Monday 2 February 2015

DAR UBUNGO, KINONDONI NA KAWE – UKAWA INAWEZA KUWIKA KOTE

Na. Julius Mtatiro,Former Deputy  Secretary General of CUF.




Mkoa wa Dar Es Salaam una jumla ya majimbo ya uchaguzi 8, ambayo yamo katika wilaya tatu za Kinondoni, Ilala na Temeke. Katika uchambuzi wa leo tutajikita katika majimbo matatu ya wilaya ya Kinondoni, ambayo ni Ubungo, Kinondoni na Ilala.
Kinondoni ni wilaya yenye ukubwa wa kilomita za mraba 531 na imepakana na Wilaya ya Bagamoyo upande wa Kaskazini, upande wa Kaskazini Mashariki inapakana na Bahari ya Hindi, upande wa Kusini inapakana na Manispaa ya Ilala, upande wa Kusini Magharibi inapakana na Wilaya ya Kisarawe na upande wa Magharibi inapakana na Wilaya ya Kibaha.
Kutokana na sensa ya mwaka 2012 wilaya ya Kinondoni ina watu 1,775,049 ambapo wanaume ni 860,802 na wanawake 914,247 na ina ongezeko la watu kwa wastani wa asilimia 5 kwa mwaka.
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imegawanyika katika Tarafa 4, Kata 34, Jumla ya Mitaa ni 171, Idadi ya Majimbo ya Uchaguzi ni matatu (3) ambayo ni Kawe, Kinondoni na Ubungo.

JIMBO LA UBUNGO:
Kisiasa jimbo la Ubungo limekuwa chini ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) muda wote tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania. Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2000 na 2005 ulishuhudia ushindani mkubwa wa kisiasa na CCM haikupata usingizi.
Mwaka 2000 mgombea wa CUF Hussein Mmasy alimtikisa Keenja wa CCM ambapo Ndugu Mmasy alipata zaidi ya asilimia 40 ya kura zote.
Katika uchaguzi wa mwaka 2005 kijana mwingine, John Mnyika wa CHADEMA aliitikisa CCM ipasavyo. Jumla ya wapiga kura 314,065 walijiandikisha na kura 9,776 ziliharibika. Mgombea wa CCM wakati huo Charles Keenja kupata kura 93,493 sawa na asilimia 51.6 dhidi ya John Mnyika wa Chadema aliyepata kura 45,164 sawa na asilimia 24.9 huku wagombea wa CUF na NCCR kwa pamoja wakipata jumla ya kura 37,735 sawa na asilimia 20.8.
Pia CCM ilishinda viti vya udiwani 11 katika kata 11 za jimbo la ubungo wakati huo. Pamoja na matokeo hayo, vyama vya upinzania havikuwa vimejipanga vya kutosha na uchaguzi uliambatana na hila nyingi kutoka kwa CCM.
Mwaka 2010 ulikuwa na nuru ya pekee ambapo jimbo la Ubungo liliangukia mikononi mwa CHADEMA, Mgombea wake John Mnyika alipigiwa kura 66,742 sawa na asilimia 49.56 wakati mgombea wa CCM Bi. Hawa Ng’umbi alipata kura 50,544 sawa na asilimia 37.53 na Julius Mtatiro wa CUF alipata kura 12,964 sawa na asilimia 9.63 ya kura zote.
Kati ya mwaka 2010 na 2014 mbunge wa Ubungo, mhe. John Mnyika amejipambanua kama kiongozi anayewajibika kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa, na hiyo ni sifa muhimu mno kwa siasa za sasa. Katika utekelezaji wa ilani yake ya uchaguzi kwa kiasi kikubwa hajafanikiwa katika suala la uhaba wa maji.
Maji ni tatizo kubwa sana katika jimbo la Ubungo, pamoja na juhudi zote alizofanya jambo hili limekuwa gumu. Taarifa za ndani zinaonesha kuwa, serikali haijawekeza nguvu kubwa katika miradi ya maji Ubungo kwa kuhofia kumpa sifa Mnyika na kufanya jimbo hilo lisirudi CCM kirahisi katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Pamoja na hisia hizo, ukweli ni kuwa Mahitaji ya maji katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa sasa ni mita za ujazo 170,760 kwa siku lakini huduma inayopatikana kutoka katika mifumo ya maji ya DAWASA ni chini ya asilimia 45 ya mahitaji halisi na eneo linaloathirika zaidi na uhaba wa maji ni jimbo la Ubungo ambalo linaongozwa na Mnyika. Kwa sababu jukumu la kuleta maji ni la serikali huku kazi ya mbunge ikiwa ni kuhimiza na kushauri, John Mnyika hatakosa cha kuwaeleza wapiga kura kuhusu suala hili.
Wapiga kura wengi wa jimbo la Ubungo ambao ni vijana wanaendelea kumuunga mkono John Mnyika kwa sababu mara kwa mara anatoa taarifa ya mambo yaliyoshindikana na kwa nini imekuwa hivyo na kwa hakika, kati ya majimbo ambayo hayawezi kurudi CCM katika uchaguzi wa 2015 ni pamoja na hili la Mnyika. Hii inachangiwa hasa na ushirikiano wa vyama vya UKAWA, ikiwa UKAWA itamuunga mkono mgombea mmoja tu, John Mnyika atashinda tena kirahisi lakini UKAWA isiposimamisha mgombea mmoja kuna uwezekano mkubwa kwamba CCM wakajaribu kulichukua jimbo la Ubungo ukizingatia kuwa linachangia kwa kiasi kikubwa katika kujenga uchumi wa jiji la Dar Es Salaam na taifa kwa ujumla. Hili si jambo la kupuuza hata kidogo.
JIMBO LA KINONDONI:
Jimbo la Kinodoni limekuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi kwa muda mrefu. Kwa vipindi kadhaa, mbunge wa sasa Idd Azzan Mohamed ameendelea kushinda chaguzi. Pamoja na suala la kukosekana kwa usawa wa ushindani wa kisiasa na upendeleo ambao wagombea wa CCM wamekuwa wakipata kutoka kwa vyombo vya dola, Sababu kubwa ya kufanya jimbo hili liendelee kuwa chini ya CCM ni wagombea wasiotoa ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.
Mwaka 2005 wagombea wa CUF na CHADEMA walipata jumla ya kura 41,775 sawa na asilimia 29. 9 huku CCM chini ya Idd Azzan ikishinda kwa kura 94,387 sawa asilimia 67.7. Ushindi wa CCM ulipungua kwa kasi mwaka 2010 ambapo wagombea wa CUF na CHADEMA walipata jumla ya kura 50,015 sawa na asilimia 47.88 wakati CCM chini ya Idd Azzan ikipata kura 51, 372 sawa na asilimia 49.18, kwa hiyo katika uchaguzi wa 2010 CCM iliwazidi wagombea wa CHADEMA na CUF kwa kura 1357 sawa na tofauti ya asilimia 1.3.
Kwa hali ilivyo sasa,wananchi wanaonesha kumchoka mbunge Idd Azzan wa CCM na chama chake kinaweza kumleta mgombea mwingine ili kubadilisha ladha, kuweka mikakati mipya na kuwafanya wananchi wajione wako chini ya mtu mwingine. UKAWA pia itapaswa kumuweka mgombea mmoja kwa sababu nguvu ya CHADEMA na CUF kwa kura katika uchaguzi wa mwaka 2010 zilipishana kidogo tu (zinakaribiana mno).
Inajionesha wazi kwamba katika uchaguzi wa mwaka 2015 CCM itapoteza jimbo la Kinondoni hata kama itabadilisha mgombea. Sharti moja tu ambalo litaifanya CCM ishinde tena ni ikiwa vyama vya CHADEMA na CUF vitaweka wagombea tofauti, lakini kwa msimamo wa pamoja wa UKAWA ikiwa vyama vinavyounda UKAWA vitaweka mgombea mmoja imara na vikajipanga, jimbo hili halitaongozwa na CCM baada ya uchaguzi huo na kwa hiyo litaangukia mikononi mwa vyama vya UKAWA.
Kwa hakika hatuwezi kusema kwamba jimbo la Kinondoni limekuwa na mafanikio yoyote makubwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Matatizo makuu ya wananchi katika maeneo ya uchumi, biashara na vipato yameendelea kuwa palepale, huduma za kijamii zinapatikana vizuri kwa wananchi walio na kipato: kwa ujumla matatizo ya jimbo la Kinondoni ni sawasawa na matatizo ya Ubungo, Kawe na Dar Es Salaam, wananchi watapenda kuona mbunge anayekuwa karibu nao zaidi na atakayefanya juhudi za wazi kuwatoa sehemu moja kuwapeleka nyingine.
JIMBO LA KAWE:
Jimbo la Kawe ni kati ya majimbo yaliyopata bahati njema ya kuongozwa na wabunge wanawake katika nyakati kadhaa. Bi. Rita Mlaki wa CCM ameliongoza jimbo hilo kuanzia mwaka 2000 hadi 2010. Katika uchaguzi wa mwaka 2005 Bi.Mlaki alipata ushindi mkubwa wa asilimia 63 uliotokana na kura 64,074 dhidi ya vyama 11 vilivyoweka wagombea katika uchaguzi huo. Vyama vya CUF na CHADEMA kwa pamoja vilipata asilimia 33 iliyotokana na kura 33,522 huku vyama vingine 8 vikipata asilimia 3.1 kutokana na kura 4163.
Nguvu ya mwanamama mwingine, Bi. Halima James Mdee wa CHADEMA ilifanya mabadiliko makubwa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ambao ilitarajiwa angepambana na Bi. Lita Mlaki(Aliyeshindwa dhidi ya Bi. Angela Kizigha katika kura za maoni ndani ya CCM). Katika kinyang’anyiro hicho kilichowakutanisha kina mama wawili dhidi ya mwanasiasa maarufu na nguli mhe. James Francis Mbatia wa NCCR, nyota ya Bi. Halima Mdee wa CHADEMA iling’ara na akapata ushidi wa kura 43,365 sawa na asilimia 43.17 akifuatiwa na mwanamama mwenzie Bi. Angela Kizingha wa CCM aliyepata kura 34,412 sawa na asilimia 34.26 huku James Mbatia wa NCCR na Mapeyo Shaabani wa CUF kwa pamoja wakipata kura 21,091sawa na asilimia 21, na wakati huohuo, vyama vingine 5 vilivyoweka wagombea katika uchaguzi huo vikiambulia kura 1528 sawa na asilimia 1.58 ya kura zote.
Tangu kuchaguliwa kwake, Bi. Halima Mdee amejipambanua kama mwanamke jasiri na mpambanaji. Mara kadhaa amejitosa katika mapambano ya kudai haki za umiliki wa ardhi kwa wananchi huku akijaribu kusimamia suala la uporwaji wa maeneo ya wazi unaofanywa na vigogo na hata serikali yenyewe. Ujana wa Halima Mdee, kuwa karibu na wapiga kura na faida ya kuwa mwanamke kunamfanya awe na nafasi kubwa kutetea kiti chake katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015.
Kitisho chochote cha CCM kumshinda Bi. Halima Mdee katika uchaguzi ujao kitaondolewa na uwepo wa UKAWA, kwa maana kwamba kama UKAWA ikimsimamisha kama mgombea pekee, atapata faida ya kupigiwa kura za NCCR na CUF ambazo ni asilimia zaidi ya 20 na hivyo anaweza kupata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 60.
Katika jimbo la Kawe mwaka 2015, sera muhimu zitajikita katika masuala yaleyale yanayowakabili wananchi wa Dar Es Salaam hususani makazi (kwa sababu Kawe ni mji unaokua), ukosefu wa ajira, uhakika wa huduma za kijamii ikiwemo upatikanaji wa maji n.k.
(Julius Mtatiro amewahi kuwa kiongozi wa juu wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania “DARUSO & TAHLISO, 2006 – 2008”. Pia, amekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Tanzania Bara (2011 – 2014). Ana shahada ya Elimu ya Sanaa (B.A) na Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A). Hivi sasa ni mfasiri, mshauri mtaalamu na mchambuzi. Mtatiro ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa shahada ya sheria (L LB) – 0787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).

No comments: