Tuesday, 29 December 2015

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kufuatia taarifa iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana Zanzibar juzi, tarehe 27 Desemba, 2015, waandishi wengi wa habari wametupigia simu wakitaka kujua Chama Cha Wananchi (CUF) kimepokea vipi taarifa ile.

Vikao vya CCM ni vikao vya CCM. Si kawaida yetu kutolea taarifa maamuzi ya vikao vya vyama vyengine. Hata hivyo, tunaelewa ni kwa nini kumekuwepo na shauku ya kusikia CUF inasema nini kwa sababu yale yaliyokuwemo kwenye taarifa hiyo yaligusia pia mazungumzo yanayofanyika Ikulu Zanzibar yanayolenga kupata ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.

Baada ya kuipitia taarifa ya CCM na mengine yaliyoelezwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar wakati akitoa ufafanuzi wa yale yaliyomo kwenye taarifa hiyo, CUF tunapenda kuwaeleza Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla haya yafuatayo:

1.      Taarifa yenyewe haionekani kama imeandaliwa na watu makini wala haioneshi kama walioitoa wanajua nini kilichopo. Hilo liko wazi kutokana na taarifa yenyewe kuwa na maudhui yanayopingana ambayo yamekuja kukorogwa zaidi na maelezo yaliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar mbele ya waandishi wa habari na kuoneshwa katika vituo kadhaa vya televisheni:
(a)     Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini papo hapo inaeleza kwamba kikao kimeridhia mazungumzo yanayoendelea Ikulu Zanzibar. Taarifa haisemi iwapo maamuzi ya vikao vya mazungumzo hayatakuwa na suala la kurudiwa uchaguzi, upi ni mwelekeo wa CCM.

(b)     Taarifa inazungumzia uchaguzi wa marudio lakini papo hapo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar anasema CCM haina imani na Tume ya Uchaguzi iliyopo na kwa hivyo uchaguzi huo wa marudio lazima ufanyike chini ya Tume mpya. Baada ya hapo hasemi Tume iliyopo ambayo muda wa utumishi wa Makamishna wake unalindwa kikatiba itaondolewa  vipi na Tume mpya itapatikana vipi.
(c)     Taarifa inawataka wanachama wa CCM wajiandae na uchaguzi wa marudio lakini Katibu wa itikadi na Uenezi anasema hata usiporudiwa ndani ya siku 90, bado Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais.
Nukta hizi tatu ambazo haziwezi zote kusimama kwa pamoja bila ya kupingana moja dhidi ya nyengine zinaonesha tu ni kwa kiasi gani viongozi wa CCM Zanzibar wamepoteza mwelekeo na hawana uhakika wa nini kitatokea katika kuondokana na mgogoro huu wa kutengenezwa.

2.       Taarifa ya CCM haiwasaidii wanachama wa CCM wala wananchi wa Zanzibar kwa kuwapa matumaini ya kumalizika kwa mgogoro wa kutengenezwa wa uchaguzi wa Zanzibar na badala yake inaonekana imelenga kuwachanganya zaidi wananchi kwa maelezo yanayopingana.
3.      Taarifa inaonyesha ni jinsi gani CCM kilivyopoteza mvuto kwa kujiweka mbali na wananchi. Taarifa hiyo inapongeza eti kuwepo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii wakati wananchi wa Zanzibar, bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, siyo tu wanumia kutokana na sera mbovu za CCM lakini sasa wanazidi kuteketea na maisha yao kuwa magumu zaidi kutokana na fadhaa (tension) na taharuki iliyopo katika nchi kutokana na kutokuwepo kwa Serikali yenye ridhaa yao. Harakati za maisha zimeathirika sana huku bidhaa vikiwemo vyakula vikipanda bei. Viongozi wa CCM hawaonekani kujali hali hii mradi wao yao yanawaendea. Tabia hii ya CCM kutowajali wananchi wanyonge wa nchi hii ndiyo iliyopelekea wananchi kukiadhibu chama hicho katika uchaguzi mkuu na kupelekea mgombea wake wa Urais wa Zanzibar na wagombea Uwakilishi kushindwa vibaya kwa tofauti ya zaidi ya kura 25,831.

4.      Taarifa inaendeleza utamaduni wa unafiki wa kisiasa kwa eti kuwapongeza viongozi wa CCM na jumuiya zake kwa kazi ya kukiimarisha chama chao huku wakijua kwamba viongozi wao hasa wale walioongoza Kamati ya Kitaifa ya Kampeni za CCM Zanzibar walishindwa kazi na kupoteza mwelekeo. Matokeo ya kazi mbovu ya Kamati ya Kampeni ya CCM Zanzibar ni kukisababishia chama hicho kipigo kikubwa katika uchaguzi huo kilichopelekea kushindwa katika nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa zaidi ya kura 25,831 na kupoteza viti tisa (9) vya Uwakilishi kisiwani Unguja mbali ya kutopata hata kiti kimoja kisiwani Pemba. Viongozi hao walishindwa kuwajibika licha ya kutumia mabilioni ya fedha walizopewa kwa ajili ya kampeni.
5.      Katika maelezo yake ya ufafanuzi kwa waandishi wa habari, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar anaitupia lawama Tume nzima ya Uchaguzi ya Zanzibar kwa kushindwa kazi huku akijua na ikijulikana na kila mmoja kwamba tamko la kufuta uchaguzi limetolewa na Jecha Salim Jecha kinyume na Katiba, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na kinyume na maadili ya kazi yake. Katiba inataka Jecha achukuliwe hatua za kufukuzwa kazi kwa kuanza na kumuundia Tume Maalum ya kumchunguza, na siyo kutafuta mbinu za kumlinda kwa kuwaingiza wasiokuwemo.
6.      Maelezo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar kwamba Dk. Ali Mohamed Shein ataendelea kuwa Rais hata baada ya miezi mitatu ni kielelezo na ushahidi mwengine wa jinsi CCM isivyoheshimu Katiba. Kwa hakika, hili suala la kutaja siku 90 ambalo linatajwa sana na CCM na wapambe wake haijulikani hata linatokea wapi. Hakuna pahala popote katika Katiba ya Zanzibar wala Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar panapotajwa sharti la kurudiwa uchaguzi ndani ya siku 90 kwa sababu Katiba yenyewe na Sheria ya Uchaguzi haina sehemu yoyote inayozungumzia kufuta uchaguzi na kufanya uchaguzi wa marudio.
7.      Kwa ujumla, taarifa ya CCM Zanzibar iliyotolewa na Katibu wake wa itikadi na Uenezi inaonyesha jinsi chama hicho kisivyojali madhila wanayoyapata raia, fedheha iliyopata taifa na hali ya kiuchumi inayozidi kudorora kila siku Zanzibar ikiwaathiri mno wananchi wanyonge.

Baada ya uchambuzi huo wa taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, CUF inapenda kuwaeleza Wazanzibari yafuatayo:

1.      Waipuuze taarifa hiyo ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar kwani haina lolote jipya zaidi ya kutaka kufunika kombe kutokana na hali ngumu inayotokana na hoja za viongozi wa ngazi za chini na wanachama wa CCM wanaotaka maelezo ya kwa nini chama hicho licha ya kutumia mabilioni ya shilingi kimeshindwa vibaya katika uchaguzi mkuu.
2.      Wazanzibari wasubiri taarifa rasmi ya matokeo ya mazungumzo yanayowahusisha viongozi wakuu wa kisiasa yanayofanyika Ikulu Zanzibar ambayo yamo katika hatua za mwisho kumalizika.
3.      Wampe nafasi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli, ambaye anaendelea na juhudi katika ngazi za juu kabisa za kuhimiza kupatikana ufumbuzi wa haraka wa mgogoro wa uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
4.      CUF inawahakikishia Wazanzibari kwamba haitotetereka na itasimamia kwa dhati maamuzi yao waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao.
5.      Mwisho kabisa, inaendelea kuwapongeza Wazanzibari kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 ambayo inaashiria ujenzi wa Zanzibar Mpya.

HAKI SAWA KWA WOTE

ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA – CUF
29 DESEMBA, 2015

No comments: