Monday 18 January 2016

Fitna za Mgawiko wa Zanzibar

Hoja Za uchotara na ubaguzi ni hoja ya makosa makubwa aliyoyafanya Nyerere kwa kusudi au kwa sadfa, ni hilo la kuwafanya wananchi wenzake waache kufikiri na wawe wanayafuata tu aliyokuwa akiyasema bila ya kuyazingatia au kuyapima.Miongoni mwa aliyowahi kuyasema Nyerere ni kuwa ati iwapo Zanzibar itaachana na Tanganyika basi Tanganyika kutakuwa shuwari lakini Wazanzibari wataanza kubaguana baina ya Wapemba na Waunguja na halafu wataendelea kutafutana asili zao. 
Tangu wiki iliyopita waandishi kadhaa wa Bara wamekuwa wakiyanukuu haya kana kwamba ni maneno yenye ukweli usiopingika.  Hii ni fitna tu; na inatumiwa kuwatisha na kuwagawa Wazanzibari.Wakoloni walipowaona wanaowatawala wanaungana kuwapinga, basi walitumia mbinu ya kuwagawa wazidhoofishe nguvu zao ili waendelee kuwatawala. 
Mbinu kama hiyo inatumiwa siku hizi na baadhi ya viongozi wa CCM wa Bara pamoja na baadhi ya waandishi wa huko huko Bara ‘walioshtushwa’ na mwamko wa kisiasa uliowafanya Wazanzibari wawe na ujasiri wa kuujadili kwa mapana na marefu Muungano wa Tanzania. 
Ujasiri huo umewafanya wengi wao waseme kwamba ama wanaupinga muundo wa sasa wa Muungano au hawautaki kabisa na wanataka Zanzibar iwe dola huru yenye mamlaka yake kamili.
Huo si mwamko wa leo au wa jana; tumekuwa tukiugusia miaka nenda miaka rudi lakini tukionekana kuwa ni wazushi na wazandiki.  Sasa mambo yanajidhihiri yenyewe.  Matokeo yake ni kwamba waliokuwa wakijidanganya sasa wamegutuka na hawajui jinsi ya kulizuia hilo wimbi la uzalendo Wakizanzibari minghairi ya kutumia hoja finyu za kikabila na udini.
Mmoja amefika hadi ya kuandika kuhusu ‘Waarabu’ na ‘watu Weusi’ kana kwamba hao wanaonasibishwa na uarabu ni wa rangi aina ya pekee iliyo tofauti kabisa na ya Wazanzibari wasio na asili ya Kiarabu.  Mwandishi huyohuyo alitishwa na sura rahimu ya Sheikh Farid Hadi Ahmed, mmoja wa viongozi wakuu wa Uamsho. 


Aliandika kwamba baada ya kuiona picha ya Sheikh Farid yalimjia mawazo kwamba Uamsho si jumuiya ya kidini na wala si ya Wazanzibari na kwamba Sheikh Farid ametumwa (hakusema na nani) kuwafitinisha Wazanzibari.  Alichotaka kusema mwandishi huyo ni kwamba kwa vile Sheikh Farid ana asili ya Kiarabu basi Uamsho inataka kuurejesha usultani.
Ni uchambuzi uchwara, tena wenye kutumia lugha ya kibri. Unashtua kwa vile ni ‘uchambuzi’ wa hatari unaofanana na simulizi za  Wahutu wa Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo.  Hizi fitna za ‘Upemba’ na ‘Uunguja’, za ‘ubwana’ na ‘utwana’ na za ‘ugaidi’ wa Uamsho ni fitna zinazotiwa na watu walio maluuni.  Lengo lao kubwa ni kuwapotosha Wazanzibari wauzime mjadala wa Muungano.  Hawajali iwapo watalitimiza lengo hilo kwa kuyakiuka maadili ya uongozi au ya uandishi.  Hila wanazotumia ni kwanza, kuwafitinisha Wazanzibari kwa kutia fitna za kikabila na za kidini.  Kwa mfano, wanawatisha wahafidhina wa CCM/Zanzibar, wale wenye kusherehekea kaulimbiu ya ‘Mapinduzi Daima’, kwa kuwaonya ya kuwa Uamsho ina “msukumo wa kiarabu”  na kwamba kusudio lake ni hatimaye kuyapinga Mapinduzi na kuirejesha Zanzibar katika ‘utumwa’. Maneno ya kijinga kabisa.


Hila yao ya pili ni kuwagonganisha vichwa Waunguja na Wapemba kwa kutumia hoja zisizo na mshiko wowote wa kimantiki.  Wanasema wamewapata Wapemba wengi wenye kutaka Muungano uendelee kama ulivyo. Wamewahoji na matamshi yao kusambazwa na magazeti fulani nchini.  Huu ni mfano mzuri wa propaganda ya kitoto.
Hila yao ya tatu ni kutumia lugha kuparaganya mambo.  Ingawa Uamsho ni jumuiya kamili wao badala yake wanasema kuwa hiki ni kikundi. Sio kundi bali ‘kikundi.’  Na wanaishtumu jumuiya hiyo kuwa ‘inawatumia’ baadhi ya vijana kufanya vitendo vya kihuni vya kuchoma moto makanisa. Hakuna ushahidi wa hili.Nne, wanajaribu kuwatisha Watanzania na hasa wakuu wa dunia hii kwa kuifananisha Jumuiya ya Uamsho na mitandao ya kigaidi ya Al-Qa’eda, Boko Haram na Al-Shabab.  Bila ya shaka wenye kueneza fitna hii hawajui walisemalo na wanajikashifu si mbele ya Watanzania wenzao tu bali hata machoni mwa balozi za nchi za Magharibi. 
Sijui kama wanaelewa ya kuwa maofisa wa baadhi ya balozi za Magharibi wameshakutana na viongozi wa Uamsho katika juhudi zao za kuitathmini Jumuiya hiyo na wanayaelewa makusudio halisi ya Uamsho.


Kwa hakika, kinyume na wanavyoandika baadhi ya waandishi wa Bara, Jumuiya ya Uamsho haikuzuka juzi. Imekuwako kwa muda wa takriban miaka 10 sasa.  Jumuiya hii ni kama mwavuli ambao chini yake kuna jumuiya mbalimbali za Kiislamu, pamoja na ile ya maimamu. 
Uamsho imekuwa ikiendesha harakati zake kwa msaada wa taasisi za nchi za Magharibi.  Ilikuwa miongoni mwa  waangalizi rasmi wa Uchaguzi Mkuu uliopita na ripoti yake kuhusu uchaguzi huo ni ya kupigiwa mfano kwa maelezo yake ya kina.  Kati ya wafadhili wa Jumuiya hiyo katika harakati hizo za kuangalia uchaguzi lilikuwa shirika la USAID la Marekani.  Hata vizibao wanavovaa baadhi ya viongozi wa Uamsho na vikuza sauti vyao walipewa na Wamarekani wakati huo wa uchaguzi uliopita.Wenye kujuwa mambo watakwambia kwamba kuna tofauti kubwa kama ya mbingu na ardhi kati ya jumuiya ya Uamsho na mtandao wa Al-Qa’eda au kundi la al-Shabab.  Huwezi kabisa kuzifananisha falsafa zao au makusidio yao.  Hata Boko Haram nayo licha ya mbinu inazozitumia inatofautiana sana na al-Qa’eda.Huko Zanzibar mafatani hawa wana washirika wanaojulikana.  Nao ni wale wanaochomwa na kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).  Ndiyo maana wakaruka harakaharaka kuwatupia lawama za machafuko ya hivi karibuni viongozi wa CUF waliomo kwenye SUK na kutaka watimuliwe kutoka serikalini.  Na ni wao waliohusika na vipeperushi vilivyotolewa wiki iliyopita kuwafitinisha Wapemba na Waunguja.
Na ni haohao wenye kujaribu kuwachimba waasisi wakuu wa Maridhiano yaani Rais mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.


Inasikitisha kuwaona baadhi ya Wabara wenye kujigamba kuwa ni wasomi wakitaka mijadala ya kisiasa ipigwe marufuku katika majukwaa ya kidini. Hawaelewi kwamba ni dhima ya dini za Ukristo na Uislamu kuzungumzia na kuyatafutia ufumbuzi mambo yanayoyagusa maisha ya kila siku ya waumini wa dini hizo. Na mambo hayo yawe yepi kama si ya kisiasa?
La kutisha ni kuwa  ‘wasomi’ hao wanamtaka Rais Jakaya Kikwete awachukulie hatua za kimabavu wakuu wenzake walio serikalini kwa kisingizio kuwa ati wanaunga mkono harakati za Uamsho. 
Ulimwengu haukufunga macho wala haukuziba masikio.  Unawaona na kuwasikia.  La ajabu ni kwamba wanasiasa na waandishi wenye kuchochea hisia kama hizo wamesahau ni nyakati gani tulizo nazo na ni ulimwengu gani tulio nao.  Katika ulimwengu wao wa leo Wazanzibari wanasema hawakubali tena kugawanywa kwa propaganda za kikabila au za kidini. 
Inatisha kwamba kuna wanasiasa na waandishi waliosahau kwamba siku hizi kuna Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) na mahakama nyingine mahsusi za kimataifa, mithili ya ile Mahakama Maalumu ya Sierra Leone. Mahakama kama ile ya Sierra Leone inaweza kuundwa mara moja na Umoja wa Mataifa kuwatia adabu wenye kupalilia fitna zinazoweza kuzusha mauaji ya kimbari. 
Ni hiyo Mahakama Maalumu ya Sierra Leone iliyomhukumu Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia, kifungo cha miaka 80 baada ya kupatikana na hatia ya  kuishushia nakama Sierra Leone.
Dhana waliyonayo baadhi ya wasomi na waandishi wa Bara ni kwamba viongozi wa Uamsho ni mijitu isiyosoma.  Kuna mmoja aliyepandwa na jeuri na kuandika kwamba mbali na kujua kusoma Qur’an viongozi hao ni watu wasiojuwa kuandika wala kusoma. Ukweli ni kwamba viongozi wa Uamsho ni wasomi waliohitimu masomo ya chuo kikuu na wana shahada za juu za uzamili katika fani mbalimbali kama vile za uhandisi, sayansi na jiografia.  Ni wasomi wa nyanja zote — za dini na dunia. Mfano mzuri ni Sheikh Msellem ambaye mbali na kuwa gwiji wa tafsiri ya Qur’an pia alisomea taaluma ya hali ya hewa.  Baadhi yao walisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako walivutiwa na hotuba za kidini za Professor Malik, mtaalamu wa fani ya hesabati, ambazo ziliwashajiisha na kuwafanya wawe na mwamko wa Kiislamu.  Wengine walisoma kwenye vyuo vikuu vya nje vikiwemo vile vya Sudan, Saudi Arabia na Qatar.
Ni wazi kutokana na ripoti na taarifa zao kwamba baadhi ya wasomi na waandishi wetu wa Bara wanawadharau Wazanzibari. Nadhani hizo dharau zao ndizo zinazowafumba macho wasiweze kuona nani hasa aliyechochea fukuto hili la upinzani dhidi ya makandamizo ya walioshika hatamu za utawala wa Muungano.Maandishi yao yamebainisha wazi kwamba hawaamini ya kuwa Unguja na Pemba si majimbo wala koloni za Bara.  Inakirihisha kuona namna wengi wao wanavyozitapika hadharani chuki zao (na udini uliowapamba) bila ya hata staha na uvumilivu wa kimaadili

No comments: