Thursday 25 June 2015

Mjadala Mkubwa ulioikumba CCM ZANZIBAR na wanaharakati wa Zanzibar juu ya kuingia kwa Augustino Ramadhani kwenye Mbio za Urais wa Muungano ?




Jaji Augustino Ramadhan
                                                  Jaji Augustino Ramadhan Na Ahmed Rajab CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) ni marekebu inayoelea shelabela katika bahari iliyochafuka. Imo safarini, ikipanda na kushuka juu ya mawimbi yenye hasira, ikiwa haijui tena iendako au hata ilikopanga kwenda.
Si siri kwamba chombo hicho kimepoteza dira. Tena kina manahodha wengi. Na kama wajuavyo wenye uzoefu wa ubaharia, penye manahodha wengi, chombo huenda kikenda mrama.Inavyoonyesha ni kuwa, kwa kila hali, chombo hicho kinajiendesha kitatanishi.  Hata hivyo, yaliyokifika CCM huvifika vyama vya siasa vyenye kuselelea kwa muda mrefu madarakani. Chama aina hiyo hujisahau na, hatimaye, wafuasi wake nao hukisahau.Si kwamba vyama hivyo huwa havina walio wazuri. Huwa nao. CCM nacho kina wazuri wake. Kina makada wanaoweza kukiokoa. Ni watu wenye uwezo na fikra za kuipatia nchi maendeleo kwa njia za kidemokrasia.Kwa bahati mbaya, watu wa aina hiyo hukabwa na mfumo wa chama. Wanalazimika kufunga midomo yao kwa sababu ya namna chama kinavyoiendesha nchi kupitia viongozi wake walio serikalini.
images
Tunaweza kuwalinganisha viongozi aina hiyo wa CCM na wa vyama vya Kikomunisti vya nchi kadhaa za Ulaya ya Mashariki kabla ya utawala wa Kikomunisti kuporomoka.  Vyama vya nchi hizo navyo vilikuwa na wazuri wao. Lakini yao yalikuwa ni macho tu.Walijizuia kufungua midomo wakichelea wasinyang’anywe njia za kuendeshea maisha. Wakiogopa, kwa vile mfumo wa kuendesha nchi, kutoka ngazi za juu mpaka chini, ukidhibitiwa na chama. Hata hivyo, walikuwepo makada jasiri waliothubutu kukiambia chama chao ukweli ambao viongozi hawakutaka kuusikia. Nitatoa mfano mmoja tu wa Rudolf Bahro, kada wa chama cha Kisoshalisti cha SDE, kilichokuwa kikitawala Ujerumani ya Mashariki. Chama hicho kikifuata nadharia ya Umarx.
jaji
Bahro alikuwa mpinzani wa sera za kijamaa za chama chake. Si kwamba hakuwa akiiamini itikadi ya Umarx lakini akisema kwamba huo mfumo uliokuwa ukifuatwa na chama hicho haukuwa mfumo wa kijamaa. Akiamini kwamba ulikuwapo mfumo mbadala wa ujamaa, wa ujamaa wa kweli.Bahro alikuwa na hoja zake za kinadharia. Aidha, alikuwa na maswali mengi ya kuwauliza wakuu wa chama chake. Aliyauliza kwa ujasiri na uwazi. Bahro aliandika kitabu kilichochapishwa Ujerumani ya Magharibi 1977 akielezea msimamo wake wa siasa mbadala.

images (1)
Baada ya kitabu hicho kuchapishwa alikamatwa na akashtakiwa kwa uhaini. Alihukumiwa kifungo cha miaka minane. Aliachiwa 1980, akaruhusiwa kwenda kuishi uhamishoni Ujerumani ya Magharibi ambako nako akihubiri siasa zilizokuwa zikenda kinyume na mfumo tawala.Aghalabu wanapochomoza wanasiasa kama Bahro ndani ya vyama vilivyochoka ndipo vyama hivyo vinapoanza kumomonyoka. Waasi walio chamani ama hufukuzwa au hutoka chamani kwa hiyari yao. Halafu hukimbilia upande wa upinzani na kuunda vyama vipya au hujiunga na vingine, kama vipo.
unnamed (34)
Baada ya kuporomoka kwa mfumo wa Kikomunisti katika Ulaya ya Mashariki viliundwa vyama vyingi vya kisiasa vilivyotaka kuleta maendeleo ya demokrasia. Wengi wa viongozi wao walikuwa makada wa vyama vilivyokuwa vikitawala Viongozi hao walionyesha ujuzi na uwezo wa kuendesha vyama, na hata nchi, kwa njia za demokrasia. Mfano mzuri ni viongozi waliochomoza Hungary na Bulgaria. Tanzania pia tunao viongozi wa upinzani waliowahi kuwa makada au viongozi wa CCM. Ndio maana mara kwa mara huendesha mambo ki-CCM. Hufanya hivyo kwa sababu ya mazoea yao ndani ya CCM walikolelewa kisiasa.Kama nilivyokwishagusia, wapo viongozi walio wazuri ndani ya CCM. Mmoja ni waziri wa zamani aliyezungumzwa kwenye toleo la wiki iliyopita la Raia Mwema. Huyu alikataa kuingia katika kinyang’ariro cha urais baada ya kuahidiwa shilingi bilioni nne afanye hivyo.
ja3
Mwanasiasa huyo alisema waliompa ahadi hiyo walikuwa ni wafanyabiashara. Unajiuliza: kwa nini wafanyabiashara hao wazitolee mhanga fedha zote hizo?
Kuna na mwengine aliyetangaza nia ya kuwania urais na aliyeliambia Raia Mwema kwamba aliukataa mchango wa shilingi bilioni moja aliopewa na mfanyabiashara anayehusishwa na ufisadi.Unajiuliza tena: kwa nini mfanyabiashara huyo alikuwa tayari kumsabilia mwanasiasa huyo shilingi bilioni moja? Akitaraji alipwe nini baadaye? Mifano hiyo miwili ni ushahidi kwamba CCM hakina ukosefu wa makada walio waadilifu. Wamo hata miongoni mwa orodha ya wanachama wake wasiopungua 37 walio katika mbio za kuuwania urais.Orodha hiyo ina viongozi wa sampuli nyingi. Ina waliochoka. Ina wasiojiamini. Ina magarasa.  Inayo pia watu waliokaa kama waliojivisha vinyago usoni. Huwajui wao hasa ni nani na pengine hata wenyewe hawajijui.

Na kuna wenye kuonekana kuwa ni waadilifu. Mmojawao ni Agostino Ramadhani, Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar na Tanzania, aliyekuwa Brigadia-Jenerali jeshini na aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake makuu Arusha.
unnamed24
Anajijuwa yeye ni nani, anakijuwa anachotaka kukitekeleza na, muhimu zaidi, anajiamini. Anasifika kuwa si mtu wa makundi, si mtu wa majungu. Simtaji yeye kwa sababu ni Mzanzibari mwenzangu kwani Makamu wa Rais, Dakta Mohamed Gharib Bilal, naye pia ana uwezo wa kuliongoza taifa la Tanzania. Kadhalika, kama alivyo Ramadhani, hajaguswa na ufisadi wala shutuma nyingine za uovu.Wana CCM walioazimia kukisafisha chama chao wanataka Rais atayetoka kwao awe na sifa fulani. Miongoni mwazo ni kwamba mtu huyo asiwe na hata doa la ufisadi, akubalike pande zote mbili za Muungano na, zaidi ya yote, akiweze kibarua cha kuizuia Zanzibar isiponyoke kutoka kwenye mikono ya Muungano.
Wanaamini kwamba Ramadhani anazo sifa zote hizo.
Agostino Ramadhani alianza kutajika alipochomolewa na Rais wa zamani wa Zanzibar Aboud Jumbe kutoka Bara, alipokuwa mwanasheria jeshini, na kurejeshwa kwao. Kwanza alipelekwa Pemba kuyasimamia mahakama kisiwani humo. Siku hizo mfumo wa kisheria na muundo wa mahakama ulikuwa dhaifu sana visiwani Zanzibar.huko Zanzibar alikuwa Jaji Mkuu kwa kipindi cha takriban miaka kumi na alifanya mengi kuurejesha mfumo wa kisheria uliokuwa umechafuliwa baada ya Mapinduzi ya 1964. Ni yeye aliyechukuwa hatua za mwanzo za kuwaruhusu mawakili warudi kufanya kazi visiwani humo. Walikuwa wamepigwa marufuku tangu baada tu ya Mapinduzi.
Huko Zanzibar ndiko alipozidi kuonyesha uungwana wake na jinsi anavyochukizwa na rushwa. Nimehadithiwa kwamba safari moja aliwahi kukwaruzana na Rais wa zamani Idris Abdulwakil pale Rais alipompelekea kijibarua kumtaka abadili hukumu aliyoitoa mahakamani kuhusu umilikaji wa ardhi. Ramadhani alisimama kidete na, inasemekana, mwishowe Abdulwakil alimtaka radhi.Ni mtu mwenye heshima kubwa, na jinsi anavyouchukia ufisadi na ulaji rushwa anajulikana kwamba si mtu wa kusaidia rafiki wala jamaa. Ni mtu aliyefanya mengi kuubadili mfumo wa Mahakama ya Zanzibar.Alipokuwa Jaji Mkuu visiwani, mawaziri na wakuu wengine wa serikali walipewa magari ya fahari ya aina ya Nissan Gloria, ambayo mitaani watu wakiita “michele” au “mitumba”. Ramadhani hakupewa. Lakini hakulalamika apewe. Ni waziri kiongozi wa siku hizo, Seif Sharif Hamadi, aliyeidhinisha apewe na awekewe mlinzi.Agostino Ramadhani alizaliwa Unguja na ni mtu aliyechanganya damu kwa kuukeni kwake. Mama yake mzazi, Mama Bridget, aliyefariki Februari mwaka huu, ni mzalia wa Pemba aliyehamia Unguja baada ya kuolewa.Baba yake, Mathew Ramadhani, alikuwa mwalimu wa skuli. Alifariki katika ajali ya treni jijini London alikopelekwa na serikali ya Kikoloni kwa masomo ya juu katika miaka ya 1950. Baada ya kifo cha babake, ami yake, Askofu Mstaafu John Ramadhani, ndiye aliyejitwika dhamana ya kuisaidia kifedha familia yao. Hadi leo John Ramadhani ndiye mshauri mkuu wa Agostino kwa mengi.Agostino Ramadhani amekulia Bara alikosoma, akafanya kazi na kuoa. Mkewe, Saada Mbarouk, ambaye pia alikuwa mwanajeshi wa cheo cha juu, ametokea Arusha. Mara zote Ramadhani amekuwa akijiandikisha na kupiga kura Bar. Ingawa yeye ni Mkristo wa madhehebu ya Kiprotestanti, hata hivyo baadhi ya jamaa zake wa karibu sana ni Waislamu na kuna mmoja aliwahi kuwa Mwislamu akatanasari.Kwa vile anaonekana kuwa ni mtu mpole, kuna wanaohofia kwamba endapo atakuwa Rais anaweza akatawala chini ya kivuli cha Rais mstaafu Benjamin Mkapa kwani ni watu wenye kusikilizana sana.Kweli ni mpole lakini hakubali kuonewa. Ikimlazimu, na akitaka, anaweza kujigeuza paka shume na akaparura ingawa kwa kutumia sheria na si kwa makucha ya chuma.Chambilecho mwenyewe alipohojiwa karibuni katika Radio ya Sauti ya Ujerumani na kuambiwa kwamba yeye ni mpole kuhimili changamoto za urais. Ramadhani alijibu hivi:“Mimi nimeshakuwa jeshini na kufikia cheo cha Brigadia-Jenerali. Nimeshakuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na wa Muungano, sasa sijui hao wanaozungumza kuwa mimi ni mpole wana maana gani. Sijui wanataka mtu upige watu viboko? Kiongozi anaongoza nchi kwa kufuata sheria ya nchi.”Ramadhani anazungumza lugha fasaha na akizungumza unamsikiliza kwa sababu ana sauti ya kuaminika.
Anakumbukwa Zanzibar kwa kuanzisha mpango wa kuwafundisha watu sheria kwenye jengo la iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ambalo sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA). Waliohitimu masomo hayo wakitunukiwa stashhada.Ni mchungaji, mzee wa kanisa na mpiga piano na kinanda hodari kanisani. Siku hizi hupiga kinanda katika kanisa la St.Albino, Dar es Salaam, na hata alipokuwa Zanzibar yeye ndiye aliyekuwa mpiga kinanda katika kanisa la Mkunazini. Kadhalika, alikuwa mwalimu wa kwaya Mkunazini na St. Albino.Wazanzibari wenzake watamtaka, sio yeye tu bali mgombea yeyote wa urais, aeleze wazi kuhusu msimamo wake juu ya suala la Muungano. Ingawa alikuwa kaimu mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu, si lazima kuwa huo ndio msimamo wake yeye mwenyewe binafsi. Kwa hakika, inavyojulikana ni kuwa yeye ni muumini mkubwa wa mfumo wa Muungano wa Serikali mbili kuelekea moja.Kwa sababu hiyo, Ramadhani anaonekana kuwa ni “mpini” madhubuti wa kutumika katika jitihada za kuidhibiti Zanzibar isifurukute; na hatimaye kuhakikisha kuwa inamezwa kabisa ndani ya tumbo la Tanganyika.Kuna wenye kumtia dosari kwamba baadhi ya hukumu alizowahi kuzitoa alipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania zinathibitisha kuwa yeye ni mwanasheria mwenye utashi wa kuibeba na kuiunga mkono Serikali hata kama kufanya hivyo ni kwenda kinyume na tafsiri sahihi ya sheria au maslahi mapana ya Taifa. Wanaitaja hasa ile hukumu aliyoitoa kuhusiana na mgombea huru asiye na chama katika uchaguzi wa urais wa Tanzania.Juu ya yote hayo, Ramadhani anazo sifa za kumfanya aungwe mkono na wenye kufikiri kuwa anaweza kuisaidia CCM iwashinde wapinzani na kuwafanya Watanzania walio wengi waamini kuwa wamepata mgombea msafi, mwenye kuwachukia mafisadi na wala rushwa; na, akiipita mitihani yote inayomkabili na akachaguliwa Rais, atauimarisha Muungano.

CHANZO: Raia  Mwema

No comments: