Thursday, 6 February 2014

UCHAMBUZI WA UCHAGUZI MDOGO WA JIMBO LA KIEMBESAMAKI

MJUMBE mmoja wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokea Zanzibar alimwambia mwenzangu mara tu baada ya matokeo ya uchaguzi mdogo wa Kiembesamaki kwamba walipaswa kufanya waliyoyafanya, kwanza, kumkomoa Mansoor Yusuf Himidi na, pili, kuangalia ikiwa mbinu zao bado zinaendelea kufanya kazi. Na kweli zimefanya.
Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo (kushoto), akipongezwa na mwakilishi wa Bububu.
Mwakilishi wa Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo (kushoto), akipongezwa na mwakilishi wa Bububu.Kwa mara nyengine tena CCM imeshinda katika uchaguzi mdogo tokea Uchaguzi Mkuu wa 2010, ambapo CCM ilitwaa urais kupitia Dk. Ali Mohamed Shein na Chama cha Wananchi (CUF) kushindwa kwa mara nyengine tena kama 1995, 2000 na 2005 kupitia mgombea wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwa Unguja, chaguzi ndogo ambazo CCM itakuwa imeshinda ni ule wa Uzi, wa Bububu, huu wa Kiembesamaki na ule wa Pemba, jimbo la Chambani ulikuwa ni wa CUF.Nimetaka kuzungumzia uchaguzi huu kwa sababu nyingi: huu ni wa jimbo madhubuti la CCM ambapo si rahisi kutarajia CUF kushinda lakini pia jimbo hili la Kiembesamaki liliachwa wazi na Mansoor Yusuf Himid ambaye alifukuzwa na CCM kwa sababu ya kuunga mkono wale wanaotaka mamlaka zaidi kwa Zanzibar.
Bildschirmfoto 2013-09-21 um 11.40.56Kwa hivyo, uchaguzi huu ulikuwa na ushindani wa kila aina, huku wengine wakitaraji ungelikuwa wa kuonyesha taswira ya Katiba Mpya na wengine wakienda mbali zaidi kuamini utatoa sura ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mimi si katika ambao waliamini yote hayo. Siasa za Zanzibar haziko hivyo na siku zote ni ngumu kutabirika. Na kwa siasa za Zanzibar si rahisi jimbo kugeuka katika uchaguzi mdogo au kwa ghafla kama hivyo.
Kwa hali hiyo, hasa macho yangu kwanza yalikuwa ni kutizama mgawanyo wa kura utakavyokwenda ili kupima hali ya baadaye na pili kutizama utaratibu wenyewe na kuupima kwa kulinganisha na hali ya picha kubwa ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uchaguzi ambapo Mansoor alikuwa mgombea, CCM ilipata kura 3,275 au asilimia 79.9 na CUF ikapata kura 826 sawa na asilimia 20.1 kimahesabu. Uchaguzi huu, CCM imepata kura 1,856 asilimia 76.5 na CUF asilimia 18.3 kwa kura 445.Tukubaliane kuwa hali huwa hivyo kwenye chaguzi ndogo, yaani kiwango cha wanaojitokeza kupiga kura hushuka kulinganishwa na uchaguzi mkuu, lakini pia ni ukweli kuwa wapiga kura wengi wamesusa au wamejiepusha kujitokeza. Hii haiwezi kuwa bure. Kuna sababu kwa pande zote mbili.
Kwa CUF, wapiga kura 381 hawakujitokeza na kwa upande wa CCM wapiga kura 1,429 hawakujitokeza. Na hii ni mbali ya waaandikishwa wapya ambao kila chama kilishawishi wajiandikishe ili kinufaike na kura hizo mpya.Kwa hivyo, ingawa CCM inaonekana imebakisha asilimia yake ya ushindi, lakini ndio iliyopoteza zaidi katika uchaguzi huo, maana chama hicho kitakuwa na masuali  mengi ya kujiuliza: Ilikuwaje? Hivi wanachama wake au wapiga kura wake karibu 1,500 wamekwenda wapi?
Na CUF nao pia wana masuali mengi ya kujiuliza. Kwa nini kura zao hazikuongezeka hata iwapo mazingira mengi yalionyesha uwezekano huo? Je, hata baada ya kile kinachoitwa “Mansoor Factor”, bado watu wa Kiembesamaki wameshindwa kuiamini vya kutosha CUF? Je, ndio wakate tama moja kwa moja ya kushinda jimbo hili? Basi hata kutaraji kura zaidi za rais mwaka 2015?
Hata hivyo, uchaguzi huu kama ulivyokuwa wa Bububu, uligubikwa na madai ya wizi  na upandikizaji wa wapiga kura na hayo yalifanyika wazi wazi. Hii inatoa changamoto ya kimaadili kwa mshindi, Mahmoud Thabit Kombo kukubali ushindi huo katika mazingira kama hayo.Hadi lini wagombea wa CCM wa Zanzibar wataendelea kujibereuza na kujidai hawajui kuwa ushindi wao unasaidiwa na mbinu za wizi na ghilba? Hadi lini watashindwa kujiamini kuwa kwenye mazingira ya uwazi, haki na uhuru hawezi kushinda hata jimbo ambalo kiasili ni lao wenyewe?
Hapa ndipo nataka kuingia katika eneo la pili la makala haya – yaani kutizama chaguzi hizo na suala zima la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ilianza 2010 kufuataia mivutano katika uchaguzi wa 1995, 2000 na ule wa 2005.Ni uchaguzi mkuu wa 2010 pekee ndio uliokuwa salama na ni kwa sababu kuwa kulikuwa na makubaliano baina ya viongozi wakuu, Amani Karume na Maalim Seif Shariff Hamad, ya Novemba 2009.Kwa wengi walitaraji kuwa dhana ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ingesambaa na kuenea kuliko tu kwenye uundwaji wa serikali na kukomea huko huko kileleni. Chaguzi ndogo ambazo zimetokea tangu kumalizika uchaguzi mkuu wa 2010, bila ya shaka ni picha ya uchaguzi mkuu wa 2015.
Hali inavyokwenda kuna kila dalili kuwa kinyume na ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2010, hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka 2015 kwa sababu bado kuna fikra za kutumia nguvu na hila kwenye uchaguzi ili chama tawala kishinde.Ilikuwa wazi katika uchaguzi mdogo wa Kiembesamaki, kama maelezo na ushahidi uliodaiwa ni wa kweli, kwamba wapiga kura wasiohusika walipelekwa kwa magari na ilipotokea baadhi ya watu kupinga, ni wao wapingaji waliokamatwa na kudaiwa walipigwa na polisi. Na kwamba polisi na vikosi vya Serikali ya Zanzibar vililaumiwa waziwazi kusaidia kubeba na kuwasindikiza wapigakura hao mamluki.
Ni fikra zangu kuwa bado hakuna nia ya kisiasa katika kujenga demokrasia ambapo kila ushindi katika kila ngazi utapatikana kwa njia ya haki, uwazi na usawa, ambapo kila mshindani atakuwa na fursa sawa na mwengine.Tushukuru kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwa hivyo kuendelea kuwepo kwake kumewekwa kikatiba na hilo ndio salama kwetu. Lau kuwepo kwa muundo huu wa serikali kungelikuwa ni kule kwa Kenya na Zimbabwe, basi kitambo ingelikwishakatwa roho, kwa sababu bado kuna kundi lenye nguvu za kutumia taasisi za dola ambalo halijawa tayari kwa Maridhiano na Umoja wa Kitaifa.Na hili la kukosa utayari ndio ambalo nina hofu nalo. Ni bora kila mmoja wetu akajaribu kulizuia tokea sasa na tusisubiri kuja kutibu katika uchaguzi mkuu wa 2015.
Ugonjwa na uchu wa kupata madaraka kwa njia yoyote ile usipewe nafasi kuila jamii yetu. Tunayo nafasi ya kuwaambia wagombea na vyama vyetu kuwa nchi ni mwanzo kuliko nafsi zetu na tamaa zetu za vyeo.
Huu hapa  ndio ulikua utabiri wa Dira yetu dirayetu

No comments: