Mbunge wa wa Chunya, Njelu Kasaka. Mbunge wa zamani wa Chunya, Njelu Kasaka, amekosoa mfumo uliopendekezwa na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wa kutumia kura za siri na ya wazi kuwa ni udhaifu mkubwa.Aidha, amehoji kwanini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaogopa kura ya siri wakati kimekuwa kikijipambanua kuwa ni chama kikubwa na chenye wasomi. Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV, alisema alitegemea CCM ambacho ni chama kikongwe kingeongoza mambo yaende vizuri katika Bunge hilo ikiwa ni pamoja na kukubali itumike kura ya siri.“CCM ni chama kikubwa, kina wanachama wengi, wajumbe ni wengi Bungeni na kinajiamini kinaendesha mambo yake kihalali, kinaogopa nini kura ya siri, kama unafanya mambo yako halali una wanachama safi kwa nini uogope,” alihoji Kasaka. Kasaka ambaye aliwahi kuwa mkuu wa mkoa na naibu waziri, alisema mvutano uliopo katika Bunge hilo unatokana na baadhi ya watu ambao wanataka mambo yao yafanikiwe hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015.
Alisema kama viongozi wa CCM wanataka kutengeneza katiba ili waendelee kukaa madarakani, hilo ni kosa kwani wananchi wanataka katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa wote.“Mfano CCM wameingia na msimamo wa serikali mbili, hii kosa sababu tayari unakuwa umeunda katiba ukiwa nje ya Bunge, Rasimu ya Katiba imetokana na maoni ya sasa inapotokea unasema wamekosea basi usingekuwa na haja ya kuwauliza,”alisema. Alisema utaratibu wote ambao unatumika katika mikutano katika uchaguzi wa vyama ni kupiga kura ya siri hata katika kumchagua diwani, mbunge, rais na mwenyekiti. Alisema inashangaza kuona baadhi ya wanachama wa CCM wanataka kura ya wazi jambo ambalo linatia wasiwasi kama Katiba itapatikana kwa wakati. Kasaka aliwashangaa baadhi ya viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri ambao wanaita baadhi ya makundi pembeni kuzungumza nao kuwashawishi, jambo ambalo alisema ni hatari kwa mstakabiri wa nchi.
“Kura ya wazi ina madhara, nimekuwa kiongozi ndani ya chama na serikali, ninaelewa mkianza kupiga kura ya wazi kama wakubwa zako hawataki kitu fulani ukapiga tofauti wataanza kusema huyu si mwenzetu na watakufukuza,”alisema. Aliongeza kuwa tatizo Tanzania ni kuwa watu wana nidhamu ya uoga, wenye ujasiri ni wachache, na kimsingi watu wanachukuliwa hatua wakienda kinyume na misimamo ya chama chao. Alisema mvutano unaendelea hivi sasa katika bunge hilo umetokana na hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa na kueleza msimamo wa chama chake kutaka muundo wa serikali mbili. Kasaka ndiye aliyeongoza kundi la wabunge 55 maarufu kwa jina la G55 waliojenga hoja bungeni mwaka 1993 na kuilazimisha serikali ikubali kuundwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya Muungani, ingawa uamuzi huo ulizimwa baadaye na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
No comments:
Post a Comment