MAELEZO YA MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI TAIFA MHE. JULIUS MTATIRO MBELE YA WAANDISHI WA HABARI [PRESS CONFERENCE] ILIYOFANYIKA LEO JUMATATU TAREHE 26 FEBRUARI, 2018 KATIKA OFISI YA WABUNGE WA CUF MAGOMENI-DAR ES SALAAM.
TULIREJESHE TAIFA LETU KWENYE MISINGI:
Ndugu wanahabari,
Leo tumewaiteni hapa kwa sababu mwelekeo wa Taifa letuni mbaya sana, sisi kama moja ya vyama vya siasa makini na vyenye nguvu hapa nchini, tunalo jukumu la kusema kwa niaba ya wananchi wa Taifa letu –jukumu hilo kikatiba ni kuishauri serikali, kuikosoa, kuchunguza mwenendo wake na kuutolea maoni na mapendekezo ili ijirekebishe.
1. MAUAJI, UTEKAJI NA MASHAMBULIZI;
A. Mauaji ya kinyama
Ndugu wanahabari, Taifa zima linafahamu kuwa vitendo vya mauaji ya kutisha, utekaji na uteswaji wa watu na mashambulizi yenye madhara ya kifo au kuumiza, kwa sasa ni mambo ya kawaida kabisa hapa Tanzania. Kwa kifupi tunawakumbusha matukio ya kutisha ya mauaji ambayo yamelitia taifa leo madoa ya damu slakini hadi sasa vyombo vyenye dhamana havina majibu ya matukio hayo:
1.1 Mauaji ya MKIRU
Mwaka jana kulizuka mauaji mabaya sana ambayo yaliangamiza watu mbalimbali katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Mauaji yale yalitokomeza roho za viongozi wa CCM zaidi ya 15 na takribani dazani nzima ya vijana wetu wa Jeshi la polisi. Wabunge walitaka kujadili jambo hilo wakakatazwa na hadi leo watanzania hawajui chochote, nani alikuwa anaua watu MKIRU, alikuwa ana ajenda gani, je alikamatwa, je amefikishwa kwenye mamlaka gani? Haijulikani.
1.2 Tarehe 01 Februari 2016, Diwani wa kata ya Kimwani iliyoko Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, Silvester Miga (CUF) aliuawa kikatili kwa kukatwakatwa. Baadaye Jeshi la Polisi liliwakamata watu wawili na kumuacha mtuhumiwa mkuu kwa sababu yeye ni kada wa CCM.
1.3 Tarehe 14 Novemba 2015, Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Geita ndugu Alphonce Mawazo aliuawa kikatili kwa kukatwakatwa na silaha zenye ncha kali huko Katoro. Ushahidi unaonesha kuwa waliomshambulia ni vijana wa Green Guard wa CCM na vijana hao wanajulikana mpaka kwa majina yao. Lakini wauaji hawakuwahi kuchukuliwa hatua.
1.4 Tarehe 28 Septemba 2017, Kaimu Mwenyekiti wa CUF Jimbo la Mto Pepo, Zanzibar, Ndugu. Ali Juma Suleiman aliuawa kikatili na ‘Mazombi’, kikosi maalum cha mauaji na utesaji ambacho kila mara huwalenga wanachama wa CUF. Hadi leo, SMZ haina mpango wa kukikomesha kikundi hicho kwa sababu kinaisaidia CCM kupunguza nguvu wafuasi wa CUF kwa kutumia njia haramu na za kinyama.
1.5 Kada na kiongozi wa CHADEMA kata ya Hananasifu Jimbo la Kinondoni, Daniel John, alitekwa tarehe 12 Februari 2018, kesho yake mwili wake uliokotwa katika ufukwe wa Bahari wa Coco-Beach ulioko jijini Dar es Salaam ukiwa na majeraha makubwa, inaonekana aliteswa sana kabla ya kuuawa. Hadi sasa polisi wanapiga danadana.
1.6. Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Bi Akwilina Akwilin, aliuawa kinyama kwa kudunguliwa na risasi ambayo iliingilia upande mmoja wa kichwa chake na kutokea upande mwingine. Akwilina aliuawa tarehe 16 Februari 2018 wakati akiwa kwenye daladala akienda kwenye majukumu yake. Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalum, Lazaro Mambosasa, alieleza askari wote waliofyatua risasi zile wamekamatwa. Baadaye Kamishna huyu wa polisi alikanusha taarifa zake yeye mwenyewe, baadaye zikazimwa na wakubwa zake – hasa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani – mpaka sasa polisi wanatupiana mpira.
1.7. Wilayani Kilombero katika mji wa Ifakara, diwani wa kata ya Namawala, Godfrey Luena (CHADEMA) ameuawa usiku wa 22 Februari 2018 kwa kukatwa mapanga mwili mzima. Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei ameeleza kuwa kada huyo wa CHADEMA ameuawa na watu waliokuwa wanalipiza kisasi. Jambo la kushangaza ni kwamba, Matei hajawakamata walipiza kisasi hao.
1.8 Mwaka wa 2017 ulishuhudia mambo ya kutisha sana. Miili ya wanaume ilikuwa inaopolewa majini na kwenye fukwe za bahari na kwenye mito. Miili hiyo ama ilikuwa kwenye mifuko ya sandarusi, au imefungwa kamba, au ina majeraha makubwa au imefungwa mawe n.k. Tulipodai uchunguzi wa kina na wazi juu ya miili ile, serikali ilikimbilia kutoa jibu kwamba miili hiyo ni ya wakimbizi! Bunge lilipotaka kujadili likakatazwa.
B. Utekwaji;
1.9. Ndugu waandishi wa habari, Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania kwa sasa imegeuka kuwa nchi ya watekaji. Ndugu. Ben Saanane aliondoka nyumbani kwake Tarehe 18 Novemba 2016 asubuhi, hadi sasa hajulikani alipo. Tarehe 21 Novemba 2017, Mwandishi wa Habari wa gazeti la Mwananchi, Ndugu Azory Gwanda alitekwa mchana kweupe, na hadi leo hajulikani alipo.
C. Majaribio ya kuua wanasiasa
Tukio kubwa kabisa la shambulizi baya katika miongo ya hivi karibuni ni lile lilimmkuta mwenzetu Tundu Lissu [MB]. Lissu alishambuliwa kwa risasi takribani 38 na zaidi ya risasi 10 zikampata na kumdhuru vibaya. Hadi tuzungumzavyo, waliojaribu kumuua Lissu kikatili, hawajakamatwa na hakuna uchunguzi unaoendelea.
2. MASHAMBULIZI DHIDI DEMOKRASIA
Ndugu waandishi wa habari. Tangu Uongozi wa awamu ya tano uingie madarakani, kumekuwa na jitihada kubwa za kuua demokrasia na mfumo wa vyama vingi hapa nchini, na bila kupepesa macho, juhudi hizo zinafanywa na yeye mwenyewe, Rais wetu mpendwa:
A. Kuua demokrasia, vyama vya upinzani na taasisi za kiraia na vyombo vya habari;
2.1. Rais Magufuli na serikali yake kupiga marufuku shughuli za kisiasa kwa ajili ya kuvidhibiti vyama vya upinzani kinyume na ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (haki za kujumuika, kukutana na kuchanganyika) pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa.
2.2. Kukithiri kwa matukio ya kuwabambikizia kesi viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani na kuwanyima dhamana.
2.3. Kuwafilisi baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani kama mkakati wa kuwadhofisha.
2.4. Udhibiti wa vyombo vya habari.
B. Kuwadhibiti viongozi wa dini kwa kutumia taasisi za serikali;
2.4. Mwezi Disemba 2017, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ngara, Mhashamu Severin Niwemugizi alihojiwa na Maafisa wa Idara ya Uhamiaji Tanzania akituhumiwa kwamba yeye si raia wa Tanzania, siku chache baada ya yeye kutoa maoni yake akiionya na kukosoa mwenendo wa serikali ya Rais Magufuli.
2.5. Mwezi Disemba 2017, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilitangaza kuwa ingelimfanyia uchunguzi mkubwa sana kiongozi wa Kanisa la Gospel Bible Fellowship Church (GBFC), Askofu Zacharia Kakobe kwa sababu za ajabu kabisa.
C. Ununuzi wa madiwani na wabunge:
2.6 Hadi sasa chama chetu kinakadiria kwamba huenda Tume ya Taifa ya uchaguzi imekwishatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 10 ili kufanikisha chaguzi mpya kwenye kata na majimbo ambayo madiwani wameondoka na kujiunga CCM. Taifa linaingia hasara kubwa kwa sababu CCM wameamua fedha za walipa kodi zikatekeleza masuala ya kijinga tu.
Vitendo vya CCM kununua madiwani na wabunge wa upinzani ni kielelezo tosha kwamba CCM HAIKUBALIKI, HAICHAGULIKI NA INASHIRIKI VITENDO VYA UFISADI NA RUSHWA KUBWA KABISA YA KIMFUMO [SYSTEMIC GRAND CORRUPTION], ufisadi wa kununua watu kwa fedha ni mbaya mno, ni sawa na biashara ya kuuza na kununua watumwa.
D. Hujuma za jeshi la polisi dhidi ya taaasisi, mali za watu na maisha yao;
2.7 Uvamizi wa makao makuu ya The Civic United Front (CUF) – Chama Cha Wananchi;
Tarehe 18 Februari 2018, Askari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, walivamia na kuiweka chini ya Ulinzi, Makao Makuu ya Chama cha Wananchi CUF yaliyoko Mtendeni, Unguja. Baadaye walifunguliwa ofisi hiyo na kufanya upekuzi kwa madai kuwa wanatafuta silaha aina ya SMG na vifaa vya miripuko ambavyo waliambiwa vimefichwa ofisini hapo. Kupekuliwa kwa Makao Makuu ya chama chetu kwa kuhusishwa kuficha silaha hatari si kitendo cha kawaida. Ni kitendo cha hujuma na chama chetu kinakichukulia kwa uzito wa hali ya juu.
Tuna taarifa za uhakika mbili kuhusu uvamizi ule; Kwanza ulikuwa na lengo la kupandikiza vilipuzi na silaha kwenye Makao Makuu yetu na kisha viongozi wetu wabambikiziwe kesi mbaya.
Pili ulikuwa na lengo la kukagua ndani na nje na kuweka mkakati wa kiulinzi ambao baadaye unaweza kutumiwa na Bwana Yule akisaidiwa na vikosi vya SMZ kuvamia na kukalia Makao Makuu ya chama kama ambavyo Bwana Yule alisaidiwa na Polisi na Usalama wa Taifa hapa Dar es Salaam na kuikalia Ofisi Kuu ya chama Buguruni.
Tunatambua pia kwamba Tarehe 02 Februari 2018, Msajili wa Vyama vya siasa, Jaji Mutungi, alikiuka agizo la Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kumuwekea Bwana Yule na genge lake kiasi cha Shilingi Milioni 139 ambapo sehemu ya pesa hizo zilipelekwa Zanzibar ili kusimamia mkakati wa hujuma nilizozitaja hapo juu.
Tunalionya jeshi la Polisi, likome kushiriki kwenye hujuma hizo. Vitendo vya kuvamia ofisi za vyama vya siasa si tu kwamba vinahatarisha usalama wa wanachama na viongozi wao, lakini pia vinalengo la kuweka madoa kwa vyama ambavyo vinaheshimika na kuaminika kama CUF.
3. MIHIMILI YA DOLA KUWEKWA MFUKONI MWA SERIKALI.
3.1 Katika uongozi wa awamu ya tano, mhimili mmoja (serikali), umejipa mamlaka makubwa kiasi cha kuidhibiti mihimili mingine. Mfano, serikali ya sasa inapanga mipango mingi na inatumia fedha nyingi za Taifa letu kwenye miradi mbalimbali bila kulihusisha Bunge. Mradi wa Ujenzi wa Uwanja wa Ndege Chato wa takribani bilioni 40. Dhana ya Bunge kuisimamia serikali imekufa, hivi sasa tunalo Bunge linalosimamiwa na serikali.
3.2 Kwa upande mwingine, mahakama yetu imelemewa na nguvu za serikali na inapoteza ule ukuu na uhuru wake. Mhimili wa mahakama unakemewa na mkuu wa serikali mithili ya mtoto akemewavyo na mama yake. Majaji wanaonywa hadharani na mkuu wa nchi, wanasakamwa na kutishwa hadharani. Tuna mifano mingi kabisa juu ya hili. Taifa letu haliwezi kuendelea kuvumilia hali hii.
3.3. Kidemokrasia, upo mhimili mwingine muhimu kwenye nchi, japo haujaandikwa kwenye katiba za nchi zote duniani. Mhimili huu ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tunayo mifano ya nchi nyingi mno ambazo zilitumbukia kwenye machafuko na umwagaji damu kwa sababu tu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa umuhimu wake, NEC ya Tanzania na ZEC ya Zanzibar ni taasisi muhimu sana – pamoja na kuwa miaka yote taasisi hizi hazijawahi kuwa huru, lakini katika utawala wa awamu ya tano zimenyang’anywa kila kilichokuwa kimebaki.
3.4. Kuongoza hujuma na uporaji wa haki za wananchi kwenye masanduku ya kura.
NEC imeshikana na dola na vyombo na watendaji wa dola ili kuhakikisha kuwa CCM inashinda kwa njia yoypote ile. Hivi sasa tunashuhudia kuwa sharti la kuwa msimizi wa Uchaguzi wa Kata au Jimbo ni lazima uwe kada wa CCM kindakindaki. Ndiyo maana mawakala wa vyama vya upinzani wanabebwa mzobe mzobe na kutolewa vituoni, masanduku ya kura yanachukuliwa vituoni mbele ya wasimamizi na polisi na baadaye yanarejeshwa yamejaa kura na mawakala wakiyakataa masanduku hayo wanatolewa vituoni kwa nguvu ya dola. Njia hizo zikishindwa mawakala wanawalazimishwa kusaini matokeo feki, mawakala wakikataa wanatolewa vituoni kwa nguvu na msimamizi anabandika matokeo yake aliyoelekezwa. TANZANIA IMEPOTEZA UWEZO WA KUFANYA UCHAGUZI ULIO HURU NA WA HAKI!
4. HALI YA UCHUMI WA NCHI;
4.1. Tafsiri rahisi ya uchumi imara ni uwezo wa wananchi kupata kupata fedha halali za kutosha na kufanya matumizi yao ya msingi bila tatizo. Tafsiri hii ina maana uchumi imara umo mfukoni mwa wananchi, siyo serikalini. Watanzania kwa sasa wana hali mbaya mno na hawana fedha mifukoni mwao.
4.2 Taarifa za wazi za namna serikali inavyosaka mikopo mpaka ile yenye riba za juu na za hatari, ni dalili ya wazi kuwa tuna hali mbaya. Mfumuko wa bei za bidhaa na hasa bidhaa za chakula ni kiashiria tosha kwamba tunaanguka kiuchumi. Kudorora na ama kushuka kwa uwezo wa mabenki na taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ni dalili kuwa tunaanguka kiuchumi.
4.3 Chama chetu cha CUF kinajua kwamba Tanzania imeendelea kuwa na uchumi unaokua huko IMF, Benki ya Dunia, ADB, kwa wanasiasa wa CCM, Ikulu n.k. Tunatambua kuwa uchumi wa Tanzania unakua midomoni na unaelekea kuanguka vibaya na au kufa kabisa katika hali halisi.
5. KUVUNJWA KWA HAKI NA KUKITHIRI KWA VITENDO VYA UPENDELEO
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu John Pombe Magufuli, inaongoza Taifa kwa kuwa na ‘Double Standard’, Kujuana na upendeleo wa hali ya juu. Siku Dk. Magufuli atakapomaliza awamu yake ya uongozi, wapo watu wengi watakiri kuwa awamu yake ilikithiri vitendo hivyo. Mifano halisi michache:
5.1 Bomoa bomoa ya Kimara vs Bomoa bomoa ya Mwanza;
Pamoja na kuwa na umiliki halali (hati) na zuio la mahakama likitaka nyumba zao zisibomolewe, serikali ilizibomoa kwa nguvu nyumba za wananchi wa Kimara waliotuhumiwa kujenga kwenye hifadhi ya barabara. Huko Mwanza jana, Rais JPM amebatilisha mpango wa Waziri Lukuvi wa "uliokuwa unafuata sheria" wa kubomoa nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya Uwanja wa Ndege, huku wahusika wakiwa hawana umiliki halali (hati).
5.2 Babu Seya vs Masheikh wa Uamsho
Rais JPM alitoa msamaha kwa wafungwa wa muda mrefu ambao ni Babu Seya na mwanaye, ambao mimi ni mshabiki wao. Pamoja na kwamba wanamuziki hawa wanaishi na hatia ya ubakaji, Rais aliwapa msamaha wa vifungo vyao – lakini kuna masheikh wa Taasisi ya uamsho ya Zanzibar ambao wako gerezani kwa miaka 5 sasa, na kesi yao haisikilizwi, wanateswa kimakusudi na dola. Tumeweza kuwasamehe “wenye hatia ya ubakaji” lakini tunaendelea kuwashikilia na kuwatesa mashehe “wenye tuhuma” tu, tena kinyume na sheria. Uongozi wa Double Standard!
HITIMISHO
1. THE CIVIC UNITED FRONT [CUF-CHAMA CHA WANANCHI] kinatoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuikumbusha serikali, kuikosoa, kuishauri, kuionya na kuinasihi. Tunawataka Maaskofu wenye nia njema na taifa letu, Mashehe, Wachungaji, Wanaharakati, Taasisi za ndani na nje ya nchi, Wawakilishi na Mabalozi waendelee kukemea hali hii na kupiga kelele, kelele zipigwe mchana, usiku na asubuhi. Chama chetu kitaungana na taasisi zote za ndani ya nchi kuanzisha mjadala na Mazungumzo Kitaifa na kuirudisha serikali yetu kwenye mstari.
2. Chama chetu kinawaasa wananchi kuondoa kasumba na mazoea ya kudhani kuwa wenye jukumu la kuirekebisha serikali ni wanasiasa peke yao. Tunataka wananchi watambue kuwa jukumu lao kubwa kuliko yote ni kulinda haki zao za msingi na kuhakikisha maslahi yao hayachezewi. Tunawataka watanzania wote waungane nasi ili kwa pamoja tupiganie uhuru wa pili wa Taifa letu ambao ni ulinzi wa Katiba yetu ya sasa, ulinzi wa mfumowa demokrasia na upatikanaji wa Katiba Mpya ya Wananchi.
3. Chama chetu kimejiridhisha kwamba vyombo vyetu vya DOLA NA HASA POLISI NA USALAMA WA TAIFA, vimekuwa mstari wa mbele kuvunja haki za wananchi, kuwaonea, kuwatweza, kuwatisha, kuwadhalilisha, kuwaumiza, kuwaua, kuwabambikizia kesi na kuwafanyia wananchi kila hujuma vikiwa na lengo la kuilinda CCM. Taasisi hizi zote ikiwemo idara ya uhamiaji, zinahitaji mabadiliko makubwa yatakayozilazimisha zitumikie matakwa ya Taifa letu na kuweka kando matakwa ya Chama kimoja. CUF itakuwa mstari wa mbele kupigania mabadiliko hayo na ni jukumu la wananchi wote kudai REFORMS kwenye vyombo hivyo.
4. Leo tunaitangaza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kama majanga ya kitaifa naadui mwingine wa taifa kwenye ile orodha ya Mwalimu Nyerere. Taasisi hizi zikiachwa ziendelee na hujuma zake dhidi ya matakwa ya kidemokrasia ya wananchi, tutaipoteza nchi yetu. Watanzania wanajua kwamba tuna tume ambazo zimejigeuza kuwa matawi ya CCM, tume hizo zitaitumbukiza nchi kwenye machafuko. Hatutaki kuona nchi yetu ikiharibika kwa ajili ya taasisi hizi mbili. Tunaendelea na mazungumzo na wadau mbalimbali ili kuweka mkazo na mibinyo itakayowezesha kuwe na mabadiliko makubwa ya dharura na tunaahidi kwamba tutayadai mabadiliko hayo kwa nguvu zetu zote.
5. Kwa sababu ni wazi kwamba vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeshindwa (kwa makusudi au kwa bahati mbaya au kwa kutokuwa na uwezo) kuchunguza matukio mabaya ya kikatili ambayo yamelikumba taifa letu yakihusisha mauaji ya kinyama, mashambulizi ya kimwili na utekaji – tunaitaka serikali iruhusu uchunguzi huru kutoka nje ya Tanzania, ili kutoa majibu ya matukio hayo. Au la, kama serikali haiwezi kuchunguza matukio hayo na haiwezi kuruhusu wachunguzi huru kutoka nje, basi serikali ijitangaze kwamba inahusika na matukio hayo. Tunawataka watanzania kuungana kwa pamoja kupinga mauaji haya na kutaka uwajibikaji wa haraka – kama serikali haitatoa majibu ya mauaji na matukio haya tutaendelea kuwaunganisha wananchi ili baadaye tutumie njia za kikatiba za kudai wajibikaji wa lazima.
6. Tunamtaka Jaji Mkuu wa Tanzania na Spika wa Bunge la Tanzania watafakari ikiwa ni jambo salama mamlaka na mihimili waliyokabidhiwa tena wakiwa na kinga, kuendelea kuingiliwa na kuhujumiwa na dola. Jaji Mkuu na Spika wa Bunge watambue kuwa wajibu wao ni mkubwa mno kikatiba na kwamba wasipoulinda wajibu huo wanatengeneza upenyo mbaya siku za mbele ambapo serikali itaendelea kupokonya na kupoka uhuru, haki, ukuu na majukumu ya kikatiba ya Bunge na mahakama. Wakuu wa vyombo hivi viwili watambue kwamba kuiacha mihimili hii imezwe na dola ni kuua misingi ya haki katika taifa letu.
7. Serikali ikubaliane na hali halisi kwamba uchumi wa taifa letu unaangamia kwa vitendo na unakua kwa maneno – serikali ikubali kurudi kwenye misingi ya ukuaji wa uchumi kwa kuwekeza kwenye kilimo, ajira, mikopo, biashara ndogo ndogo n.k. Moja kati ya kaulimbiu za kichumi za CUF ni kukomesha kabisa tabia ya siasa kuongoza uchumi. Ili tutoke hapa tulipo ni lazima wanasiasa waache kuongoza uchumi, Rais wetu awasikilize wachumi kuliko wanasiasa. Tutengeneze mipango ya uhakika ya kufufua ajira kwa vijana wetu, kupambana na umasikini wa kipato na kujenga uwezo wa watu wetu kumudu bei za bidhaa zinazotokana na chakula. Ikiwa serikali itaendelea na wimbo wa uchumi unakua huku hali ni mbaya, kwa hakika tutakuwa tunafanya mchezo wa kutunza bomu mfukoni.
8. Mwalimu Nyerere aliongoza taifa hili kwa miaka 25, hadi anamaliza muda wake Mwalimu alikuwa mtu mwenye misimamo na maadili makubwa. Lile ambalo Mwalimu alimtendea mwananchi wa Butiama ndilo hilo ambalo angelimtendea mwananchi wa Morogoro. Tunaitaka serikali na Rais wetu, watafakari sana juu ya maamuzi tofauti ambayo wanayafanya kuhusu jambo moja kwenye maeneo tofauti. Serikali itambue kuwa upendeleo ni dhuluma kubwa mno, hujenga chuki, visasi na manung’uniko na huwafanya wananchi waanza kugawanyika. Tukomeshe migawanyiko inayotokana na serikali kupendelea sehemu fulani.
9. Taifa letu linao wazee, linao waasisi, linao viongozi wastaafu. Kwa sababu mambo hayako sawa kwenye nchi yetu, wazee wetu Mwinyi, Mkapa, Kikwete, Warioba, Butiku na wengine wote, simameni na mwambieni JPM arudi kwenye mstari. Hakuna mtanzania ambaye angelipenda kupoteza muda wake kumkosoa rais na serikali yake, lakini watanzania wanawajibika kufanya hivyo kwa sababu maamuzi ya rais na utendaji wa serikali yake vina athari za moja kwa moja kwa maisha ya kizazi chetu na kijacho. Wazee hawa wakumbuke kuwa tulikabidhiwa dunia hii ili nasi tukabidhi dunia bora zaidi ya hii kwa kizazi cha mbele.
Julius Mtatiro,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi.
Jumatatu, 26 Januari 2018.
No comments:
Post a Comment