Friday, 10 July 2020

WASIFU WA DKT HUSSEIN ALLY MWINYI:



Dk Hussein Mwinyi ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa katika Serikali ya Awamu ya Tano, ameteuliwa katika baraza la mwanzo la mawaziri la Rais John Magufuli. Kiongozi huyu pia ni mbunge wa jimbo la Kwahani lililoko Unguja, Zanzibar.

Dk Hussein Mwinyi Alizaliwa Desemba 23, 1966 kwenye kisiwa cha Unguja, Zanzibar. Dk Mwinyi ni mtoto wa Mzee Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) na mama Sitti Mwinyi ambaye amekuwa (First Lady) katika awamu ya pili.

Kwa sababu ya kazi za baba yake mzazi, Dk Mwinyi alianza elimu ya Msingi jijini Dar es Salaam kati ya mwaka 1972 – 1976 akisoma katika Shule ya Msingi Oysterbay. Mwaka 1984 hadi 1985 wazazi wake walimhamishia Misri ambako aliendelea na masomo ya elimu ya msingi hadi kuhitimu katika Shule ya Msingi “Manor House Junior”.

Shule hii ilikuwa na hadhi ya “Middle School za Tanzania” kwa wakati huo. Hussein Mwinyi alipelekwa Misri kwa sababu baba yake (Ali Hassan Mwinyi) alihamishiwa nchini Misri kikazi kama balozi wa Tanzania nchini Misri wakati huo.

Hussein Mwinyi alirejea Tanzania na kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Sekondari Azania ambako alisoma kidato cha kwanza hadi cha nne mwaka 1982 – 1984. Alipohitimu kidato cha nne alifaulu na kupangiwa Shule ya Sekondari Tambaza kusoma kidato cha tano na cha sita, hata hivyo aliishia kusoma kidato cha tano peke yake mwaka 1984/1985, mwaka huo huo 1985 alienda nchini Uturuki kusomea utabibu wa binadamu. Alianza masomo ya udaktari nchini Uturuki mwaka 1985 kwenye Shule ya Utabibu ya Chuo Kikuu cha Marmara na kuhitimu Shahada ya Utabibu wa Binadamu mwaka 1992.

Kwa sababu hakumaliza kidato cha sita, alipokuwa huko ughaibuni alipitia masomo ya mwaka mmoja ya kujiandaa na udahili wa Chuo Kikuu “Pre University Studies”. Wakti huo Chuo cha Marmara kilikuwa kinapokea hata wanafunzi wa kidato cha nne kuanza kusomea shahada ya utabibu, lakini lazima wapitie mwaka mmoja wa maandalizi kama alivyofanya Mwinyi. (Sikufanikiwa kupata mawasiliano na chuo hiki ili kujiridhisha ikiwa hadi sasa wanatumia utaratibu huo)

Mwaka 1993, Mwinyi alikwenda nchini Uingereza kujiendeleza zaidi kielimu, aliendelea na masomo ya juu ya utabibu katika Hospitali ya Hammersmith ambako alihitimu shahada ya uzamili ya utabibu mwaka 1994 na kuunganisha shahada ya uzamivu ya udaktari hapohapo Hammersmith ambayo aliihitimu mwaka 1997.

Dk Mwinyi amemuoa Mariam Herman na wana watoto wanne; Ibrahim, Jamila, Tariq na Sitti.

Dk Mwinyi hakuishia tu kuwa daktari wa mdomoni, amefanya kazi za kidaktari. Alipohitimu shahada ya kwanza ya utabibu alirejea Tanzania na kufanya kazi kwa mwaka mmoja katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Na hata baada ya ya kuhitimu shahada ya uzamivu nchini Uingereza, alirejea nchini kwa mara nyingine na kufanya kazi katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Herbert Kairuki (HKMU) kwa miaka miwili hadi mwaka 1999.

Kiongozi huyu alijitosa kwenye siasa mwaka 1999 akiliwania Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani (Bara) na kushinda. Alipokuwa mbunge, Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, alikaa katika wadhifa huo hadi mwaka 2005.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Dk Mwinyi alijitosa tena jimboni, lakini safari hii siyo Mkuranga. Ilikuwa ni jimbo la Kwahani, Zanzibar – ambako alipambana na kuwashinda wagombea sita kutoka vyama vingine akipata kura 6,239 sawa na asilimia 85.6 akifuatiwa na Mussa Haji Khamis wa CUF aliyeambulia kura 921 sawa na asilimia 12.6. Baada ya kuwa mbunge kwa mara ya pili, Serikali ya Awamu ya Nne chini ya uongozi wa Jakaya Kikwete na Dk Mwinyi ilimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na alidumu hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa alikokaa hadi mwaka 2010.

Mwinyi alirejea tena na kugombea ubunge katika jimbo la Kwahani mwaka 2010, akashindana na yuleyule hasimu wake wa mwaka 2005, Haji wa CUF, mara hii vyama vingine havikuweka wagombea na Dk Mwinyi hakupata shida kushinda kwa kura 5,277 sawa na asilimia 83.0 dhidi ya kura 1,085 sawa na asilimia 17.0 za CUF. Mara baada ya uchaguzi wa mwaka 2010 Rais Kikwete akamteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi kabla ya kumrejesha Wizara ya Afya mwaka 2012 na miezi 19 baadaye (yaani Januari, 2014) kwa mara nyingine tena akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi aliyodumu hadi mwaka 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Dk Mwinyi alirudi tena katika jimbo la Kwahani, hii ikiwa ni mara ya nne akisaka nafasi ya kuwawakilisha wananchi, akafanikiwa kumshinda Khalid Rajab Mgana wa CUF na kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha nne. Rais JPM amemteua Mwinyi kuwa Waziri wa Ulinzi na Kujenga Taifa na hivyo kumuongezea rekodi ya kuongoza wizara hiyo kwa kitambo cha kutosha.

Mwaka 2015 Dk Mwinyi alitajwa sana kama mmoja wa wanasiasa wanaoweza kuvaa viatu vya JK ikiwa CCM ingeamua mrithi huyo atokee upande wa Zanzibar, hata hivyo yeye mwenyewe hakuwa na nia na hakuchukua hata fomu kwa ajili ya kuwania kiti hicho.

Ndani ya CCM Dk Mwinyi anashikilia nyadhifa mbalimbali, Mwaka 2000 aligombea na kushinda ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akashinda tena mwaka 2007 na kushinda na tangu wakati huo aliteuliwa kuingia kwenye Kamati Kuu ya CCM hadi hivi sasa.

Dk Mwinyi ni mmoja kati ya mawaziri wenye rekodi za kuwa shahada tatu za ubobezi wa taaluma na elimu ya juu katika fani moja. Amesoma kwa uhakika na ni mtu mwenye uwezo wa kutumia stadi za ubobezi wake kujenga weledi wa jumla unaomfanya atoe uongozi wa kudumu hadi hivi, nina hakika kuwa ubobezi wake utaendelea kumbeba hata kwenye uteuzi wa sasa.

Jambo la pili ni uzoefu wa kibunge wa miaka 20 unaoambatana na uzoefu wa uwaziri kwa miaka 15. Mwinyi ana rekodi nyingine tena, ni kati ya wabunge walioweza kukaa bungeni kwa vipindi vitatu mfululizo (2000 – 2020). Huyu ni mmoja kati ya viongozi wa zama za sasa waliokaa muda mrefu kwenye utumishi wa ngazi ya juu na ikumbukwe kwamba muda wote huo amekuwa kwenye nafasi za uwaziri. Uzoefu wake wa pamoja unamtofautisha na mawaziri wengine wengi wanaojifunza kazi na huwenda ukamjengea kujiamini zaidi na kufanya vizuri zaidi.

No comments: