Friday 21 August 2009

Rais Kikwete ahusishwa na Vurugu za Uandikishaji Zanzibar


Serikali ya Zanzibar yatangaza vita Pemba
• Dk. Slaa asema historia itamhukumu Rais Kikwete

na Esther Mbussi na Kulwa Karedia



SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza rasmi kutumia nguvu za dola
kupambana na makundi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya kigaidi katika
Kisiwa cha Pemba. Msimamo huo ulitolewa jana na Waziri wa Nchi Afisi ya
Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es
Salaam wakati wa kongamano la siku moja, lililoandaliwa na Chama cha
Wananchi (CUF) kwa lengo la kujadili hali ya kisiasa kisiwani Zanzibar.
“Napenda kutoa msimamo wa SMZ juu ya vitendo hivi, kuanzia sasa tunasema
tutatumia nguvu zote kushughulikia magaidi wa aina yoyote watakaojaribu
kuvunja amani na utulivu uliopo… hatutawavulimia hata kidogo,” alisema
Waziri Juma.

Alisema kwa vile serikali ipo kwa ajili ya kuwalinda wananchi wake,
haitakubali kuona hali ya uvunjifu wa amani inachukua nafasi kubwa wakati
huu wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010. “Suala la amani halipaswi
kuchezewa hata kidogo, wananchi wetu wamekuwa wakipandikizwa chuki na
wanasiasa ambao yakitokea matatizo utakuta hawapo, lakini wanaoumia ni hao
hao wananchi,” alisema Waziri Juma.

Alisema kutokana na hali hiyo, SMZ inatoa tahadhari kali kwa wananchi ambao
watagundulika kujiandikisha zaidi ya mara moja wakati wana vitambulisho.
“Tunafanya utafiti juu ya suala hili na tukigundua vitambulisho vyao vipo na
wanafanya vurugu za makusudi, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,
kwani wanasababisha wenzao kukosa haki zao na siasa ya Zanzibar kuonekana
haifai, si kweli, siasa ya Zanzibar haiko kama inavyoelezwa,” alisema Waziri
Juma.

Alisema suala la uandikishaji wananchi limegeuzwa kuwa la kisiasa zaidi
kuliko hali halisi. Aliwataka wanasiasa visiwani kufanya kazi zao za siasa
na si kuingia katika masuala ya kisheria.

Akichangia katika kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, alimtupia lawama Rais Jakaya Kikwete
kwa kusema amekuwa kimya mno tangu fujo hizo kutokea. Alisema historia
itamhukumu Rais Kikwete kwa ukimya wake, kwa vile anaonekana wazi amebariki
hali hiyo kuwepo katika Kisiwa cha Pemba. “Serikali yoyote inaposikia kelele
au manung’uniko, jambo la kwanza ni kusikiliza na kusuluhisha na si kutumia
ubabe… amani haiteremki kutoka mbinguni, inajengwa, hatutaki kuyaona tena ya
mwaka 1995, 2000 na 2005 yanatokea, tunataka tufanye uchaguzi kwa amani
tusitunishiane misuli,” alisema Dk. Slaa.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Slaa aliitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC)
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kukutana mara moja ili kujadili kasoro
zilizojitokeza katika suala zima la uandikishaji na utoaji wa vitambulisho.
“Tume hizi zinapaswa kukutana haraka kujadili kasoro zilizojitokeza ili
kuepuka matatizo kama yale yaliyotokea Burundi na Rwanda… hatutaki kufika
huko,” alisema Dk. Slaa.

Naye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema machafuko
yanayotokea visiwani humo yanahusishwa moja kwa moja na Rais Kikwete kwa
vile ameruhusu vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na vifaru
kupelekwa Pemba. “Yeye kama Amiri Jeshi Mkuu, anahusika katika hili, kwa
sababu amebariki vifaru na askari wa JWTZ kupelekwa Pemba, utadhani kuna
machafuko makubwa… huku ni kutisha wananchi, nawaambia historia itamhukumu,”
alisema Maalim Seif. Alisema katika hali ya kushangaza, hakuna mwanachama
hata mmoja wa CCM aliyenyimwa kitambulisho, kitendo ambacho kinadhihirisha
wazi kuna mipango maalumu ya kudhoofisha upinzani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vitambulisho Zanzibar, Mohamed Juma Amme,
aliwatuhumu wanasiasa kuwa wamekuwa wakichochea wananchi kufanya vurugu ili
kuharibu zoezi la uandikishaji. “Suala hili ni dogo, lakini limekuzwa na
wanasiasa wetu ili kupotosha hali halisi iliyopo, serikali ilifanya makusudi
kutumia vitambulisho vya kura kwa maana nzuri tu, kuna vitambulisho zaidi ya
7,000 viko vituoni, lakini wananchi wamegoma kwenda kuvichukua, sasa nani wa
kulaumiwa?” alihoji Amme. Alisema ofisi yake haitasita kuwafungulia
mashitaka wanasiasa wanaotoa kauli za uchochezi bila ya kuwa na uthibitisho.


Kongamano hilo la siku moja, lililokuwa chini ya Uenyekiti wa Profesa
Ibrahim Lipumba, lilikuwa na lengo la kujadili na kupata ufumbuzi wa athari
za uandikishaji kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar na matumizi
mabaya ya vyombo vya dola. Baadhi ya viongozi wengine waliohudhuria
kongamano hilo ni pamoja na Msuluhishi wa Mgogoro wa Darfur, Dk. Salim
Ahmed, Salim, Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, Brigedia Jenerali mstaafu
Hashim Mbita, wabunge na viongozi wengine mbalimbali.

No comments: