Saturday, 12 September 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Chama Cha Wananchi (CUF) kinalaani vikali na kwa nguvu zote kitendo cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvuruga mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad uliokuwa ukifanyika jana tarehe 11 Septemba, 2015 kwenye Viwanja vya KwaBinti Amrani, jimbo la Mpendae, Wilaya ya Mjini Unguja.
Kwa makusudi kabisa, wakati mkutano wa kampeni unaendelea na Mgombea Urais, Maalim Seif, akiwa kwenye jukwaa anahutubia, vijana wa CCM walipita kwenye mkutano huo wakiwa na gari la matangazo lenye namba Z 458 GC ambalo lilikuwa linapiga muziki kwa sauti ya juu na kusababisha kuingiliana sauti na hotuba ya mgombea. Kitendo hicho cha uchokozi wa makusudi kilizua tafrani kubwa miongoni mwa wananchi waliokuja kuhudhuria na kusikiliza mkutano huo. Kutokana na hekima na busara kubwa alizo nazo Maalim Seif aliamua kukatisha hotuba yake na kuteremka juu ya jukwaa na hivyo kuuvunja mkutano huo kabla ya muda wake. Busara na hekima za Maalim Seif ziliepusha shari iliyokuwa ikitafutwa na CCM kwa makusudi.
CUF tumesikitishwa zaidi na hatua ya Polisi wakitumia gari mbili za defenders kuipatia ulinzi mbele na nyuma ya gari hiyo ya matangazo ya CCM wakati inafanya uchokozi huo wa makusudi. Hatukutegemea kitendo hicho kufanywa na Polisi. Tulitegemea Polisi ambao ndiyo wenye dhamana ya kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni kuwazuia vijana hao wa CCM na gari yao wasipite eneo lile. Badala yake Polisi ndiyo waliowapa ulinzi vijana hao wa CCM kuendesha hujuma na uchokozi wao.
Baada ya tukio hilo, Mjumbe wa Timu ya Kampeni ya CUF, Ismail Jussa, aliwasiliana kwa njia ya simu na Kamishna wa Polisi Zanzibar na kumueleza juu ya tukio hilo.
CUF tunasema tumesikitishwa na hatua ya Polisi kwa sababu Polisi wakiongozwa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, CP Hamdani Omar Makame, waliitisha kikao kati yao na vyama vya CUF na CCM siku ya Ijumaa, tarehe 28 Agosti, 2015 hapo Ziwani kwenye makao makuu ya jeshi hilo Zanzibar na kuzungumza namna bora ya kushirikiana baina yetu ili kuepusha vitendo vya vurugu na fujo na kuhakikisha tunaendesha kampeni na harakati nyengine za uchaguzi kwa salama na amani.
Ni kwa sababu ya mazungumzo hayo ndiyo maana CUF tokea siku ya uzinduzi wa kampeni zetu tarehe 9 Septemba hadi jana kwenye mkutano huo wa Mpendae tumekuwa tukiwaeleza wafuasi wetu na wananchi kwa ujumla juu ya umuhimu wa kushirikiana kutunza amani na utulivu nchini kwetu. Hatukutegemea kwamba wakati sisi tunafanya hivyo, wenzetu waendelee na vitimbi vyao vinavyolenga kuchafua amani na utulivu ulioonekanwa tokea tumeanza kampeni.
CUF leo hii tutaiandikia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwaeleza juu ya uchokozi huu wa CCM, kuwataka wakionye Chama Cha Mapinduzi juu ya vitendo vyake hivi na pia kuwataka Tume kusimamia ratiba ya kampeni ambayo tulikubaliana kwa pamoja baina ya vyama vyote vya siasa, Tume yenyewe na Jeshi la Polisi katika mkutano ulioandaliwa na ZEC tarehe 4 Septemba, 2015. Pia tutamuandikia Kamishna wa Polisi kumueleza malalamiko na masikitiko yetu kutokana na kitendo cha Polisi wake kushindwa kuwazuia vijana hao wa CCM na badala yake kuwalinda ili waweze kufanikisha uchokozi wao.
Mwisho, CUF tunaendelea kusisitiza kwamba tukiwa chama makini kinachojiandaa kuongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kupewa ridhaa na wananchi wa Zanzibar tutalinda amani na utulivu uliopo na hatutoingia katika mtego wa njama za CCM ambao wamedhamiria kuvuruga amani iliopo baada ya kukata tama juu ya uwezekano wa kushinda uchaguzi.
CUF tunaendelea kutoa wito kwa wanachama na wafuasi wetu na wananchi wote kwa ujumla kufuata sheria na pia maelekezo ya viongozi wetu katika kutunza amani na utulivu wakati wote wakijua kwamba tunaelekea katika ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

HAKI SAWA KWA WOTE

ISMAIL JUSSA
MKURUGENZI WA MAWASILIANO – TIMU YA KAMPENI YA CUF
ZANZIBAR – 12 SEPTEMBA, 2015

No comments: