Friday 21 August 2009

MWANASIASA MKONGWE WA ZANZIBAR HASSAN NASSOR MOYO AMETOA MAONI YAKE NA KUSEMA KUNAHITAJIKA KATIBA MPYA ILI KUUIMARISHA MUUNGANO

Hassan Nassor Moyo: Tutengeneze Katiba mpya
kuimarisha Muungano

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pamoja na kuwa hivi sasa una miaka 45
lakini umekuwa ukitikiswa mara kwa mara na hivyo kuwa na wasiwasi kwamba
huenda ukavunjika. Katika makala hii, Mwandishi Wetu, HAWRA SHAMTE
aliyetembelea Zanzibar hivi karibuni alipata bahati ya kuzungumza na
mwanasiasa mkongwe, Hassan Nassor Moyo, aliyewahi kushika nyadhifa mbali
mbali za uwaziri katika Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar…

Swali: Wewe umekuwa kiongozi kwa muda mrefu na ulikuwa kiongozi wakati wa
serikali ya awamu ya kwanza ya marais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na
Sheikh Abeid Karume, je, unaweza kulinganisha uongozi wa wakati ule na wa
sasa?

Jibu: Mimi nimekuwa katika serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar kuanzia tarehe ya Mapinduzi, halafu nimekuwa katika serikali ya
Muungano, na mote humo nimebahatika kuwa Waziri. Kwa hiyo kwa kiasi fulani
mpaka nastaafu mwaka 1985, nimepata kuona mengi sana. Sasa unaponiuliza
nazionaje siasa za leo, kwanza wakati ule pamoja na viongozi wetu wote,
Mwalimu Nyerere, Mzee Karume, Aboud Jumbe kwa wakati wake, tulikuwa
tunaangalia zaidi hali za watu wetu, viongozi walikuwa hawaangalii maslahi
yao bali maslahi ya wananchi. Nimepata kumsikia Rais Kikwete, hivi karibuni
akisema kwamba "wanachoudhika wananchi ni kumuona kiongozi kapata nafasi
hiyo ya uongozi kwa muda mfupi, mara wakamuona na mambo ya ajabu ajabu hivi,
amekuwa tajiri, wapi kaupata, vipi kaupata utajiri huo, wananchi wakiuliza
wanapaswa kupata majibu.

Swali: Tunapozungumzia utawala bora na misingi ya uongozi, wakati wenu
ilikuwa uongozi una kanuni zake, amri ikitoka ni amri ya kiongozi ambayo
inapaswa kuheshimiwa au kutekelezwa, lakini hivi sasa ndani ya Chama kimoja
utasikia kauli zinazosigana za viongozi, nini maana ya hali hii?

Jibu: Hiyo inatokana na kuwa viongozi hawako wamoja katika mambo yao,
haiwezekani kama viongozi wako wamoja katika jambo lao, basi leo huyu aseme
hili, mwengine aseme lile, katika kile kile chama kimoja, lakini zaidi ni
kuwa wanapokutana huwa hawaambizani ukweli. Kadhalika nadhani leo
kunakosekana 'commitment' kwamba kiongozi anapaswa kuwatumikia watu. Sisi
tulikuwa na maadili, tulikuwa tunajua tunalolitaka, tulikuwa tunajua watu
wetu wanataka nini na ndio maana viongozi wetu wengi wamekufa masikini, kwa
sababu tulikuwa na dhamira ya uhuru, tumepigania uhuru ili kubadilisha
maisha ya watu wetu.

Swali: Sasa hivi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unahojiwa sana, kwanza
napenda utufahamishe ule mkataba wa asili wa Muungano ulikuwaje, ulikuwa na
mambo gani na ni mambo gani hasa yaliyoongezeka au yaliyopungua.

Jibu: Hapa ninayo sheria ya Muungano. Ninayo 'article' ya 'Union' ambayo
ilipitishwa katika Bunge la Tanganyika. Wakati huo Serikali ya Mapinduzi
ilikuwa imeshaikubali ile 'article.' Mwalimu Nyerere alikuja kumuona Karume
Aprili 22, 1964, *alikuja na draft ya article yake mkononi*, akazungumza na
Karume, kisha Baraza la Mapinduzi lililokuwa na watu 32 tulikaa tukaangalia
ile article na tukasema kuwa haina matatizo yoyote na likaikubali ile
article. Asiyekuwapo kwenye kikao kile alikuwa ni Aboud Jumbe tu, alikuwa
katumwa Pemba, aliporudi na kwenda kwa mzee Karume alimwambia "tushaungana
na wenzetu."

Ukifuatilia historia ya nchi zetu hizi mbili, Muungano wetu haukuwa ni jambo
zito, kwa sababu ya uhusiano tuliokuwa nao kwa muda mrefu. Tuna uhusiano wa
kidugu wa kibiashara na kadhalika kwa hivyo hakukuwa na uzito wowote
kukubali kushirikiana. Tarehe 25 sote tulikuwa pale Karimjee, Wabunge
walipokutana na kuidhinisha mkataba wa Muungano, sisi tulikuwapo na
tulishuhudia, *na japo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haikuwa na Bunge
lakini kulikuwa na Baraza la Mapinduzi na Baraza hili lilipitisha ule
Mkataba wa Muungano kwa ridhaa. *Mkataba wa awali ulikuwa na mambo 11,
lakini baadaye yakaongezeka moja baada ya moja kwa 'interest' ya Muungano
wetu.

Swali: katika hili suala la kuongezwa mambo ya Muungano, inasemekana kuwa
yaliongezwa kiholela, kimizengwe mizengwe, je nini ukweli wa suala hilo?

Jibu: Hapana, hilo si kweli, mambo ya Muungano yaliongezwa kutokana na
makubaliano, kadiri mchakato wa Muungano ulivyoendelea, ndivyo kadiri
tulivyokuwa tunaongeza. *Lakini mimi nathubutu kusema kuwa haya yote ya
ziada mbali na yale 11, shauri ya kuongeza lililetwa na wenzetu wa
Bara,*tulilipokea kutokana na kuona kuwa inafaa kuyaongeza mambo
fulani fulani
katika Muungano wetu, kwa ridhaa yetu tulikubali kuongeza moja baada ya
moja, kwa ridhaa yetu tulikubali pamoja na hili la gesi, lakini hili la gesi
halikuja hivi, lilikuja wakati mwenyewe Mzee Karume yuhai na lililetwa kwa
mwelekeo wa kuwa masuala yote ya rasilimali za asili (Natural resources)
yawe mambo ya Muungano.

'Natural resources' ni neno pana, linaingia kila kitu, lakini katika Mkataba
imeandikwa 'mineral oil resources,' hili naweza kusema kuwa limeingizwa
kinyemela, kwani 'natural resources' ni kitu tofauti na 'mineral oil
resources' kwa sababu neno maliasili linakusanya vitu vingi, almasi,
dhahabu, nishati, misitu na kadhalika; lakini unaposema 'mineral oil
resources’ umeainisha ni rasilimali ya mafuta tu.

Swali: Imekuaje kwa muda wote huo, tokea mwaka 1968 lilipoingizwa suala hilo
katika mambo ya Muungano, ilikuwaje Wazanzibari wasigutuke kama hicho
kipengele sicho mulivyokubaliana?

Jibu: Wakati ule kulikuwa hakuna watu wa kugutuka, mimi si nilikuwapo mbona
sikugutuka, pengine sikuelewa, lakini kutokuelewa kwangu hakunifanyi mimi
kama kuna kosa nikakataa kosa, lakini sasa angalia kama kuna kosa je,
nilifanya kwa makusudi, au bahati kwa mbaya? Au nilipitiwa au ni yale
mapenzi tuliyokuwa nayo kwa kuona kuwa hawa ni ndugu zetu, *kwa kuwa
Muungano wetu haukuwa mzito hivyo kila walichokuwa wakikileta ndugu zetu
sisi tulikuwa tukisema hayana shaka yoyote haya, hayo yote yametokea kwa
sababu ya kuaminiana. *

*Lakini leo kwa sababu vijana wetu wamesoma, wanabaini mambo, wanajua
sheria, tusiwazuie kusema*. Haiwezekani kuwazuia vijana wetu kuzungumza
masuala ya Katiba, aidha ni mafuta au ni fedha au chochote, haki hiyo ya
kuzungumza wanayo. Muungano huu una miaka 45, mimi nimekaa na Muungano huu
kwa miaka 45 na watoto wangu wanataka kukaa na Muungano kwa miaka mingine
45, lakini wanasema baadhi ya mambo yanafaa kufanyiwa marekebisho,
tusiwakatalie, ndio watu wanapozungumza kuwa hii katiba inafaa iangaliwe,
iangaliwe kweli kwa sababu kuna mambo mengi yanafaa kuangaliwa. Ni kweli
kuna mambo mengi ambayo sisi tuliyapitisha lakini bado yale tuliyoyapitisha
inafaa watu wayaangalie kwa sababu wanafuatana na wakati.

Swali: Sasa tatizo lililopo katika kuangalia, watu wanapozungumza kuhusu
masuala haya huambiwa kuwa wanahatarisha Muungano na kwa mujibu wa Kipengele
cha 37, kipengele kidogo cha pili cha Katiba ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar
anaweza kushitakiwa iwapo ameivunja Katiba ya Zanzibar au anaonyesha
mwenendo unaohatarisha Muungano, sasa kwa Rais kuruhusu wasaidizi wake
wazungumze masuala tete kuhusu Muungano tena katika chombo cha kutunga
sheria, Baraza la Wawakilishi na yeye akakaa kimya, watu wanasema kwamba ni
wazi kuwa kitendo hicho cha Rais Karume, Mawaziri wake na Baraza la
Mapinduzi, wanahatarisha Muungano. Nini maoni yako kuhusu hili.

Jibu: Mimi katika suala la Rais kuhatarisha Muungano, hilo siliingii, kwa
sababu sijui kwanini akakaa kimya, japokuwa wakati mwengine kukaa kimya
inasaidia, kuliko kuliingia jambo kwa haraka haraka. Wakati mwengine ni
jambo zuri sana kwa mtu ukachukua subira, hata mwanao ukimsikia kapayuka
payuka basi wewe usimkaripie kwa wakati ule, chukua subira kidogo. Lala
pengine na mama watoto, upate mapenzi ya mama watoto, asubuhi ukiamka
utamuita yule mtoto kwa njia za utaratibu, lakini ukifumka palepale,
mtagombana bure. Sasa katika mambo ya uongozi vile vile kila mmoja ana
subira zake na ana taratibu zake za kuongoza, inaweza kuwa jambo linamuudhi
lakini akasema, ah, acha kwanza nisubiri. Lakini mimi nasema watu wa
Zanzibar na watu wa Bara wana haki ya kuangalia katiba yao, hii katiba
tuliyoitengeneza na kuitia viraka viraka sisi wazee wao mimi nasema wana
haki ya kuviangalia kimoja kimoja.

Swali: Je, unadhani kuna haja ya kutengeneza Katiba mpya au tuendelee kutia
viraka?

Jibu: Siyo nadhani, ni uhakika, tunapaswa kutengeneza Katiba mpya, huo ndio
msimamo mzuri, kwanini tutie viraka viraka? Viraka tumetia sisi wazee, sasa
watoto wetu wanasema hapana viraka, tukae kitako tutengeneze kitu kipya,
kuna ugomvi gani? Tutengeneze kitu kipya kwa sababu ya kuuimarisha umoja
wetu, tukiyaondosha yale mambo madogo madogo na tukaweka mambo kwa
ukamilifu, umoja wetu utakuwa na nguvu zaidi. Hakuna mtu anayetaka kuuvunja
Muungano. Wabara na Wazanzibari wakae kitako wazungumze kuhusu Muungano wao.
Hakuna ubaya wowote hivi leo kukaa kitako na kujadili upya Muungano wetu,
upande mmoja ukiona jambo hili silo na ukaamua kumpelekea mwenzio ili mkae
mlizungumze, ni vema kuketi na kuzungumza.

"Bwana mimi nafikiri jambo hili hapana, wakati wake sasa umekwisha,
tulibadilishe", hiyo haki ipo! Wenzetu Bara wasing’ang’anie wakafikiri huu
Muungano ni mali yao, wala sisi tusing’ang’anie tukaufanya kama Muungano huu
ni mali yetu. Huu Muungano ni mali yetu sote watu wawili; kwa hiyo mmoja
katika upande fulani akiona jambo silo, akimpelekea mwenziwe, asifikie
kwamba huyu anataka kuvunja Muungano, mawazo hayo ni ‘very wrong.’

Swali: Kinachosemwa ni kwamba Wazanzibari wanauchokonoa chokonoa sana
Muungano na hivi karibuni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alitoa kauli Bungeni ya
kwamba Muungano ukivunjika, upande mmoja utasaga meno, je wewe unadhani
vipi?

Jibu: Yule aliyejibu hivyo hajui kitu, kwanini unafikiria kwamba Muungao
utavunjika, ile kufikiria tu kwamba Muungano utavunjika ni makosa, kwani huu
Muungano unafikiri umeundwa kwa sababu ya mafuta? Huu sio Muungano wa
mafuta, sasa mtu yeyote anayefikiria kuwa kwa sababu tunataka mafuta tuyatoe
katika Muungano ndio tunataka kuvunja Muungano, huyo ni mjinga huyo. Huu
Muungano haukuwa wa mafuta huu. Huu ni Muungano wa nchi mbili, tena ziko
sawa sawa. Huu Muungano hauvunjiki kwa sababu fulani alisema.

Swali: Ikiwa huu Muungano ni wa nchi mbili zilizo sawa, lakini mbona kuna
hisia kwamba kuna nchi moja kubwa inaimeza nyingine iliyo ndogo?

Jibu: Bahati mbaya mimi mawazo hayo huwa siyakubali sana. Ingawa unaweza
kusema kwamba kwa kuwa mimi ni miongoni mwa viongozi walioanzisha Muungano,
kwa hiyo lazima nitetee. Lakini sitetei, ila natetea ukweli kwamba tunataka
Muungano ubakie na tunataka Muungano uendelee kuwa imara, kazi yetu kubwa
sasa ni kuendelea kuimarisha Muungano, maana Muungano upo, mambo madogo
madogo hayawezi kuvunja Muungano. Makosa ya viongozi wetu ni kwamba hawakai
kitako wakazungumza. Kama Waswahili wanavyosema ‘usipoziba ufa utajenga
ukuta.' Unafikiri wakati ule wa Marehemu Karume na Mwalimu Nyerere unadhani
kulikuwa hakutokei matatizo? Yalikuwapo mengi na mengine tukikwambieni
mtashituka. Lakini watu wazima walikuwa wakikutana na kuzungumza mambo haya
kwa ukweli na yalikuwa yanakwisha.

Swali: Lakini kuna maneno yanasemwa kuwa Mzee karume aliwahi kusema kuwa
"Muungano ni kama koti likinibana nitalivua."

Jibu: Enhe, ni kweli, kasema, lakini maana yake nini? Maana yake ni kwamba
ukisema, utasema utasema, lakini husemi barabarani, utasema katika vikao,
lakini ikifika pahala mwenzio hakubali, kweli utamwambia basi, kwa sababu
ulimwambia na hataki, sasa utafanyaje? Utavua koti!

Swali: Nini ushauri wako katika kulikabili tatizo hili?

Jibu: Ushauri wangu viongozi wakuu wa Serikali zote mbili wazungumze masuala
ya Muungano. Watoe mamlaka kwa wafuasi wao wazungumze masuala ya Muungano;
Katiba izungumzwe, hakuna watu kuogopa kuizungumza Katiba. Katiba ndiyo
chombo kikubwa cha kuendesha Muungano wetu. Unajua tatizo letu ni kuwa
imefika wakati tunaogopa hata vivuli vyetu, kumbe vivuli vyetu ndivyo
vinavyoakisi uwepo wetu, hatuna sababu ya kuviogopa!

No comments: