Thursday, 26 March 2015

KUELEKEA MAJIMBONI 2015: Ukawa haina kitu majimbo ya Handeni na Korogwe

Uchambuzi wa Julius Mtatiro Kuelekea Majimboni 2015.
Leo tunaendelea na uchambuzi wa Mkoa wa Tanga kwa kuangalia majimbo ya Handeni, Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini.
Jimbo la Handeni linagusa eneo lote la Wilaya ya Handeni. Jimbo hili lina mji mmoja na maeneo ya vijijini. Eneo la Mjini ni pale Handeni Mjini ambako kuna kata 12 na mitaa 60 na maeneo ya vijijini yanayounda wilaya hii ni kata 20, vijiji 91 na vitongoji 775.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Handeni kuna wakazi 276,646. Majimbo ya Korogwe Mjini na Korogwe Vijijini yako Wilaya ya Korogwe na ndiyo yanayotengeneza Wilaya hii yenye kata 20, vijiji 118 na vitongoji 610, huku ikiwa na wakazi 242,038.

Jimbo la Handeni

Kuna watu hukaa vijiweni na kusema kuwa CCM inakufa kirahisi. Jambo hili ni la mjadala mpana, ukitaka kuona bado CCM iko hai, nenda Handeni upime maneno yangu. Jimbo la Handeni limeweka rekodi muhimu kwa CCM tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi. Ni jimbo linalostaajabisha kwa namna wananchi wake walivyo wavumilivu na watiifu kwa chama hicho.Mwaka 1995 wakati mfumo wa vyama vingi unaanza, CCM haikufanya ajizi, ilijipanga kwa kutumia mtandao wake imara na ikampata mgombea imara, Dk Abdallah Omar Kigoda. Dk Kigoda ambaye kitaaluma ni mtaalamu wa uchumi na kilimo akiwa amepata shahada yake ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975, Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Vanderbilt (Marekani) mwaka 1980 na shahada ya uzamivu katika masuala ya Uchumi wa Kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Missouri Colombia, ndiye aliyepewa baraka zote na CCM kupambana na wapinzani.


Mipango ya NCCR na vyama vingine vilivyokuwa na mwamko wa mageuzi wakati huo haikuwa na tija kubwa kutoa ushindani baina ya vyama hivyo na CCM. Mwishowe Kigoda aliwashinda wapinzani wake na akakabidhiwa kiti cha ubunge wa Handeni kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.Rais Benjamini Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara tangu mwaka 1995 – 1996, kisha akahamishiwa Wizara ya Nishati na Madini mwaka 1997 – 2000.

Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000, Kigoda akiwa Waziri na Mbunge aliyemaliza kipindi cha kwanza, akapewa tena kazi na wana CCM kuifanya Handeni iendelee kuwa chini ya chama hicho. Akajitosa na kukutana na upinzani dhaifu, akashinda kwa kura nyingi na kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha pili.Rais Mkapa pia akamwongeza mzigo wa uwaziri, mara hii akipangiwa Wizara ya Mipango na Ubinafsishaji (kuyashughulikia mashirika ya umma ambayo kwa mujibu wa Mkapa, yalikuwa mzigo kwa Serikali yake). Dk Kigoda alidumu kwenye wadhifa huu hadi mwaka 2005 ulipokoma uongozi wa Mkapa.Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CCM haikuwa na tatizo na Kigoda, ikamrejesha tena kutetea nafasi yake kwa mara ya tatu. Kulikuwa na kila dalili kuwa udhaifu wa vyama vya upinzani ulioonyeshwa miaka ya 1995 na 2000 ungeweza pia kutokea mwaka 2005.

Lisemwalo lipo na hutokea; kweli, kura zilipopigwa Dk Kigoda akapata ushindi wa ‘kutikisa’ wa asilimia 85.1 (sawa na kura 64,874), akifuatiwa kwa mbali na Salehe Mbweto wa CUF aliyepata asilimia 13.0 (sawa na kura 9,925) na Richard Robinson Kilango wa Chausta aliyeshika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 1.8 ya kura zote. Dk Kigoda akapewa nafasi ya kuongoza kipindi cha tatu. Safari hii Serikali ya Rais Kikwete ikimuweka pembeni kwenye uwaziri.

Ilipotimu 2010 na majimbo kuwa wazi tena, Dk Kigoda alijitosa na kushinda kura ya maoni. Aliyekuwa mgombea na mwanachama mtiifu wa CUF mwaka 2005 kwenye jimbo hili, Salehe Mbweto, alihamia Chadema na kuwa mgombea kwa tiketi ya chama hicho, jambo lililoifanya CUF itafute mgombea mwingine. Ikampata Remmy Shundi. Ulikuwa ukiwatizama wagombea hawa watatu mwaka 2010, ungeona kila dalili ya upinzani kuparurana na kuiachia CCM njia. Naam, yalitokea, Mbweto wa Chadema na Shundi wa CUF wakaishia kuitana kila aina ya majina mabaya huku CCM ikikusanya kura. Baada ya upinzani kuparurana, msimamizi wa uchaguzi akaweka bayana matokeo yaliyompa Dk Kigoda ushindi wa asilimia 69.98 (kura 31,537), Mbweto wa Chadema akashika nafasi ya pili kwa asilimia 13.6 (kura 6,131) na Shundi wa CUF akawa wa tatu kwa asilimia 12.2 (kura 5,498). Dk Kigoda akajichukulia ubunge kwa kipindi cha nne, yaani kupata fursa ya kuwaongoza wananchi kwa miaka takribani 20.

Miaka 20 ya uongozi wa Dk Kigoda jimboni hapa inamalizika huku wananchi wakiwa na hali mbaya kiuchumi. Handeni ni kati ya maeneo ambayo umaskini umetamalaki, huku kukiwa na hali mbaya ya upatikanaji wa huduma muhimu na za uhakika kwa wananchi.
Mathalan, wananchi wa wilaya hiyo wanalazimika kutembea makumi ya kilomita kutafuta maji na wakiyataka majumbani watanunua ndoo moja kwa Sh500 hadi Sh1,000.Pamoja na yote hayo, matokeo ya Serikali za Mitaa katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana, yanaonyesha CCM ikiwa imeshinda Handeni kwa zaidi ya asilimia 90.Kama kuna watu wa kulaumiwa kuhusu hali ya wilaya hii kisiasa ni vyama vya upinzani. Handeni haijapata mpinzani wa kweli anayeweza kuzunguka vijijini, akijitolea kwa hali na mali kuwaelimisha wananchi na kupanga mikakati madhubuti ya ujenzi wa mtandao wa mabadiliko.Dk Kigoda mwenyewe tayari ameonyesha nia ya kutaka kuliongoza jimbo hili kwa kipindi cha tano na anaweza kupita kwenye kura ya maoni ya chama chake. Hadi sasa upande wa upinzani hauna mtu imara na naweza kuhitimisha kirahisi kuwa jimbo hili litachukuliwa na CCM tena kwa kura nyingi.

Jimbo la Korogwe Mjini


Jimbo la Korogwe Mjini liliitwa Korogwe Mashariki katika uchaguzi wa mwaka 1995 na mwaka 2000. Baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ililipatia jina jipya la “Korogwe Mjini” jina ambalo linatumika hadi sasa.Mwaka 1995, Korogwe Mjini iliingia katika mchakato wa kumpata mbunge. Vyama kadhaa vya siasa ikiwamo CCM vilionyesha nia na kupambana vilivyo.Ushindani mkubwa uliotokea jimboni hapa ulihitimishwa kwa Joel Bendera wa CCM kupewa ridhaa ya uongozi. Bendera aliongoza na kulifikisha jimbo hili kwenye uchaguzi uliofuatia.

Mwaka 2000 Joel Bendera alitupa karata yake kwa mara ya pili, mara hii kama ilivyokuwa kwa majimbo mengi, vyama vya upinzani vikitetereka kidogo tofauti na ilivyokuwa mwaka 1995. Bendera alishinda kirahisi na kupata nafasi ya uongozi wa awamu ya pili.
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, haukuwa mwepesi kwa CCM. Vyama vya upinzani, hususani CUF vilikuwa vimejizatiti na kuweza kufanya shughuli nyingi za kisiasa kati ya mwaka 2000 – 2005. CCM ilimpa Joel Bendera fursa ya tatu kuwapigisha kwata wapinzani na matokeo ya mwisho yalimpa Bendera fursa nyingine ya kuongoza kwa mara ya tatu.
Wananchi walimpigia kura 12,070 (asilimia 63.5) akifuatiwa na mgombea wa CUF, Jamaa Magogo aliyepata kura 5,369 (asilimia 28.3) wakati mgombea wa Chadema David Chamshama kipata kura 1,369 (asilimia 7.2). Pamoja na kujizatiti kwa CUF mwaka huo, ukweli unabakia kuwa hawakujipanga kulichukua jimbo ambalo mbunge wake alikuwa amechokwa.Wananchi wa Korogwe wanasema hakuna mwaka uliokuwa mwepesi katika kumwangusha Bendera kama 2005, lakini maji yakishamwagika hayazoleki! Siasa za Korogwe zilibadilika ghafla na kwa nguvu mwaka 2010. Mosi, CCM ilikuwa na nguvu ya ziada kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa uongozi wa CUF na kukosekana kwa harakati za kisiasa zilizozoeleka kufanywa na chama hicho.

Pili, Chadema ilichukua nafasi ya CUF japo kwa udhaifu wa hali ya juu. Joel Bendera alisimama tena kutaka wana CCM wampe ridhaa ya kugombea ubunge kwa mara ya nne na nusura jambo hilo litokee, ila akabwagwa kwa kura chache na Abdallah Nassir Yusuph (tofauti ya kura 255 tu) kwenye kura ya maoni ya ndani ya CCM.Kura za jumla kwenye ubunge zilipopigwa, Abdallah Nassir Yusuph wa CCM aliwavunjavunja wapinzani akipata asilimia 82.7 (kura 12,090) na aliyemfuatia ni mgombea wa Chadema Amiri Calistus akipata asilimia 11.69 (kura 1,722) na Jumaa Magogo wa CUF akaambulia asilimia 2.72 (kura 400).Wananchi niliozungumza nao wanasema CUF haikufanya shughuli za kisiasa Korogwe Mjini kati ya mwaka 2005 – 2010 na kwamba kukosekana kujitokeza kwa vijana kulimlazimu mgombea wake achukue fomu kugombea tena huku akiwa mgonjwa. Laiti kama Magogo angekuwa na uwezo wa kufanya kampeni vizuri inasemekana hadhi ya CUF ingesimama imara.Kwa sasa, CCM imeidhibiti Korogwe Mjini kwa asilimia 100, upinzani haufurukuti hata mita moja. Mbunge wa sasa ana nafasi kubwa tena ya kuchaguliwa na wana CCM na hata wananchi kuendelea kuongoza. Pia, tayari chama chake (CCM) kimekwishamtengenezea njia thabiti kurudi bungeni kwa kushinda vijiji na mitaa yote kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda takriban asilimia 100 ya vijiji na vitongoji. Hii ina maana kwamba ama upinzani umekufa Korogwe Mjini au bado unapanga mipango ya “kufufuka” hapo baadaye. Lakini ukweli kuntu unabakia kuwa jimbo hili si la upinzani kwa asilimia 100 mwaka huu.Jimbo la Korogwe Vijijini

Jimbo la Korogwe Vijijini liliitwa Korogwe Magharibi katika uchaguzi wa mwaka 1995 na mwaka 2000. Baadaye likapewa jina jipya la Korogwe Vijijini jina ambalo linatumika hadi sasa.Kihistoria na kwa vipimo vya hali ya kisiasa, jimbo hili linafanana kwa kiasi kikubwa na lile la Korogwe Mjini katika vipindi vyote vya uchaguzi.Tofauti iliyopo ni kwamba hili la Korogwe Vijijini halikuwahi kuwa na upinzani thabiti kuing’oa CCM kama lile la Korogwe Mjini.

Sababu nyingine ni kuwa jimbo hili halikuwahi kuongozwa na mbunge mmoja katika vipindi viwili, kila aliyejaribu aliambulia kipindi kimoja na kuondoka.Mwaka 1995 wananchi walishuhudia mvutano wa kisiasa wa vyama vingi uliowapa ishara za mabadiliko makubwa ya kidemokrasia nchini.Vyama vya upinzani vilikuwa vimejipanga na viling’arishwa na NCCR pamoja na kwamba CCM ilishinda uchaguzi na mbunge aliyechaguliwa akiwa ni Kizango. Aliongoza hadi kumaliza kipindi chake cha kwanza na hakurudi tena.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 ulikutanisha CCM na vyama dhaifu vya upinzani. Mara hii CCM iliwakilishwa na Lupatu Mussa, mtaalamu aliyekuwa na shahada ya uzamili uchumi wa kilimo. Enzi za Lupatu zilidumu kwa miaka mitano tu kama mbunge. CCM wakaandaa mbadala wake uchaguzi uliofuatia.Ilikuwa ni mwaka 2005 ambapo CCM ilimleta Omari Laus, CUF ikampanga Ezra Msangi. Baada ya mpambano dhaifu kutoka upande wa vyama vya upinzani, CUF iliambulia kura 9,272 na vyama vya Chausta na TLP kwa pamoja vikipata asilimia 2.3 ya kura zote, huku CCM ikishinda kwa ushindi mkubwa wa kura 59,373.

Mhina naye hakudumu, aliongoza kwa kipindi kimoja na baadaye kuondoshwa kupitia kura za maoni ndani ya CCM, mbabe wake akiwa ni Stephen Hilary Ngonyani au Profesa Majimarefu.Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haukuwa na jambo jipya la maana kiushindani hapa Korogwe Vijijini. Maji Marefu” (Mganga wa Jadi) na mtu maarufu wilayani Korogwe) ndiye alikuwa mgombea wa CCM, Chadema ilimleta Mohammed Maalim Siu na CUF ikamuweka Joseph Mashuve.Mchuano dhaifu ukatokea katika jimbo hili, huku kila mtu akijua kuwa Profesa Majimarefu atatwaa kiti bila ubishi, jambo hilo lilitokea kwani alifanikiwa kushinda kwa kishindo.ipata kura 41,377 akifuatiwa kwa mbali na mgombea wa CUF aliyeambulia kura 3,233 na yule wa Chadema akiwa wa tatu na mfunga orodha ya wagombea kwa kupata kura 2,570.

Ukuu wa CCM hapa Korogwe Vijijini umejionyesha pia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambapo CCM ilitwaa vijiji 119 kati ya 122, Chadema ilipata vijiji viwili na CUF kimoja.

Matokeo haya ya ushindi wa CCM kwa asilimia 99 yana maana kuwa upinzani hauna jambo la kujivunia. Jimbo hili limekosa mpinzani wa kulijenga na ni ngome tiifu kwa CCM, hivyo Profesa Majimarefu atarejea tena na kushinda kura za maoni ndani ya CCM na atakuwa mbunge wa jimbo hili kwa mara ya pili, labda kwa kuvunja rekodi za nyuma zilizozuia jambo hili lisitokee.Wananchi wataichagua CCM bila kujali kuwa haijafanya jambo lolote la kuwatoa katika umaskini mkubwa.Jumamosi ya wiki hii (28 Machi) tutaendelea na majimbo ya Lushoto, Bumbuli na Mlalo, yote ya Mkoa wa Tanga.

(Julius Mtatiro ni kiongozi mzoefu katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759,

No comments: