Thursday 17 December 2015

Barua ya Waziri kwa Magufuli. By Hon Ally Saleh. Member of the Union Parliament  (Malindi Constituency)Mheshimiwa

Amiri Jeshi Mkuu

Ikulu, Dar es salaam

Asssalam alaykum,

Natumai hujambo na familia na unaendelea na kazi kama msemo wako wa HAPA KAZI TU ulivyo. Inshallah Mungu atakupa afya na uzima uendelee. Pili nakupongeza kwa kuchagua Baraza la Mawaziri ambalo litafanya kazi na wewe, na sisi kama Wabunge kwa faida ya taifa.

Ingawaje hata hivyo, sikubaliani na wewe juu ya baadhi ya teuzi zako, kama vile kuwanyima fursa ya kutosha Wazanzibari na kuonekana Baraza lako kuwa ni la Tanzania Bara  zaidi na kutufanya wadogo zaidi na wanyonge zaidi ndani ya Muungano.

Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, hata hivyo nilotaka kukuandikia leo ni kuhusiana na hali ya usalama hapa kwetu Zanzibar na tishio la kutokuwepo Amani  ambapo naamini wasaidizi wako watakuwa wamekuarifu, lakini nakuandikia nikiwa Mbunge wa Malindi kwa tukio lilotokea usiku wa juzi Jumamosi.

Tukio hilo la kuvunjwa vunjwa barza ya wana CUF katika eneo la Michenzani, Mjini Unguja kwa hakika ni muendelezo wa matukio mengi yanayofanywa na watu wanaoitwa wasiojulikana na ambayo yalishamiri sana wakati wa uchaguzi lakini hata baada ya uchaguzi yamekuwa yakiendelea.

Watu waliosemwa wakitumia magari rasmi ya Vikosi vya Zanzibar na wakiwa na silaha walifika eneo hilo usiku mkubwa na kufunga njia na kisha wakifanya ukhabithi huo, na Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu sehemu hiyo ni mita mia tatu tu kutoka Kituo cha Polisi cha Madema.

Tunajiuliza kwa nini tukio hilo lifanywe usiku kama ni zoezi la kawaida la kusafisha mji? Na hilo tunajua kuwa lilitanguliwa na siku chache nyuma gari moja iliyopita na kutangaza kwa bomba kuwa sehemu hiyo ivunjwe, bila ya kuonyeshwa amri halali ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, sehemu hiyo maarufu huitwa Commonwealth na hadi leo haijaripotiwa kuwa na kitendo chochote kile cha ukosefu wa Amani tokea ilipoanzishwa.

Mita 100 tu upande wa pili kuna ile inayoitwa Maskani Mama ya Kisonge ambayo hiyo haiguswi wala haiulizwi na Polisi yoyote yule. Tokea kuanzishwa kwake hadi leo imekuwa na ubao unaoitwa Sauti ya Kisonge ambao umekuwa na matusi na kejeli kwa viongozi na hasa viongozi wa upinzani.

Ubao huo umekuwa ukichochea fujo, kutoa lugha ya kibaguzi na mara nyingi imekuwa ni chanzo cha kuzusha hamasa za kisiasa hapa Zanzibar, lakini inalindwa utafikiri ni taasisi rasmi ya kiserikali.

Siku chache nyuma, watu wasiojulikana wakiwa na silaha pia walivamia studio ya Hits FM wakati wa usiku na kuichoma moto na kutia hasara kubwa. Lakini hasara kubwa zaidi ni kuzima sauti za watu na kukaba uhuru wa maoni na kujieleza.

Wakati wa Kampeni makundi hayo pia yalitishia Amani ya wana habari kwa kumpiga mwana habari mmoja na kuvamia kituo cha radio cha Coconut FM mchana kweup wakiwa na silaha kama marungu, mapanga, msemeno wa kukatia miti na bunduki.

Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, sitaki nikuchoshe kwa mlolongo wa matukio ya makundi hayo katika kupiga watu, kuvunja na kuchoma sehemu kadhaa, lakini nataka nikuhakikishie kuwa hakuna sauti yoyote ya kukemea iliotoka kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa uhakika Rais wa Zanzibar wakati huo, Dk. Ali Muhammed Shein alisema “ hana habari”; Waziri wa Vikosi wakati huo Haji Omar Kheir alisema “ hakuna ukweli” na Polisi walisema “hawajawaona watu kama hao.”

Dhamana ya usalama wa nchi nzima ni yako wewe. Sitaki niamini kuwa tuna utawala ulioshindwa (failed state) kwa sababu ya Zanzibar ambapo makundi haramu yanafanya yanavyotaka na hakuna wa kuwauliza. Hakunonekani kuna nia ya kisiasa wala ya kiutendaji kwa wasaidizi wako wa Zanzibar kulikabili na kulimaliza jambo hili.

Hakuna nia hizo kwa sababu makundi hayo wameyaunda wao kwa faida zao za kisiasa. Ila naamini katika picha kubwa ya taifa makundi haya yanaharibu sifa yako na yanajuburi ( challenge) mamlaka yako.

Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, kuendelea kwa vitendo hivi hapana shaka kutashusha Imani ya wananchi kwa vyombo vyetu vya ulinzi vikiwemo Polisi na Jeshi la Wananchi na vikiwa chini yako. Na kushuka kwa imani hiyo kuna maana kuelekea kwenye fujo na vurugu (riot na anarchy).

Kanuni ya kuonewa inasema wazi kuwa anaeonewa hataonewa siku zote maana iko siku atasema basi na atajitetea hata katika hali yake ya udhaifu kuonesha msimamo wake na makundi haya yameonea sana watu wa Chama cha Wananchi CUF na nina hofu ya wanaononewa kusema wamechoka.

Wakati bado tumo kwenye kutafuta njia ya kutoka kwenye mkwamo ambao pia unatokana na ukweli kuwa Chama cha Mapinduzi hakina na hakijawahi kuwa na nia ya kutoa nchi kwa njia za kidemokrasia, matukio kama haya yana nia ya kuzidi kukwamisha kupatikana suluhu.

Haikubaliki kabisa, raia kuonewa, kunyanyaswa ndani ya mipaka yao, tena wafanye hao wa uonevu wakiwa ni wale waliopewa dhamana ya kuwalinda. Au kama wanaofanya hivyo sio wao, kufumba macho wenye nia hiyo chafu wakitekeleza dhamira mbovu.

Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, naamini si kuwa kadhia zote hizi hazijafika mezani huko Magogoni jumba kuu, lakini pengine ushauri ulitolewa kuwa hili ni jambo la kupita na dogo tu. Lakini napenda kusema kama cheche huzaa moto na dogo huzaa kubwa.

Sina haki ya kukushauri kama hujaniuliza ushauri wangu kwa heshima yako, lakini napenda kusema hili lisimamie mwenyewe utake kujua undani utandu na ukoko. Kisha ulishikia fimbo limalizwe na wanaohusika kuliwachia wachukuliwe hatua.

Zanzibar leo imekuwa eneo la khofu. Khofu ya mchana ambapo katika malindo yanayofanywa na askari wa JWTZ wananchi wamekuwa wakipigwa mchura wanafanya makossa na usiku makundi mengine yakifanya hujuma na kutishia maisha na Amani. Tushukuru Mungu kuwa mpaka leo hakuna maisha yaliopotea.

Mheshimiwa Amiri Jeshi Mkuu, ya Burundi, ya Burkina faso, ya Ivory Coast na kwengine tusiyaone yako mbali. Siku hizi tuna nafasi ya kujifunza mambo haraka na kuyazuia na naamini utalifanyia kazi hili ili nchi mshirika wa Muungano watu wake wafaidi uhuru wao wa kila kitu na isiwe kujikunyata.

Nashukuru na Mungu akubariki katika kazi na maisha yako.

Mwandishi wa Makala hii ni mshairi, mchambuzi wa siasa, mtunzi wa vitabu, mwanasheria na Mbunge wa Jimbo la Malindi

No comments: