Friday, 11 September 2009

Tukomeshe ubaguzi huu Zanzibar

Tukomeshe ubaguzi huu Zanzibar Umeanza kwa Wapemba sasa Wangazija ?

Salim Said Salim


NINAKUMBUKA nilipokuja Zanzibar kwa likizo kutoka mkoani Tanga nilipokuwa ninafanya kazi kama mwandishi wa magazeti ya Tanganyika Standard (sasa Daily/Sunday News) nilipata ujumbe kutoka ofisini ulionitaka nihudhurie mkutano wa Wangazija ulioitishwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar, hayati mzee Abeid Aman Karume.
Mzee Karume, aliwaambia Wangazija, wengi wakiwa wamezaliwa Zanzibar na hata kujukuu, lakini asili yao ikiwa ni visiwa vya Comoro. Wangazija walilalamika na kusema ule ulikuwa uonevu, ubaguzi na udhalilishaji na lengo lilikuwa ni kuwanyanyasa kwa vile walikataa kujiingiza katika vitendo vya kuua watu licha ya wazee wao wengi kuuawa katika mazingira yasiyoeleweka hadi leo.
Wapo waliokubali kutii amri ile kwa shingo upande na kuomba uraia, kama vile vyeti vyao vya kuzaliwa Zanzibar vilikuwa havina maana kama ilivyo leo wale wanaojiita Wazanzibari wanapovionyesha kutaka waandikishwe kuwa wapiga kura. Wengine, akiwamo swahiba wangu na mwandishi wa habari maarufu aliyesema kweli hadi siku za mwisho za maisha yake, marehemu Ali Nabwa, waliipuuza amri ile kwa vile waliiona ni ya kifashisti.
“ Kama ni kuomba uraia, basi iwe kwa wote…wenye asili ya Arabuni, India, China, Malawi, Msumbiji na kwingineko. Au watu wote waondoke Zanzibar na waletwe watu wawili, mwanamume aitwe Adam na mwanamke aitwe Hawa na waanze kupanda mbegu mpya ya Wazanzibari,” marehemu Nabwa alisema wazi, sitasahau na nitaendelea kumheshimu kwa kusema kweli ingawa hao wanaojiita wakubwa hawapendi kuambiwa kweli.
Baadhi ya wazee wa Kingazija ambao walikuwa mstari wa mbele kama viongozi wa Chama cha Afro Shirazi Party (ASP) walishangazwa na uamuzi wa kupokony wa uraia na walipoteza heshima waliyokuwa nayo mbele ya jamii. Baadhi ya jamaa zao waliwaambia walistahili yawakute kwa kusahau kuwa fadhila ya punda ni mateke.
Wazee hawa walihisi walisalitiwa na watu waliowaona wenzao wa karibu na kulalamika kuwa mchango wao katika ukombozi wa Zanzibar umesahauliwa.
Wangazija wengi walikwenda kuishi Comoro kama wakimbizi , lakini baadhi yao kutokana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutofurahishwa na mwenendo ule waliweza kurudi Visiwani baada ya kifo cha mzee Karume mwaka 1972.
Sasa ni miaka 41 tangu Wangazija kuandamwa na kusakamwa na tunaona historia iliyoandikwa wakati wa utawala wa mzee Abeid Karume inajirudia wakati wa utawala mwanawe, Rais Amani.
Tunaambiwa ni sheria ndiyo inafanya kazi yake, lakini mtu wa kawaida hujiuliza sheria inayowabana Wangazija ilifanya kazi wakati wa utawala wa Mzee Karume na sasa wakati wa mwanawe Amani akiwa madarakani tu?
Ilikuwa wapi sheria hii waka ti wa utawala wa Sheikh Ali Hassan Mwinyi, Sheikh Idris Abdulwakil na komandoo Salmin Amour? Taireni jamani, waacheni Wangazija wapumue.
Wanaofurahia hali hii wajue wanakaanga mbuyu na kuwaachia vibogoyo kutafuna. Watawaponza watu na kufikiriwa ubaya wakati hawana mkono wala kauli katika uovu huu wa kuwaandamama Wangazija.
Tunaambiwa kuwa uamuzi wakuwaandama Wangazija ni wa serikali, lakini kwa mwananchi wa kawaida unapozungumzia serikali basi moja kwa moja huenda kwa Rais aliyekuwa madarakani ambaye kwa ninavyomjua miongoni mwa maswahiba wake wakubwa ni watu wenye asili ya Comoro. Sijui yupo katika hali gani juu ya suala hili na anawatazama vipi Wangazija anapokutana nao.
Wapo wanaodai tatizo wanalokabili Wangazija lilitokana na baadhi ya wazee wao, mara baada ya Mapinduzi ya 1964, walikataa kutambulika kama Watanzania na kujidai utiifu wao ulikuwa kwa Comoro ambayo ilikuwa inatawaliwa na Mfaransa kwa hiyo wao ni raia wa Kifaransa. Hili sina hakika nalo, lakini hata ikiwa kweli kwa nini kauli za wazee wawili au watatu ziamue hatima ya mamia ya watu, wakiwamo ambao walikuwa hawajazaliwa?
Tukianza kuhukumu watu kwa yaliotendwa na wazee wetu, iwe wa kutuzaa, wa kifamilia au wa kupachikwa, tujue tunatafuta balaa.
Wazanzibari watashindwa kutazamana usoni wakiyachambua machafu yaliyotendeka Visiwani katika nusu karne iliyopita. Baadhi ya wazee wetu walifanya unyama ambao hata Manyara, Ngorongoro na Serengeti hauonekani, je, watoto wao wahukumiwe kwa waliyoyatenda wazee wao?
Kama ni suala wazazi kuwa na asili ya nje ya visiwa vya Unguja na Pemba kwa nini Wanamsumbiji waliokuja wakati wa kupigania ukombozi kutoka kwa Mreno nao wasitakiwe kuomba uraia? Wapo wengi na baadhi yao hupiga kura wakati wa uchaguzi.
Kwa vyovyote vile wanayotendewa Wangazija ambao wamekuwa wakisema hawathaminiwi Visiwani na ndiyo maana hakuna Mngazija mmoja aliyewahi kuchaguliwa kuwa waziri katika orodha ya zaidi ya mawaziri 250 walioitumikia SMZ tangu mwaka 1964.
Lakini wapo Wangazija waliowahi kuwa mawaziri katika Serikali ya Muungano na wengine kuwa mabalozi wetu nje ya nchi.
Idara ya Uhamiaji imesema hakuna mtu atayenyang’anywa hati ya usafiri wakati hilo limefanyika na wengi kusumbuliwa hadi sasa kwa suala la uraia. Kosa lao ni kwa babu zao kuzaliwa Comoro.
Ni vizuri Rais Amani Karume ahakikishe kabla ya kumaliza muda wake madarakani analimaliza suala hili moja kwa moja ili kumbukumbu zisimjumuishe kuwa miongoni mwa wale waliofumbia macho madhila waliofanyiwa Wangazija waliozaliwa Zanzibar, baadhi ya wakati wakifanyiwa vioja hivi na watu ambao wenyewe hawakuzaliwa Zanzibar.

No comments: