WAZANZIBARI WANATAKA KUTOKA HAPA TULIPO, WANATAKA ZANZIBAR MPYA, WANATAKA ZANZIBAR TUNAYOSTAHIKI
Na: Othman Masoud Othman
Nimeutafakari Waraka wa Dk. Harith Ghassany na naamini tutakubaliana kuna ya msingi ya kutafakari.
Moja na kubwa ametaja Mkataba wa Magna Carta (Mkataba wa Uhuru au wa Haki za Binadamu). Mkataba huu ulikuja baada ya figisu figisu nyingi baina ya Bunge na Mfalme wa Uingereza. Bunge lilijinasibu na watu wa kawaida na Mfalme alijinasibu na utawala. Kanisa nalo likijinasibu na kulinda sheria na maadili. Magna Carta ikaja kama maridhiano.
Suala muhimu ni kuwa je, Magna Carta ndio iliyoikomboa na kuijenga Uingereza katika ustaarabu mpya wa utawala, demokrasia na maridhiano? Jibu la wazi ni kuwa HAPANA. Sababu kubwa ni kukosekana kwa nia ya dhati ya kuheshimu sheria na utaifa. Aidha kukosekana taasisi madhubuti za utawala.
Mapambano baina ya Ufalme na Bunge yalishamiri tena hasa alipoingia Mfame Charles I. Alituhumiwa kutawala kibabe na kutoheshimu Bunge na haki za raia. Mapambano hayo yalipelekea Mapinduzi ya Oliver Cromwell ya 1649 lakini akaanza kutawala rasmi kama Lord Protector katika mfumo wa Republic (Jamhuri) na sio Monarchy (Ufalme). Lakini na yeye akaja na Umagu wake. Akawa mbabe kuliko huyo Mfalme. Na ndio mana alipofariki mwaka 1658 wabunge na raia wakaona bora Mfalme arudi lakini ule Mkataba wa Magna Carta utekelezwe kwa vitendo. Ndio maana Charles II akafuatwa Ufaransa alikokuwa uhamishoni akaja kutawala kwa masharti ya kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Magna Carta. Jambo hilo ndio lililokuwa msingi wa Maridhiano ya Uingereza na hata Uingereza na Scotland. Ndio mana pia hata Muungano rasmi wa Scotland na Uingereza ukawa rahisi kufanyika rasmi mwaka 1707.
Tunachojifunza hapa nahisi kipo wazi, kwamba Maridhiano yanajengwa na pande mbili zenye kukinzana na yanajengwa juu ya msingi wa kuweka mbele maslahi ya taifa. Si mfumo, mkataba wala mrengu unaojenga maridhiano. Moja lipo wazi, kuondokana na kasumba za yaliyopita ni muhimu sana. Hakuna lilipopita zuri zaidi ya kuzaliwa. Hata uzuri basi unaporomoka kutokana na wakati... kisura mrembo akawa chapwa hata wabaya wakamcheka!!!
Mimi nahisi hapa tulipofika kwa asimia 99 kizazi cha Zanzibar cha leo hakiguswi wala hakiabudu na pengine hakijui yaliyopita. Wanachokijua ni ule uzuri wa milele, uzuri wa kuzaliwa. Kwamba Zanzibar ilizaliwa na ipo na inastahiki kuendelea mbele kama Zanzibar. Hilo lipo wazi.
Wakati ninasomesha darasa za Redet kuhusu Demokrasia Zanzibar, washiriki kila msimu walikuwa ni vijana wa CCM na CUF kwa idadi sawa. Lakini wakati wa kujadili mustakbali wa Zanzibar ndani ya Muungano ilikuwa huwezi kumjua yupi kijana wa CCM na yupi wa CUF. Kusema kweli wakati mwengine wale vijana waliojinasibu kuwa wa CCM walikuwa wakali zaidi na hoja nzito zaidi kuliko za Mhe. Mansoor Yussuf Himid, utadhani aliwawekea darsa akawafunda. Niwe mkweli nilipata insipiration (kutiwa nguvu) kubwa sana kutokana na hoja na mwelekeo wa vijana wale. Darsa zaidi ya 20 za Redet zilinipa na mimi darsa kubwa sana na hazina ya imani kwa nchi yangu.
Miongo miwili ya siasa za vyama vingi vya siasa za Zanzibar zimedhihirisha jambo moja kubwa sana. Kwamba Wazanzibari wengi wanataka kutoka hapa tulipo. Wanataka Zanzibar mpya; wanataka Zanzibar tunayostahiki.
Mimi sioni kama kuna tatizo la uongozi katika mageuzi. Tatizo liliopo ni kama la nchi nyingi zilizopata bahati mbaya kuwa katika hali kama ya kwetu. Hali ambayo mna wenzenu wamejisahau, wamelewa ubinafsi, wamelewa maslahi yao. Hao walikuwepo wakati wa kupigania uhuru katika nchi zote. Walikuwepo Afrika Kusini wakati Wazungu walikuwa na sera ya wazi ya kuwabagua Waafrika na bado walikuwepo Waafrika waliokuwa wakitumiwa na Wazungu kuhujumu ukombozi. Watu kama hao leo wapo Palestina wakiwachongea wanaopambana na udhalimu uliokithiri wa Wazayuni dhidi ya Wafalastin.
Udhaifu unaoonekana kama udhaifu kwa uongozi wa siasa wa upinzani unahitaji tafakuri kubwa. Tafakuri hiyo nahisi si rahisi kuifanya kwa kigezo cha ushindi na kupewa Serikali. Wengi wanaona hilo limeshindikana labda kwa ubwege (samahani kwa lugha isiyopendeza) wa upinzani. Wanasahau kwamba mwizi haibi kwa sababu anayeibiwa ni bwege bali anaiba kwa sababu ni mwizi na mazingira yanamruhusu aibe bila kukamatwa. Ndio mana wapo wezi wanamuibia hata Mungu; misikiti, zaka na mali za yatima ambazo zote hizo ni mali za Mungu. Haziibiwi kwa sababu Mungu ni dhaifu bali Mungu mwenyewe anayawacha yatokee ili iwe funzo kwa binaadamu juu ya kiwango cha udhalimu wa binadamu.
Mimi nahisi tukubali kwamba upande mmoja katika equation ya mustakbali wa Zanzibar ipo wazi kwamba inataka Maridhiano na Zanzibar mpya na upande wa pili bado hawajaleuka katika pombe ya maslahi yao.
Tatizo si Wazanzibari. Tatizo ni Wazanzibari waliolala na waliolewa. Dawa si kulaumu chombo cha kutupeleka katika safari ya kuwaamsha bali dawa ni kutovunjika moyo katika safari hiyo. Tukianza kulaumiana manahodha, sarahange na abiria, tutachelewa. La mwanzo lifanywe mwanzo. Tukishafika tutajua nani anafaa kuendelea na hatua ya pili ya safari. Kwa sasa ni vyema kushauri kuliko kutia shaka. Wachina wana msemo "IN TIME OF WAR EVEN A GRAIN CAN TILT THE SCALE" yaani wakati wa vita hata punje ya nafaka inaweza kuifanya mizani iinamie upande mwengine. We need everybody not somebody. Tunahitaji kila mtu na siyo baadhi ya watu.
JUST THINKING ALOUD!
No comments:
Post a Comment