Saturday, 28 June 2014

Bila UKAWA katiba mpya imekwama

Wakati umesalia mwezi mmoja na siku 10 kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza tena vikao vyake mjini Dodoma kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya itakayowaongoza Watanzania kwa zaidi ya miaka 50 ijayo, Mtendaji Mkuu wa Bunge hilo amesema kuwa bila kundi la Ukawa kurejea na kushiriki hatua zote haitawezekana kupata Katiba Mpya.Maandalizi ya Mkutano wa Pili wa Bunge Maalumu la Katiba tayari yameanza na kikao cha kwanza kikitarajiwa kufanyika Agosti 5, huku ofisi ya Bunge hilo ikiwa na matumaini kuwa kundi la Ukawa litarejea na kushiriki vikao vyote kwa manufaa ya taifa.Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Zanzibar, Katibu wa Bunge hilo Yahya Khamis Hamad, alisema kuwa kukwama kwa mchakato huo kutatokana na kutotimia kwa idadi ya wajumbe katika upigaji kura.“Kikwazo kitabaki katika upatikanaji wa theluthi mbili za uamuzi wa vikao vya Bunge hilo kwa mujibu wa kanuni zilizopo,”alisema Hamad.Kauli hiyo imekuja huku juhudi za watendaji wa Bunge hilo kuwashawishi viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani zikiendelea kwa kuwasihi waruhusu wabunge wao kurejea na kushiriki vikao vya Bunge Maalumu la Katiba ili taifa lipate Katiba Mpya mwakani.
Hamad alisema kuwa ikiwa hali ya kukosekana theluthi mbili itajitokeza, hakuna njia nyingine mbadala zaidi ya Katiba ya mwaka 1977 kuendelea kutumika na kwamba hata mfumo wa Serikali utabaki uleule.Kwa nyakati, siku tofauti na mara kadhaa juhudi zimefanyika kuwashawishi Ukawa kurejea bungeni bila mafanikio, huku viongozi wa vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi wakionekana kuweka ngumu na kutoa masharti kwa Serikali, ndipo waafiki ombi hilo na kurejea bungeni.Msimamo huo wa Ukawa unatajwa kuendelea kuliweka taifa pabaya ukiondoa matumaini ya kupatikana kwa Katiba Mpya baada ya inayotumika sasa kutimiza miaka 50 na kuonekana kuwa ipo haja ya kufanya mabadiliko.Katibu wa Bunge Maalumu, Hamad anatoboa siri akisema: “Pamoja na juhudi za Bunge kuwarejesha bungeni, bado haijafahamika kama  wabunge wa kundi la Ukawa watarejea au la.”Akitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na ofisi yake Hamad anasema ni pamoja na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel  Sitta kukutana na viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF) mwenye ushawishi mkubwa kwenye kundi la Ukawa.CUF ndicho chama chenye wawakilishi wengi katika Bunge la Katiba kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Kwa mujibu wa Hamad, Sitta akiwa Zanzibar pia alikutana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuzungumzia suala hilo akihimiza na kuwataka wajumbe hao kurejea na kuhitimisha ngwe iliyobaki.Hata hivyo, Katibu huyo wa Bunge Maalumu la Katiba alisema kuwa kuendelea kwa Ukawa kubaki nje ya Bunge kama si njia mwafaka ya kufikia suluhisho, badala yake anaamini kuwa kila jambo gumu huweza kuzungumzika na kufikia tamati.

No comments: