.

Tumeona vigezo mbalimbali ambavyo wizara yako kwa kushirikiana na HESLB mmevitoa vikionesha vipaumbele zingatiwa Katika utoaji wa mikopo.
Vigezo vingi mmevianishi mkionesha vipaumbele vyenu kwa masomo ya sayansi .
Nilishtushwa Sana na kigezo hiki kwani kimekuwa kikienda kinyume kabisa na agenda za Mh Rais kuwa yeye ni Rais wa wanyonge yaani masikini na Shule nyingi za Kata ndiko Hao masikini wanasoma na shule hizo ndizo hazina walimu wa sayansi Kuna walimu wachache tu wa masomo ya sanaa na watoto Hao hulazimika kusoma kwa shida Sana masomo hayo ya sanaa.
Sasa Leo ukiwaambia kigezo cha mikopo ni sayansi, Je watoto wa masikini waliosoma sanaa watasomaje vyuo vikuu?
Shule zenye mazingira mazuri kwa masomo ya sayansi ni zile shule nzuri za binafsi walizosoma watoto wa vibopa Kama zile za Feza, Marian, St Mary's n.k na kwa zile chache ni za mijini na zile shule maalumu Kama Iliboru, Mzumbe, Kibaha n.k . Hapa nikaona dhahiri elimu yetu inakwenda kuwa ya kimatabaka kitu ambacho ni hatari Sana.
Nikajiuliza Sana Mimi ni mwanafunzi tu nimeliona hili wewe ni profesa umeshindwaje kuiona hili au ulifanya makusudi?  na Kama ulifanya makusudi kwa malengo yapi?
UJITATHMINI.

Lakini pia mama mikopo mliyotoa ni kwa wachache mno na mnasema mtatoa kwa wanafunzi zaidi ya 20 elfu!  Sasa najiuliza mnatoa lini na wakati baadhi ya vyuo Kama UDSM, SAUT na TEKU tayari masomo yameanza na wanafunzi wanashindwa kufanya usajiri Chuoni wakisubiri mikopo.

Kama Hiyo haitoshi Hawa wachache mliowapa mikopo kwa kipaumbele wa sayansi mmetoa mikopo ya ajabu na haukukuwa na sababu ya kutoa ni heri mngewanyima kabisa kwa baadhi.
Nitoe hualisia,  hapa UDSM yupo mwanafunzi amepewa mikopo kwenye chakula na malazi amepewa Tsh 19500 atumie kwa siku 60 yaani ukigawa kwa siku hizi mwanafunzi huyo anatakiwa atumie Tsh 300 kwa siku.
Ukisimuliwa Huwezi kuamini ila Ukiona utashangaa.
Nikajiuliza mmefikiria nini kufanya hivi au Je nyie watoto wenu mnavyowapeleka shule mnawapa Tsh 300 kwa siku?
Nilishangaa Sana na nilijilazimisha tu kuamini kuwa waliotoa mikopo hii miungoni mwao yupo Profesa au maprofesa.
Mmetumia means tested kwa kila kipengele kwenye kutoa mikopo.

CHA AJABU
Baada ya malalamiko mengi tumekusikia ukiongea na TBC Oktoba 20 kuwa utaratibu wa zamani utarudi kwa pesa za kujikimu yaani Tsh 8500 kwa siku lakini ukasema kwa muhula huu na baadae utaratibu wa means tested utarudishwa pale wanafunzi watakapo patiwa elimu.
Nilicheka Sana kicheko cha butwaa na kujiuliza ni elimu gani Hiyo utatoa ili ueleweke.   !
Kwa ufupi nikuambie means tested kwenye pesa ya kujikimu,  vitabu na steshenari pamoja na mafunzo kwa vitendo haiwezekani na Hakuna haja ya elimu yoyote na hapahitaji elimu hata ya chekechea kupinga hili na halitekelezeki na wala husijaribu usije Leta mahafa ya 2011.
Suala la mikopo elimu ya juu bado hujatolea ufafanuzi wa kina nakushauri ufute kabisa badala ya kusitisha means tested kwa kila kipengele hilo halikubaliki hata na Mawe.

Mwaka 2011 ulitokea mgomo mkubwa UDSM kipindi hicho wakidai Kutokana na ugumu wa maisha pesa ya kujikimu ipande kutoka 5000 hadi 10000 madai yaliyopelekea mgomo mkubwa na kusababisha wanaharakati akina Alfonce Lusako, Ado Shaibu na wengine kufukuzwa chuo.
Mgomo huo ulipelekea kuongezeka kwa pesa hizo hadi kufikia Tsh 7500 na sasa 8500 . Sasa ugumu wa maisha unapanda siku hadi siku na hivyo 8500 haitoshjmi alafu Leo utoe 300 kwa siku hizo kama sio matusi na dharau kwa wanachuo tuitaje? Hivi ingekuwa wewe ndo mwanafunzi unapewa 300 hata maji nusu Lita haupati Je ungekubali?
JITATHMINI KISHA JIREKEBISHE.

HITIMISHO

Tatizo kubwa la taifa letu limekosa muhafaka wa elimu. Kila waziri anayekuja analeta mambo yake Kama kwamba elimu ya Tanzania ni mali ya waziri .
Nakuomba Mh Waziri japo ya kasoro zako lakini bado hatujapoteza imani moja kwa moja na wewe japo kwenye nchi za uwajibikaji ulitakiwa ujiuzulu kwa kosa la uzembe na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watoto wa masikini lakini kwa vile TZ haijafikia huko ni wakati wa kujisahihisha kwako  na endapo ukiendelea hivyo wasomi hatutakuacha ukiangamiza taifa tutakuchukulia Hatua kwa maslai MapMapana ya taifa hili.
Nakushauri shirikiana na wadau wa elimu Kama TSNP ili kutafuta muhafaka wa elimu wa taifa letu.

KAZI NJEMA.
Imeandikwa na :-

Mwl Razaq Mtele Malilo.
BAED UDSM.

0659913056
0625568417

mtelemwalimu@gmail.com

No comments: