Thursday, 6 February 2014

WARIOBA APEWA SOMO ZANZIBAR

KATIKA wakati huu ambapo wananchi wanasubiri kwa hamu kushuhudia Bunge Maalum la Katiba likijadili na hatimaye kuidhinisha Rasimu ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna chochote kitakachodhoofisha mamlaka ya Zanzibar kuliko vile ilivyokuwa siku zote.
Mwansheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman. Na Mwenyekiti  wa Tume ya Katiba Joseph Sinde Warioba.
Huu ndio mtizamo wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ambaye ametoa fursa ya mahojiano maalum na Zanzibar Daima www.zanzibardaima kuhusiana na Rasimu ya Katiba iliyotolewa Disemba 30, mwaka jana wakati ilipokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.Othman ambaye amekuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu katika Serikali ya Mapinduzi wanaoeleza maoni yao kwa ujasiri na ufasaha, anasema hakuna mgongano wowote wa kikatiba kati ya kile kilichoelezwa katika Rasimu ya Katiba na kilichopo kwenye Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa mabadiliko makubwa mwaka 2010.

Bildschirmfoto 2013-09-21 um 11.41.27Anasema hoja kwamba pendekezo la Rasimu ya Katiba mpya la kuitambua Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili, haijaathiri utambuzi wa Zanzibar kuwa ni nchi, kama ilivyobainishwa kwa uwazi wakati wa mabadiliko ya Agosti 2010.
Kwa mujibu wa pendekezo la Rasimu ya Katiba mpya ambayo Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alikabidhi kwa marais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa inatajwa waziwazi kama ifuatavyo:
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambayo kabla ya hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.”Katika Sura ya Kwanza, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyorekebishwa 2010, inatamka kwamba: “Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa Vidogo vilivyoizunguka na Bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa  Tanganyika na Zanzibar, ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.”
“Itategemea na utakavyotafsiri nini, maana ya NCHI maana neno hili lina maana nyingi, lakini kwa maoni yangu binafsi naona hapa inaimarisha unchi wa Zanzibar kuliko kuleta mgongano kama mtu anavyoweza kutafsiri akisoma Rasimu ya Katiba ilivyoeleza jambo hili,” anasema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.Othman, msomi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikochukua shahada ya kwanza na Uingereza alikosomea shahada ya pili, akizidi kueleza mtizamo wake katika suala hilo la kile wanasheria wanakiita “Ukuu wa Katiba,” anasema kilichofanywa na Zanzibar kusema ni nchi kwa maana ile, ni kuondoa “kizoro.”
“Katiba hii inayopendekezwa inaposema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi na Shirikisho naona inaunga mkono msimamo uliomo kwenye Katiba yetu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ilikuwa inaona haya kuueleza ukweli huu bayana. Tulichokifanya tuliporekebisha Katiba 2010 ni kuondoa kizoro hichi kisicho sababu,” anasema.Kizoro ni vazi la mwanamke wa Kiislam linalomfunika uso mzima isipokuwa akibakisha macho tu, staili ambayo inamhifadhi kama inavyoelekeza dini hiyo katika kumtambua mwanamke kama kiumbe anayetakiwa kutojianika.
Othman anasema kwamba ukweli ni kwamba Zanzibar imeungana na Tanganyika na kupatikana Jamhuri ya Muungano na kwamba kutokana na pendekezo la Rasimu ya Katiba mpya, ukweli huo utaendelea kubaki, kwa kuwa “Zanzibar si jimbo. Tulipoungana tuliunganisha nchi huru na kupata taifa moja, lakini kila moja ina mamlaka yake kwa mambo yake, haya ndiyo yalikuwa matarajio.“Ukizungumzia Nchi kwa hii maana ninayoieleza, basi utakuta Zanzibar ni nchi si jimbo. Zanzibar ni state (dola) na kwa maana nzima ya sasa, ni moja ya nchi washirika zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… na kwa sasa kwa mapendekezo ya katiba mpya, Tanganyika ambayo ilikuwa imejificha, nayo itakuwa ni state waziwazi kama ilivyo Zanzibar.”
Akizungumzia Ibara inayomtambua Rais wa Zanzibar kama Mkuu wa Nchi ya Zanzibar, Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa kuchukulia pia pale Rasimu ya Katiba mpya inapomtaja Rais wa Jamhuri kama Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, Othman anasema hapo vilevile hakuna mgongano wowote.“Ndivyo hali halisi ilivyo. Katiba ya Zanzibar inaelezea mamlaka ya Rais wa Zanzibar kwenye eneo lake. Rasimu ya Katiba mpya inaelezea mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa yale mambo aliyolengwa kuyasimamia kimuungano,” anasema.
Mtizamo wa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar unaondoa hisia zilizojengeka kwa baadhi ya Wazanzibari kwamba kwa pendekezo lililokuja katika Rasimu ya Katiba kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili, limesababisha kuing’oa meno Katiba ya Zanzibar inayoitambua Zanzibar kuwa ni nchi.
Alipoulizwa anadhani kutakuwa na maelewano kuhusu pendekezo la mfumo wa Muungano wa Serikali Tatu wakati Bunge Maalum la Katiba litakapokutana kama inavyotarajiwa mwezi ujao, Othman amesema hilo ni moja ya maeneo anayoona yatakuwa na ubishani ingawa, “itakuwa ni bahati mbaya tu kwa sababu jambo hili lilipaswa liwe limeshakuwa na muafaka.”Othman hakutaka kuingia kwa undani kwa suala hili lakini anajulikana alivyo na msimamo imara kuhusu umuhimu wa kuondokana na mfumo wa Serikali Mbili ambao anasema “ni ghali zaidi kwa Zanzibar.”
Agosti mwaka jana alipokuwa akifungua Baraza la Katiba la Shirikisho la Wanavyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu Zanzibar, Othman alisema kwamba chini ya mfumo wa Serikali Mbili, “maofisa waandamizi wa Serikali ya Zanzibar wamekuwa wakipishana kila uchao Dar es Salaam kufuatilia masuala mbalimbali yanayoihusu Zanzibar peke yake.”Huku akitilia shindo kukubaliwa kwa moyo mkunjufu kwa mfumo wa Serikali Tatu akiona ndio mfumo imara wa Muungano, Othman aliwaambia wanavyuo kuwa Serikali Mbili ni ghali kwa Zanzibar kuliko ilivyo kwa Tanzania Bara.
“Jamani mfumo wa Serikali Mbili hautufai. Namimi hili nalisema mara nyingi halina maslahi nasi. Ndiyo maana wenzetu wamekuwa hawashughuliki kutatua wanazoziita kero. Hawana cha kukosa, wakati akitokea mtu akifanya utafiti kwenye wizara na idara mbalimbali katika Serikali ya Zanzibar kila siku maofisa wanapishana kusafiri kwenda Dar es Salaam kufuatilia matatizo.”“Hakuna hoja za msingi za kuwa na Serikali Mbili. Kama tunataka kweli, na tumedhamiria kuimarisha Muungano wetu, basi tuone haja ya kuridhia mfumo wa Serikali Tatu ambao utaweka bayana maslahi ya kila mshirika… mfumo wa Serikali Mbili unaweza kuwa sababu ya haraka ya kuvunjika Muungano. Nawaambieni ndugu zanguni, Muungano utavunjwa na Serikali Mbili kwa sababu wapo watu kule (Tanzania Bara) wanaichukia Zanzibar, sasa ni lazima tujenge misingi ya kuulinda Muungano.”Othman alisema kujificha kwa Tanganyika kwenye Serikali ya Muungano, ni fitna kubwa inayoudhoofisha Muungano.
“Uruhani wa Tanganyika ndiyo fitna kubwa ya Muungano, Mzee Jumbe (Aboud Jumbe Mwinyi, Rais wa Pili wa Zanzibar) alitaka kuja na hirizi ya huyu ruhani akamchukue na akamzike.”“Kwa bahati mbaya alidhalilishwa mbele za watu kwa kuambiwa eti hajui hesabu moja na moja anasema tatu. Hivi kweli Mzee Jumbe msomi mzima hajui hesabu? Huu uruhani wa Tanganyika ndiyo fitna kubwa ya Muungano, ipo haipo. Lakini akipanda kichwani anasema nipo, sasa inataka kutumia jina letu la pamoja.”
Othman alikumbusha mkasa uliomtokezea Mzee Jumbe ambaye mwaka 1984, akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliandaa waraka wa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kutaka mfumo wa serikali tatu kwa kutokana na kile alichoamini kuwa “moja na moja ni tatu.” Alimaanisha serikali ya Zanzibar iliyopo wazi, serikali ya Muungano iliyopo wazi na serikali ya Tanganyika iliyojificha.Waraka huo ulinaswa na mashushushu waliokuwa Ikulu ya Zanzibar kabla hajaondoka kwenda mkutanoni Dodoma, na hatimaye akalazimishwa na Mwalimu Julius Nyerere kujiuzulu.Baada ya Tume ya Warioba kupendekeza mfumo wa serikali tatu, viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamekuwa wakipinga na kutamka kwamba watafanya kila wawezalo kukwamisha kupita.

No comments: