Katika gazeti la Mwananchi toleo la Jumatano, tarehe 23 Disemba 2015, kulichapishwa makala yenye kichwa cha maneno: "Mgogoro Zanzibar usiwe kigezo cha kutudharau".
Katika makala hiyo, Mwandishi Nuzulack Dausen, ameandika kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga amekutana kwa mara ya kwanza na mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini na kusema Tanzania inaheshimu tunu za kimataifa za haki za binadamu na demokrasia na kwamba mgogoro wa Zanzibar usiwe kigezo cha baadhi ya nchi kudharau hatua kubwa za kidemokrasia zilizofikiwa. Akizungumza na wanahabari baada ya mkutano huo jana, Balozi Mahiga aliitaka kila nchi kuheshimu na kulinda uhuru wa nyingine akisema hakuna sababu ya mataifa mengine kujiona ni makubwa au tajiri kuliko mengine.
“Wengine wanajua kabisa taratibu za kuheshimiana lakini wanaamua kwa makusudi kutumia uwezo wa kutudharau isivyopaswa. Lakini wanatakiwa kuheshimu uhuru wetu kama tunavyoheshimu wao. Uhuru wetu haujadiliki,” alisema.Kuhusu hatua iliyofikiwa Zanzibar, Balozi Mahiga alisema mazungumzo baina ya viongozi wa visiwa hivyo yanaendelea vyema na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuwa na subira. Alisema msimamo wa Tanzania unafahamika katika masuala mbalimbali ya kimataifa na kwamba haitakubali uhuru wake udharauliwe kwa sababu ya umaskini.
MAONI: Kusema kweli, inasikitisha sana kusikia kauli kama hiyo inatolewa na Balozi Augustino Maiga, mwana diplomasia mzoefu wa masuala ya kimataifa. Hivi nani anayeidharau Tanzania hapa? Hivi wahisani wetu wanapodai na kuikumbusha Tanzania kutekeleza wajibu wake katika kuheshimu misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora, ndio kuidharau Tanzania kwa sababu ya umasikini wake?
Balozi Maiga anajua fika kama ajuavyo kila mtu kuwa Tanzania, kwa hiari yake, imeridhia mikataba mbali mbali ya kikanda na kimataifa kwa madhumuni ya kuheshimu misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Na moja katika masharti ya kupewa misaada ya kiuchumi na kimaendeleo kutoka kwa wahisani wetu ni hili suala la kuheshimu misingi ya demokrasia, haki za binadamu na utawala bora.Sasa, ikiwa inaonekana wazi kuwa chimbuko la mgogoro wa Zanzibar linatokana na kushindwa kwa serikali ya Zanzibar na hasa zaidi serikali ya Tanzania kutekeleza wajibu wake, hivi itakuwa jambo la busara kutegemea kuwa Jumuiya ya Kimataifa itanyamaza kimya; kwa kuogopa kuwa itaonekana kuwa ati uhuru wa Tanzania utadharauliwa kwa sababu ya umasikini wake? Tokea lini hoja hii ikawa na mashiko wakati Tanzania, kwa muda mrefu sasa, imekuwa ikiendelea kupokea misaada mbali mbali ya kiuchumi na kimaendeleo chini ya masharti hayo hayo ya kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora? Au hii ni kwa sababu serikali ya Zanzibar na viongozi wake ni rukhsa kuendelea kufifirisha misingi ya demokrasia na utawala bora kwa mwega au mgongo wa serikali ya Tanzania, tena bila ya kuulizwa chochote?
Kwa muktadha huu, Augustino Maiga hana haja wala sababu ya kumlaumu mtu yoyote hapa kwa kudharauliwa kwa Tanzania; isipokuwa Tanzania, kama si chochote, imejidharaulisha yenyewe kwa kuruhusu kikundi cha watu wachache nchini Zanzibar kufifirisha misingi ya demokrasia na utawala bora kwa maslahi yake binafsi.Kwa upande mwengine, kama tutaangalia kwa makini uteuzi wa mawaziri katika serikali ya Rais John Pombe Magufuli, tutagundua kuwa ikiwa kuna nchi inayodharauliwa hapa bila ya sababu za msingi, basi nchi hiyo ni Zanzibar. Kwa mfano, sasa Wizara za Muungano zinachanganywa na mambo yasiyokuwa ya Muungano bila ya kujali masharti ya Katiba. Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa; Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Kama hii haitoshi, Wizara ya Mambo ya Nje sasa imechanganywa na masuala yanayohusiana na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa.
Kwa hivyo, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya Muungano, tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1964, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, kama ilivyo kuhusiana na Waziri wake, wote wawili sasa wanatoka Tanzania Bara. Augustino Maiga sasa anaweza kufanya anavyotaka kuhusu ubunifu na utekelezaji wa sera ya Mambo ya Nje bila ya mchango wala ushiriki wa Zanzibar.
No comments:
Post a Comment