Sunday, 23 August 2015

Kutapa tapa kwa Wanasiasa wanaotaka ubunge .


Modestus Kilufi
Modestus Kilufi
WIMBI la hama hama kutoka katika vyama vya siasa, lililowakumba zaidi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokatwa katika kura za maoni kwenda vyama vya upinzani, limeingia katika hatua mpya, baada ya kada mmoja kujikuta akihamia vyama vitatu ndani ya wiki moja, akisaka fursa ya kugombea ubunge.

Mwanzoni mwa wiki hii, kada huyo wa CCM, mbunge anayemaliza muda wake katika Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi, alianza kuhama chama hicho kikubwa na kikongwe katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya, ambako alitangaza kuhamia CHADEMA.

Kilufi aliyeangushwa katika kura ya maoni ndani ya CCM, alichukua hatua hiyo katika mkutano wa hadhara wa kumtambulisha mgombea wa urais wa CHADEMA, Edward Lowassa, ambaye naye alihamia huko baada ya kuanguka katika kinyang’anyiro cha kusaka mgombea urais kupitia chama hicho tawala.

Hata hivyo, Kilufi ambaye hajatimiza hata wiki moja tangu ahamie CHADEMA na kupokewa na uongozi wa Taifa wa chama hicho na mgombea urais wake, jana alikwenda katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi na kuchukua fomu ya kuwania ubunge kupitia chama cha ACT-Wazalendo.

Msimamizi Akithibitisha hatua hiyo ya Kilufi, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mbarali, Adam Mgoi, alisema mbunge huyo aliyemaliza muda wake, ni miongoni mwa wagombea wanane waliochukua fomu kugombea ubunge ambapo amewakilisha chama cha ACT Wazalendo.

Akizungumzia hatua hiyo ya mwanachama wake mgeni, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph China, alidai Kilufi ni msaliti anayeendeshwa na msukumo wa watu wachache.

China alidai Kilufi ni miongoni mwa wanasiasa wasio na msimamo na wasio wazalendo kwa Taifa lao, ndiyo sababu anapigania maslahi yake binafsi badala ya maslahi ya Watanzania wanyonge.

Hata hivyo, ujio wa Kilufi ndani ya ACT ulionekana kuleta mkanganyiko, baada ya uongozi ngazi ya wilaya kugawanyika katika kukubaliana na hatua hiyo. Mwenyekiti wa ACT, Anzuruni Anzuruni alisema anachojua ni kuwa mwanachama aliyechukua fomu kupitia chama hicho ni James Kamanga na Kilufi hamtambui.

Wakati Mwenyekiti wa ACT akitoa kauli hiyo, Katibu wake, Erasto Sanga, alithibitisha kumpokea Kilufi na kutengua uteuzi wa mgombea wa kwanza. Gazeti hili baada ya kujiridhisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi, Mwenyekiti wa Chadema na uongozi wa ACT, lilimtafuta Kilufi tangu mchana mpaka jioni, lakini simu zake zote ziliita bila majibu.
  • via HabariLeo

No comments: