Sunday, 28 December 2014

MwanaMapinduzi ajiunga na CUF

Mansour ajiunga rasmi CUF

   Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mhe. Mansour Yussuf Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja

 Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui, baada ya  kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
 Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya  kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja
 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akihutubia mkutano wa hadhara wa chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja
Wanachama wa CUF wakionyesha kuunga mkono uamuzi wa Mansour Yussuf Himid kujiunga rasmi na chama hicho kwenye viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja. (Picha na Salmin Said, OMKR).

Aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki Mhe. Mansour Yussuf Himid, 
amejiunga rasmi na chama cha wananchi CUF.

Mhe. Mansour ambaye amewahi kuitumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushika nyadhifa mbali mbali ikiwemo ya Waziri wa Kilimo, amechukua uamuzi huo leo kwenye mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.

Baada ya kukabidhiwa kadi ya CUF na Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Mhe. Mansour amesema ameamua kujiunga na CUF baada ya kubaini na kuridhika kuwa chama hicho kimebeba matumaini mapya ya wazanzibari.

Mhe. Mansour ambaye tayari alishateuliwa na chama hicho kuwa mshauri wa mikakati wa Katibu Mkuu wa CUF, amechukua kadi hiyo akiwa miongoni mwa wanachama wapya 108 waliojiunga na CUF kwenye mkutano huo.

Mapema akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, amempongeza Mhe. Mansour kwa kuamua kujiunga na chama hicho hadharani, na kukiita kitendo hicho kuwa ni cha kijasiri.

Akizungumzia mafanikio ya chama hicho, Maalim Seif amesema kimepata mafanikio makubwa katika mwaka unaomalizika wa 2014, na kutangaza maazimia mapya ya chama hicho kwa mwaka 2015.

No comments: