Warioba ameukataa unafiki, CCM inaukumbatia
Na Salim Said Salim
NINAKUMBUKA nilipokuwa mdogo kila tulipokuwa na mchezo wa kandanda na timu nyingine ya mtaani, uwe wa kugombea kikombe au wa kirafiki, tulikuwa tunalishana yamini (kula kiapo) kwa kila mmoja wetu kuhakikisha tunashinda.
Katika kiapo kile tulikuwa tunafungishana pingu ya vidole vidogo vya mkono wa kulia na baada ya kula kiapo ndipo pingu hukatwa.Kila ninapokumbuka zama zile hucheka, lakini hujitosheleza kwa kusema zile zilikuwa ni zama za utoto na zimepita.Kwa kawaida, kitendo cha kula kiapo hasa kwa waumini wa dini moja au nyingine, si jambo la mchezo wala la kulifanyia mzaha na ndiyo maana watu wanaokabidhiwa dhamana kubwa katika serikali hulishwa kiapo na rais cha kuahidi uadilifu.Lakini siku hizi tunasikia viongozi wa CCM, Zanzibar wanapokutana wanalishana kiapo cha kung’ang’ania muungano wa mfumo wa serikali mbili ambao umma tayari umeshatoa kauli ya kuagana nao na kusema unataka serikali tatu.
Viongozi wa CCM wanapaswa kuelewa kuwa umma haukulishana kiapo kufikia uamuzi wa kutaka serikali tatu, bali ilikuwa ni ridhaa yao, hivyo ndivyo walivyoielekeza kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilipozunguka Vsiwani na Bara kukusanya maoni ya wananchi.
Kwa hakika viongozi wa CCM wamechelewa kutumia kiapo kama njia ya kulazimisha kuendelea na mfumo wa serikali mbili.
Watu wamechoshwa na kauli za miaka nenda miaka rudi za kuambiwa: “Tupo mbioni.” Haujulikani mwanzo wala mwisho kumaliza kero za Muugano. Kwao matumaini ya kumaliza kero za muungano yapo kwa mfumo wa serikali tatu.
Kama ni kulishna viapo ndio kungesaidia kuendelea na mfumo wa serikali mbili basi ilikuwa vema kwa viogozi wa CCM kuzunguka nchi nzima kabla ya kuanza mchakato wa kukusanya maoni na kuwalisha watu viapo na si sasa wakati watu wameshaamua.
Kwa maana nyingine huu mwenendo wa kulishana viapo ni kama mchezo wa kitoto wanaotaka ushindi wa lazima wa mchezo wa kandanda, hata ikiwa uwezo wa kuifunga timu wanayopambana nayo haupo.
Siku hizi hubaki ninacheka tu ninapokuwa katika baraza za kahawa za mjini Unguja pale ninapowaona watu kila mara wanafanya mzaha wa kuigiza CCM kwa kulishana kiapo, hata kwa ahadi ya kukutana baadaye jioni.
Ni vizuri kwa viongozi wa CCM na vyama vingine vikawaachia viongozi na wanachama wao kuwa huru kuamua aina gani ya Katiba na mfumo wa muungano wanaoutaka. Hii ni kwa sababu Katiba na muungano si wa chama chochote kile, bali ni wananchi (wakiwemo wale wasio mashabiki wa chama chochote kile).
Hizi si tena zama za utamu wa chama kushika hatamu, bali ni zama za utamu wa umma kuamua nchi iwe na mwelekeo gani.
Kwa bahati mbaya baadhi ya viongozi wa CCM wameamua kumshikia bango kumsakama Jaji Warioba. Wanamuonea mzee huyo ambaye tume anayoiongoza haikufanya kazi hiyo kwa masilahi yake, ingawa watu walishajenga mazoea ya kuiita tume ya Warioba. Hili si jambo geni, kwakuwa tuna utaratibu wa kuipa taasisi au tume jina la kiongozi wake.
Mapendekezo yaliyotolewa na tume si ya Jaji Warioba pekee au pamoja na wajumbe wenzake wa tume, bali ni ya wananchi. Kilichofanywa na tume ni kuwasilisha yale waliyoambiwa na umma wakati wa zoezi la kukusanya maoni na kama walivyotakiwa na hadidu rejea za kazi za tume hiyo.
Labda lingelikuwa jambo la busara kama katika hadidu rejea tume ingeambiwa kitakachotakiwa na CCM ndiyo hicho hicho na wengine wasisikilizwe kwa vile “hawana akili timamu”.
Kama yupo mtu anayefaa kulaumiwa kwa kuchomoza pendekezo la serikali tatu basi ni huyo aliyeunda hiyo tume, Rais Jakaya Kikwete, lakini Waswahili wanasema: “Kamba hukatikia pabovu”.
Lakini kwa baadhi yetu tunaomwelewa vizuri Jaji Warioba kwa kufanya naye kazi kwa karibu, kwa taarifa za viongozi wa CCM wasiomjua, huyu ni mtu mkweli na huwa hayumbishwi na shinikizo wala vitisho.
Ni mtu anayejiamini na hayumbi katika kusimamia haki na viongozi wa CCM Zanzibar inafaa niwakumbushe kwamba waliomwalika katika mkutano wao katika Hoteli ya Bwawani wakati wa mtafaruku wa kisiasa aliwaambia kama Zanzibar palikuwa na matatizo basi wao viongozi wa Serikali ya Zanzibar (CCM) walikuwa na matatizo.
Niwakumbushe zaidi kuwa kauli ya Jaji Warioba ambayo iliwaudhi sana pia iliungwa mkono na Rais Kikwete ambaye wakati ule alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kwa maana hiyo, Jaji Warioba wa juzi ndiye wa jana na ndiye wa leo….hayumbi katika kusema ukweli.
Sifa yake nyingine niliyoigundua kwa kufanya naye kazi akiwa waziri mkuu, wakati nikiwa mwandishi wa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, na baadaye kwa zaidi ya miaka sita nikiwa naye pamoja katika Bodi ya Baraza la Habari la Tanzania, ni kuridhia maoni ya wengi, hata kama hakubaliani nayo.
Jaji Warioba siku zote, kwa ninavyomuelewa, amekuwa hakubali kudanganya wala kudanganywa. Mara nyingi tulipokuwa tunajadili malalamiko yaliyowasilishwa katika Baraza alikaa kimya kusikiliza wajumbe wengine, bila ya kujali ni mtu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pia waziri mkuu.
Aliheshimu sana mawazo ya wanataaluma wa habari na wanasheria wenzake ambao walikuwa na miaka michache katika taaluma hiyo kuliko yeye, kama marehemu Sengondo Mvungi na Jenerali Ulimwengu.
Kama CCM ilikuwa na nia ya kuifanya tume ifanye kazi ya “danganya toto” basi ilikosea tangu mwanzo kuchagua watu kama Jaji Warioba kuwa Mwenyekiti na wajumbe wengine kama Jaji Agustino Ramadhani, waziri mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim na mwandishi wa habari maarufu, Ally Saleh.
Hawa ni viumbe wenye kujiamini na si wale unaoweza kuwa na ndoto ya kuwaburuza na kuwatumia waseme uongo.
Nnaamini kwa dhati, kama nilivyoamini mapendekezo ya tume za marehemu Jaji Francis Nyalali na ile ya Jaji Robert Kisanga, yaliyowasilishwa na tume ya Jaji Warioba ndicho wanachokitaka Watanzania, Bara na Visiwani.
Kama CCM ilitaka kuunda tume ili iwe kama muhuri wa kuhalalisha kinachotakiwa na viongozi (baadhi yao si wote) wa CCM basi imechelewa na isifanye ujanja, mtarimbo umeganda na hauugandui kwa shoka wala mzinga, uwe wa nyuki au mwingine.
Kinachohitajika ni kuendelea kuwa na mchakato ambao watu watakuwa huru kuamua Katiba mpya iwe vipi. Inafurahisha kumsikia Rais Kikwete akiweka wazi kuwa uamuzi wa mwisho si wa chama chochote kile cha siasa, bali wa wananchi.
Si vitisho wala viapo vitakavyosaidia, bali nguvu ya hoja na itakayoeleweka kwa njia za kidiplomasia na kuheshimiana.
Inasikitsha kuwasikia baadhi ya viongozi wa CCM Zanzibar wakiwemo wale waliotimuliwa kushika nafasi za juu katika serikali, wanazungumzia nguvu za dola za kumiliki vifaru na ndege za kivita kuunganisha na hoja zao.
Sasa hizi ndege za kivita na vifaru vilivyoonyeshwa wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar zina uhusiano gani na mchakato wa Katiba au mfumo wa Muungano? Acheni kutisha watu, jitisheni wenyewe.
Tuwe watu wazima na tuachane na utoto, uwe wa kutishana au kulishana viapo. Tuukubali ukweli uliopo mbele yetu. Nao ni wa
serikali tatu na kusema kwaheri serikali mbili.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment