Monday, 31 March 2014

WARIOBA AMSHUKIA SHIVJI

Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana.  Picha: Mwananchi
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana.
Picha: Mwananchi
Dar es Salaam. Mjadala wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar, Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba walikuwa na nia njema.Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa Zanzibar.“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi isijifiche,” alisema Jaji Warioba.“Na Shivji amechochea hilo… wote wale waliokuwa wanamnukuu walikuwa wanatoa hayo kwenye maandishi yake na kwamba mpaka leo hii kuna watu wa Zanzibar wanaamini Muungano huu si halali kisheria kutokana na Shivji ambaye alisema Baraza la Mapinduzi halikuridhia articles (ibara) za Muungano.”
Alipoulizwa jana usiku kuhusu tuhuma hizo za uchochezi na chanzo cha hisia za utaifa wa Uzanzibari na Utanganyika, Profesa Shivji alisema hawezi kujibu tuhuma hizo kwa kuwa hajamsikia Jaji Warioba akizungumzia hilo.“Hey, amezungumza lini?” alihoji. “Siwezi kujibu kwa kuwa sijamsikiliza mwenyewe.”Lakini Jaji Warioba alisema watu walitumia msingi huo kudai utaifa wa Zanzibar na kusisitiza kuwa Shivji amesababisha hisia za utaifa na kwamba haya yanayoendelea sasa yanatokana uchochezi huo.“Hata kabla ya sisi kuanza mchakato huu, Shivji alikwenda Zanzibar akazungumza na Baraza la Wawakilishi na akawaambia issue kwa Zanzibar ni self determination (kujitambua), Sasa leo anaona kama hatari ni Tanganyika, lakini yeye ndio amechochea nationalism (utaifa),” alisema Jaji Warioba.Kuhusu takwimu, Jaji Warioba alisema mara ya kwanza Profesa Shivji alizungumzia takwimu za Zanzibar kuhusu muundo wa Muungano akisema kuwa waliozungumzia suala hilo walikuwa 47,000, huku watu 27,000 wakitoka Tanzania Bara na 19,000 kutoka Zanzibar.  “Safari hii ametaja zile za Tanzania Bara na kusema hiyo ni figure (namba) ndogo sana ukilinganisha na watu 300,000 waliotoa maoni,” alisema Warioba. Alisema Tume ilitumia takwimu zinatokana na watu waliozungumzia suala ambalo wameliwekea asilimia na si kwa ujumla na ndio maana anaona Profesa Shivji anataka kupotosha kwa makusudi.
Warioba alimuelezea Profesa Shivji kuwa sasa ameamua kueneza propaganda za serikali mbili kwa kuponda Rasimu ya Katiba ambayo inaonyesha kuwa muundo wa serikali tatu ndio unaoifaa Tanzani kwa sasa.Aidha, Warioba alisema msimamo wa Profesa Shivji ni kwamba Zanzibar haikukosea kubadilisha Katiba mwaka 2010. “ Nimeshangazwa na Shivji kusema kwamba kitendo cha Zanzibar kubadili Katiba yao kuwa ‘Zanzibar ni Nchi’ halikuwa jambo la ajabu,” alisema Warioba.Alisema Shivji ni msomi ambaye anafahamu kitendo cha kubadilisha Katiba kilikuwa na madhara makubwa katika muundo wa Muungano.“Nadhani mnakumbuka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipoulizwa Bungeni kama Zanzibar ni nchi au siyo nchi, alijibu kuwa Zanzibar siyo nchi, vurugu zake mnakumbuka,” alisema.
Alisema lakini msomi kama Shivji haoni kama suala hilo la ‘Zanzibar ni nchi’ lina madhara makubwa katika mstakabali wa taifa letu.Jaji Warioba alisema kama serikali tatu hazitakiwi, basi kinachotakiwa kufanywa ni kwa Zanzibar kubadili Katiba yake ili iseme kwamba Zanzibar ni sehemu ya Muungano, vinginevyo haiwezekani. “Maana kama ni kusahihisha, ni lazima kwanza Katiba ya Zanzibar itumie maneno yale yale yaliyo kwenye Katiba ya Muungano. Yaani Zanzibar iwe sehemu ya nchi. Zanzibar wakubali hilo,” alisema. “Zanzibar wakubali Rais wa Muungano ana madaraka nchi nzima maana mabadiliko ya 2010 yamemuondolea Rais wa Jamhuri ya Muungano madaraka yake.” Akitoa mfano wa mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, Jaji Warioba alisema amekuwa akidai takwimu hazionyeshi uhalisia wa maoni ya wananchi. “Kwa mfano, Jimbo la Simanjiro linakuwa na watu 100,000 lakini waliojiandikisha kupiga kura ni watu 20,000 na waliopiga kura ni watu 15,000. Hii ina maana ushindi wake utakuwa katika watu waliopiga kura na siyo idadi ya watu wa Simanjiro,” alisema Warioba
Chanzo: Mwananchi

No comments: