Wednesday 23 July 2014

Polisi Zanzibar wafikishwa mahakamani kwa utekaji nyara raia

KAMISHNA wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi, wamefunguliwa kesi mahakama kuu ya Zanzibar, baada ya watu wanane waliokamatwa wakihusishwa na matukuo ya miripuko kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani.Kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2014 imepangwa kuanza kusikilizwa kesho mbele ya Jaji wa mahakama kuu, Mkusa Issack Sepetu. Washtakiwa hao tayari wametakiwa kujibu hati za kiapo kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa. Kesi hiyo imefunguliwa na Wakili Abdallah Juma Mohamed akishirikiana na Rajab Abdallah Rajab kutoka kampuni ya uwakili ya AJM Solicitor ambao wanataka mahakama kuwaita viongozi hao ili waeleze mahali walipo wateja wanane wanaowatetea tangu walipokamatwa katika maeneo na nyakati tofauti visiwani Zanzibar. Kwa mujibu wa hati hiyo ya kiapo, watu hao ambao wanadaiwa kukamatwa na kuwekwa kizuizini ni Nassor Ahamad Abdallah, Mohamed Ishaq Yussuf, Said Kassim Ali, Hassan Bakari Suleiman, Rashid Ali Nyange Antar Homuod, Khamis Salum Amour na Salum Ali Salum. Kesi hiyo ya maombi ilianza kutajwa Ijumaa na Wakili Abdallah Juma Mohamed alidai walifungua kesi hiyo kwa kuzingatia Katiba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba ya Zanzibar ambavyo zinaelezea haki ya washtakiwa.  Mkuu wa Utawala wa jeshi la polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Aziz Juma Mohamed, ambae alifika mahakamni kwa niaba ya Kamishna wa Polisi akiwa ameandamana na Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Salum Msangi alisema wako tayari kusikilizwa kwa ombi hilo.

No comments: