Wednesday 4 June 2014

Maalim Seif Awahutubia Wananchi wa Makurumla Dar-es-Salaam


Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema juhudi zinazofanywa kuusambaratisha umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) hazitofanikiwa.

Amesema tayari kuna juhudi za hapa na pale za kutaka kuusambaratisha umoja huo lakini kwa vyovyote vile juhudi hizo zitakwama kwa kuwa umoja huo umeundwa kwa lengo la kutetea maslahi ya wananchi kupata katiba wanayoitaka na wala sio kwa maslahi binafsi.Mhe. Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alieleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika kata ya Makurumla, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Alisema binafsi alifurahishwa na kitendo cha vyama vya upinzani kuunda umoja huo, kwani vyenginevyo Chama Cha Mapinduzi kingewaburuza na kufanya maamuzi wanayotaka kinyume na matakwa ya wananchi walio wengi.Maalim Seif alifahamisha kuwa sheria ya mabadiliko ya katiba ilitaka Bunge Maalum la Katiba liijadili Rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume hiyo na wala sio kujadili Rasimu nyengine yenye matakwa ya kundi maalum, akimaanisha mrengo wa Chama Cha Mapinduzi.

Alieleza kuwa UKAWA wanaweza kurudi Bungeni iwapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Jakaya Kikwete atawahakikishia kuwa rasimu itakayojadiliwa ni ili iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na iwapo itakwenda kinyume, UKAWA wanaweza kutoka tena kwenye Bunge hilo.Akizungumzi kuhusu Muundo wa Muungano Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema hakuna mbadala mwengine wa kumaliza kero za Muungano isipokuwa ni uwepo wa Serikali tatu zitakazotoa mamlaka kwa serikali za nchi washirika.

Amehamamisha kuwa hata katiba ikitoa mamlaka kwa Zanzibar juu ya kuweza kujiunga na mashirika ya Kimataifa yakiwemo WHO, FAO na FIFA, mamlaka hayo hayatokuwa na nguvu kwani mashirika hayo yanahitaji kufanya ushirikiano na nchi zenye mamlaka kamili (Sovereign states), na kwamba mamlaka hayo ya kikatiba bila ya mamlaka kamili yatakua ni “kiini macho”.Mapema akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) Julius Mtatiro, alielezea kushangazwa na kauli za Rais Kikwete kwa kuzikubali Rasimu zote mbili zzilizowasililishwa kwake na Tume ya mabadiliko ya katiba, lakini baadaye alizikana.Alisema vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vitahakikisha kuwa vinaendelea kupigania katiba itokanayo na maoni ya wananchi ambapo alidai kuwa wengi wao waliunga mkono muundo wa Muungano wa Serikali tatu pamoja na kuwepo kwa mamlaka kamili ya Tanganyika na Zanzibar.

No comments: