Wazanzibari wanazidi kung'ang'ania mafuta
na Mwanne Mashugu, Zanzibar
MWAKILISHI wa Jimbo la Matemwe, Ame Mati Wadi (CCM), amesema hakuna kiongozi Zanzibar atakayenyang’anywa kadi ya CCM kutokana na kutetea mafuta na gesi asilia viondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, mwakilishi huyo alisema Wazanzibari wanapaswa kupigania mafuta na gesi asilia viondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano hadi tone la mwisho la jasho lao.
“Mheshimiwa Spika katika ubishi huu hakuna mmoja wetu atakayenyang’anywa kadi ya CCM, lazima tubishe na tulipiganie hadi tone la mwisho la jasho letu,” alisema mwakilishi huyo.
Alisema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na ridhaa ya nchi mbili - Zanzibar na Tanganyika, hivyo wananchi wa Zanzibar wana haki ya kupitia upya mambo ya Muungano na kuona lipi linafaa na lipi halifai.
“Kukaa na kusubiri uamuzi wa kikatiba na kuamuliwa kwa utaratibu wa theluthi tatu ya wabunge wa Zanzbar utachelewesha hoja hii, ni bora kutumia mbinu za ukaidi,” alisema.
Hata hivyo, Mwakilishi wa Jimbo la Gando, Said Ali Mbarouk, alisema suala la mafuta na gesi asilia halitaki kuamuliwa kwa sera, bali linapaswa kuamuliwa kwa sheria za kimapinduzi.
Alieleza Baraza la Mapinduzi na lile la wawakilishi ni vyombo vinavyojulikana kikatiba, hivyo maamuzi yake lazima yaheshimike.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Chambani, Abas Juma Muhunzi, alihimiza kuanzishwa kwa haraka shirika la kusimamia mafuta Zanzibar na kuanzia bajeti ijayo, mkurugenzi wa shirika hilo awe amepatikana.
Akijibu hoja za wajumbe wa baraza hilo, Naibu Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Tafana Kassim Mzee, alisema kufuatia uamuzi wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar mikataba yote iliyofikiwa katika utafiti na uchimbaji wa mafuta na Serikali ya Muungano imefutwa rasmi.
Alisema mikataba iliyofikiwa na Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC) imefutwa rasmi na wawekezaji hao watalazimika kuingia mikataba na Zanzibar.
Kampuni zilizokuwa zimeingia mikataba na TPDC ni Antrim Resource Ltd na Shell International ambazo zilikuwa zifanye utafiti wa mafuta na gesi asilia katika bahari ya mwambao wa Pemba.
Alieleza hivi sasa serikali ipo katika harakati za kutayarisha sera ya nishati inayotarajiwa kuwasilishwa katika Baraza hilo Oktoba mwaka huu.
Naibu Waziri huyo alisema, maamuzi yaliyofikiwa na Baraza la Mapinduzi ni mazito na atakabidhiwa Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha ili ayawasilishe katika kikao cha pamoja cha kujadili kero za Muungano.
Michango hiyo mikali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ilitokana na kauli ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aliposema Bunge ndilo lenye mamlaka ya kutoa kifungu chochote kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni si chombo chingine.
No comments:
Post a Comment