HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI
BUNGENI, MHE.GODBLESS JONATHAN LEMA (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI
RASMI YA UPINZANI BUNGENI KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/2014
NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI KWA
MWAKA WA FEDHA 2014/2015.
1.
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa ‘Instrument’ ya Serikali inayoainisha
majukumu kila Wizara, Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi imepewa majukumu ya
kushughulikia masuala ya Usalama wa Raia, Uhamiaji na utekelezaji wa Sera za
zima moto na uokoaji. Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inashugulikia pia
masuala ya huduma za Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji, Uraia, Vitambulisho
vya Taifa, Huduma za Wakimbizi, Usajili wa Vikundi au Vyama vya Kijamii, Huduma
za Zima Moto na Uokoaji na mambo mengine yanayohusu maendeleo ya rasilimali
watu katika Wizara hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Ukitazama majukumu ya
Wizara hii, utaona kwamba ina majukumu mazito sana
yanayohusu usalama wetu sote kama raia wa nchi
hii. Ni majukumu yanayohusu maisha yetu. Hivyo wizara hii inatakiwa iwezeshwe sana kibajeti ili iweze
kutekeleza majukumu yake ipasavyo ili wananchi na hata wageni waliopo katika
nchi yetu waweze kuishi kwa usalama na amani.
Kwa kuwa Wizara hii ina taasisi chini yake zinazohusika na ulinzi wa maisha ya watu na mali zao, hivyo ni Wizara
inayotakiwa kufuatiliwa na kusimamiwa kwa karibu sana.
2. MAPITIO YA
UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
Katika bajeti ya
Wizara hii kwa mwaka wa fedha unaomalizika
wa 2013/2014 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliitaka Serikali kufanya mambo
kadhaa ili kuboresha mapungufu
tuliyoyaona katika katika kipindi hicho. Mambo hayo ni:
i.
Kuchukua hatua kali
na madhubuti ya kukabiliana na matukio yenye sura ya ugaidi kwa mfano
kulipuliwa kwa bomu Kanisa Katoliki
katika Parokia ya Olasiti huko Arusha,
kuchomwa moto kwa makanisa huko Zanzibar na Dar es Salaam, Mapadre kuuwawa na Mashehe kumwagiwa
tindikali Arusha na Zanzibar na matukio yanayofanana na hayo.
ii.
Kuongeza posho ya
chakula (Ration allowance) kwa askari wa Jeshi la Polisi ili walau posho hiyo
ishabihiane na posho ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili
waweze kukabiliana na ugumu wa maisha. Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za bunge
(hansard) Waziri wa Fedha wa wakati huo Marehemu William Mgimwa alikubali posho
ya chakula ya shilingi 225,000/= kwa mwezi kwa kila askari. Taarifa tulizo nazo
ni kwamba posho hiyo haijalipwa mpaka leo. Je, askari waandike deni au wahesabu
kwamba wamedhulimiwa?
iii.
Kutoa mwongozo kwa maafisa
wa Jeshil la Polisi na Magereza juu ya marekebisho ya sheria kuhusu umri wao wa
kustaafu ambapo marekebisho ya sheria yaliongeza umri wa kustaafu kutoka miaka
50 kwenda miaka 55 kwa maafisa wa Polisi na kutoka miaka 55 kwenda miaka 60 kwa akari wa Magereza.
iv.
Kuondoa urasimu na
utaratibu kandamizi katika Jeshi la Magereza kuhusu Mpango wa kujiendeleza
kielimu kwa maafisa wa Magereza. Tuliitaka Serikali kufanya hivyo kwa kuwa, kwa
mujibu wa General Service Order (GSO) na sheria nyingine za kazi, mtu akiajiriwa
kwa mara ya kwanza (first appointment) na akataka kujiendeleza kimasomo nje ya
kituo chake cha kazi anatakiwa kukaa
kazini kwa muda wa miaka miwili au mitatu ndipo aweze kuomba ruhusa ya kwenda
masomoni. Lakinini tulipokea malalamiko kutoka kwa maafisa wa Magereza kwamba
sheria hiyo haifuatwi na badala yake maafisa hao wanatakiwa wakae miaka sita
kazini ndipo wapewe kibali cha kujiendeleza kimasomo.
v.
Kujenga nyumba za Askari
wa Magereza ili kuboresha mazingira yao ya kazi
na kuwafanya wasijisikie kama vile na wao ni
wafungwa.
vi.
Kuchukua hatua ya
kupunguza msongamano wa wafungwa na
mahabusu Magerezaji
vii.
Kuboresha lishe na
huduma za afya kwa Wafungwa na Mahabusu Magerezani
viii.
Kuongeza fedha kwa
ajili ya ununuzi wa vifaa vya zima moto na uokoaji kwa Jeshi la Zima Moto na
Uokoaji
ix.
Kuwachukulia hatua
askari wa Jeshi la Polisi wenye vyeo vya juu wanaowanyanyasa askari wa vyeo vya
chini.
x.
Kuacha kulitumia
Jeshi la Polisi vibaya kwa ajili ya
kulinda maslahi ya kisiasa ya CCM
xi.
Kuwachulia hatua kali
za kisheria viongozi wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali waliotoa kauli
za vitisho kwa waandishi wa habari walioandika habari za unyanyasaji unaofanywa
na Jeshi la Polisi
xii.
Kutoa ukomo wa muda
ambapo kila raia wa Tanzania
atapatiwa Kitambulisho chake cha Taifa na kuainisha ghrama zilizotumika katika
mchakato wa kutengeneza vitambulisho vya Taifa.
xiii.
,Kudhibiti kuzagaa
kwa silaha za moto ambazo hutumika katika matukio mengi ya kijambazi.
xiv.
Kuchukua hatua kali
kwa watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini
xv.
Kuchukua hatua
madhubuti za kupunguza matukio ya ajali barabarani ambayo yamepoteza maisha ya
wananchi wengi sana
wakiwemo polisi pia.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa taarifa ya utekelezaji wa masuala niliyoyataja
hivi punde wakati wa majumuisho ya bajeti ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama
ya Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi fungu 51 na randama za taasisi zilizoko
chini yake yaani Fungu 93(Idara ya Uhamiaji); fungu 28(Jesh la Polisi); fungu
29 (Magereza) na fungu 14 (Idara ya Zima Moto) hadi kufikia mwezi Machi, 2014
Wizara na taasisi zilipata mgawo wake wa kibajeti kwa wastani wa asilimia 70
isipokuwa idara ya zima moto na uokoaji ambayo ilipata asilimia 46.3 tu ya
fedha zilizoidhinishwa. Aidha kwa Mujibu wa Randama ya Jeshi la Zimamoto, fungu
14 (uk. 2) katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 hakuna fedha yoyote
iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa Jeshi la Zima Moto.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Randama
hiyo, huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji
kutotengewa fedha kwa ajili ya miradi ya Maendeleo. Kutokana na hali hiyo,
Jeshi hilo limeshindwa kuendeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu –
TAZARA, Dar es Salaam, kushindwa kukarabati na kujenga vituo vipya vya
zimamoto, kushindwa kununua vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vifaa vya maokozi
na vifaa vya kuzimia moto.
Mheshimiwa Spika,
Sote ni mashahidi wa
majanga ya moto, maghorofa kuporomoka, meli kuzama, mafuriko na kila aina ya
majanga ambapo idara ya zima moto imekuwa ikishindwa kufanya chochote na hivyo
kuwaacha wananchi wakiangamia katika majanga hayo. Kambi Rasmi ya Upinzani inashawishika kuamini
kwamba Serikali haina nia njema na usalama wa raia na ndio maana haitengi fedha
hata senti moja katika miradi ya maendeleo ya Jeshi la Zima Moto. Kama Serikali
haioni umuhimu wa Jeshi la Zima Moto ni bora kulifuta kuliko kuliacha wakati
hailiwezeshi kufanya kazi yake.
3.
HALI YA
USALAMA NCHINI .
Mheshimiwa Spika ,
Hali ya Usalama Nchini imeendelea kuwa tete
kutokana na sababu mbalimbali. Utafiti wa kiufuatiliaji uliofanywa na Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ni kwamba; sababu zifuatazo zinazorotesha hali ya
usalama na amani hapa nchini.
i.
Ukosefu
wa Ajira na Kazi zenye Kipato kwa Jamii.
Mheshimiwa
Spika,
Ukosefu wa
kazi na ajira kwa Jamii umekuwa ni sababu moja ya msingi kabisa ya kuendelea
kuhatarisha hali ya usalama na amani Nchini. Wananchi wengi hususan Vijana
wamekuwa hawana uhakika wa ajira. Mbali
na hofu na wasiwasi mkubwa walio nao, vijana hawa kutokana na kutojua hatima ya
maisha yao, bado Serikali imeendelea kuwasakama katika shughuli zao ndogo
ndogo. Kitendo cha Serikali kuwafukuza mijini vijana wajasiriamali wanaofanya
biashara ndogondogo kumesababisha vijana hawa kushindwa kabisa kuweza kumudu
hata mlo mmoja kwa siku. Jambo hili limewakatisha tamaa vijana wengi na matokeo
yake ni kwamba baadhi yao wanajiingiza katika matukio ya kihalifu ili waweze
kumudu maisha yao.
Mheshimiwa Spika,
Ili kujenga mazingira ya usalama, amani na utulivu
katika nchi yetu, ni lazima sasa Serikali itambue wajibu wake wa kukuza uchumi
na biashara kwa kasi ili kuongeza ajira na kazi zenye tija kwa jamii kwani kuachia Jeshi la Polisi kudhibiti hali ya ulinzi na
usalama katika Taifa ambalo asilimia 80% ya Vijana wake wanarandaranda mitaani
bila kuwa na kazi zenye uwezo wa kukidhi mahitaji yao muhimu ni hatari kubwa sio tu kwa walinzi
hawa wa amani bali pia kwa taifa zima.
Mheshimiwa Spika,
Hivyo ni
muhimu tukafahamu kwamba propaganda na tathimini feki kuhusu ukuaji wa uchumi zinazotelewa
kila mwaka na Serikali wakati Watu wengi
wanaendelea kuishi maisha yasiyo na matumaini na wengine wakishindwa kufurahia
ajira na kazi kwa sababu ya masilahi
duni na mfumuko wa bei za bidhaa unaosababishwa na uchumi kushuka kila mwaka,
bila shaka sasa ni kweli kabisa kuwa hali ya usalama Tanzania ni tete na Jeshi
Polisi haliwezi kujipanga kushindana na
kundi kubwa la jamii iliyojaa hasira na kupoteza matumaini na maisha .
ii.
Maslahi
ya Askari wetu katika Muktadha wa Hali ya Usalama Nchini.
Mheshimiwa
Spika,
Maisha ya
Askari wa Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto ni miongoni mwa kundi katika
jamii ambalo linaishi maisha ya umasikini wa kupindukia sana. Nyumba zao,
mishahara yao na masilahi yao mengine mbali mbali bado ni duni kiasi kwamba Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaona kuwa ni kebehi
na dharau kubwa sana kwa vikosi vya ulinzi na usalama .
Mheshimiwa
Spika,
Kazi ya
Jeshi ni wito. Ni hatari kubwa sana kuwa na Askari ambao wanafanya kazi bila
wito kwa sababu walikosa matumaini kwingineko, hivyo wakachagua kujiunga na
Jeshi kama sehemu ya biashara.
Mheshimiwa
Spika,
Ni ukweli usiopingika kuwa Askari wengi wanafanya
kazi kwa moyo uliovunjika na kupondeka. Aidha, wana msongo mkubwa wa mawazo
sababu ya ugumu wa maisha. Hali hii inaondoa
uimara wa majeshi yetu haya kwani Jeshi imara sio tu kuwa na silaha za kisasa peke yake bali ni muhimu pia kuwa na askari wanaoona
fahari kulinda raia na mali zao kama wajibu uliotukuka. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali kutambua na kuthamini kazi inayofanywa na askari wetu
ambao ni sehemu ndogo ya jamii iliyojitoa mhanga kufanya kazi za hatari hata
kwa maisha yao ili kuwalinda raia na mali zao
iii.
Rushwa
na Uadilifu kwa Jeshi la Polisi
Mheshimiwa
Spika,
Jeshi la Polisi limekuwa likitajwa kuwa kinara wa
rushwa na chanzo cha biashara nyingi haramu. Jambo hili zio zuri hata kidogo
kwa chombo kilichokabidhiwa jukumu la kuwalinda raia na mali zao. Hata hivyo,
tafiti nyingi zinaonesha kwamba mazingira mabaya ya maisha yao yaliyojengwa
katika maslahi duni ni miongoni mwa
sababu zinazowasababisha kuingia katika tabia hii mbaya ambayo ni hatari kwa
usalama wa Nchi .
Mheshimiwa
Spika
Rushwa ndani ya Majeshi yetu ya ulinzi na
usalama ni majaribu yanayo sababishwa na Serikali yetu. Hii ni
kwa sababu mishahara na makazi ya askari
wetu ni duni, vitendea kazi vichache na duni jambo linalochangia kwa kiasi
kikubwa kuwa na askari wasio na
ari na shauku ya kazi ya ulinzi na usalama.
Matokeo yake wanakosa nidhamu ya kazi na hivyo kujiingiza kwenye vitendo viovu
ikiwemo rushwa na unyanyasaji wa raia. Ili kuwa na askari wenye nidhamu ya
kazi, ni lazima kuwa na Serikali inayojua na kuthamini wajibu mkubwa wa vikosi
vya ulinzi na usalama katika taifa. Kama vile Serikali inavyotoa mishahara
mikubwa kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)na Benki kuu ili
kuwapa motisha wasiibe, vivyo hivyo Serikali ingeona umuhimu wa kuwalipa na
kuwatunza vyema askari wa vikosi vya
ulinzi na usalama kwa kuwa na askari wanaofanya kazi kwa moyo uliopondeka ni
hatari kwa ukuaji wa uchumi na usitawi wa wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa
Spika,
Kitendo cha Serikali kupuuza maslahi mbalimbali
ya askari wetu ni kuwaingiza katika majaribu mbalimbali ikiwemo rushwa,
ukandamizaji na unyasaji dhidi ya raia wanaopaswa kuwalinda. Ifahamike kwamba
kuwaingiza watu majaribuni ni dhambi. Aidha majaribu ya kumfanya mtu atende
jambo baya yanahesabika kuwa ni dhambi. Ni katika muktadha huu, hata Bwana Yesu
alipokuwa akiwafundisha wanafunzi wake kusali, aliwaambia wamwombe Mungu
wakisema “….Usitutie Majaribuni bali
utuokoe na Yule mwovu” Kwa hiyo Mheshimiwa Spika, Dhamira isiyokuwa na utu
ya Serikali hii CCM juu ya usitawi wa nchi hii na watu wake ndio chanzo kikubwa
cha askari wetu na wananchi wengine kuingia katika majaribu ya rushwa na aina
mbalimbali za uhalifu.
Mheshimiwa
Spika,
Ni kweli inawezekana kabisa binadamu akawa
muadilifu bila kuwa na masilahi bora katika jamii, lakini vile ni ukweli
usiopingika kwamba umasikini na hali duni ya maisha ndio unachangia kwa kiasi
kikubwa kuondoa uadilifu na uimara wa nidhamu katika kukabiliana vishawishi vya
rushwa na mambo mengine machafu yenye sura hizi.
Mheshimiwa
Spika,
Kutokana na Serikali kuwa ndio mlezi wa rushwa,
imekosa mamlaka ya kiuadilifu (moral authority) wa kukemea vitendo vya rushwa
vinavyofanywa na taasisi mbalimbali zilizo chini yake. Kwa mfano kwa mujibu wa
vyombo vya habari na kwa mujibu wa mjadala wa bajeti ya Serikali unaoendelea
bungeni imeibuliwa kashfa ya wizi wa fedha zaidi ya shilingi bilioni 200 ambapo
Viongozi Wakuu wa Serikali wamehusishwa. Katika jambo kama hili, Serikali
inatoa wapi nguvu na sauti ya kukemea rushwa
katika taasisi inazoziongoza kama vile
jeshi la Polisi .
Mheshimiwa
Spika,
Kama wanaopaswa kukemea na kuzuia rushwa ni wala
rushwa, ni wazi moja kwa moja kuwa,
utamaduni wa kupokea rushwa na kula rushwa katika taasisi zote za Serikali ni
jambo la Kawaida, na linaoipendeza Serikali ya CCM. Kwa hiyo, hakuna hata
Kiongozi mmoja mwenye mamalaka ya kiuadilifu kukemea jambo hili, kwa kuwa familia
zao zinaishi, zinasoma na kufurahia
maisha kwa ajili ya ufisadi, wizi
wa mali za Umma na rushwa .
Mheshimiwa
Spika,
Kwa dhati kabisa, Kambi Rasmi ya Upinzani inaikemea
Serikali kujenga mazingira ya rushwa kwa askari wetu. Kwa mfano kitendo cha
Serikali hii ya CCM kukigeuza kitengo cha Askari wa Usalama Barabarani kuwa
kitengo cha ukusanyaji mapato kwa makosa ya kutafutiwa na kulazimishiwa
barabarani ni rushwa iliyowekewa mfumo rasmi. Jambo hili ni hatari sana kwa
sababu rushwa ya aina hii haiwezi kumalizika kwa kuwa ina baraka za Serikali.
Hali ni mbaya zaidi kwa kuwa katika
kutekeleza jukumu hilo la askari kukusanya mapato, utaratibu umewekwa ambapo
kila askari anatakiwa kutafuta kwa bidi, kulazimisha na kukamata makosa
yasiyopungua sita mpaka tisa na kuyatoza faini. Mfumo huu mpya wa Serikali wa
ukusanyaji wa mapato umeifanya rushwa barabarani kuwa rasmi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inafahamu kwamba Serikali
imeishiwa fedha, lakini tunaisihi sana isitumie njia za ukandamizaji na uonevu
kujikusanyia mapato.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya kuacha jukumu lao la msingi la kusimamia
sheria za barabarani na kuanza kukusanya mapato, ajali za barabarani
zimeongezeka sana. Kwa mujibu wa Ripoti
ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013, jumla ya ajali za barabarani zilizohusisha
magari katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Pwani, Kilimanjaro, Arusha
na Morogoro zilikuwa ni 459,931, na
ajali hizi zilisababisha vifo vya
watu 2,408 na majeruhi 16,040. Kwa upande wa bodaboda watu
waliofariki kutokana na ajali ni 1,106 na
majeruhi 6,581.
Mheshimiwa
Spika,
Ripoti ya Haki za Binadamu ya 2013, inasema
kwamba nchi inapata hasara ya kati ya asilimia 1 hadi 2 ya Pato la Taifa (GDP)
kutokana na ajali za barabarani. Kwa hiyo, uamuzi wa Serikali wa kukifanya kikosi cha usalama barabarani kuwa kitengo cha
ukusanyaji mapato umekuwa ni hatari kubwa kwa maisha ya raia na uchumi wa nchi.
iv.
Ukandamizaji,
Ukatili na Uonevu Unaofanywa na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika
Hivi
karibuni kumekuwa na matukio ya mahubusu
kugoma kula , kuvua nguo hadharani na
mambo mengine yakusikitisha ili kuonyesha hisia zao juu ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa
dhidi yao. Madai makubwa ya mahabusu hao ni kwamba wanapata mateso makubwa
gerezani kwa makosa ambayo wengi wao hawajayatenda. Hii maana yake ni kwamba
Mahabusu wengi katika magereza yetu wamebambikizwa kesi jambo ambalo ni kinyume
kabisa na utawala wa sheria na haki za binadamu.
Mheshimiwa
Spika,
Ili kuondoa mwanya uliopo hivi sasa wa Polisi
kuwabambikiza raia kesi na kuwaweka mahabusu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali kufanyia marekebisho sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai
ili kuondoa fursa kwa baadhi ya askari wenye nia mbaya kutumia madaraka yao
kuwabambikizia watu kesi kutokana na chuki au sababu nyingine. Kwa mfano, kijana mmoja wa Arusha, aliingia
katika ugomvi wa mapenzi na askari polisi kwa sababu ya kumgombania binti.
Askari yule alitengeneza mazingira kwa kijana yule kumbakiziwa kesi ya wizi wa
kutumia silaha na mauaji na kuswekwa rumande. Kijana huyo wakati alipokuwa
anaendelea kuteseka mahabusu, yule askari alimwoa mwoa yule binti. Baadaye
askari huyo na binti huyo ambaye sasa ni mke wa yule askari wakaenda Magereza
kumtembelea yule kijana aliyekuwa mahabusu kwa uonevu kama ishara ya kuonyesha
umwamba!!!!!
Mheshimiwa
Spika,
Mambo kama haya hayana idadi katika magereza
zetu. Ni mengi. Uonevu na unyanyasaji unaofanywa na askari wetu katika kila
kona ya nchi yetu ulijidhihirisha pia bomu lilipolipuliwa katika mkutano wa CHADEMA wakati wakuhitimisha kampeni za
marudio ya Udiwani mwaka jana ambapo
watu wanne walifariki Dunia na wengine wengi zaidi ya 100
kujeruhiwa vibaya wakiwemo watoto wadogo
na Wanawake.
Mheshimiwa
Spika,
Tuna
ushaidi wa kutosha juu ya ni nani
alihusika na mlipuko huo wa bomu. Licha ya kuwa baadhi ya polisi walihusika na
mlipuko huo; Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilimtaka Rais mara nyingi aunde
tume ya Kijaji kwa ajili ya uchunguzi wa suala hili kubwa lakini hakufanya
hivyo mpaka sasa. Badala yake kumekuwa
na kejeli nyingi na mizaha juu ya suala hili hatari kwani waliokufa kwenye
mkutano wa CHADEMA wanaonekana hawana tofauti na mbuzi au Kondoo.
Mheshimiwa
Spika,
Sisi
walengwa tuliotaka kuuwawa tunafahamu uchungu na mashaka tuliyo nayo dhidi ya
maisha yetu. Hata hivyo mnaweza kuendelea kudharau jambo hili kwa sababu bado
Utawala na Mamlaka yenu yanaendela kuelekeza, kupanga na kuendesha Nchi. Lakini jambo dhahiri ni kwamba; mateso haya,
damu hizi, uonevu huu utafika mwisho na kama nyie hamtakuwepo basi watoto wenu
watakuwepo na ndugu zenu wengine watakuwepo kushuhudia ukomo wa ukandamizaji,
utesaji, uuaji na udhalimu huu dhidi ya raia wasio na hatia.
Mheshimiwa Spika,
Ni jambo la kusikitisha sana kwamba waliotaka
kutuua pia waliendelea kupanga mipango ya kutubambikia kesi hiyo ya mauaji na
ugaidi. Lakini Mungu akawa mwema,
walikamatwa vijana wengi, wamepigwa, wameteswa na wengine sina uhakika kama
wataweza kuwa na uwezo wa Nguvu za kuzaa tena tena kwa jinsi ya simulizi zao
walivyofanyiwa ukatili wa ajabu na wote walilazimishwa kumtaja Mbunge wa Arusha
Mjini Godbless Lema viongozi waandamizi wa CHADEMA kuwa ndio waliohusika na
mlipuko wa mabomu Kanisani Olasiti na kwenye Mkutano wa kufunga Kampeni za
Udiwani za CHADEMA mwaka jana.
Mheshimiwa
Spika ,
Katika
vijana hawa waliopatiwa mateso makali baadhi yao walitolewa gerezani wakiwa na
kesi nyingine na wakaelekezwa , wakapigwa , wakateswa na wengine kutishiwa
kuuwawa wakubali kuwa mipango ya milipuko ya mabomu kanisani Olasiti na kwenye Mkutano wa CHADEMA
yaliratibiwa na Mbunge wa Arusha Mjini na viongozi wakuu wa CHADEMA. Kwa
tafsiri hii, inaonekana kwamba; waliolipua bomu katika Kanisa la Olasiti, ndio
hao hao waliolipua bomu katika mkutano wa CHADEMA. Hii ni kwa sababu badala ya
polisi kutawatafuta wahalifu hao na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria,
wanahangaika kutafuta watu wa kuwabambikizia kesi kulipua bomu kanisani ili
wawaunganishe na tukio la mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA. Kwa sababu
wanawatafuta watu wa kuwabambikiza kesi ni dhahiri kwamba Serikali inajua
undani wa tukio hilo.
Mheshimiwa
Spika,
Uadilifu wa Jeshi la Polisi umeendelea kuwa
mashakani kwani baada ya Uchaguzi mdogo
wa Jimbo la Arumeru Mashariki , Kijana mmoja Kiongozi wa CHADEMA wa Kata ya Usa
river Msafiri Mbwambo aliuwawa kwa kuchinjwa shingo. Wauwaji
wale walikamatwa na Jeshi la Polisi lakini cha kusikitisha ni
kwamba baada ya muda mfupi
wahalifu hawa waliweza kutoroka
mbele ya Polisi kwenye chumba cha mahakama
wakiwa wamefungwa pingu eti nakufanikiwa kumpora Askari Bunduki aina ya
SMG na kukimbia nayo mpaka leo hawajaonekana wakiwa na pingu zao . Mheshimiwa
Spika, huu ni upumbavu usiofikirika.
Mheshimiwa
Spika
Hata wewe unaweza pia kuziba masikio yako kana kwamba hiki
kinachosemwa ni “blues” na ngojera lakini Mungu yule unayemfuata Kanisani kila
asubuhi kumuomba amesikia na yuko kazini .
‘Only Time will tell’.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mujibu
wa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2013 (uk.22) watu 23 waliuwawa na vyombo
vya dola kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2013. Kuna mateso makubwa wanayopitia
wananchi kutokana na uonevu wa askari wetu.
Wanalia machozi mazito lakini hakuna msaada kwani Serikali inayopaswa
kuwatazama na kuwalinda raia wake dhidi ya ukandamizaji huu , Serikali hiyo
imepoteza ladha ya utu kwa hiyo kelele na mateso wanayopata Watu kwa
kubambikiziwa kesi na kuwekwa mahabusu na kufungwa miaka mingi na kuuwawa,
mateso hayo sasa yamegeuka kuwa laana kwa Nchi yetu.
v.
Polisi Jamii
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani ina mtazamo kwamba ni vema kuwajengea wananchi utamaduni wa kuripoti
matukio ya kihalifu kwa Jeshi la Polisi kuliko kuanzisha taasisi nyingine isiyo
rasmi ndani ya Jeshi la Polisi. Tunatambua kwamba Jeshi la Polisi limeanzisha mfumo
huu wa Ulinzi shirikishi kwa sababu ya uchache wa askari iliyo nao. Katika
Randama ya Jeshi la Polisi, fungu 28, mojawapo ya changamoto zilizotajwa ni
uchache wa askari Polisi. Kwa mujibu wa randama hiyo, idadi ya askari
inayohitajika nchini kwa kiwango cha kimataifa ni 90,000 wakati waliopo sasa
hawafiki nusu ya idadi hiyo. Aidha,
Jeshi la Polisi linapata ugumu wa kupata taarifa za kihalifu kutoka kwa
wananchi kwa sababu ya uadui uliojengeka kati ya wananchi na Jeshi la Polisi .
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni Bungeni inaitaka Serikali kuongeza ufanisi katika matumizi
yake ya fedha, kuzuia ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma, kuwajengea
wananchi uwezo wa kiuchumi ili fedha zitakazopatikana zitumike kuajiri askari
ambao ni wataalamu wenye uwezo wa kuwalinda raia na mali zao badala ya kurasimisha
mfumo usio rasmi wa polisi jamii ambao wengi wao ni green guards wa CCM.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, inalaani Jeshi la Polisi kupuuzwa huko Zanzibar kwa kuvipa
mamlaka zaidi dhidi ya Jeshi la Polisi vikosi vya KMKM, JKU na KVZ katika
kusimamia shughuli za Ulinzi na Usalama wa Zanzibar. Jambo hili limeondoa
mamlaka ya Jeshi la Polisi ambalo lina wajibu wa kulinda raia na mali zao
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
vi.
Uchochezi wa Kidini na Kikabila
Mheshimiwa Spika,
Tatizo la udini na
ukabila katika taifa hili linaonekana kuendelea kukomaa. Lakini ni tatizo
ambalo halitamwacha hata mmoja wetu salama. Ni tatizo ambalo hakuna mshindi
atakayepatikana. Ni tatizo ambalo hata kama litaisambaratisha nchi, hata wale
watakaofanikiwa kuikimbia nchi hawatakuwa salama huko wanakokwenda kwa sababu
watakuwa bado na imani zao na chuki hiyo dhidi imani nyingine itaendelea popote
watakapokuwa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile jambo hili
linatishia usalama mpana wa taifa hili, ni vema sasa Serikali ikatafakari upya
na kuleta sheria mpya itakayokataza na kuwawajibisha kwa nguvu zote wale wote
watakaojaribu hata kwa maneno kueneza chuki au ubaguzi dhidi ya dini, kabila au
rangi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iombe radhi na kuwaondoa
madarakani viongozi wote wa Serikali walitotoa kauli za uchochezi wa kidini,
kikabila na rangi.
4. MAHUSIANO YA
SERIKALI KATIKA BIASHARA HARAMU YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, haina sababu ya kupoteza muda eneo hili kwani ni ukweli
usiopingika kuwa biashara hii inafanywa na viongozi wakuu wa Serikali, hivyo basi waamue wao wenyewe kama wangependa kuendelea kuwa sehemu ya
mateso na mauaji ya vijana wetu katika
jamii ya watu inaowaongoza.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya
Upinzani imelazimika kufikia uamuzi huu kwa kuwa viongozi wakuu wa nchi hii
walishakiri hadharani kuwa wanawafahamu kwa majina watu wanaojishughulisha na
biashara hii. Ni ajabu na ni kituko kama Rais wa Nchi ambaye ndiye amiri jeshi
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama anaogopa kuwataja wafanyabiashara haramu
wa dawa za kulevya ambao alisema kuwa anawafahamu kwa majina. Tunashawishika
kuamini kwamba bila shaka watu hao ambao mpaka Rais anagwaya kuwataja watakuwa
ni malaika kutoka mbinguni au Mungu.
Mheshimiwa Spika,
Ni
vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao
ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za
kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa
na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea
kulifumbia macho jambo hili ni kulihujumu taifa na huo ni usaliti mkubwa.
MAUAJI YA RAIA NA POLISI
Mheshimiwa
Spika,
Toka mwaka 2011 katika hotuba zetu kuhusu Wizara
hii tumeendelea kuonesha mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola
likiwemo Jeshi la Polisi. Wakati akihitimisha hoja yake hapa Bungeni Mhe.
Waziri Mku Mizengo Pinda aliahidi mbele ya Bunge lako tukufu kuwa serikali
ingeunda Mahakama ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo hivyo kwa mujibu wa
Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye utata (Inquest Act).
Mheshimiwa
Spika,
Serikali ilirudia kutoa ahadi ya kuanzisha Mahakama
hiyo ya Korona kwa ajili ya kuchunguza vifo vilivyosababishwa na Operesheni ya
kuondoa Majangili “Tokomeza” miezi
michache iliyopita.
Mheshimiwa
Spika,
Hadi leo ahadi hiyo ya Waziri Mkuu haijatekelezwa
na badala yake Rais ameamua kuunda tume nyingine huku Bunge lako tukufu likiwa
limewasilisha taarifa kuhusu Tokomeza jambo ambalo linaonesha serikali
kutoamini taarifa ya Kamati ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa
Spika,
Kwa mwaka wa 2013 taarifa zinaonesha kuwa watu 23
waliuwawa na vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Waziri
mwenye dhamana ya Wizara hii kueleza Bunge lako tukufu juu ya kukithiri kwa
tabia hii isiyokoma mwaka hadi mwaka na ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya
askari wanaohusika na mauaji haya.
Mheshimiwa
Spika,
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mkuu wa
Jeshi la Polisi mpya kuchukulia hali kama janga ndani ya Jeshi la Polisi na
hivyo awe na mkakati wa kuzuia hali hii.
Mheshimiwa
Spika,
Katika hali ya kushangaza hata wananchi wameanza
kuchukua sheria mkononi kwa kuwadhuru na hata kuwaua askari polisi. Kwa mwaka
2013 vituo vya polisi takribani vitano vilivamiwa na wananchi na mali kadhaa za
Jeshi hilo kuharibiwa, aidha vifo kadhaa vya askari viliripotiwa kutokea katika
maeneo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa
Spika,
Kama matukio hayo hayatoshi wananchi kwa makundi
yao katika maeneo mbalimbali ya nchi walizidi kujichukulia sheria mkononi kwa
kuwaua watu mbalimbali ambao wametuhumiwa kufanya makosa ya jinai kama vile
wizi. Kwa mwaka jana pekee watu 1669 waliuwawa[1].
Mheshimiwa
Spika,
Upo uhalifu mwingine ambao
umejitokeza katika nchi yetu ambapo watu wamekuwa wakizikwa wakiwa hai. Matukio
kama ya hayo yametokea katika Wilaya Chunya na maeneo mengine katika Mkoa
Mbeya.
Mheshimiwa
Spika,
Hali hii ya mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo
vya dola na pia mauaji yanayofanywa na wananchi kwa wahalifu na pia kuvamia na
hata kuua Polisi sio jambo la kulifanyia mzaha kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka serikali kuchukua hatua za dharura na kutoa taarifa Bungeni na
bila kufanya hivyo italazimika kuamini kuwa serikali iliyopo madarakani imetoa
Baraka kuhusu vitendo hivi vya kinyama kuendelea kutokea katika nchi yetu.
5. UHAMIAJI HARAMU NA USALAMA KATIKA MIPAKA YA
NCHI YETU
Mheshimiwa
Spika,
Mipaka ya Tanzania haipo salama kabisa kwa sababu
imeendelea kuwa kichaka kwa wahamiaji haramu. Hali hiyo pia inathibitika na
kile kilichosemwa na Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi Bungeni katika Wizara ya
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu
kung’olewa kwa alama (beacons) za
mipaka yetu katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, mahusiano mabaya ya
Tanzania na baadhi ya jirani zake yanafanya hali ya usalama mipakani kuwa ya
hatari zaidi. Kwa mfano, kumekuwa na mvutano kati ya Rais Kikwete na Rais
Kagame kwa mujibu wa vyombo vya habari. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inahoji, kutofautiana kwa maneno kati ya Rais Kikwete na Kagame kunatosha kuwa
ugomvi kati ya nchi hizi mbili kwani hili lisipotazamwa vizuri linaweza
kufifisha matumani ya wananchi wa nchi hizi mbili kuishi kama ndugu ndani na
nje ya mipaka yetu.
Mheshimiwa
Spika,
Tanzania imejaa wageni wengi kutoka nchi
mbalimbali kama vile Bangladesh, India, China, Pakistan, na nchi nyingene za
Afrika na Afrika Mashariki wanaofanya kazi hapa nchini katika fani na taaluma
ambazo watu wetu wanazo. Kambi Rasmi ya
Upinzani inahoji kama ni sera ya Serikali hii ya CCM kutoa kipaumbele cha ajira
kwa wageni katika fani, ujuzi na taaluma ambazo watanzania wanazo. Aidha,
tunaitaka serikali kupitia idara ya uhamiaji na idara nyingine za serikali
kupitia takwimu za wageni waliopo nchini na shughuli wanazozifanya ili kuona
kama wageni hao wana uhalali wa kuendelea kuwepo na kufanya kazi nchini ikiwa
hakuna kazi inayohitaji taaluma maalumu (special skills) ambazo watu wetu
hawana.
6. HITIMISHO
Mheshimiwa
Spika,
Kila aliyepata fursa ya kusikiliza kwa makini
maoni haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni angetaka kuona tunatoa suluhisho gani juu
ya nini kifanyike kuhusu mambo haya.
Hata sisi Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni tunafikiri ni vyema kushauri na
kusaidia kuonyesha njia muafaka ili kuliokoa taifa letu na mateso haya, lakini
tunapata wakati mgumu kuishauri Serikali ambayo imepoteza thamani ya utu dhidi
ya watu wake. Hivyo basi, kama kuna
mambo ya kushauri, basi tungeshauri yafuatayo:
Moja: Mungu
asaidie Serikali hii ya CCM iondoke madarakani mapema kabla haijaharibu mfumo
wa kumpata kiongozi kwa njia ya demokrasia kwani hali ikiendelea hivi; iko siku
watu wataingia barabarani. Hali hii tayari imeshaanza kujitokeza kwani mwaka
Kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2013 pekee watu 1669 waliuwawa kwa sababu
ya watu kujichukulia sheria mkononi.
Tunajua watu watakapojitokeza kudai haki zao na kupinga uonevu watapigwa
mabomu ya machozi, risasi, na vitisho na mateso mbali mbali lakini
tunajua hawatarudi nyuma; kwani watakuwa wamedhamiria kujitetea na kuwatetea
ndugu zao na nchi yao dhidi ya mateso, ukandamizaji, uonevu na dhiki
inayotokana na mambo hayo. Kinyume
chake, yatakapotokea hayo, Serikali
itakuwa imetangaza ukomo wa utawala wa kidemokrasia na hilo linaweza kuwa
chimbuko la machafuko na umwagaji damu, hivyo ni vyema waumini wa imani
mbalimbali wafanye dua na sala ili Serikali hii ya CCM iondoshwe madarakani
katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani.
Pili: Siku Serikali hii ya CCM
ikijua kuwa nguvu ya Mfalme ni watu na
sio bunduki na mabomu ya machozi, siku
hiyo ndipo mtakapoanza kupata hekima ya kuheshimu utu wa binadamu na kile
kinachoonekana sasa kama mateso, udhalimu na ukandamizaji vinaweza kurekebishwa.
Tatu: Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutambua kuwa heshima ya kiongozi haijengwi
kwa uwezo wa mali wala utawala bali katika kazi njema, heshima, utu, na upendo.
Ikiwa Serikali itaelewa hivyo; basi wajibu wake katika kutafuta na kupigania
maisha ya mtu mmoja mnyonge anayeteswa na kudhalilishwa itakuwa ndio hazina na
heshima kubwa kwa viongozi wa serikali na taifa kwa jumla.
Mwisho: Tunafahamu kwamba ndani ya Serikali kuna watu
wengi waadilifu na wenye dhamira njema na nchi yetu. Hata hivyo, wanashindwa
kuchukua uamuzi wa kukemea uovu kutokana na utamaduni wa Serikili kuwatisha na
kuwawekea vikwazo mbalimbali watu wa namna hiyo. Kutokana na hali hiyo, jamii
yetu imejengwa katika fikra za hofu na woga kwa mambo ambayo yanahitaji uamuzi
thabiti na kauli za kijasiri ili kulinusuru taifa na maangamizi.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka Serikali ijue na wananchi wote wajue kwamba; “Dhambi
mbaya na kubwa kuliko zote Duniani ni woga”. Hivyo Basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inawaasa viongozi wachache wenye dhamira njema
kwamba waache woga wasimamie misingi ya haki na ukweli hata kama gharama zake ni Maisha yao kwani
msingi wa Taifa letu la kesho unajengwa na viongozi na utawala ulioko madarakani leo.
Mheshimiwa
Spika,
Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, naomba kuwasilisha.
Godbless Jonathan Lema (Mb)
MSEMAJI MKUU
WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI NA
WAZIRI
KIVULI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI
Imesomwa
leo, tarehe 15 Mei, 2014
No comments:
Post a Comment