HATARI ZANZIBAR SI KAMA INAVYONENWA
MOSHI mweusi umefunika Zanzibar, nuru haipo. Kila anayejaribu kufumbua, unajaa machoni, machozi yanamtoka. Ni nyakati za tafakuri, zile hasa zinazolazimisha kuusujudia ukweli.
Mwanafasihi Shannon Alder angesema: "The moment you realize that no one is your enemy, except yourself".
Kiswahili: Nyakati za kuukiri ukweli kuwa hakuna adui yako, isipokuwa wewe mwenyewe.
Huu siyo wakati wa mapambio. Ni muda wa kushughulika na uhaini. Ajulikane mhaini nani, Dk Ali Mohamed Shein anayeitwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mapinduzi wakati hana serikali? Je, ni Seif Sharif Hamad aliyejitangaza mshindi katika kipindi ambacho hata Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ilikuwa hata haijakamilisha majumuisho?
Je, mhaini ni Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa Zec, aliyetangaza kufuta matokeo ya Uchaguzi wa Rais Zanzibar kisinema-sinema?
Tusiache kuuomba ukweli; Seif alifanya maandalizi gani ya haraka mpaka kukamilisha majumuisho ya kura kabla ya Zec? Ana rasilimali kuliko Zec? Jecha ni marehemu Samuel Kiviutu? Yule aliyekuwa mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Uchaguzi Kenya, aliyemtangaza Mwai Kibaki mshindi Desemba 2007 wakati alizidiwa kura na Raila Odinga.
Je, Jecha aliogopa kutangaza matokeo yenye kuonesha Shein ameshindwa ndiyo maana alifuta matokeo? Au aliyafuta kwa shinikizo la Shein mwenyewe?
Lazima jipu litumbuliwe; Kuna usahihi upi kuhusu idadi ya kura za Pemba kuwa nyingi kuliko idadi ya kwenye daftari la Zec? Mchezo umefanywa na nani? Jecha alipotangaza kufuta matokeo na kutaka uchaguzi urudiwe, hizo gharama za marudio zinalipwa na nani? Mfukoni kwake? Serikali tena?
Suala la dosari za uchaguzi Zanzibar halihitaji kufikirishana, linatakiwa lionekane na lidhihirike kwa kila mtu. Vigezo vizingatiwe. Pamoja na kuonekana, vema ijulikane akina nani wamesababisha madudu. Wachukuliwe hatua. Watanzania waoneshwe kila kitu na wajue, siyo kukaririshana. Jecha ameshindwa kuwafanya Watanzania na pengine dunia yote ielewe kuwa Zanzibar zilitokea dosari nyingi na kubwa mpaka kusababisha matokeo ya uchaguzi kufutwa.
Tusiache kujiuliza na maswali haya; Kwa nini Chama cha Wananchi (Cuf), hakitaki kusikia habari ya marudio ya uchaguzi? Je, kinaona kinadhulumiwa? Haki yake itapotea? Kilifanya uhuni wa kura ambao kinajua hakitaweza kuurudia? Tuchekeche ubongo hapa. Kama kweli wapigakura ni walewale, Cuf hofu yake inatoka wapi? Si uchaguzi ukirudiwa walewale watapiga kura? Je, CCM na Shein kama kweli wameshindwa, wanataka kulazimisha utwala usio na ridhaa ya asilimia kubwa ya wananchi?
Katika somo la Sayansi ya Siasa (Political Science), legitimacy ni ridhaa ya wengi katika kuikubali mamlaka. Je, Shein na Seif nani ambaye haheshimu legitimacy? Ni Shein mwenye kukaa Ikulu kwa mabavu? Ni Seif anautaka urais kwa udanganyifu?
Mwandishi Malcolm Gladwell, raia wa Canada anaielezea legitimacy kuwa hushamirishwa na mambo matatu. Mosi ni watu wenye kutakiwa kutii mamlaka, wao wenyewe wajione wanayo sauti, kwamba wakizungumza wanasikika. Pili ni sheria iwe wazi na itabirike, kusiwe na konakona katika masuala kuhusu haki na sheria. Huyu hukumu yake ni hii mwingine ni ile wakati jambo ni la aina moja. Tatu ni mamlaka kufanya mambo yake kwa usawa.
Zanzibar legitimacy inachezewa. Ni jambo lisilo na heshima kwa mtu asiye na legitimacy kuongoza. Ni utovu wa demokrasia!
Shida kubwa ambayo imekuwepo Zanzibar ni haki kutoonekana ikitendeka. Tangu mwaka 1995, kumekuwa na mgawanyiko, Cuf wamekuwa wakidai kushinda uchaguzi kisha kuporwa na CCM.
Anza na muhula wa pili wa Dk Salmin Amour (1995-2000), kisha mihula yote miwili ya Dk Aman Abeid Karume (2000-2010), lipo kundi la Wazanzibar waliona tawala hizo ni za mabavu. Ni Shein kati ya mwaka 2010 mpaka 2015 ndiye angalau aliheshimika kisawasawa kwa sababu utawala wake uliridhiwa na Cuf, kisha kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
ZANZIBAR IMEFIKAJE HUKU?
Kiswahili kinafanya yake, kwamba bandu bandu humaliza gogo, kisha Kiingereza kinajibu, cutting small chips finishes the log, ni sawa tu na msemo mzaha mzaha hutumbua usaha. Mwandishi wa Marekani mwenye asili ya Ukraine, Charles Michael Palahniuk, maarufu kama Chuck Palahniuk, anasema: "When we don't know who to hate, we hate ourselves". Kiswahili: Tunapokuwa hatujui mtu wa kumchukia, huchukiana sisi wenyewe.
Shida kubwa iliyopo Zanzibar ni chuki ya "sisi kwa sisi", na katika eneo hili Cuf na CCM kwa pamoja wanao mzigo wa lawama ambao lazima waubebe. Pemba kila uchaguzi, huubeba kama mchakato wa kudai uhuru wao. Wanajiona kama wanakaliwa kwa mabavu. Ni kwa nini imekuwa hivyo?
Sasa jiulize; Ni kwa nini Pemba hupiga kura ya upendo kwa Cuf na chuki kwa CCM? Wapemba wana nini ndani ya mioyo yao? Ni kwa nini misimamo ya Wapemba ipo wazi kabisa kuwa bora kupigia kura jiwe kuliko mgombea bora wa CCM?
Ni kwa vipi siasa Pemba zinabebwa kama imani kutoka mbinguni? Kwamba kuwa Cuf ndiyo njia ya Mungu na CCM ni upagani.
Mwisho sasa jiulize ni kwa nini dosari za uchaguzi zimetokea Pemba ambako siku zote CCM hawana chao? Je, Cuf walitumia kiburi kuwa wenyewe ndiyo wanaoshikilia mamlaka zote za kisiwa hicho kuongeza kura za wizi? Je, Cuf walijua kuwa hawawezi kuongoza kwa kura nyingi Unguja hivyo kujijazia kura Pemba ili zifidie upungufu wa Unguja na kushinda? Au CCM wanaamua kutafuta kisingizio kama ilivyo mfa maji na kutapatapa?
Ni kwa nini Jecha hakufuta matokeo haraka baada ya kugundua dosari na kusubiri dakika za mwishoni? CCM wenyewe ndiyo wataalam wa mizungu ya uchaguzi, ilikuwaje wakaibiwa kura na Cuf ambao wamejifunzia siasa kutoka kwao?
Zanzibar isitazamwe kwa jicho la siasa peke yake. Acha mhemuko, achana na siasa za Cuf na CCM, kisha itazame kwa jicho dadisi, dodosa historia, mwisho utapata jibu kuwa hatari iliyopo ni zaidi ya inavyonenwa.
Watu hawajiulizi ni kwa nini Uchaguzi Mkuu 2015, wimbo ulioimbwa sana ulihusu Zanzibar na Mamlaka Kamili? Nini kilichokuwa kinatafutwa? Mamlaka kamili kutoka wapi kama siyo Tanganyika? Ni kwa nini wapo Wazanzibar wanaishi nje na hawataki kurudi nyumbani kwa madai kuwa nchi yao imekaliwa kwa mabavu na Tanganyika? Chuki hii dhidi ya muungano nani aliianzisha? Na kwa nini Seikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda mrefu imepoteza umaarufu (popularity) Zanzibar, hususan Pemba?
Nani hajui? Wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya kuundwa kwa Katiba Mpya, Zanzibar kulikuwa na harakati za kutaka sauti ya Wazanzibar isikike kuhusu uhai wa muungano. Walitakiwa kuchagua miongoni mwa mambo matatu. Mosi muungano uendelee kama ulivyo. Pili muungano uwepo wa mkataba. Tatu waachwe wapumue. Kwa kunukuu ?watuache tupumue.? Wenye kauli "watuache tupumue" ndiyo hao waliomzunguka Seif. Mpaza sauti mkuu alikuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Cuf, Ismail Jussa Ladhu.
Je, hili nalo ni la kupuuzwa? Wanawezaje kusema waachwe wapumue kama hawajioni wanaminywa mpaka wanashindwa kupumua? Lazima chuki ya Zanzibar ishughulikiwe kwa viwango vyake. Wala Zanzibar shida siyo maendeleo. Katika miaka 20 ya CCM kutokukubalika Pemba, kumekuwa na jitihada nyingi za kupeleka maendeleo yenye kuonekana kisiwani humo. Shein pia kwa miaka yake mitano amejitahidi mno.
Kuna zaidi ya siasa, na ndiyo inayotakiwa imulikwe. Mchezo wa kuzunguka kichaka hautakiwi. Ni lazima kuingia katikati na kumkabili adui. Zanzibar ilipofikia na kule iendako haipaswi kutazamwa kwa jicho la siasa za kawaida. Taswira yake inatakiwa iangaliwe katika macho yenye kuona mbali. Macho yenye tiba na suluhu ya ukakika. Maana Zanzibar hakuna mgogoro wa kisiasa, kuna chuki.
Siyo kuitazama kwa jicho la uchaguzi kurudiwa au Seif kutangazwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hali halisi inataka Zanzibar iangaliwe kwa jicho la tiba. Tiba mahsusi, tiba ya kudumu!
Hali ilivyo sasa ni kuwa unapoiondoa Tanganyika, hutaikuta Zanzibar, bali vitakuwepo visiwa vya Unguja na Pemba. Kama watu hawathubutu kuwaza hili basi wanafanya kosa kubwa mno la kiufundi. Unapoutazama ustawi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unapata jawabu kuwa ipo kazi ya kufanya kuhakikisha kuwa Wazanzibar na Watanganyika kwa pamoja wanaufurahia muungano wao.
Lipo jukumu la kutekeleza kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna kazi ambayo haihitaji kupuuzwa. Hii inahusu maoni ya walio wengi kuhusu kuendelezwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wachache pia wasikilizwe, nini kinachowauma? Mbegu ipi imepandikizwa kwenye nyoyo zao? Mbona Shein ni Mpemba mwenzao lakini hiyo haijawafanya wakikumbatie Chama Cha Mapinduzi?
Hapo unapata jawabu kuwa hoja siyo Upemba, sasa kuna nini kingine? Tuzame katikati ya kichaka! Tusikariri majibu wala hatutakiwi kuongozwa na dhana.
Tusipuuze ile hoja ya kuwa kuna malodi Uarabuni wanaifuatilia Zanzibar mithili ya fisi anavyoumendea mkono wa binadam kwa nyuma akiamini utaanguka ale kitoweo. Kwamba malodi waliopo Uarabuni shida yao kubwa ni kuona muungano unavunjika na Zanzibar inakuwa jamhuri kamili. Baada ya hapo ndipo waanze kufaidi rasilimali za Wazanzibar.
Inaelezwa kuwa sasa hivi wanashindwa kuzifikia mali za Wazanzibar kwa sababu visiwa hivyo vimeatamiwa na Tanganyika. Kila hoja itazamwe kwa upana wake. Na hapa ukweli upo wapi? Je, ni kweli kuwa chuki za Wapemba kwa CCM nyuma yake kuna mkono wa malodi wa Uarabuni? Hawalitaki zimwi linalowajua, wanataka jipya.
Hoja ya ugaidi inazungumzwa pia, nayo ipewe nafasi. Eti Zanzibar ikiachwa peke yake, magaidi watavifanya visiwa hivyo kuwa ngome yao ya kujitanua, hivyo kutanua wigo wa magaidi katika Pwani ya Afrika Mashariki, Afrika na duniani kwa jumla.
Hofu hii inathibitishwaje? Kwa nini yawe maisha kama unajimu wa marehemu Sheikh Yahya Hussein?
Na kama ni kweli hofu hiyo ipo na CCM wanaogopa kuwapa Cuf Zanzibar waitawale, sasa uchaguzi unafanyika wa nini? Kutumia fedha za walalahoi kufanya uchaguzi ambao matokeo kinzani kwa CCM hayataheshimiwa ni ufisadi. Je, ni uchaguzi wa marembo kuzionesha jumuiya ya kimataifa kuwa Tanzania kuna demokrasia? Tiba mahsusi ni ile ambayo inatolewa baada ya mgonjwa kupimwa na kugundulika anachoumwa. Zanzibar inahitaji vipimo.
Usifanye kosa kubwa kwa kusahau kuhusu uwepo wa hofu ya kutaabika baada ya matokeo (aftermath). Kwamba Waunguja wamekuwa wakifaidi zaidi keki ya Zanzibar kuliko Wapemba tangu Muingereza na Sultan wake walipotimuliwa. Kwamba Waunguja wameshawafanyia mambo mengi ya hovyo Wapemba. Kwa maana hiyo wanahofia kisasi baada ya Seif kukabidhiwa nchi.
Kwamba malodi (elites) wa Unguja ndani ya CCM, wameshafanya matukio ya kuwafunga jela, kuwadhalilisha vigogo wa Cuf, wapo waliopata ulemavu wa maisha na hata baadhi kufariki dunia, hofu ipo kuwa je kisasi kitalipwa? Seif alitamka kuwa hakuna kisasi kwenye misamiati yake kichwani lakini nani anaamini kuwa hatageuka baada ya kukabidhiwa rungu? Kila dhana itazamwe kwa uzito wake.
Lingine ni kuhusu afya ya muungano, inadaiwa kuwa hofu kubwa ni kuwa Seif akipewa Zanzibar ataleta usumbufu wa kutaka muungano ufe. Tunapaswa kushiba hoja nyoofu. Je, hili lina uzani gani katika uhalisi wa jambo?
KUHUSU MUUNGANO
Kila upande hautakiwi kuwa kipofu, moja ya tunu bora kama Watanzania ni uwepo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Matatizo yashughulikiwe kinagaubaga.
Hata hivyo, hatutakiwa kusahau kuwa zipo dola zilizoungana, zilizokuwa na nguvu kubwa ya kijeshi, kirasilimali na kimamlaka lakini ziligawanyika vipandevipande. Upo wapi Muungano wa USSR, yaani Jamhuri za Kijamaa za Sovieti?
USSR walifikia uwezo mpaka wa kumiliki nyuklia. Urusi haikuwa yenye kukamatika ulimwenguni. Ni USSR na Marekani pekee zilizotamba kiuchumi na kijeshi duniani baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Urusi kama baba mwenye nyumba wa USSR, inabaki kulaumu kuwa iliangushwa kwa sababu ya vita ya ubebari na ujamaa. Marekani bepari mkuu na Urusi baba wa ujamaa. Ukweli upewe heshima yake kuwa hata kama Marekani ilihusika kuiparanganyisha USSR lakini sababu ni matundu ambayo Urusi iliyatengeneza yenyewe. Kwamba dola nyingi ziliona zinapunjwa, kwamba Urusi ilizitumia kujiimarisha.
Hii dhana ya Tanzania Bara kuonekana kama inaitumia Zanzibar kujiimarisha haipaswi kuachwa ikatawala kwenye vichwa vya watu. Ni tatizo kubwa! Wanandoa wenye maelewano huwa hawafarakanishwi na maneno ya pembeni. Ila neno la uchonganishi hupata nguvu kwenye ndoa ya watu wenye migongano. Marekani walifanikiwa kuiua USSR kwa sababu wao wenyewe ndani kwa ndani walikuwa na migongano.
Ulikuwepo muungano mzuri wa kijamaa wa Czechoslovakia, ulikwenda na maji kisha kuacha nchi mbili Jamhuri ya Czech na Slovakia, sababu ni kama zinazosemwa kuhusu Zanzibar na Tanganyika. Slovakia iliona Czech inanufaika kuliko yenyewe. Rejea kwenye kifo cha muungano wa Dola ya Yugoslavia kisha uone kuwa Tanganyika na Zanzibar inaweza kuifanya Tanzania isiwepo. Muhimu ni kutambua kuwa heshima ya muungano lazima izingatie mahitaji na matakwa ya kila upande.
Naiona hofu kuu kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muhimu zaidi katika kuifanya Zanzibar iwepo kama dola moja. Kinyume chake zitakuwepo dola mbili, ile ya Unguja na Pemba. Maana hawaaminiani kwa sababu hawapendani, na wasiopendana huchukiana.
Mimi ni mjumbe tu, nafikisha, maana atangazaye mirimo si mwana wa ruwari (mjumbe hauawi). Mvumo wa Zanzibar unanipa hofu. Tusiache kukumbuka matukio ya Januari 26 na 27, 2001. Watu walikufa, wengine wakawa wakimbizi. Chanzo kilikuwa uchaguzi. Atambaaye na nyasi, mtambulie ni nyoka!
Baada ya Mwafaka wa Zanzibar wa mwaka 2001, wengi walisema ?tusahau yaliyopita tugange yajayo? lakini aliyekuwa Mwenyekiti wa Cuf, Prof Ibrahim Lipumba alisema: ?Tunasamehe lakini hatupaswi kusahau, tukisahau yatajirudia.? Naona kweli watu wamesahau, na yapo njiani kujirudia!
Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema: "Whoever does not miss the Soviet Union has no heart. Whoever wants it back has no brain". Kiswahili: Yeyote ambaye haukumbuki wa Umoja wa Soviet hana moyo. Yeyote anayetaka umoja huo urejee hana ubongo.
Tusipoona mbali Tanzania itafika zama hizo za kutoa matamshi kama ya Putin, nyakati ambazo haitwezekana tena kuuhuisha Umoja wa Tanganyika na Zanzibar. Umakini unahitajika. Upendo uishi ndani yetu, haki iheshimiwe.
By Luqman Maloto
No comments:
Post a Comment