Thursday 11 February 2016

CHOTARA WA KIZANZIBARI ALIEJENGA HESHIMA YA TANZANIA

KUNA wanaoamini kuwa Dk. Salim Ahmed Salim (74) mwanasiasa na mwanadiplomasia maarufu nchini, ni ‘rais’ mzuri ambaye Tanzania haitakuja kumpata.
Ni kama Ghana wanavyosema kuhusu Kofi Annan, aliyepata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), kwamba walipata fursa ya kuweza kumfanya awe rais wao, na pengine angeweza kuja kuwa kiongozi wao mzuri, lakini kwa sababu ya siasa za ndani ya nchi yao, hilo limeshindikana.Ni vigumu kueleza baadhi ya mambo. Kwamba, mtu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kuwa Balozi maarufu zaidi wa Tanzania ( na pengine Afrika) katika UN na kuongoza tume na harakati ngumu na muhimu zaidi za kibara na kimataifa, kuonekana hafai kuongoza nchi kama Tanzania.Wiki iliyopita, kitabu kipya kinachomueleza Dk. Salim na maisha yake kama mwanadiplomasia na mwanasiasa: Salim Ahmed Salim: Son of Africa, kilizinduliwa rasmi jijini Dar es Salaam.

Kusema ukweli, si kitabu kwa maana ya kitabu. Ni mfululizo wa insha zilizoandikwa na waandishi tofauti; wakiwamo Watanzania wawili, Profesa Gaudence Mpangala na Dk. Lucy Shule, kueleza harakati za Dk. Salim katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ya utumishi.
Baada ya kusoma kitabu hicho, nimeona kwamba ni wazi Dk. Salim anahitaji kuandika kitabu kamili kuhusu maisha yake. Kama asipofanya hivyo, atakuwa amewanyima Watanzania, na dunia kwa ujumla, fursa nzuri ya kufahamu kile alichopitia na mafunzo anayoweza kuiachia dunia.Ni bahati mbaya kwamba, vitabu vya historia ya Tanzania vina mapungufu mengi. Mwanafunzi anayemaliza kidato cha sita nchini, anaweza kutoka shule pasipo kuwahi kusikia jina la nguli huyu.


Si historia inayomwambia mwanafunzi kuhusu mchango ambao Tanzania imeutoa kwenye Ukombozi wa Nchi za Kusini mwa Afrika, si historia inayoeleza mchango wa watu kama Salim, Kanali Ali Mahfoudh, Abdul Sykes, Laurean Kardinali Rugambwa, John Steven Akhwari na wengine.
Namna pekee ya kuweka historia hiyo vema ni kwa watu kama Dk. Salim kuacha maandishi yasiyofutika milele. Pengine, historia yetu itakuja kuwekwa vizuri na vizazi vijavyo.
Ni nani huyu Salim Ahmed Salim?
Kwa ajili ya kumbukumbu tu, huyu ndiye mwanadiplomasia aliyeweka rekodi ya kipekee katika historia ya Tanzania kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri akiwa na umri wa miaka 22 tu ! Tanzania haijawahi tena kuwa na balozi mwenye umri mdogo kama huo.
Wakati wa uzinduzi wa kitabu chake hicho, Dk. Salim aliwachekesha waliohudhuria kwa kuwapa mifano ya makosa aliyowahi kufanya kama balozi kutokana na kupewa nafasi hiyo bila kupitia mafunzo yoyote wala kuwa na uzoefu wa aina yoyote kabla wa masuala hayo.
Alisimulia kuhusu siku ambayo aliyekuwa Rais wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alipotembelea Misri. Kwa kawaida, Rais akitembelea nchi iliko na ubalozi, ni lazima balozi awe na Rais popote alipo.
Sasa Salim hakujua hilo. Yeye alikwenda kumpokea Mwalimu na baada ya kumfikisha hotelini alikofikia, alikwenda zake kulala nyumbani kwake! Ilibidi atafutwe baadaye lakini Mwalimu alimsamehe kwa vile alijua Dk. Salim alikosea kwa sababu hakuwa anajua.
Dk. Salim alikuwa balozi katika nchi za Misri, China na India. Wakati akisoma uchambuzi wa kitabu hicho, Profesa Issa Shivji, alisema kwa wakati huo, Misri, India na China zilikuwa na ushawishi mkubwa kwa Mwalimu.
Kwamba, kwa Mwalimu kumpeleka Salim kuwa balozi katika nchi hizo, kulimaanisha imani yake kubwa aliyokuwa nayo kwake. Wakati huo, viongozi wa juu wa nchi hizo tatu; Gamal Abdel Nasser, Jawahral Nehru na Mao Tse Tung, walikuwa miongoni mwa vinara wa kupinga ubeberu.
Ni katika nchi hizi tatu; ndipo Dk. Salim Ahmed Salim alipong’olewa meno yake ya utoto na kuingia katika dunia ya harakati na ya diplomasia ya aina yake.
Nyakati za Salim UN
Hatimaye, Mwalimu alimteua Salim kuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa mnamo mwaka 1970. Pamoja na nafasi hiyo, kwa wakati huohuo, akawa pia balozi katika nchi za Cuba, Barbados, Jamaica na pia Trinidad na Tobago.
Hata hivyo, akiwa na umri wa miaka 19, mnamo mwaka 1961, Salim alikuwa mwakilishi msaidizi wa chama cha kisiasa cha Zanzibar Nationalist (ZNP) nchini Cuba. Hicho kilikuwa chama cha kwanza cha kimapinduzi nje ya Cuba kufungua ofisi kwenye kisiwa hicho.
Dk. Salim alikuwa na wakati mzuri UN alipohudumu kwa muda wa miaka kumi. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, hicho ndicho kipindi ambacho “ kama mtu alikuwa ametoka nje ya ukumbi wa UN kwenda kuvuta sigara, alizima sigara na kukimbia kurudi ndani, aliposikia kwamba Tanzania inataka kuzungumza”.
Profesa Shivji anasema huo ndiyo wakati ambao mabeberu walikuwa wanagombana wenyewe kwa sababu ya sera za ubepari na ujamaa. Waafrika walikuwa wamejitambua na wanapigania utu na haki zao.
Dk. Salim, alikuwa mbele ya harakati hizi. Yeye alikuwa mmoja wa vinara wa kampeni kali za kutaka China ipewe nafasi ya kuwa mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo kuwa na haki ya kura ya turufu (veto).
Suala hilo lilikuwa la kijasiri kwa sababu lilikuwa likipingwa na mataifa yote ya kibeberu yakiongozwa na Marekani. Hata hivyo, Mtanzania huyu hakuhofu chochote na aliendelea na mapambano. Hatimaye China ikapata nafasi hiyo na Marekani ikamuwekea kinyongo Dk. Salim na ikaja kulipiza kisasi katika mwaka 1981. Hilo nitalieleza punde.
Salim alifanya kazi ya kusifika. Alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuondoa Makoloni Afrika (iliyokuwa na kazi ya kuhakikisha dunia inakuwa huru kwenye ukoloni wa namna yoyote).
Yeye na wenzake katika UN walipambana kuhakikisha Msumbiji na Angola zinakuwa huru. Alikuwa mtetezi wa Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM). Mwaka 1976, alikuwa Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Mwaka 1981, Salim alijitosa kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kama angefaulu, yeye angekuwa Mwafrika wa Kwanza kupata nafasi hiyo. Akiungwa mkono na nchi za Afrika, Asia na Amerika Kusini, wengi walimwona kama mgombea makini zaidi.
Lakini Marekani, ikiwa bado na shonde kwa kile kilichotokea nyuma wakati Salim akiongoza kampeni za China, akiwatetea akina Castro na akipambana na wakoloni wa Kusini mwa Afrika, wakaamua kumzuia.
Kwa mujibu wa kitabu cha Dr. Salim: Son of Africa, Marekani ilikuwa ikiweka pingamizi kila wakati wa upigaji kura ulipofika. Kwa mujibu wa taratibu za UN, Katibu Mkuu anapaswa kuungwa mkono na mataifa yote matano yenye kura ya turufu.
Mvutano huo, kitabu kinaeleza, ulidumu kwa muda wa wiki tano na huku kura zikirudiwa takribani mara 16. Lakini mara zote hizo, Marekani ikikataa.
Hatimaye, akidhihirisha tabia yake ya kutopenda mitafaruku, Dk. Salim aliamua kuondoa jina lake kwenye kinyang’anyiro hicho. Hakuna anayejua nini kingetokea endapo angeendelea na msimamo wake huo.
Kujitoa kwa Salim kukatoa nafasi ya historia mpya kuandikwa. Ingawa Marekani ilitaka raia wa Austria, Kurt Waldheim, achukue nafasi hiyo, waliomuunga mkono Mtanzania huyo wote wakahamia kwa raia wa Peru, Javier Perez de Cuellar na akaibuka mshindi.
Bara la Amerika Kusini likafanikiwa kutoa Katibu Mkuu kwa mara ya kwanza. Yote kwa sababu ya Dk. Salim.
Kilicho wazi, na kitabu hiki kipya kinasema hivyo, ni kwamba ile hatua ya Salim kujitokeza kuwania nafasi hiyo kulionyesha namna Waafrika walivyokuwa tayari kukabidhiwa madaraka makubwa. Kuongoza mataifa makubwa.
Ni yeye ndiye ambaye hatimaye alifanya iwezekane kwa Boutros-Boutros Ghali na baadaye Kofi Annan waje kuwa Makatibu Wakuu wa UN zaidi kidogo ya muongo mmoja baada ya Dk. Salim kujitokeza kwa mara ya kwanza.
Salim na siasa za Tanzania
Kuna sura maalumu kwenye kitabu hiki inayozungumzia mwanzo wa Salim katika siasa za Tanzania na athari zake kwake.
Baada ya kukaa kwenye duru za kidiplomasia kwa takribani miongo miwili, Salim alirejea Tanzania. Akawa Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Ulinzi na baadaye Naibu Waziri Mkuu.
Kitabu kinaeleza kuwa mara baada ya kifo cha ghafla cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, Mwalimu Nyerere alimteua Salim kumrithi Sokoine. Lakini Mwalimu alikuwa amelenga mbali zaidi ya uwaziri mkuu. Kama alivyokuwa akimuandaa Sokoine kumrithi, baada ya kifo, alihamishia fikra zake kwa Salim.
Alikuwa na walau sifa zote. Mzanzibari, muungwana, mwerevu na kijana kuliko Mwalimu. Kitabu kimeeleza yote hayo lakini kama ambavyo Profesa Shivji alikuja kueleza baadaye, kimeshindwa kueleza ilikuwaje Salim akashindwa kumrithi Nyerere?
Hilo ni somo ambalo Profesa Shivji amewahi kuliandika kwenye kitabu cha Pan Africanism or Pragmatism kinachoeleza kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Ingawa Profesa Mpangala na Dk. Shule hawakutaka kujiingiza kwenye undani wa nini hasa kilimkosesha Dk. Salim urais, Profesa Shivji alieleza kwenye kitabu chake hicho kwamba kulikuwa na harufu ya ubaguzi.
Kwenye uzinduzi wa kitabu hicho, Profesa Shivji ambaye alikuwa akitazamwa kwa makini na Dk. Salim mwenyewe wakati akizungumza kuhusu tukio hilo, alisema kuwa kwa bahati mbaya, ingawa Nyerere alikuwa akipiga vita siasa za kibaguzi, wenzake hawakuwa na imani hiyo.
Hivyo, kwa mujibu wa Profesa Shivji, watu hao wenye siasa finyu za kibaguzi, wakaja wakashinda na kumnyima Dk. Salim nafasi ambayo kwa hakika alistahili wakati huo.
Profesa Shivji alisema kukosa urais kwa Dk. Salim mwaka 1985 ni miongoni mwa mambo yanayohitaji kufanyiwa utafiti na kuelezwa vizuri zaidi kwa faida ya vizazi vijavyo.
Mapema mwaka huu, nilifanya mahojiano na mwanasiasa mwingine mkongwe, Gertrude Mongella, kuhusu jambo hili. Yeye alikuwa mmoja wa wanasiasa waliotajwa kuwa mstari wa mbele kuzuia Dk. Salim asiwe rais.
Kwa maelezo yake, aliniambia katika mahojiano yake na Raia Mwema, kwamba hakukuwa na ubaguzi kwenye tukio hilo isipokuwa kwamba kuliwekwa vigezo ambavyo vilimuondoa Dk. Salim kwenye kinyang’anyiro hicho.
Kuna mambo mawili nimejifunza katika sakata la Dk. Salim kushindwa kwenye urais na Ukatibu Mkuu wa UN. Lakini, nimepata wazo jipya kuhusu kwanini Nyerere aliruhusu chaguo lake lishindwe kupata urais.
Mara baada ya kumalizika kwa uzinduzi wa kitabu kile, mmoja wa wasomi maarufu nchini na ambaye amefahamiana na Dk. Salim kwa muda mrefu, aliniambia nje ya mkutano kuwa mwanadiplomasia huyo alikosa nafasi hizo mbili kwa sababu ya tabia zake.
Kwa sababu ni Dk. Salim Ahmed Salim.
Kwamba hapendi kugombana na watu. Hapendi kuweka maslahi yake binafsi mbele. Na hawezi kugombania jambo la kibinafsi kwa kutumia nguvu zake zote. Haya, kwa mujibu wa msomi huyo, ndiyo sehemu ya mapungufu ya Dk. Salim.
Kuna sehemu, kwenye kitabu hicho cha Dk. Salim, waandishi wanaeleza kuhusu mahojiano waliyowahi kufanya naye na wakamuuliza kwanini amekuwa kimya na hatoi matamko makali makali kama walivyo watu wengi wa hadhi yake. jibu lake lilikuwa rahisi na rahimu pia; “ Wakati mwingine, kukaa kimya nalo ni tamko”.
Kwenye siku za nyuma, niliwahi kupata bahati ya kuzungumza na Ami Mpungwe, aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini. Yeye ni mmoja wa wanadiplomasia waliowahi kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu Nyerere mara baada ya kustaafu kwake urais.
Mpungwe alitoboa siri ya kwanini Mwalimu hakutaka kuingilia kati wakati wahafidhina walipoungana kukataa Salim asiwe Rais wa Tanzania.
“ Siku moja niliwahi kukaa na Mwalimu na kumuuliza ilikuaje alishindwa kumfanya Dk. Salim awe mrithi wake. Alinijibu kwamba yeye alifanya hivyo kwa maslahi ya taifa. Alisema nilitaka kulazimisha lakini nikawakumbuka nyinyi vijana.
“Sikutaka kutengeneza Taifa ambalo Rais anayemaliza muda wake, anawalazimisha watu wamchague mtu anayemtaka yeye. Kama ningelazimisha kwa Salim, maana yake Mwinyi naye angechagua anayemtaka yeye. Ingekuwa tumetengeneza tabia mbaya kabisa,” Mpungwe alimnukuu Mwalimu.
Inaonekana, kanuni hii inafanya kazi hadi sasa. Inaaminika kuwa Mwinyi alipendelea John Malecela awe mrithi wake, ikashindikana. Benjamin Mkapa alipendelea hayati Abdallah Kigoda awe mrithi wake, ikashindikana. Jakaya Kikwete naye anafahamika kutaka Bernard Membe amrithi kwenye urais, lakini napo imeshindikana.
Pamoja na marais wanaomaliza muda wao kutofanikiwa kuwalazimisha wagombea wao washinde, bado Tanzania haikuingia kwenye machafuko.
Pengine, ni kwa sababu, Nyerere alianzisha utaratibu mzuri mwaka 1985, wakati alipokubali Dk. Salim Ahmed Salim akose urais.
Hii inaweza kuwa mojawapo ya hiba (legacy) ya Mwalimu Nyerere. Inaweza kuwa mojawapo ya mambo mengi ambayo Dk. Salim anahusika nayo lakini hayafahamiki kwa sababu bado hayajaandikwa vema.
Kwa bahati nzuri, Dk. Salim mwenyewe ameahidi kwamba atajitahidi kuhakikisha historia yake inaandikwa vema na kuhifadhiwa kwenye kumbukumbu zetu.
Itakuwa vibaya kama Watanzania hawatapata fursa ya kujua mawazo na mtazamo wake kuhusu miaka yake 50 ya utumishi wa Tanzania na Afrika.
Kwa namna hali ilivyo, na kwa sababu kizazi kijacho kinahitaji kujua yaliyowahi kuikuta Tanzania na watu walioitumikia kwa utumishi uliotukuka, Dk. Salim Ahmed Salim, hawezi tena kukaa kimya.
Tanzania inataka kusoma kitabu cha Dk. Salim Ahmed Salim. Kwa maneno na hisia zake. Inshallah siku hiyo itafika. - See more at: http://raiamwema.co.tz/dk-salim-ahmed-salim-mwana-wa-afrika#sthash.4FA8IPPU.dpuf

No comments: