Sunday, 8 February 2015

SERIKALI YA CCM NA MBINYO WA HAKI ZA WAISLAMU

Aibu ya Watawala? Hakuna Viongozi wa Dini Ambao ni Wanawake?
Muungano wa Jumuiya ya Kiislamu Tanzania, umesema hautoshiriki katika Kura ya Maoni ya Katiba  Inayopendekezwa, mpaka serikali itakapotatua tatizo lao la kupitishwa kwa Mahakama ya Kadhi ndani ya Katiba hiyo.  Akisoma Tamko hilo jana jijini Dar es Salaam, lililosainiwa na Makamu Mwenyekiti wa taasisi ya Hay Atul (Ulamaa), Sheikh Abdallah Bawazir, Naibu Katibu wa Jumuiya ya Jashura ya Maimu, Rajab Katimba, alisema endapo serikali itapuuza tamko lao, basi watasusia mchakato huo.
Katimba, alisema muungano huo unazihusisha taasisi zaidi ya 11, zikiwamo Baraza Kuu, Jumuiya ya wanataaluma wa Kiislamu nchini (Tampro), Baraza la Taasisi za Answar Sunnah Tanzania (Basuta), Jamaat Answar Sunna nchini (Jasuta),Taasisi  ya kuweka na kukopa (IPC ), Umoja wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Haiyat Ulamaa), pamoja na Shura ya Maimam Tanzania.  
Alisema, maamuzi hayo yamekuja  baada ya taasisi hizo kutoa maoni  kuhusu muswada wa mahakama ya kadhi, ambapo yalipatikana baada ya mchakato uliowahusisha wanachama na wawakilishi wa asasi hizo nchi nzima.  
“Hivyo siyo kweli kwamba taasisi hizi zinawakilisha maoni ya wachache bali hoja yetu inadhihirisha hofu ya mshikamano wa muungano huo katika kukabiliana na suala zima la Mahakama ya Kadhi,” alisema Katimba.
Alisema serikali imekuwa ikiyatumia makundi ya taasisi za kiislamu katika kipindi cha uchaguzi, kama ilivyokuwa 2010, ambapo iliahidi ingeruhusu uwapo wa Mahakama ya Kadhi, lakini baada ya uchaguzi suala hilo halikutekelezwa.  Kadhalika, aliishawishi serikali kutowalazimisha waumini wa kiislamu kumkubali Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, kama kiongozi wao mkuu na ndiye anayestahili kuteua makadhi  nchini jambo amabalo sio sahihi, kwasababu kila  taasisi  ina  muundo wake.
Alifafanua kitendo cha kumshinikiza Sheikh Mufti, kutambulika kama kiongozi mkuu wa waislamu, mwenye malmaka ya kuteua makadhi  yanalenga kupotosha hoja ya msingi , kwani hana mamlaka yoyote yanayohusu Mahakama ya Kadhi. “Mufti huyu awe wa Bakwata au taasisi nyingine siyo chombo kinachoundwa na sheria bali taasisi husika, hivyo kitendo cha Mahakama ya Kadhi kuwekwa chini ya Mufti, ni kuifanya mamlaka hiyo muhimu ya kutoa haki kuwa chombo kilicho chini ya taasisi binafsi.  Katika hilo, alisema Ibara ya 20 (1), ya Katiba ya Tanzania, inatoa uhuru wa kujumuika na kujiunga katika jumuiya mbalimbali, hivyo  kuendelea kuwalazimisha  waislamu kuwa chini ya Bakwata, au katika taasisi ya Mufti, ni kuvunja katiba hiyo.

No comments: