Ni wasomi, wanasheria, viongozi wa dini Imeonyesha ukomavu wa hali ya juu Wasomi, wanasheria na viongozi wa dini wamesifu uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuonyesha ukomavu wa kutangaza kuahirisha zoezi la kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na kukataa kuburuzwa. Hatua hiyo, imekuja siku moja tu baada ya NEC kutangaza kuahirishwa kwa zoezi hilo kwa muda usiojulikana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana na NIPASHE, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani, Benson Banna alisema kuwa Tume hiyo imeonyesha ukomavu wa hali ya juu na imetambulika kama tume huru isiyosukumwa na maslahi ya kisiasa. “Tunaipongeza tume ya uchaguzi kwa kufanya maamuzi magumu kinyume na mawazo ya wengi, na iko kwa maslahi ya Watanzania na sio kisiasa,” alisema Banna. Alisema viongozi wa juu walitaka Tume ikubali kupiga kura ya maoni mwezi huu, lakini imethamini maslahi ya wananchi na sio ya chama wala ya kisiasa. Mkurugenzi wa Nyerere Foundation, Joseph Butiku, alisema kuwa Watanzania watapata muda wa kukamilisha zoezi la uandikishaji kwenye daftari la wapiga kura. Alisema kuwa muda utatosha kwa wananchi kuisoma Katiba inayopendekezwa na kufanya maamuzi sahihi, kulinganisha maoni ya Tume ya Jaji Warioba na yale yaliyoandikwa na Tume katika Rasimu ya pili ya Tume.
”Hakuna haraka ya kuchanganya kura ya maoni na uchaguzi mkuu ni vizuri kura ya maoni ifanyike baada ya uchaguzi mkuu, haraka ya nini,” alihoji. Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia, alisema Tume imeonyesha kuwa ni huru. Alisema hivyo ndivyo inavyotakiwa kusimamia masilahi ya wananchi na kutokubali kunyang’anywa madaraka. Alisema kuwa Tume hiyo inatakiwa kuongezewa nguvu wakati wa kikao cha Bunge lijalo ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya Katiba iliyopo ili kuwezesha uchaguzi mkuu kufanyika. Sungusia alisema kuwa mambo yanayotakiwa kufanyiwa marekebisho wakati wa kikao cha Bunge ni pamoja na kuhakikisha usawa wa viti 50/50 kwa wanaume na wanawake, tume huru ya uchanguzi, kuruhusu vyama kuwa na umoja unaotambulika, kupunguza madaraka ya Rais, kuwapa wananchi haki ya kuwawajibisha wabunge wao. Juzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza uamuzi wa kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyopangwa kufanyika Aprili 30, kutokana na kutokamilika kwa uandikishaji wa Daftari la Wapiga kura kwa kutumia treknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR).
KKKT YASIFU
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma limesema kuwa kuahirishwa kwa kura ya maoni kumewaondolea Watanzania kuburuzwa kuipigia kura ya maoni Katiba inayopendekezwa.Kauli hiyo imetolewa na Msaidizi wa Askofu wa kanisa hilo, Mchungaji Samweli Mshana wakati alipokuwa akihubiri kwenye ibada ya Ijumaa Kuu ya Pasaka iliyofanyika kanisa la KKKT Usharika wa Dodoma mjini. Alisema kuwa hatua hiyo itawawezesha Watanzania kuisoma na kuielewa kwa makini katiba hiyo. “Kwa kweli tuna kila sababu ya kuipongeza NEC kwa uamuzi huo ambao kwa upande wa baadhi ya viongozi walitaka kutupeleka kama mifugo inayoenda kuchinjwa bila wao kutambua,” alisema Mshana. Alisema serikali inatakiwa kuelewa kuwa Katiba hiyo iliyokuwa ikipigiwa makelele ni mali ya Watanzania wote na si baadhi ya viongozi.
Aidha, akihubiri katika ibada hiyo alizishukuru pia taasisi mbalimbali zikiwamo madhehebu ya dini pamoja na mashauriano ya mwanasheria mkuu wa zamani Mark Bomani kwa kuweza kuishinikiza NEC itangaze kuahairishwa. Wakati huo huo, Mchungaji huyo amelaani tukio la kushambuliwa na kuuawa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya ambapo zaidi ya wanafunzi 70 waliuawa huku wengine 80 wakijeruhiwa na kundi la Al Shabaab. Alisema tukio hilo linafundisha Watanzania kuendelea kuilinda na kuombea amani iliyopo ili mauaji ya aina hiyo yakomeshwe na wahusika wamgeukie Mungu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment