Wednesday, 13 January 2016Miaka 52 ya MApinduzi ya Zanzibar ilivyotumiwa kuwagawa wazanzibari kwa Mafungu

KALAMU YA GHASSANI

CCM haina la kuomba radhi kwa “siasa za uchotara”13 Januari 2016

Kizazi kipya kinacholishwa sumu ya uabaguzi Zanzibar
   
Taarifa iliyotolewa siku ya tarehe 12 Januari 2016 na Daniel Chongolo, aliyejitambulisha kuwa mkuu wa mawasiliano na umma wa Chama cha Mapinduzi (CCM) inasema chama hicho “kimesikitishwa sana na ujumbe wenye maudhui ya ubaguzi ulioandikwa kwenye moja ya mabango yaliyobebwa na mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 za Mapinduzi ya Zanzibar” na kwa hilo chama hicho tawala kinaomba radhi, kinapinga na kinakemea.

Taarifa hiyo kwa umma inafuatia shinikizo la wachangiaji wengi kwenye mitandao ya kijamii, baada ya kusambaa kwa picha zinawaonesha vijana wa CCM visiwani Zanzibar wakipita na mabango yanayosomeka “Machotara wa Hizbu, Zanzibar ni nchi ya Waafrika” na au “Machotara Vibaraka wa Sultani watupishe na Mapinduzi yetu” mbele ya viongozi wa CCM na serikali ya Muungano, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Balozi Seif Ali Iddi na Makamu wa Rais wa Tanzania, Bi Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Januari 2016, ikiwa sehemu ya sherehe hizo. Lau ingelikuwa si hiyo nguvu ya mitandao ya kijamii, hakuna ajuwaye ikiwa CCM ingelijipa tabu ya kuandika waraka wake wa aya tatu na kuusambaza mitandaoni kwa haraka ile.

Mimi ni mmoja wa wanaodhani kuwa Chongolo alifanya haraka mno kutoa tamko lake na zaidi imekuwa bahati mbaya sana kwamba amelitoa. CCM haina la kujutia wala la kulikemea kwenye hili, kwa kuwa chuki za kibaguzi ndio uzi uliolifuma guo linaloitwa CCM Zanzibar. Kujaribu kuukata uzi huo ni kutaka kulirarua guo lenyewe, na sidhani ikiwa CCM Taifa inapendelea hivyo. Historia inaonesha kuwa Dodoma inaweza kupoteza kila kitu – ikiwemo heshima yake ya kitaifa na kimataifa – lakini sio kuiwajibisha CCM Zanzibar pale inapochupa mstari.

CCM Zanzibar na chuki za ubaguzi ni mfano wa samaki na maji. Kama ambavyo samaki hawezi kuishi nje ya maji, ndivyo nayo  isivyoweza kuishi nje ya mduara wa chuki za kibaguzi. Ndani ya mduara huo, ndimo ulimo “uhalali”, pumzi na maisha yake. Wimbo mmoja maarufu wa mwimbaji wa taarab wa Zanzibar, Fatma Issa, unauliza: “Hutaki Mwanakwerekwe, mwenzangu uzikwe wapi?” Suali hilo hilo pia linaweza kuulizwa kwenye muktadha huu: ikiwa CCM haitaki chuki za kibaguzi, iishi kwa njia  gani?

Huu ni ukweli ambao CCM Taifa unaujuwa vyema na inafaidika nao. Chuki za kibaguzi ni sehemu ya mfumo ulioiunda na unaoiendesha CCM yao upande wa Zanzibar nayo imekuwa ikiutumia ipasavyo. Mara kadhaa wenyeviti wa CCM Taifa katika awamu mbali mbali, wakiwa madarakani na wakiwa wastaafu,  wamekuwa wakiitumia kete hiyo hiyo kuendeleza maslahi yao.

Katika sherehe kama hizi za Mapinduzi za mwaka 2004, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa wakati huo, Benjamin Mkapa, alisimama pale uwanja wa Amani akinadi: “Tusemeni Mapinduzi Daima kwa sauti kubwa hadi vitukuu na virembwe vya masultani na mahizbu watusikie, kwa sababu bado wangalipo”. Kwenye jukwaa kuu, ilikuwepo familia ya Rais Mstaafu Amani Karume, ambayo yenyewe ni sehemu ya vitukuu hivyo. Disemba 2005, Rais Jakaya Kikwete alisema kwenye mahojiano yake na gazeti la Mwananchi kuwa kisiwa cha Unguja ni ngome ya chama chake isipokuwa tu kwenye Mji Mkongwe kwa kuwa hapo pana Wapemba wengi. Tarehe 23 Oktoba 2015, wakati akifunga kampeni za CCM kwenye uwanja wa Kibandamaiti, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi, akitumia wimbo wa “Msegeju ana ng’ombe”, alisema utawala wa Zanzibar ni miliki ya Afro-Shirazi wa Unguja na sio Wapemba kwani wao hawakuguswa na Mapinduzi, bali wamealikwa tu kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Kwa hivyo, mfumo wa chuki za kibaguzi dhidi ya kundi fulani la Wazanzibari ni wa kitaasisi ndani ya CCM. Si jambo la jana kwenye sherehe za mwaka huu za Mapinduzi tu. Lina mizizi mirefu na inayofahamika ndani ya tabaka tawala. Kwa mfano, wakati wa harakati za madai ya Katiba Mpya, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alipanda jukwaani na kuwataka wafuasi wake kuimba na kutosahau wimbo wa “Mwana wa Nyoka ni Nyoka”, akijibu hatua ya Chama cha Wananchi (CUF) kutumia wimbo wa wanamapinduzi “Sisi Sote Tumegomboka”.

Kwa uwazi kabisa, mfumo huu wa chuki za kibaguzi umejengewa hoja kuwa madaraka ya kuiongoza Zanzibar hayawezi kukabidhiwa kwa yeyote ambaye si mwana-CCM mwenye mizizi ya kibaguzi na chuki dhidi ya Wazanzibari wengine. Yaani haitoshi tu kuwa mwana-CCM, lakini pia awe mwenye chuki za kutosha ya kibaguzi na ukatili wa kutosha. Mwana-CCM anayeonekana kukengeuka hilo na kuzungumzia umoja wa Wazanzibari, mshikamano na mapenzi kwa dhati, hafai. Ndiyo yanayomkumba Amani Karume kwa kuwa amethibitisha kutoka nje ya mduara huo.

Ndio maana, wengine hatuoni mantiki ya CCM kujipa tabu ya kuomba radhi kwa kitu ambacho ni sehemu yake, kwa sababu haitaweza kukiwacha na ikikiwacha itakufa. Haitakuwa tena CCM hii ambayo ilijiamulia kurithi kila mabaya ya mtangulizi wake, ASP, na kuyaacha yote mema ya chama hicho kikongwe visiwani Zanzibar.

Na bado kuna sababu nyengine ya CCM kutopaswa kuomba radhi – Wazanzibari wanaobaguliwa kwa mabango kama haya ni watu madhubuti na imara zaidi kuliko chuki zenyewe dhidi yao. Maneno yaliyomo kwenye mabango kama hayo yamekuwa yakisemwa takribani kwa mwaka wa 50 huu, na bado wanaosemwa hawakuwahi kuvunjika moyo wala kurudi nyuma. Kinyume chake, wamekuwa wakiendeleza imani yao kuwa Zanzibar ni nchi yetu sote kwa pamoja na kwamba sisi ndio wenye haki ya kuamua khatima yake kwa njia za kistaarabu. Matokeo yake wamekuwa wakiwavutia wengine waliokuwa na mtazamo huo huo wa kibaguzi dhidi yao.

Leo hii, kwa aliye mkweli wa nafsi yake anaujuwa ukweli mmoja – CCM imegeuka kuwa chama cha wachache visiwani Zanzibar – uchache wa wafuasi na uchache njema ya kuiendesha nchi. Ukubwa pekee ilionao CCM kwa Zanzibar sasa ni uungwaji mkono inaoupata kutoka vyombo vya dola vya Muungano.

No comments: