Tuesday, 20 January 2015

MTIKILA AMEWEZA KUANDIKA HISTORIA YA UTETEZI TANZANIA


Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeandika historia katika nchi yetu, baada ya kutoa hukumu iliyohitimisha safari ndefu ya wananchi kutaka wagombea binafsi waruhusiwe katika chaguzi za serikali za mitaa, ubunge na urais. Tunasema mahakama hiyo imeandika historia kutokana na suala hilo kukataliwa na Serikali yapata zaidi ya miongo minne sasa, hata pale mahakama za juu nchini zilipotamka kwamba kuwapo kwa mgombea binafsi ni haki ya kila raia kikatiba.Pengine wananchi wengi hawajui kwamba nchi yetu iliwahi kuwa na wagombea binafsi. Katika Uchaguzi Mkuu wa vyama vingi wa mwaka 1960, chama tawala cha TANU kilipoteza kiti cha ubunge katika Jimbo la Mbulu, baada ya Herman Elias Sarwatt aliyegombea kiti hicho kama mgombea binafsi kushinda.
Ushindi huo na mwingine wa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani ulikishtua chama hicho tawala na ndipo kilipotumia wingi wa wabunge wake bungeni kubadilisha Katiba na kufuta vyama vya upinzani na wagombea binafsi, hivyo kuifanya Tanganyika nchi ya utawala wa chama kimoja.Hivyo kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kuliibua suala la mgombea binafsi. Serikali iliendelea kumkataa mgombea binafsi, ikisema lazima kila mgombea awe mwanachama wa chama cha siasa. Ndipo mwaka 1993 Mchungaji Christopher Mtikila alipofungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma iliyosikilizwa na Jaji Kawha Lugakingira ambaye alikubaliana na hoja zake, kwamba kugombea kama mtu binafsi ni haki ya kila raia kwa mujibu wa Katiba, kwa maana ya haki ya kuchagua viongozi na haki ya kugombea uongozi.
Lakini katika hali ya kushangaza mwaka 1994, Serikali kwa kutumia wingi wa wabunge wake bungeni ilihakikisha chombo hicho kinafanya mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 kwa kuzuia wagombea binafsi. Ndipo mwaka 2005, Mchungaji Mtikila alifungua kesi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam akipinga marekebisho hayo ya Katiba. Hatimaye, jopo la majaji watatu chini ya Jaji Kiongozi, Amiri Manento lilikubali hoja za Mchungaji Mtikila na kuruhusu mgombea binafsi.Iliwashangaza wengi mwaka 2010 kuona Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufaa. Majaji saba wa mahakama hiyo walisikiliza kesi hiyo chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu Augustino Ramadhani. Serikali ilidai katika rufaa yake kwamba hakuna mahakama yoyote nchini yenye uwezo kisheria kusikiliza kesi inayotaka mgombea binafsi na kwamba mahakama za chini zilijipachika madaraka ya kibunge ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri. Katika hukumu iliyokosolewa na wengi, mahakama hiyo, pamoja na kukubaliana na hoja ya haki ya kila raia kuchagua au kuchaguliwa bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa, ilisema siyo jukumu la mahakama kujielekeza katika masuala ya kisiasa.
Ndipo Mchungaji Mtikila alikata rufaa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliyoko Arusha na Juni mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa mrufani na kuitaka Serikali ya Tanzania kutoa taarifa ndani ya miezi sita kuhusu namna inavyotekeleza hukumu hiyo.Ni jambo jema sasa kwamba Serikali imesema imo katika mchakato wa kisheria utakaoruhusu mgombea binafsi. Sisi tumetiwa moyo na hali hiyo na tunaitaka Serikali itambue kwamba suala hilo halina mjadala tena.

No comments: