Sunday 7 April 2019

CCM YAMUOGOPA MAALIM SEIF ?


WASOMI: Tatizo ni Maalim Seif.
LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM
KINACHOENDELEA kati ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini na Chama cha ACT-Wazalendo, kimeelezwa na wasomi kuwa tatizo si chama hicho, bali ni nguvu ya kisiasa aliyonayo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Tangu Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo Machi 19, mwaka huu kumekuwa na kauli na lugha za kubeza kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa.
Mapema wiki hii, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeeleza nia yake ya kukifutia usajili chama cha ACT-Wazalendo na imekipa siku 14 kuanzia jana kuwasilisha maelezo kwa nini kisichukuliwe hatua.
Hatua hiyo inakuja ikiwa ni wiki moja baada ya chama hicho kumpokea aliyekuwa katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekihama chama hicho akiwa na wafuasi wake kwenda ACT.
Maalim Seif alihama baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF.
Wafuasi wengi wa CUF hasa upande wa Zanzibar walimfuata Maalim Seif pamoja na wakishusha bendera za chama hicho na kupandisha za ACT, na pia baadhi ya ofisi kubadilishwa rangi.
Vitendo hivyo ndivyo vilivyoifanya ofisi ya msajili kuiandikia chama hicho barua iliyosainiwa na msajili msaidizi, Sisty Nyahoza ikieleza nia hiyo na kutoa siku 14 kwa chama hicho kieleze kwa nini kisifutwe.
Barua hiyo inaeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, msajili anapotaka kufuta usajili wa chama cha siasa anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa chama husika.
MADAI
Barua hiyo imeyataja mambo yanayodaiwa kukiukwa na ACT kuwa ni vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kuchoma moto bendera za CUF baada ya Mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016.
Kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao ya kijamii wakipandisha bendera ya ACT-Wazalendo kwa kutumia tamko takatifu la dini ya Kiislamu (Takbira), kitendo kinachokiuka kifungu cha 9 (1)(C) cha sheria hiyo.
Chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei 5, 2014 kinakabiliwa na adhabu nyingine ya kutowasilisha hesabu za ukaguzi za 2013/2014.
Barua hiyo imenukuu barua ya Mei 22, 2018 kwenda chama hicho iliyokuwa inasitisha ruzuku sambamba na kuhitaji hesabu za miaka mitatu ya 2013/14, 2015/16 na 2017/17 lakini kilipojibu kilitoa hesabu za miaka miwili bila kuweka za 2013/2014.
Alisema kutowasilisha hesabu za mwaka wa fedha wa 2013/14 kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya barua ya msajili wa vyama vya siasa, hivyo kinakuwa kimekiuka sheria ya vyama vya siasa sura ya 258.
Kutokana na barua hiyo baadhi ya wasomi wa kada mbalimbali wameweka wazi kuwa hakuna hoja za msingi bali nia ya wahusika ni kupambana na Maalim Seif.
Mhadhiri katika Idara ya Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda, aliliambia RAI kuwa tatizo analoliona ni ujio wa Maalim Seif ndani ya ACT-Wazalendo.
“Mi nadhani tatizo ni maalim Seif, kama mwanasiasa huyu asingeenda ACT tusingeyaona hayo, chama hiki sijawahi hata kusikia kikihusishwa na udini.
“Kimsingi ujio wa Maalim Seif umetikisa, tulikuwa tunategemea chochote kitokee, lakini hii hatua ya Msajili imevunja rekodi.
“Msajili kazi yake kubwa ni kuvilea vyama vya siasa na hata uhalali wake unatokana na vyama hivyo, hatukutegemea kama matamko kama haya yangetoka kwake, kukifutia chama usajili ni hatua ya mwisho na ni lazima uwe na sababu ya msingi sana, lakini hili naona limechukuliwa kwa urahisi sana.”
Kuhusu madai ya Msajili kwa ACT-Wazalendo, Dk. Mbunda alisema hoja ya ukaguzi wa fedha imeingizwa tu ili kuimarisha madai ya usajili, lakini haoni kama ina msingi kwani hakuna sababu ya msingi ya kudai hesabu hizo sasa.
“Kuchoma kadi na bendera ni mihemko ya kisiasa kwa wanachama na wapenzi wa vyama na wanasiasa na hata salamu ya kidini mbona imekuwa ni jambo la kawaida kwenye mikutano ya kisiasa.
“Tena naona sasa limekuwa jambo la kawaida kwenye mikutano lazima awepo Padre na awepo Shehe na hata salamu wanazozitoa wanasiasa ni aidha Salama Aleikum, Bwana Yesu asifiwe au Tumsifu Yesu Kristo, sasa uamuzi huu wa Msajili unanipa mashaka na kushindwa kujua yuko upande gani, ni mlezi wa wote au analea baadhi ya vyama tu,”alihoji.
Msomi wa masuala ya elimu Dk. George Kahangwa  ambaye pia ni mwanasiasa alisema  kuwa kinachoonekana kwa juu juu ni nia ya kuishughulikia ACT-Wazalendo baada ya kumpokea Maalim Seif.
Alisema awali kulikuwa na madai kuwa serikali inaivuruga CUF na yote yaliyotokea watu wote wameyashugudia.
“Katika hali ya aina hii, hiyo assumption (dhana) kwamba labda Msajili wa Vyama vya siasa anamshughulikia Maalim Seif inaweza ikaingia. Sasa kwa kuwa yameingia mashaka hayo basi inakuwa ni wajibu wa Msajili wa Vyama kuthibitisha kwamba siyo kweli.
“Na kwa kuwa ametoa tuhuma hizo kwa chama cha ACT, yeye kama Msajili wa Vyama anajua hata kwenye sheria tunasema ‘burden of truth’ yeye ndiye awajibike kuthibitisha kweli kabisa kosa limetendeka na limetendwa na wana ACT.
Dk. Kahangwa alisema katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia taifa moja lilivaa sura ya taifa jingine likaenda kushambulia taifa la tatu na wale wanaoshambuliwa wakadhani anayewashambulia ni taifa X ilihali aliyewashambulia ni taifa Y.
Alisema inawezekana kabisa waliochoma bendera wala siyo wanachama wa ACT na kama walikuwa wafuasi wa Maalim Seif pengine walikuwa hawajajiunga na hiyo ACT.
“Lakini mchoma bendera anaweza kuwa mtu yeyote hata kama si mwanachama wa ACT au wafuasi wa Maalim Seif bali akawa mtu yeyote ambaye ana nia mbaya anaweza kuchoma.
“Kwa hiyo ofisi ya msajili ilipaswa kutamka kwa mfano kwamba imejiridhisha ina uhakika waliofanya tukio hilo ni wanachama wa ACT, vinginevyo bila kujiridhisha inakuwa inarusha kutuma zisizokuwa na uthibitisho.”
Dk. Kahangwa aliongeza kuwa ili isionekana ofisi ya msajili inamwandama Maalim Seif au chama alichojiunga nacho ni lazima wathibitishe pasi na shaka waliofanya hivyo ni wanachama wa chama wanachokituhumu.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema kulingana maelezo yaliyopo katika barua ya Msajili kwenda kwa ACT yanaonesha vitendo vilivyofanywa si vya kiungwana.
Profesa Safari alisema Serikali inaweza kuvikomesha vitendo hivyo kwa kuwapata wale waliovifanya vitendo hivyo.
“Ni vitu ambayo kwa kweli Serikali ingeweza kuwa-extract wale watu wanahusika na hivyo vitu, mimi ninaona ndiyo umuhimu mkubwa. Sasa ile imetokana na mkwamo kwa Maali Seif viko collected vimekutana na watu ambao wamekuwa wameghadhabika kutokana na mazingira ya kisiasa yanayomhusisha kiongozi wao.
Alisema amefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Msajili kuiandikia ACT barua ya kuwakanya kwa sababu ndiyo kazi yake.
Profesa Safari alisema kuwa ili kuhakikisha ACT inakuwa na utulivu ni lazima viongozi wawatulize wafuasi wao  na kuachana na mpango wowote wa kuchukua mali zinazomilikiwa na CUF kisheria.
“Kutaka kuchukua properties (mali) zinazomilikiwa na CUF kisheria watakua wanatenda makosa ni kama CCM inavyoevunja sheria kwa kuendelea kumiliki mali ambazo tume ya Jaji Nyalali ilielekeza zirudi Serikalini. CCM wao wanajisahau, ukisoma ripoti ya Nyalali ya mwaka 1992 volume’ 2 inazungumzia mali zote hizi ambazo zinatakiwa kisheria zirudi serikalini CCM wamezifanya zao” alisema Profesa Safari.
WARAKA WA ZITO
Mwanzoni mwa wiki hii Kiongozi wa act- Wazalendo, Zitto Kabwe alieleza kile ambacho wamekibaini juu ya barua ya Msajili.
Tulipokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yenye kumbukumbu Na. HA. 322/362/20/98 ambayo; pamoja na mambo mengine, ilieleza juu ya kusudio la Serikali kutaka kukifuta Chama cha ACT Wazalendo.
Barua hiyo ilieleza kuhusu mambo matatu yaliyosababisha Ofisi ya Msajili itangaze kusudio hilo ovu juu yetu. Kwanza ilizungumza kuhusu hoja zinazohusiana na ukaguzi wa hesabu za chama uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pili kuhusu vitendo vya kuchomwa hadharani kwa bendera na kadi za chama cha CUF na tatu matumizi ya neno takbira kama yalivyoonekana katika baadhi ya video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii.
Naomba niwaeleze kwa kina kuhusu hoja moja baada ya nyingine kabla ya kutoa maoni yetu na mwelekeo wa chama baada ya kupata barua hii.
1. Kuhusu Ukaguzi wa CAG
Barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa inadai kwamba ACT imekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kutopeleka kwake hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka wa fedha 2013/2014 kama sheria inavyotaka.
Tuhuma hizi hazina ukweli wowote. ACT Wazalendo ilianzishwa na kupewa Usajili wa Kudumu tarehe 5 Mei, 2014 na kwa hivyo, kwa mwaka huo wa fedha (2013/14) Chama chetu kilikuwa na miezi miwili tu ya kukaguliwa. Kazi yetu ACT Wazalendo kama chama cha siasa ni kuwasilisha ripoti kwa ajili ya kukaguliwa na CAG. Ripoti ya hesabu za 2013/14 imewasilishwa kwa CAG kwa barua. 
Kwa kutumia Kanuni za Kimataifa za Kihasibu na kwa ushauri wa CAG, chama chetu kilielezwa kinaweza kuunganisha hesabu za mwaka 2013/2014 na 2014/2015 katika ripoti moja, wakieleza kuwa hilo jambo la kawaida kabisa katika kanuni za uhasibu kwani inaruhusiwa kuunganisha hadi miezi 18. Kwa kuunganisha huku hesabu, ACT ilikuwa na miezi 14 tu.
Kabla ya kuchukua uamuzi wa kukubali ushauri huu wa kuunganisha hesabu kutoka Ofisi ya CAG, Chama chetu kilimwandikia Msajili wa Vyama vya Siasa (Kwa barua mbili zenye kumbukumbu namba AC/HQ/MSJ/2015/006 na AC/HQ/MSJ/2015/008 za tarehe za tarehe 22 na 29 Januari 2015) naye akajibu na kuridhia hesabu za miezi miwili ya mwaka 2013/2014 kuunganishwa kwenye mwaka wa fedha 2014/2015 (kwa barua yenye kumbukumbu Na. KA/ 322/20/60 ya tarehe 16 Februari 2015).
Taarifa zote hizi ziko wazi kwa kwake mwenyewe Msajili na kwenye Ofisi ya CAG, kuanzia barua za kutaarifiwa Juu ya kukusanywa kwa pamoja kwa taarifa ya Ukaguzi wa Mahesabu ya ACT Wazalendo kwa miezi 14 ya mwanzoni (miezi miwili ya mwaka 2013/14 na miezi 12 ya mwaka 2014/15), mpaka ripoti husika ya Ukaguzi kutoka kwa CAG. Tumeshangaa sana anaposema ana nia ya kutufuta kwa kutokupeleka ripoti ambayo tayari anayo Ofisini kwake.
ACT Wazalendo tunajua kuwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa haina utaalamu wa Masuala ya Ukaguzi wa Fedha na Matumizi ya Vyama. Hivyo tunajua kuwa upo uwezekano kuwa wameshindwa kuisoma, kuichambua na kuielewa ripoti hiyo ya Ukaguzi wa Hesabu za ACT Wazalendo kwa mwaka wa Fedha wa 2014/15, hatuwalaumu kwa jambo hilo. Ndio maana kisheria kazi hiyo ya ukaguzi amepewa CAG. 
Lakini Msajili wa Vyama vya Siasa nchini angekuwa na nia njema, angeweza tu kuomba ufafanuzi au uchambuzi wa taarifa husika kutoka kwa CAG au hata kwetu ACT Wazalendo, Chama chenye uzoefu wa kuchambua hizo ripoti za CAG, na angepewa taarifa husika. Taharuki hii aliyoisababisha haikuwa na sababu yeyote, ni suala la uelewa tu. 
Tunawaahidi wanachama wa ACT Wazalendo kuwa sisi Viongozi wao tutajibu barua hii ya msajili kwa kumwelewesha. Zaidi tunaishauri Ofisi ya Msajili kuwa ni vyema basi wakishindwa kuzielewa taarifa tunazowapelekea warudi kwanza kwa CAG ama kwetu kuomba ufafanuzi na uchambuzi kabla ya kuandika hizi barua za kutishia kutufuta.
2. Kuhusu Kuchoma bendera na kadi
Barua yenyewe ya Msajili iliyotufikia inasema kwamba imeona picha zinazoonyesha “wanaodaiwa” kuwa wanachama wa ACT Wazalendo wakichoma bendera na kadi za chama cha CUF. Katika hili, Msajili mwenyewe anaonyesha kwamba hana uhakika kama kweli wahusika ni wanachama wa ACT. 
Si ilibidi Msajili ajiridhishe kwanza kuwa wale ni Wanachama wa ACT Wazalendo? Kama hajaridhisha anawezaje kutangaza NIA ya kutaka kufuta Usajili wa Chama chetu kwa jambo hilo? Watanzania waone Ofisi ya Msajili ilivyo na NIA Mbaya na Chama chetu, Watanzania waone namna Ofisi ya Msajili, inayoongozwa na Jaji inavyotoa tuhuma pamoja na kutoa hukumu bila hata ya kuwa na Ushahidi.
Chama chetu HAKIHUSIKI kabisa na uchomaji wa bendera wala kadi za Chama chochote. Kihistoria sisi ni Chama cha Masuala, tunaojikita juu ya Utetezi wa Wakulima wa Korosho, Mahindi, Giligilani, Karafuu, Mkonge na Mbaazi wanaokosa masoko ya bidhaa zao. Sisi tumezoeleka kuwa ni wapaza Sauti za Wafuagaji wanaotaifishiwa Mifugo yao na Wavuvi wanaonyang’anywa nyavu zao. 
ACT Wazalendo tunatambulika kwa Uchambuzi wa Bajeti na kupinga Sera mbaya za kuongoza Uchumi zinazowafanya wananchi waishi maisha magumu. Matumaini ya wananchi kwetu ni kwa sababu wamezoea kutuona tukichambua ripoti za CAG na kuhoji kutokuonekana kwa TZS 1.5 trilioni na kusimamia uwajibikaji wa Serikali. Chama chetu utambulisho wake ni utetezi wa wanyonge wanaoonewa popote pale duniani, iwe ni Sahara Magharibi, Palestine au MKIRU (Mkuranga, Kibiti na Rufiji). Rekodi zetu zinatutambulisha hivyo. 
Tumesikitika sana Ofisi ya Msajili hata kuwaza tu kuwa Chama cha Masuala cha namna hiyo kinaweza kuhusika na mambo ya Uchomaji wa bendera na kadi za vyama vingine. Tumesikitika sana.
3. Kuhusu “Takbira”
Barua hiyo ya Msajili inaeleza pia kwamba chama chetu kimevunja sheria ya vyama vya siasa kwa sababu “wanaodaiwa kuwa wanachama wetu” wametumia maneno takbira kwenye shughuli za kichama na kwamba maneno hayo yana udini. Majibu ya hili ni kama kwenye suala la kudaiwa kuchoma kadi na bendera. Msajili hajaainisha hao wanaodaiwa kuwa ni wanachama wetu wana kadi namba ngapi za uanachama na ni kutoka tawi gani la chama chetu.
ACT Wazalendo ni chama cha siasa cha watu wa matabaka na dini zote na hata wale wasio na dini. Katika Katiba yetu ya chama tumeonesha wazi kwamba hatufungamani na dini yoyote na ndiyo sababu tumeruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa. 
Tuna ushauri tu kwa Ofisi ya Msajili, katika nchi ambayo Viongozi karibu wote wa Serikali wanaanza hotuba zao kwa salamu za kidini za “Bwana Yesu Asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo na Assalaam Aleykum” ni rahisi kwa “wanaodaiwa kuwa wanachama wa ACT Wazalendo” kutumia kaulimbiu za Dini zao kama wanavyofanya Viongozi wa Serikali.
4. Mtazamo Wetu
Barua ya Msajili haina nia njema kwa ACT Wazalendo na wapenda demokrasia wote hapa nchini. Kukosekana kwa nia njema kulionekana mapema kabisa baada ya barua iliyotakiwa kutumwa kwetu kusambazwa kwanza katika mitandao ya kijamii kabla hata haijatufikia ofisini. Taswira tunayopata ni kwamba ilivujishwa makusudi na ofisi ya msajili kutimiza dhamira ovu waliyonayo dhidi yetu.
Serikali na Chama cha CCM vimepata mchecheto na ufuasi mkubwa wa chama chetu, hasa baada ya Maalim Seif Sharif Hamad na waliokuwa Viongozi wenzake kutoka chama cha CUF kuhamia ACT Wazalendo. Wameogopa zaidi kuwa sasa ACT Wazalendo ndio kimbilio la Wazanzibari wote waliomchagua Maalim Seif kuwa Rais wao kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015. 
Ushauri tu kwa CCM na Serikali yake, hata wasiwaze tu kuifuta ACT Wazalendo, hatua mbaya ya namna hiyo ya kionevu itawanyima fursa karibu theluthi moja ya Watanzania ya kufanya siasa kwa njia halali za kisheria. Watu hawa wakinyimwa fursa hii kionevu kupitia ACT Wazalendo watatumia njia nyengine zinazoweza hata kuleta mpasuko kwa Taifa letu. Ikifika hatua hiyo, sisi Viongozi wa ACT Wazalendo hatutakuwa na sauti ya kuwakataza watu hawa watakaodhulumiwa fursa ya kufanya siasa kwa njia halali za kisheria.
Tunachukua nafasi hii pia kuzitaka Taasisi za Dini, Asasi za Kiraia, Nchi marafiki na wahisani kupaza sauti juu ya jambo hili. Wasikae kimya wanapoona uonevu unataka kufanyika.
5. HATURUDI NYUMA
Kwa wanachama wa ACT Wazalendo, wafuasi na Watanzania kwa ujumla, barua hii ya Msajili haijatutisha wala kututikisa. Na tutaazima busara za mwanachama wetu mwandamizi, Maalim Seif, kuwa TUSICHOKOZEKE. Na hatutachokozeka.!
Tamko langu hili kwenu liwe ni ishara kwenu kuwa Chama kiko salama na imara, na kwamba barua hii ya Msajili itajibiwa kwa hoja, na ushahidi wa hoja kabla ya hizo siku 14 alizozitoa. Ulinzi wa chama hichi ni wajibu wenu, sisi viongozi wenu tuko hapa kutoa dira na mwongozo. 
Endeleeni kugawa kadi na shughuli nyengine za uenezi wa Chama chetu, ziara zetu sisi viongozi kuja kukagua shughuli zenu ziko kama ilivyo ratiba yetu. Huko mliko mtembee kwa fahari mkijua kuwa wapinzani wetu sasa wanatuogopa, hawataki tena kusubiri uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, wanataka kutufuta kwa hila. Tunajua hawataweza.
     CHANZO: MTANZANIA


No comments: