Anaandika Dr.Christopher Cyrilo (MD).
____________________
Pongezi kiduchu zimfikie Nape Nnauye kwa kuonesha kuwa kinyume na ufedhuli, lakini pongezi hizo kiduchu na hatua yake ya kuwa kinyume na ufedhuli, havifuti ufedhuli wake. (Nape ni fedhuli anayevuna alichopanda).
Kwa maneno machache tu;
1. Nape na vijana wenzake wa CCM ndio waliozunguka nchi nzima kumtukana Lowassa, ambaye wakati huo alikuwa moja kati ya watu muhimu ndani ya Chama chao. Lakini kwa sababu ya kutumikia makambi na makundi ya chama, wakazunguka kutukana na kupakaza uongo kwa manufaa ya kundi fulani.
2. Nape ndiye aliyetangaza ushindi wa CCM hata kwa goli la mkono, akijua kabisa ni kinyume cha demokrasia.
3. Nape ndiye aliyewatolea maneno machafu waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi mkuu mwaka 2015, waliodai uchaguzi ulikua na mapungufu mengi.
4. Nape ndiye aliyetangaza kulifungia MILELE gazeti la Mawio, kwa madai ya uchochezi, kwa sababu tu liliandika habari zisizowafurahisha watawala.
5. Nape ndiye aliyelifungia gazeti la Mseto kwa miezi 36 (miaka mitatu) kwa madai ya kuandika habari zenye kumchafua Naibu waziri wa Ujenzi Edwin Ngonyani.
6. Nape ndiye aliyefungia Radio Magic Fm na Radio Five Arusha kwa madai ya uchochezi, kisa tu radio hizo zilikua zilitoa nafasi kwa viongozi wa upinzani kuongea na wananchi.
7. Nape ndiye aliyewasilisha hoja bungeni ya kufuta bunge Live, na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kufuatilia kazi za viongozi wao bungeni.
8. Nape ndiye anayedaiwa kuagiza Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Lindi Selemani Mathew afungwe gerezani kwa kufanya mkutano bila kibali, kwa sababu Mathew alimshinda kwenye kura za maoni jimbo la Mtama mwaka 2015 akakatwa, na kwenda Chadema.
9. Nape akiwa Katibu Mwenezi wa CCM ndiye aliyesema CCM haiwezi kuondolewa madarakani kwa vipande vya karatasi.
10. Nape ndiye aliyetengeneza propaganda ya kusema Lowassa ni mgonjwa na hafai kuwa Rais. Propaganda hiyo ilitumika na viongozi wa CCM kumchafua Lowassa na kumpunguzia kura.
11. Nape akiwa mkoani Ruvuma kwenye kampeni za uchaguzi, alimuita Magufuli Rais hata kabla ya uchaguzi. Yani alijiona kama Mwenyekiti wa Tume ya ucjaguzi mwenye uwezo wa kupanga matokeo na kuamua nani awe kiongozi.
12. Nape akiwa Katibu Mwenezi wa NEC na mjumbe wa Kamati Kuu ndiye aliyewasilisha azimio kwenye Kamati ya maadili la kumkata Lowassa katika hatua za awali za mchujo. Azimio hilo liliungwa mkono na wajumbe wengine na Lowassa hakupita hata kwenye 5 bora.
13. Nape ndiye aliyeshawishi wafuasi wa Lowassa waliobaki CCM watimuliwe akiwemo Mhe.Sophia Simba ambaye amevuliwa uanachama na kupoteza ubunge wake na uenyekiti wa UWT.
14. Nape ndiye aliyekuwa injinia wa kupitisha muswada wa sheria mbaya kuliko zote ya habari, ambao tofauti na lengo linaloelezwa, ukiisoma sheria ile na kuielewa, utagundua sio tu inaminya uhuru wa kupashana habari lakini pia inapingana na stratejia za kupambana na ufisadi, stratejia ya 'Whistle blower policy' inayotajwa kuwa bora kabisa katika kupamabana na ufisadi, inawekewa ukinzani na sheria ya Habari ambayo Nape alihusika moja kwa moja katika kuipitisha.
15. Nape ndiye aliyepigania sheria ya mitandao ipitishwe akiwa Katibu Mwenezi wa CCM ili kuzuia nguvu ya vijana wa upinzani kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
16. Nape ameongoza juhudi za waandishi kunyanyaswa, kupuuzwa na kudharauliwa. Hakuna kipindi waandishi wameishi kwenye mateso kama kipindi cha utawala wa Nape.
17. Nape ndiye aliyewasilisha hoja bungeni ya kutaka vyombo vyote vya habari (Radio na TV) vijiunge na TBC kila siku saa 2 usiku kwa ajili ya taarifa ya habari.
18. Nape ndiye aliyepitisha muswada wa habari (ambao kwa sasa ni sheria) ya kulazimisha waandishi wote wa habari kuwa na degree moja kabla ya mwaka 2021. Mwandishi ambaye hatakuwa na degree wakati huo HATATAMBULIKA kama mwandishi wa habari.
Huyo ndiye Nape Moses Nnauye ambaye leo kuna watu wanamuona shujaa, kwa sababu amevuliwa uwaziri. Hivi yeye ni mtu wa kwanza kuvuliwa uwaziri? Mgogoro wake na Makonda haumfanyi kuwa shujaa.
Kuna watu wanasema ni shujaa eti kwa sababu ya kuunda kamati ya Uchunguzi uvamizi wa Clouds. Lile ni jukumu lale kama Waziri. Na asingefanya hivyo umma ungemuwajibisha. Sasa mnamuonaje shujaa mtu aliyetimiza wajibu wake? Hivi housegirl wako akideki nyumbani utamuona shujaa wakati ametimiza wajibu wake?
Labda tumpongeze kwa ujasiri wa kujitokeza hadharani na kupinga udikteta wa Rais wake. Udikteta ambao Lissu ameupinga kwa muda mrefu. Wakati akina Lissu wanaongea akina Nape walidhani hawahusiki, kwa hiyo wakakaa kimya. Leo yamewakuta wao wanataka kufanya ni msiba wa kitaifa.
Yani wakati Lema anakamatwa na kudhalilishwa akina Nape walikaa kimya. Lissu kukamatwa na kudhalilishwa Nape kimya. Vijana wa upinzani kunyanyaswa, kupigwa (refer Mdude), kufungwa magerezani (refer Mwaifunga) na wengine kupotezwa (refer Ben Saanane) Nape na wenzie walikaa kimya kama vile hayawahusu, leo yamemkuta yeye anaonekana shujaa?
Ukweli ni kwamba Nape hajawahi kuwa mtu muhimu kwa taifa, bali amekuwa mtu muhimu sana kwa CCM. Ameisaidia CCM, ameipigania CCM, alijitoa kwa ajili ya CCM. Alifanya kila aliloweza kuhakikisha CCM inabaki madarakani. Nape, January na Mwigulu ndio waliomuweka JPM madarakani kwa kutumia mbinu halali na haramu. Bila hawa watu watatu pengine tungekuwa tunaongea mengine kwa sasa.
Kwahiyo kinachomtokea Nape ni matokeo ya kile walichokitengeneza wenyewe. Anavuna matunda ya ufedhuli wake. Nape kafanya uovu mkubwa sana kwenye nchi hii ili kuisaidia CCM. Ni uovu wenye manufaa kwa CCM, sio kwa Taifa.
Kwa hivyo, ikiwa Nape anahitaji huruma, basi atahitaji zaidi kuonewa huruma na wanaCCM wenzake kuliko watanzania aliowanyanyasa, kuwakebehi na kuwadharau kwa muda mrefu.
Ushauri wa bure: Nape kama mwanasiasa mwingine yeyote ana tamaa ya madaraka makubwa zaidi kuliko aliyowahi kushika. Kwahiyo ni vema akawa mkimya kwa kipindi hiki kuliko kipindi chochote kile. Akae kimya, arudi kuwatumikia watu wa Mtama. Asome kitabu cha Robert Green; 48 laws of power, aangalie amekosea wapi.
Zaidi ya hayo, amtafute mzee Lowassa amuombe msamaha na kuomba somo zaidi la siasa. Ajifunze kwa nini Lowassa bado ni mtu mwenye ushawishi mkubwa pengine kuliko aliyemteua na kumtumbua. Alamsiki.!
©Dr.Chiss Cyrilo, 23/03/2017.
No comments:
Post a Comment