Sunday, 29 November 2015

Wahafidhina wa CCM Zanzibar wasiiteke Nyara nchi mzima kwa ajili ya matumbo yao.Viongozi wa dini wataka Shein, Hamad kukubali matokeo ili kuunda SUK
NA MWANDISHI WETU
29th November 2015
Rais Dokta Ali Mohamed Shein na Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad ndiyo waliobeba amani na utulivu wa Zanzibar.
Viongozi hao ambao ni Rais na Makamu wake wa kwanza, wanahimizwa kutenda haki na kuepuka kuukuza mgogoro wa Zanzibar ambao sasa umeanza kutishia mipango ya maendeleo ya taifa.
Wakuu hawa ndiyo wanaotakiwa kufahamu dhamana hiyo na wasiwasikilize wapambe ambao mara nyingi hutazama maslahi binafsi badala ya ustawi wa nchi.
Mgogoro wa Zanzibar wiki hii umetishia kuinyima Tanzania Shilingi trilioni moja (bilioni 999) zinazotolewa na Shirika la Changamoto za Milenia la Marekani (MCC).
Viongozi wa dini wakiwamo, maaskofu na masheikh kutoka Tanzania Bara na Visiwani na wa mataifa wa Maziwa Makuu , wapo Zanzibar kuzungumzia mgogoro huo.
Wanasema waamini kuwa jibu la amani ya Zanzibar ni Dk Shein na Hamad.
Wanawataka wawili hawa kuutendea haki Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015 na kumtangaza mshindi wa Urais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Jopo hilo la viongozi wa kiroho wanaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili , Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu, lipo Zanzibar kutathmin mgogoro huo.
Viongozi hao watatembelea majimbo yote ya Pemba na Unguja huku wakiwahimiza wanasiasa kuangalia maslahi na ustawi wa Wanzabari badala ya mambo yanayotishia amani ya taifa.
Wanawakumbusha viongozi suala la Nigeria ambako mshindwa alijipambanua kuwa ameshindwa hata baada ya wapambe kumlazimisha akatae matokeo.
Kama viongozi hao walikiri kushindwa hapo Zanzibar tatizo ni nini ? Mshindi anajulikana au hafahamiki? Katiba inawaagiza iunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) basi aliyeshinda aunde serikali hiyo.
Kamati hiyo yenye wataalam wa haki, sheria na utawala bora, imetaka serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayomaliza muda wake , kukubali matokeo ya uchaguzi uliopita na kuunda serikali mpya ya umoja kwa mujibu wa katiba.
Wanaamini kuwa kufikiwa hatua hiyo kutaendelea kuin’garisha Zanzibar badala ya kuendeleza mivutano ya chuki inayohamasishwa na chuki za kisiasa na mambo ya kizamani ambayo yanasambaratisha umoja na mshikamano wa wananchi.
Wanasema makubaliano yanayoendelea sasa yawe ni kumpa ushindi aliyechomoza na ushindi kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba ambayo ndiyo kwa upande wa Bara yalimchagua Rais John Magufuli, kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Akitoa mchango wake Sheikh Profesa Haduo-Ally Seleman wa Nigeria, anaonya kuwa chaguzi nyingi za marudio kwenye nchi za Afrika ndiyo chanzo cha vurugu kwani kila mgombea hutafuta mbinu chafu za kutaka kushinda.
Anataja mbinu hizo kutumia vitisho vya vyombo vya dola , ahadi hewa, rushwa na udanganyifu hivyo kuwa chanzo cha vurugu na kukosekana amani.
Profesa Seleman anasema maridhiano ya Zanzibar lazima yalenge kuwaondoa watendaji ambao kwa makusudi waliingiza kasoro zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi.
Kwa upande wa serikali, wanatoa wito kuwa Zanzibar kumpa haki mshindi badala ya kurudia uchaguzi kwani hayo ndiyo matakwa ya kweli ya wananchi kutambua haki yao kwenye boksi la kura.
Kadhalika waliwataka viongozi na wanasiasa barani Afrika kujifunza yaliyotokea kwenye Uchaguzi Mkuu Nigeria pale Rais Good Luck Jonathan aliyeshindwa alipomkabidhi Jenerali Mohamadu Buhari, Ikulu bila kelele hata baada ya wapambe kumshauri akatae matokeo.
Viongozi hao waliopo Unguja na Pemba wataomba dua ya haki kama nguzo kubwa ya kukuza amani ,uhuru na ustawi wa jamii kwa wote.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: