Wednesday 7 October 2015

TUME YA UCHAGUZI YATUHUMIWA KUPANGA UDANGANYIFU


UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na vyama vinne vya upinzani vimedai kubaini mchezo mchafu ambao unataka kufanywa na serikali ya CCM kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC). Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).
Hali hiyo imejitokeza kutokana na kile kinachodaiwa kuwa NEC imetoa takwimu za upotoshaji ambazo zinalenga kuwapa ushindi CCM na kutimiza adhima yao ya ushindi wa goli la mkono.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mgombea Mwenza wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa mwanvuli wa Ukawa, Juma Duni Haji alipokuwa akizungumza na waandishi mjini hapa.
Mgombea huyo alisema kuwa takwimu zilizotolewa na NEC hazina ukweli wowote na kuna kila sababu ya kutolewa ufafanuzi takwimu hizo wamezipataje.
Amesema kwa mujibu wa tume ya uchaguzi inaonesha watu ambao wanastahili kupiga kura ni milioni 23.7 na vituo vyote vya kupigia kura vitakuwa ni 72,000 na kila kituo kitakuwa na watu 450.
Amesema katika kufanya ujanja ujanja NEC inaonekana kuwa na wapiga kura hewa milioni tisa ambapo kuna vituo hewa 20,000 kwa ni vituo halisi vinatakiwa kuwa 53,000 na siyo 72,000.
Mbali na hilo Haji alifafanua kuwa kwa hesabu ya kuwa na vituo 72,000 kama hesabu ya Tume inavyoelekeza ni wazi wapiga kura wanatakiwa kuwa milioni 32 na siyo milioni 23 tena.
Kutokana na hali hiyo Duni amemtaka mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jaji Damian Lubuva kuhakikisha anatoa mchanganuo mzuri wa mahesabu ya wapiga kura vituo utoa.
“Kamwe hatuwezi kukubali tume kwa kushirikiana na serikali kutafuta ushindi wa goli la mkoni kama ilivyozoeleka kwa chama hicho.
“Hata hivyo natahadharisha serikali ikilazimisha kutaka inachokitaka wao, bila kusikiliza watu wanataka nini, ni wazi kuwa kunaweza kutokea machafuko kwani watanzania kwa sasa wamechoka na wanataka mabadiliko,” alisisitiza Duni.
Akizungumzia kuhusu safari zake, amesema mpaka sasa kafanya mikutano katika majimbo 130 ambayo mengi yao yapo vijiji na watanzania wanamalalamiko yanayofanana.
Amesema wananchi wamechoshwa na manyanyaso kwani wamekuwa wakimbizi katika nchi yao na mbaya zaidi wananyanyaswa na wazawa wenzao na wala siyo wageni.
Amesema watanzania wamechoshwa na mipango isiyokwisha ambayo uchangishwa kwa lazima bila kuona mabadiliko yoyote ya ambayo wanatakiwa kuyapata.
Almesema watanzania wengi wanakumbwa na huduma mbovu ya afya, elimu, miundombinu, ukosefu wa walimu mashuleni pamoja na shule nyingi kukosa madawati.
Mbali na hilo alieleza kuwa amebaini kwamba wanachi wengi hawana uhuru kwa kufanya kile wanachokitaka kutokana na watawala wengi kuwatisha wananchi.
“Inasikitisha jinsi askari wanyama pori wanavyowashambulia wananchi hususani wale wanaoishi karibu na hifadhi jambo ambalo linaanyima haki wananchi kufanya maamuzi,” amesema Duni.
SOURSE MWANAHALISI

No comments: