Thursday, 25 June 2015

Augustino Ramadhani: Kutoka Brigedia Jenerali, Jaji Mkuu hadi uchungaji sasa anataka Uraisi !


Jaji Augustino Ramadhani akiingia katika Kanisa la Anglikana Zanzibar kuendelea na huduma za kutangaza neno la Mungu.
KWA UFUPI
  • Watu wengi hutumia jina la cheo juu kabisa alichopata kukitumikia katika  moja ya kipindi cha uhai wake na anapenda kuitwa  hivyo hadi uzeeni mpaka siku ya mwisho wa maisha yake hapa duniani ingawa wengine hupenda kuwa na jina la kazi ya kwanza aliyoanza kufanya, mfano Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
 

Z.Baba wa Taifa alipendelea sana kuitwa Mwalimu, kazi aliyoanza kufanya kabla ya kuwa Rais wa kwanza na hadi anastaafu urais jina la Mwalimu hakuliacha hadi mauti yalipomkuta.
Hii inakuwa ni vigumu kwa mtu aliyetumikia nafasi nyingi kwa nyakati tofauti na kwa mafanikio mazuri, nasema mazuri kwa sababu Jaji Augustino Ramadhani aliyestafu Ujaji Mkuu alipaswa pia kuitwa Brigedia Jenerali kwa kuwa pia alilitumikia Jeshi hadi kufikia ngazi hiyo ya Brigedia Jenerali kabla ya kuitwa katika sekta  ya sheria na kutumikia Mahakama hadi kufikia ngazi ya juu kabisa ambayo pia wengi hupenda kuandikwa kwa vyeo walivyowahi kutumikia na kwa sasa amepewa kazi ya ukasisi.
Mbali na kustaafu ujaji, wiki iliyopita alipewa kazi ya ukasisi, alitawazwa rasmi kuwa Mchungaji wa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana lililopo Mkunazini Zanzibar  na hivyo kustahili kuitwa cheo cha Mchungaji Augustino Ramadhani.
Mchungaji Augustino aliiambia Mwananchi kuwa alizaliwa Visiwani Zanzibar, Mtaa wa Kisima Majongoo kwenye familia ya watoto wanne wa Mwalimu Mathew Douglas Ramadhani na Bridget Anna Constance Masoud akiwa ni mtoto wa pili katika familia hiyo, aliishi kwa miaka mitatu Visiwani huko na kisha alikuja Tanzania Bara (Tanganyika) akiwa na umri wa kuanza masomo hadi alipohitimu  masomo ya sekondari katika Shule ya Wavulana Tabora na wakati akiwa sekondari ndipo alilpojifunza kupiga kinanda akirithi kipaji cha babu yake Augustino Ramadhani.
Jaji Ramadhani alihitimu elimu ya sekondari mwaka 1965 na kujiunga na elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika fani ya sheria hadi mwaka 1970 alipojiunga katika Jeshi la kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, baadaye aliajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) alikofanya kazi za sheria.
Mafanikio zaidi
Alifafanua kuwa aliitwa na aliyekuwa Rais wa pili wa visiwa hivyo, Alhaji Aboud Jumbe mwaka 1978 na kumteua kuwa Naibu Jaji Mkuu kabla ya kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mwaka huo huo aliitwa tena jeshini kwa ajili ya kushiriki vita ya Kagera, alipelekwa Uganda na kukaa kwa zaidi ya miezi kumi.
Baada ya vita kumalizika alirudi Tanzania kuendelea na kazi katika sekta ya Sheria na mwaka 1980 aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Anasema, mfumo wa Mahakama  Visiwani haukuwa wa kisheria na alifanikiwa kuubadilisha na kuweka mfumo wenye ngazi za Kimahakama kutoka Wilaya,  Mkoa hadi Mahakama Kuu. Anabainisha kuwa hii ilitokana na kutokuwepo na watu waliosomea sheria ili kuajiriwa katika sekta ya sheria.
“Nilifanikiwa kuondoa mfumo wa mabaraza (Peoples Court) na kuweka mfumo wa mahakama uliofuata ngazi za kimahakama na mahakama ya Rufaa haikuwepo kabisa”, anasema.
Pia aliapishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa mwaka 1989, mwaka 1990 alihamia jijini Dar es Salaam na Mwaka 1993 hadi 2003 aliteuliwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania Bara na mnamo mwaka 2002-2007  aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na katika kipindi hicho hicho alikuwa mmoja wa Majaji sita wa Mahakama ya Afrika Mashariki, pia alikuwa ni mmojawapo wa Majaji 11 waliochaguliwa na Marais wa Afrika kwa ajili ya kuitumikia Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na ndipo mwaka 2006 alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Baada ya kustaafu kazi ya Ujaji Mkuu mwaka 2010, Jaji Augustino Ramadhani alikataa kuendelea na kipindi kingine baada ya kufanikiwa kufafanua kifungu kinachokataza Jaji kuendelea na kazi ya Ujaji baada ya umri wake wa kustaafu na kuendelea kwa  mkataba  wa ajira, ila anaruhusiwa kuongeza kipindi kimoja tu hata kama bado anazo nguvu za kutumikia Taifa.Mara baada ya kusimikwa kuwa Mchungaji anasema,  hakuna tofauti kati ya kazi ya Mahakama na kazi ya  Uchungaji kwani zote ni kazi za kufanya maamuzi ya watu wanaodai wapatiwe haki na kubainisha kazi za mahakama ukiamua umeamua ila za kanisa zinataka makubaliano na maridhiano japo zote ni kazi za Mungu.
“Kazi hii ya uchungaji mimi sikuifikiria hata siku moja kwamba nitaifanya ingawa nilisomea nchini Uingereza  na kutunukiwa stashahada. Pia nilikuwa nikishiriki katika shughuli za madhabahuni hasa wakati wa kuwasimika maaskofu kwa kuwa nilikuwa mwanasheria wa kanisa hili hadi nilipoteuliwa kuwa Jaji Mkuu ndipo nilipoamua kuacha wadhifa huo ili kuepuka migongano,”anasema Jaji Ramadhani.
Atafutwa
“Askofu alinifuata mara kwa mara ingawa nilikuwa nikimkatalia lakini mwisho nilikubali kwa kuona kuwa ni sauti ya Mungu iliyokuwa ikiniita kupitia kwake na ndio  leo hii baada ya kutumikia ushemazi kwa zaidi ya miezi sita  nimesimikwa rasmi kuwa mhudumu wa madhabahuni.”.Kwa upande mwingine Jaji anasema, lengo lake lilikuwa baada ya kustaafu akafundishe na lengo hilo limetimia kwani pia kwa sasa ni  Makamu Mkuu wa Chuo cha Tumaini Iringa anapofundisha sheria.Pia itakumbukwa kuwa wiki hii amekamilisha kazi ya kuunda rasimu mpya ya katiba alipoteuliwa mwaka jana kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.
Hali ya Zanzibar
Akizungumzia hali ya vugu vugu la hali ya visiwani humu kuhusu kushambuliwa kwa viongozi wa dini na kuharibiwa kwa nyumba za ibada anasema tangu miaka ya nyuma akiwa mdogo anakumbuka jinsi walivyokuwa wakishirikiana vizuri na majirani zao kuadhimimisha sikukuu za kidini bila kujali tofauti ya za dini.
“ Nakumbuka wazazi wangu walikuwa wanamwita Mwislamu kuja kuchinja kuku ili wasikwazike wanapokaribishwa kujumuika katika chakula, kwa kuwa walijua kuwa nyama wanayokula  imechinjwa kwa taratibu za dini yao na haitamkwaza na wao pia walikuwa wakitualika kwenye sikuku zao na tulikuwa tukifurahia pamoja.”
Mwananchi pia ilishuhudia amani iliyokuwepo wakati misa ya kumwapisha Jaji Mstaafu Augustino Ramadhani ilipokuwa ikifanyika na hakuwa na uvunjivu wa aina yoyote ya amani licha kuwepo na ulinzi wa kawaida na hakukuwa na Polisi  kama ilivyokuwa wakati wa mkesha wa Siku Kuu ya Krismasi.Wageni walikuwa wengi na kanisa lilijaa watu waliokuja kushuhudia tukio hilo la kusimikwa kwake.

No comments: