MKASA mkubwa, na wenye kusikitisha, ulitokea Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita. Ni ishara moja yenye kuthibitisha kwamba kweli Tanzania ina utawala mbovu, tena wa hatari.
Mkasa wenyewe ni kukamatwa Mosena Nyambabe, Katibu Mkuu wa chama cha NCCR-Mageuzi. Sababu ya kisa kilichomfika ni hotuba aliyoitoa saa kadhaa kabla hajakamatwa kwenye mkutano wa hadhara wa UKAWA uliokuwa unawaelimisha wananchi kuhusu mchakato wa Katiba. Mkutano huo ulihutubiwa pia na Mwenyekiti wa Vijana (Taifa) wa CHADEMA, John Heche, na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Ashura Mustafa. Wawili hao nao walisakwa na Polisi lakini walinusurika kunaswa.Yaliyojiri ni haya: mwendo wa saa tano za usiku Polisi wa Kigoma waliingia katika hoteli waliyofikia viongozi hao katika kijiji cha Nguruka, Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma. Askari kanzu wanne waliingia hotelini wakiwa na dhamiri ya kuwakamata wote watatu. Lakini walimkuta Nyambabe peke yake kwa vile Heche na Ashura walikuwa wameteremka Kigoma Mjini.Nje, hoteli ilizungukwa na askari wengine sita waliokuwa na silaha.Baadaye Nyambabe alisema kwamba alielezwa na Polisi kwamba walimkamata kwa sababu katika hotuba yake alimdhalilisha Rais Jakaya Kikwete.
Ni wazi kwamba Nyambabe alimkosoa Kikwete na mfumo wake wa utawala. Hiyo ilikuwa ni haki yake. Si yake yeye peke yake bali kila raia ana haki yakufanya hivyo akiwa katika taifa linalojigamba kwamba lina mfumo wa demokrasia ilimradi asiwe tu amemtukana Rais matusi ya nguoni.Lakini vyombo vya dola vina mantiki ya kivyao.Vilimbandika Nyambabe lakabu ya “mchochezi”. Vikaamua kwamba lazima “ashughulikiwe”.Kwa hakika, Nyambabe alifanya kosa. Kosa lakeni kusahau kwamba katika taifa lenye utawala mbovu hutakiwi useme kweli. Unachotarajiwa kufanya ni kuzifuata nyendo na tabia za viongozi wa nchi za kudanganya na kuuita mchana usiku na usiku mchana. Kufungua mdomo na kutamka kweli huwa ni dhambi.
Ukimuona mtawala amekaa uchi unatakiwa useme amevaa joho na kilemba. Na amependeza. Katika mazingira kama hayo kunena kunakuwa kufuru.
“Kuno kunena kwa nini, kukanikomeya kuno?
Kwani kunena kunani, kukashikwa kani vino?
Kani iso na kiini, na kuninuniya mno
Kanama nako kunena, kwaonekana ni kuwi!”
Abdilatif Abdalla, mzalia wa Mombasa na gwiji wa mashairi, aliuandika ubeti huo katika moja ya mashairi yaliyo katika diwani yake “Sauti ya Dhiki”. Aliionja athari ya kunena kuonekana kubaya na watawala dhalimu. Aliuona uchungu wake.
Abdilatif alikamatwa, akafikishwa mahakamani na akafungwa Kenya kwa kuukosoa utawala wa Jomo Kenyatta kwenye waraka aliouandika na uliokuwa na ilani iliyouliza swali: “Kenya Twendapi?”
Alipokuwa korokoroni katika gereza la Shimo la Tewa, nje kidogo ya Mombasa, alishangaa, akatafakari na akajiuliza huku kunena (kunena yaliyo kweli) kuna nini? Na kwa nini kukamsababisha atiwe ndani?
Alipofunguliwa alihamia Tanzania wakati Tanzania ilipokuwa na heshima yake na akawa radhi nchi hiyo iwe mlezi wake. Sijui kama Tanzania ya leo ingemvutia hivyo.
Siku hizi ukiukwaji wa haki za binadamu unazidi kuwa jambo la kawaida nchini Tanzania na inavyoonyesha Polisi wanajifanyia watakavyo kwa vile wanajiona kuwa wana nguvu za kufanya hivyo bila ya kuwajibika. Hii kadhia ya Nyambabe inaeleza mengi. Moja ni jinsi vyombo vya dola vinavyokiuka haki za binadamu.Nyambabe amesema kwamba alipokataa kutoa maelezo saa sita za usiku katika Kituo cha Polisi cha Nguruka kwa vile wakili wake hakuwako Polisi walimpeleka kituo cha Wilaya ya Uvinza.Waliwasili huko milango ya saa saba za usiku. Wakamtaka tena atoe maelezo; naye akakataa akishikilia kwamba lazima awepo wakili wake ndipo atoe maelezo. Jaza yake ni kuwekwa juu ya benchi hadi saa 12 za alfajiri alipopelekwa Kituo cha Kati Kigoma.Sina hakika iwapo Polisi wa Kigoma walimfanyia waliyomfanyia Nyambabe kwa kutii amri ya wakubwa wao au iwapo ni mazoea yao kuwasumbua wananchi na kuzikiuka haki zao za kimsingi wanazohakikishiwa katika Katiba ya nchi.Lakini hadi sasa ninavyoyaandika haya, siku tatu baada ya tukio hilo, sikusikia kama kuna mkubwa yeyote wa Jeshi la Polisi aliyemuomba radhi Nyambabe kwa namna askari wa Kigoma walivyoziingilia haki zake
.Alhasil ya mambo ni kwamba yaliyomfika Nyambabe huko Kigoma ni ishara moja tu ya utawala mbovu uliopo Tanzania na jinsi taifa lilipo ukingoni karibu kutumbukia katika shimo la maangamizi. Viongozi wetu wasipokuwa makini wakachukua hadhari wataweza mara moja kulitumbukiza taifa zima katika nakama ambayo hata kuifikiria tu inatisha.Wajue na kutambua kwamba taifa likiangamia na wao pamoja na walio wao nao pia wataangamia.
Tuonavyo ni kwamba kuna baadhi ya viongozi ambao kama wanashindana nani atakayekuwa wa mwanzo kuliangamiza taifa. Yanayojiri Zanzibar tu yanatosha kuthibitisha dhana hiyo.
Ukweli ni kwamba Zanzibar imo hatarini. Wananchi wameingiwa na hofu. Wawekezaji wameanza kuuliza uliza iwapo rasilmali zao zitasalimika na hazitokwenda arijojo. Wasiwasi wote huo unasababishwa na matamshi ya chuki ya viongozi ambao wanaonyesha kutoridhishwa na hali ya amani na utulivu wa kisiasa Visiwani humo na wanaotamani kuirejesha Zanzibar katika hali yake ya zamani ya chuki na uhasama. Kwa mara ya kwanza tangu iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hivi sasa wapinzani wake wamejitokeza wakitaka pasiwepo tena Serikali ya muundo huo baada ya Uchaguzi Mkuu ujao 2015.
SUK imeundwa kutokana na Maridhiano yaliyofikiwa mwishoni mwa 2010 baina ya Rais wa Zanzibar wa siku hizo Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi. Viongozi hao walikubaliana pamoja na vyama vyao kuwa na Maridhiano ili kuuzika uadui baina ya Wazanzibari wa itikadi tafauti za kisiasa. Lakini kuna wenye ajenda ya kuyachimba Maridhiano hayo na kuifufua hali ya uadui wa kufika hadi ya wafuasi wa CCM na wa CUF kuuana. Kipaumbele chao cha kwanza ni kuiua SUK. Hadi sasa wapinzani wa SUK waliojitokeza wazi ni baadhi ya viongozi wa CCM/Zanzibar wakiungwa mkono na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Nape Nnauye. Kuna mambo kadhaa yanayostahili kuzingatiwa na wale wanaochochea pasiwepo tena serikali ya ubia Zanzibar. Hapa tutayataja machache tu.
Moja ni kwamba dunia nzima inajua ya kuwa kuasisiwa kwa SUK kuliinusuru Zanzibar. La pili ni kwamba serikali za kigeni zilizoisusia Zanzibar kwa misaada zilirudi kuisaidia pale tu ilipoundwa serikali ya ubia.La tatu ni kwamba wengi wa Wazanzibari hawataki kabisa kurejeshwa katika mazingira ya chuki na machafuko ya kisiasa. La nne ni kwamba Wazanzibari wa leo wameerevuka. Wanazijua sheria, wanazitambua haki zao chini ya sheria na wanajuwa namna ya kuzitumia hata kufika katika mahakama kuu za kimataifa.
Siasa za majungu si ngeni nchini Tanzania. Zilianza tangu enzi za mfumo wa chama kimoja na zinaendelea hadi sasa ambapo si haramu kuwa na chama chenye kupingana rasmi na chama kinachotawala.Kama kuna tafauti basi labda tafauti iliyopo ni kwamba katika enzi hizo za mfumo wa chama kimoja wanasiasa wakipikiana majungu ndani ya chama chao ili wajipendekeze kwa wakubwa wa chama.Siku hizi baadhi yao wanapika majungu si kuwafisidi wanasiasa wenzao tu bali kuifisidi nchi nzima kwa manufaa yao na ya chama chao. Ndiyo maana ingawa nilishtushwa lakini sikustaajabu niliposikia kwamba kuna jungu kubwa linalopikwa kuichafua hali ya kisiasa visiwani Zanzibar.Wenye kula njama hiyo wanaiandaa mipango yao kwa ujasiri mkubwa wakiamini kwamba wakuu wa juu kabisa wa chama chao hawana ubavu wa kuwachukulia hatua kwa kuwa nao wanakubaliana na shabaha yao.
Baadhi ya wakubwa hao katika chama na Serikali zote mbili, za Muungano na Zanzibar, hawakuwa na junaa kutamka maneno yenye lengo la kuisambaratisha SUK, kuleta ubaguzi, kuchochea chuki na kuwafitinisha Wazanzibari.Lazima wakubwa hao waambiwe ukweli. Tusibanie banie ama kwa kuwaogopa au kuwaendekeza. Ni wajibu wetu si tu kuwa na uhuru wa kuwaambia yaliyo kweli lakini kuufanya ukweli uwe huru.Kwa mintarafu ya haya ningependa hapa kumdhukuru mshairi mwingine ambaye alikuwa pia mwandishi wa tamthiliya, mwanafalsafa, muasi na mwanasiasa.Huyu ni Václav Havel aliyekuwa Rais wa tisa na wa mwisho wa Czechoslovakia na Rais wa mwanzo wa jamhuri mpya ya Czech.
Havel aliwahi kuandika maneno ambayo mara nyingi hayanitoki kichwani. Aliandika kwamba “Ukweli usipopewa uhuru kamili, uhuru unakuwa haukamiliki.” Ninayathamini sana maneno hayo ya Havel ijapokuwa mimi si mshabiki hivyo wa siasa zake kama nilivyo mshabiki wa siasa na mashairi ya Abdilatif.
Labda nihitimishe makala kwa kuwakumbusha watawala wetu ubeti mwingine wa Abdilatif. Ikiwa wao hawataki kuyasikia yanayonenwa basi kuna wasioona ubaya kusema kweli.
Basi ndio tuache kuwaambia kweli ikiwa ukweli unakuchomeni? Au ndo tukome kusema na kulalamika ikiwa mnaona kusema kunanuka? Abdilatif hakulisema hili lakini angeweza kusema kwamba vinukavyo, kwa hakika, ni vitendo vyenu, enyi viongozi wenye kuukimbia ukweli.
-
No comments:
Post a Comment