Monday, 20 July 2015

Vipi Magufuli aliwaangusha Wagombea Wenzake ?


Kwa mara nyengine tena siasa imejidhihirisha katika uso wake wa pili. Kwamba uso wa kwanza wa makeke, matangazo na majigambo husaidia kulea ushindi, lakini uso wa pili wa mbinu za chini, kimya kimya nao pia ni mkakati wa kuelekea ushindi. Tumeona staili mbili tofauti za kuelekea kupata mgombea mmoja wa CCM ambapo wengi wa wagombea walitoumia gia ya juu kujinadi, kujiuza, kujisogeza mbele ya umma na wanachama wa chama hicho, lakini mtu ambaye alikuja kuwa mshindi hakufanya hivyo kabisa.
John Pombe Magufuli ametangaza nia kimya kimya, amekwenda mikoani kimya kimya na hakuna rekodi yoyoe ile iloonyesha kukutana na waandishi wa habari au kufanya manjojo yoyote yale. Kuna wakati hata mtu aliwea kusahau kuwa Magufuli nae alikwemo katika orodha ya wagombea.
Kwa kuwa waliotumia sana na kupata kuonekana na kusikika haikuwa rahisi mtu wa kawaida kufikiria kuwa Magufuli alikuwa na nafasi katika mbio hizo. Katika hali ilivyoonekana kuwa Magufuli hata kidogo hakuwa akiingia katika 5 bora labda kwenye 10 bora.
Si kwamba walimsahau au hawakumjua machachari yake na makeke yake lakini alichagua kutojiuza hadharani nap engine sasa inadhihirika kuwa pengine mbinu zake zilikuwa zikienda mbali zaidi na kama wenzio waliotumia pesa kwenye matangazo yeye pengine alitumia kama ni pesa kuwafika watu au kupenyea kujenga msingi.Maana pia Magufuli hakuonekana katika jicho la jumla kuwa na msingi wa chini na ndani kwenye chama kulinganisha na wale waliokuwa wakitajwa zaidi, pamoja na kwamba aliingia chama hicho cha CCM awali kabisa kilipoanzishwa akiwa kijana mbichi hapo 1977.
Labda kule kutoshika nafasi za wazi za kichama katika ngazi za juu kabisa ndiko kulikoonekana kukisiwa kuwa hana mashiko makubwa kichama, kumbe watu walisahau kuwa Kanda ya Ziwa ni kanda yenye nguvu na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania, na maamini Magufuli alifanya kazi sana eneo hilo.
Pia siasa za mwaka huu zimetufahamisha kuwa mwanasiasa anaweza kuwa kama fisi ambaye hufaidika kwa mzoga na ikawa ndio shibe yake na kupata chakula bila hata taabu ya kuwinda, na ndio ilivyokuwa kwa Magufuli, ila sijui kama hilo lilikuwa ni sehemu ya mkakati wake.
Hali ilionekana wazi kuwa watu waliokuwa wakitajwa mbele walikuwa na mvutano mkubwa kupita kiasi na kwamba mpasuko baina yao ulikuwa dhahiri na hata ulitishia kukigawa chama hicho kikongwe kuliko vyote nchini. Na hata baada ya kupata mgombea wake na kujitahidi kuziba mpasuko huo lakini ni hakika kuwa upo na kama kuzibwa ndio utazibwa kuelekea kwenye ushindi wao dhidi ya UKAWA iliyotokana na madai ya Katiba Mpya nchini.
Kwa hivyo alipofanikiwa tu kupenya katika 5 bora Magufuli au watu wake ama walisubiri mdondo wa mzoga kutokana na kambi zilizoshindwa hasa kambi iliyokuwa kubwa kabisa au waliifuata hasa na kuwa na mazungumzo nayo kuwa ihamishie kura zao kwenye kambi yake. Na hili si ajabu kwenye siasa.
Inawezekana kabisa makubaliano hayo yalifanywa na ushahidi wa hilo utakuja kuonekana jinsi ambavyo timu ya kampeni ya Magufuli itavyoundwa na pia pale atakapouunda Serikali yake kama akishinda na ulipaji wa hisani ya kusogezewa wapiga kura utaoonekana, nalo pia siajabu.
Maana katika hali ya kawaida, haiingia akilini kabisa ghafla moja Magufuli aibuke na kitita cha kura Halmashauri Kuu na kisha agonge asilimia zaidi ya 80 kwenye Mkutano Mkuu. Sifikiri kuwa mchambuzi yoyote wa siasa anaweza kulipinga hili.
Isipokuwa maelezo mengineyo katika ngazi ya 3 bora ni kuwa aliendelea kupata kura za kambi kuu iliyovunjika katika nia ya kuzikomoa kambi nyengine na pia akafaidi kura za wale ambao hawakuwa na kambi maalum na maamauzi yao yalisubiri dakika ya mwisho.
Nataasafu kusema Magufuli kanyimwa kura za kutoka Zanzibar kwa wingi wake, ambapo naamini walimpigia kwa wingi Bi Amina Salim Ali wakitaraji wangelaza mizani, lakini kura hazikutosha.
Nasema hivi kwa sababu haikuwa imejitokeza Wazanzibari wengi kutajwa kuhusika na Magufuli, kama walikuwepo walifanya siri siri, maana farasi wa Magufuli hakutarajiwa kufika mfundoni.
Tukimtaja Bi Amina tunajifunza jambo jengine katika siasa nalo ni chaguo. Pamoja na Bi Amina kuvutia wengi ndani ya CCM na kudhihirika ana ukomavu na uzoefu, na kutuhbutu kura nyingi,
lakini hakuwa chaguo la Magufuli kuwa Mgombea Mwenza wake.
Kwa hakika wana CCM wasingelalamika hata kidogo kama ikiwa jawabu ni Mgombea Mwenza mwanamke na awe anatoka Zanzibar basi Bi Amina alitosha sana, lakini funzo tuliptalo hapa moja ni lile la fisi ambapo Bi Samia Suluhu alisubiri fupa lidondoke.
Funzo la chaguo ni kuwa mara nyingi maaumuzi kama haya yanakuwa yameshafanywa mara nyingi na dili za chini kwa chini nyingi zimeshafanywa. Chaguo la Magufuli kwa Samia ni chaguo lilofikiriwa sana, ingawa chati ya Samia ilionekana kupanda zaidi kwenye Bunge la Katiba ambapo alikuwa Makamo Mwenyekiti na mwishoni mwishoni alichombezewa hiyo nyimbo ya kuwa Makamo wa Rais, lakini akianzia Mgombea Mwenza.
Naam Team CCM ya Magufuli na Samia imeshajulikana na sasa cha kungojea kwa hamu ni Team UKAWA ya kupambana nayo. Tunataraji kuwa UKAWA hatataduwazwa na chochote, hawatakwazwa na jambo lolote ili vyvoyote iwavyo, tofauti zote walizonazo walimalize ili tupate Mgombea Urais na Mgombea Mwenza.
Wengi tunataraji kuwa UKAWA wanaweza kabisa kuijuburi CCM katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu na kutuhbutu kwa mara ya kwanza kuiondoa madarakani, maana kwa kiasi kikubwa CCM sio tu imechoka lakini ina kiburi cha ushindi wa kila mwaka.
Katika hali ambayo UKAWA inaweza kuwa na nguvu na umoja CCM imefanya makosa mengi, imedorora, imekuwa na jeuri kiasi ambacho inafaa kutiwa adabu kisiasa na kuwekwa benchi ili umma wa Tanzania uweze kuona uendeshaji tofauti wa nchi na sio huu ambao rushwa, upendeleo, ukwepaji kodi, ukiukwaji wa haki za binadamu, kutojali sheria kwa viongozi kuwa ndio mambo yaliotamalaki.
UKAWA inaweza kuivusha nchi hatua nyengine na taifa likaona kumbe tunaweza kutoka katika umasikini uliotopea pamoja na utajiri ambao nchi hii tunao na kuwa basi angalau tufanane miaka yetu ya uhuru, uwezo wa uchumi na taswira ya nchi yetu. Ni aibu nchi hii kuendelea kuomba na tumekuwa ombaomba chini ya CCM kwa miongo mitano sasa.
UKAWA isije ikafanya kosa la kutosikiliza kilio cha umma na chochote kile cha kushindwa kwao kutoa mgombea mmoja itakuwa ni kifo cha kisiasa kwa kila chama na ni kuipa CCM hati miliki ya kuiongoza Tanzania milele, Mungu aliepushe hilo.Imeandikwa na MWandishi Ally Saleh ,Zanzibar 

No comments: