Tuesday 4 August 2020

BILA YA UMOJA HATUTAIONDOA CCM


Hakuna mwaka utakaokuwa mgumu katika Uchaguzi Mkuu wa Tanzania kama msimu huu wa 2020. Ni mgumu kwa sababu nyingi, lakini ugumu zaidi unakuja kwa kuwa CCM inaweza kupeta tena na kushinda, iwapo Wapinzani tutaruhusu. Uamuzi wa kuisimamisha CCM uko mikononi mwetu.

Nasema kuruhusu kwa sababu ruhusa hio tunayo mikononi mwetu. Kuitoa au kuizuia. Kuitoa ni kwa kuacha kila kitu, nasema kila kitu ili wawe kitu kimoja kujiburi CCM katika uchaguzi huu wa 2020

Na kuizuia, ni kujibakisha katika ubinafsi wao wa kisiasa (political egoism) na kuwaruhusu CCM wapete. Chaguo kwa kweli ni letu na hatutakuwa na mtu wa kumlamumu.

Nasema haya kwa kujua kuwa mazungumzo yanaendelea, na najua kwa undani kuwa yamechelewa, lakini naamini kwa umahiri na uimara (maturity and strength) ya vyama vyetu vikuu Chadema na ACT Wazalendo, bado kuna muda wa mpaka kufikia tarehe ya Uteuzi wa Wagombea, au hata haraka inavyo wezekana, kutekeleza wajibu huu muhimu.

Huu ni wajibu muhimu kuliko wowote ambao wananchi wanaoamini katika upinzani kuvitwika vyama hivyo tokea siasa za vyama vingi zianze 1992 na uchaguzi wa kwanza kuwa 1995 na moja kwa moja nguvu za upinzani kuanza kuonekana, isipokuwa kwa kukosa kujipanga na kujumuisha nguvu hizo.

Najua sana ugumu wa mazungumzo kama haya kwa sababu nilikuwemo katika Think Tank ya Mwaka 2015 ambapo tulipewa kazi ya awali kufanya ramani ya kisiasa (Political Mapping) ya nchi tukiwa vyama vya NCCR Mageuzi, CUF na Chadema. Najua mivutano na sifa ya kujipendelea ya vyama kila kimoja kikitaka kupate steki na mnofu zaidi.

Kwa sasa tuambizane ukweli hatuna raha hiyo ( no that luxury). Msajili wa vyama ametufuma pabaya kuzuia umoja wa vyama akisema tumepitwa na muda na kilichobaki ni ushirikiano kwa njia ya kuachiana. Yaani hatuna njia zaidi ya hio.

Mimi nimekuwa nikisema na wengi pia wamesema kuwa CCM inaondosheka kabisa. Mimi nimekuwa nasema wala hatuna haja ya kutumia nguvu nyingi kukanusha kuwa CCM haiajfanya kitu, jambo ambalo halitufikishi mbali, bali nimekuwa nikiamini tunayo mengi ya kusema katika hayo wanayojigamba kuwa wamefanya.

Pia tuna mengi ya kusema kwa yale ambayo hawakufanya pamoja na kuaminiwa kupewa dola na kwa maana hiyo kuwa na dhamana ya rasilmali zote za nchi, na mamlaka yote ya nchi na katika hayo mamlaka tuna mengi ya kusema kuwa kama taifa hatukutimiziwa hasa kwenye haki zetu.

Umma unajua pia kipindi hiki jinsi Serikali ilivyopeleka sheria nyingi zenye ukandamizi na kupoka haki za watu na kupitishwa na Bunge lenye idadi kubwa ya wajumbe wa CCM. Sheria hizo zimekuwa vitanzi kwa wananchi.

Na kwa hivyo tuna kasi nzuri (we have good momentum) ambayo kwa nguvu za muungano wa CDM na ACT tutaitikisa CCM mpaka kwenye mizizi ( we shall shake CCM to the roots). Tunaweza kuipeleka CCM ukutani mpaka ishindwe kutoa hoja zaidi ya kujibu hoja.

Ila ukweli kama Wapinzani tuna muda mchache wa kuamua. Tuamue kwa sababu tuna wajibu mkubwa wa kuikoa nchi hii isiingie katika kipindi chengine cha miaka mitano chini ya CCM. Tujue tukiruhusu CCM ichukue tena madaraka itakuwa ngumu kuja kupapatua huko mbele.

Najua kila chama ACT na Chadema kimekuwa kijipanga kwa kuchukua dola. Lakini tusipoungana na wazi kura zetu zitagawaika na tutaukosa usukuani yaani Urais ambao ni lengo kuu la kila chama, kwa mfumo wetu ili kushika dola.

Ni vyema tukasimama katika wakati huu kwa vyama vyetu, vyote vina wagombea wazuri kila ngazi, vyote vina maeneo ambayo vinajidai kwayo, na wote tabaan watakuwa na wagombea wazuri katika ngazi za Urais, hasa nafasi ya Urais wa Tanzania.

Tunaomba viongozi wetu waliopo kwenye mazungumzo wajue wajibu mkubwa wanaobeba katika mabega yao kipindi hiki, kutuvusha katika hili, yaani kufikia makubaliano ambapo wana siasa maarufu kadhaa wamekuwa wakiyahimiza, yafikiwe kwa maslahi ya upinzani.

Mgombea wa chaguo la CDM akiwa ni mwanasheria tuliosoma darasa moja na kufanya kazi Bungeni nikiwa ni msaidizi wake Tundu Lissu na chaguo la ACT Wazalendo likiwa ni mwana dipolomaisa na jasusi mbobezi Bernard Membe, ni hakika wananchi watatuuunga mkono kwa yeyote katika wao.

Kwa wananchi muhimu ni kauli ya vyama vyao, na kwa sababu ACT na CDM vyote vina wanachama watiifu watafuata maagizo watayopewa na wengi tunaamini tukichanga kura zetu basi tunaweza kupita kama walivyopita Malawi hivi karibuni, ingawa kuna mifano mengine ya vyama vikongwe kushindwa Barani Afrika.

Kwa sasa CCM CCM kuna ukweli, ijapo hawaupendi kuwa kinashikilia dola kwa sapoti ya vyombo vya dola kama alivyosema Katibu Mkuu Dk Bashiru Ally kuwa si aula kwa chama kilicho madarakani kuaacha kutumia nguvu za dola kujibakisha madarakani.

Najua wananchi wengi wanataka CCM iondoke madarakani, na kwa hivyo wao wanategemea busara na uamuzi wa viongozi wetu waliopo kwenye majdadiliano hivi, sasa ambao tunajua kuwa wanaelewa kuwa tunapambana na muda.

Kama ninavyoamini mimi, naamini pia wapenda mageuzi wenzangu wako nyuma ya viongozi wetu ambao wanajua dhima walionayo kuizuia CCM isije ikapeta tena katika uchaguzi huu. Wasia wangu vyama viache kujitizama kama vyama vyenyewe bali vitizame maslahi makubwa na ya muda mrefu ya umma kwa kutoka na msimamo wa pamoja.

Tutakuwa tunahesabu kila nukta, dakika na saa itayokwenda na tukiwaomba viongozi wetu wa ACT na CDM wasishindwe katika hili kwa sababu hakuna mbadala, hakuna mbadala na hakuna mbadala zaidi ya kuja na msimamo mmoja wa kuindoa CCM madarakani.

Tusipofanya hivyo tutaingia Bungeni vipande vipande, kuukosa Urais na kupata viti vichache Bungeni, na mara hii CCM itakuja na hasira zaidi.

Wananchi wanasubiri zawadi kubwa ambayo hawajawahi kuipata tokea kuingia mfumo wa vyama vingi 1992. Zawadi hio ni ile ya kushika dola ya Tanzania na kama nilivyosema kwa 2020 hilo liko mikononi mwetu wenyewe.
 



No comments: