Thursday 20 March 2014

KAULI YA MBUNGE WA KATIBA JULIUS MTATIRO


KARIBU RAIS KIKWETE, UMEKUWA NGUZO YA KUTAFUTA KATIBA MPYA!

Kuna propaganda zinaenezwa na CCM kuwa baadhi ya wajumbe wa bunge la katiba wamepanga kumzomea Rais atakapokuja kulihutubia bunge kesho.Wengine wamekwenda mbali kabisa na kunihusisha mimi na mhe. Mkosamali na njama hizo. Napenda watanzania wote wafahamu kuwa kwanza katika maisha yangu sina tabia za kuzomea, kama nina mtizamo tofauti na jambo fulani hupenda kuliweka wazi bila njia za woga.Nataka kusema kuwa, kati ya watu wanaosubiri kwa hamu hotuba yoyote atakayotoa mhe. Rais ni pamoja na mimi. Nimekuwa na kawaida ya kuzisikiliza sana hotuba za Rais na kisha kuzifanyia uchambuzi wa kimakala kwa kupongeza na kukosoa pale ambapo nadhani hayuko sawasawa, nimekuwa nikifanya hivyo kwa viongozi wengine wowote wale, nami pia napenda kukosolewa, ila hupenda lugha iwe ya staha.

Tuhuma hizo pia zimekuwa zikielekezwa kwa kundi la UKAWA (UMOJA WA KATIBA YA WANANCHI), napenda pia kuthibitisha kuwa kundi hili kwa pamoja lilikubaliana kumpokea Rais kwa mikono miwili kwa sababu linatambua mchango mkubwa wa mhe. Kikwete(at personal capacity) katika kuusimamia mchakato wa katiba. Ikumbukwe kuwa Rais Kikwete anapigwa vita hata ndani ya CCM na wanamlaumu sana eti kwa kile wanachokiita "KUANZISHA MCHAKATO WA KATIBA BILA KUKUBALIANA NA CHAMA CHAKE NA ETI WATANZANIA WALIHITAJI TUME HURU YA UCHAGUZI NA MGOMBEA BINAFSI TU NA SIYO KATIBA MPYA", shutuma hizi Rais kikwete amekuwa akipewa na wana CCM wengi tu tena wenye madaraka makubwa sana ndani ya CCM na sisi tumekuwa tukizithibitisha kila kukicha hapa Dodoma.


Na niwakumbushe tena, kwamba kila CCM walipotaka kukwamisha mchakato wa katiba aidha kwa kuutungia sheria mbovu na isiyotenda haki n.k, Ni Rais Kikwete huyuhuyu ndiye aliyekuwa akiviita vyama vya upinzani na makundi mengine mezani ili kunyoosha mchakato wa katiba. Sisi tunathamini sana na kuenzi mchango wa Rais katika suala la Katiba mpya na tunajua chama chake kinampiga vita ya kutosha katika suala hili.  Siku Rais alipohutubia mkutano wa Halmashauri kuu ya CCM mjini Dodoma, alipoongelea katiba mpya aliwakumbusha wenzake kwamba "wajiandae kisaikolojia kupokea serikali zozote zitakazoamuliwa na wananchi, wajumbe wenzake walimzodoa, kumzomea na kumuweka kitimoto ati msimamo wa chama chao ni Serikali mbili si vinginevyo, wengine walimuita ati anataka kuwasaliti"(Magazeti karibu yote yaliandika habari hii).

Leo, CCM waliomzomea Mwenyekiti wao na Rais wetu katika kikao cha Halmashauri kuu wanajidai ati wao ndo wanampenda sana. Leo wao ndo wanajidai eti kuibua njama za uongo na kweli na za kupikwa kuwa baadhi ya wajumbe wakiwemo mtatiro, Mkosamali na ama kundi la UKAWA wanataka kumzomea Rais.....CCM ni wanafiki sana. Na ukitaka kujua CCM ni wanafiki angalia hotuba ya juzi ya jaji Warioba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali 3, Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania chini ya chama kimoja liliwahi kuidhinisha mfumo wa serikali tatu, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar limetoa maoni yake kupendekeza serikali 3, Baraza la wawakilishi la Zanzibar limependekeza serikali tatu. Leo, watu walewale wanakwenda kwenye TV kukanusha walichokiamua na kukisema jana, huu unafiki umepitiliza. Ndio kama hili la kumzomea Rais, wamzomee wao wenyewe kwenye Halmashauri Kuu halafu leo wajidai watakatifu eti wanatetea ASIZOMEWE.

Nasisitiza kuwa katika mchakato huu tunamuunga mkono Rais Kikwete kwa sababu yeye pia ametuunga mkono kila mara tulipokuwa na madai ya msingi.

Ambacho tunataka watanzania wafahamu ni kuwa, tutasimama kidete kupigania haki katika bunge maalum, tutapigana kiume kuhakikisha maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya Warioba hayapuuzwi, tutasimama imara kuhakikisha kuwa chama kimoja CCM hakihodhi mchakato huu wa katiba. Na katika kufikia azma hiyo, hata kama kamera za Samweli Sitta zitawekwa 1000 tutatetea haki kila zitakapopindishwa, hatutakubali kuburuzwa, udikteta na kila njama za CCM.

Ifahamike kuwa, mchakato huu wa katiba siyo hisani ya CCM, ni haki ya watanzania kupata katiba inayokidhi matakwa yao, sisi tulioko Dodoma tuna kazi ya kuhakikisha matakwa ya wananchi yanatekelezwa na si kuyakwamisha au kuanza kuweka ujanja ujanja wa kutaka vyama vyetu vinufaike. Kama CCM wanadhani wanataka katiba yao, ni vema wakakutane kwenye mkutano mkuu wao waandike, Lakini kama wamekubali tuandike katiba ya watanzania wote lazima tuheshimiane, turidhiane na kukubaliana bila kutishana na kudharauliana.

Mungu Ibariki Tanzania!

J. Mtatiro,
Mjumbe - Bunge Maalum la Katiba.

No comments: