Friday 22 January 2016

Kwa uhai wa Zanzibar, tushukeni vituoni


Masaa machache yaliyopita, Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imetangaza tarehe ya marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar kufanyika Machi 20, takriban miezi miwili kutokea leo. Hii imetokana na kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25 na Mwenyekiti wa Tume yenyewe, Jecha Salim Jecha, tarehe 28 Oktoba wakati zoezi la majumuisho na kutangaza kura likiwa linaendelea katika kituo cha majumuisho, Bwawani, mjini Unguja.Kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi hakikuwa cha kisheria na kilifanyika zaidi kwa utashi wa kisiasa, hasa pale ilipoonekana kuwa chama kikongwe kinachoshikilia madaraka ya Serikali na Dola, CCM, kimepoteza kiti cha urais wa Zanzibar baada ya hesabu zilizothibitishwa na fomu za vituo vya kupigia kura kuonyesha hivyo.Licha ya vikao 9 vilivyowashirikisha wagombea wa urais kutoka CCM na CUF wakiwemo viongozi wastaafu kutafuta suluhu ya mkwamo huo, hakuna muafaka uliofikiwa kwa vile hoja kuu ambayo ni kukosekana kwa uhalali wa kisheria katika ufutwaji wa uchaguzi kukumbana na masikio mazito na msimamo mkali wa kambi ya chama tawala iliyoshinikiza marejeo ya uchaguzi, ambayo kwao ndio njia salama ya kujipanga upya kufuatia kushidwa katika uchaguzi wa Oktoba 25.

Kwa hivyo, kwa jicho la kawaida, kurejewa kwa uchaguzi ni faraja kwa CCM na ni pigo kwa CUF, maana ni CCM iliyomshinikiza Jecha kufuta uchaguzi kinyume cha sheria, ni CCM iliyotaka uchaguzi mwengine ufanyike, na ni CCM iliyomuambia tena Jecha atangaze tarehe ya uchaguzi mpya.
Lakini kuna upande ambao unaelezea kushindwa vibaya kwa CCM, hata kama uchaguzi utarejewa. CCM ilishindwa, inashindwa na itashindwa kupata uungaji mkono wa Wazanzibari walio wengi kwa kuwa CCM haina nia, uwezo wala sababu za kukidhi mahitaji ya sasa ya Wazanzibari. Upande huo ndiko ushindi wa siku zote wa chama cha CUF. CCM Zanzibar wameshindwa kabisa kuitetea nafasi ya Zanzibar katika Muungano, na pia kuyasimamia malengo ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari 1964.Wazanzibari walikipigia kura chama cha CUF katika uchaguzi wa Oktoba 25 kwa sababu ya sera nzuri zinazoashiria mabadiliko ya kweli katika sekta za kijamii, kiuchumi na kisiasa. Makubwa zaidi katika hayo ni imani yao kuwa CUF ndicho chama pekee visiwani Zanzibar kinachoamini kwa dhati kwenye umoja wa Wazanzibari na mamlaka kamili ya visiwa hivi kwenye Muungano uliosimama juu ya misingi ya usawa, heshima na uhuru wa kila mshirika.Wengi ya Wazanzibari wangependa kuona umoja wa kitaifa uliozaliwa baada ya Maridhiano ya 2009 unaendelezwa na kutanuliwa kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi ya juu kabisa. Hakikisho la hilo wanalipata kwa CUF pekee, kwani kwa CCM wanatishwa kila mara kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itavunjwavunjwa.Pia wengi wa Wazanzibari wanataka kuiona aina ya Muungano ambao uliasisiwa na viongozi wawili ambao ni baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na baba wa Taifa la Tanganyika, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, tarehe 26 Aprili 1964 ambao ulizikutanisha nchi mbili huru zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Ni siri isiyofichika kuwa CUF ilishinda kwa sababu sio tu kina sera nzuri za kuleta maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa, bali pia kimebeba matumaini ya Wazanzibari ya kuujenga umoja wao wa kitaifa na pia kupata aina ya Muungano wanaoutaka. Ndio maana hata wale waasisi wa Muungano huo – kama vile Mzee Hassan Nassor Moyo – wameungana na harakati za CUF kwa dhana ya kuleta Muungano ulio sawa na kuiondoa Zanzibar kwenye nafasi ya kuwa koloni la Tanganyika iliyojivisha koti la Serikali ya Muungano wa Tanzania.
Ni kwa mtazamo huo wa tafsiri halisi ya ushindi visiwani Zanzibar, ndio maana kuwaachia CCM washiriki marejeo ya uchaguzi peke yao ni sawa na kuwapa hati ya kuuzika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vile wao wanaamini juu ya mfumo wa Serikali Mbili kuelekea Moja.Pia ni sawa na kuwapa hati miliki ya kufanya wapendayo katika kutunga sheria ndani ya Baraza la Wawakilishi kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo kwao wao imekuwa mwiba uliowakaa kooni na unaowazuwia kuitawala Zanzibar kama walivyozowea – shamba la bibi. CCM itatumia pia fursa ya kuwa peke yao kwenye vyombo vya maamuzi na kisheria kupitisha sheria kandamizi dhidi ya wakosoaji wao na wananchi kwa ujumla kwa vile watakosa mtetezi.

Ile Katiba Inayopendekezwa, ambayo inapigiwa debe na CCM baada ya kutupwa kwa maoni ya wananchi kupitia katiba ya wananchi chini iliyosimamiwa na Jaji Joseph Warioba, ndio itakayopata nafasi ya kupitishwa na kuizika kabisa Zanzibar katika ramani ya dunia. Ile ndoto yao ya kuifanya Zanzibar kuwa mkoa miongoni mwa mikoa ya Tanganyika na hapo baadaye kujulikana kwa jina moja tu la Tanzania itakuwa imefanikiwa.Kwa mantiki hiyo, nikiwa kijana wa Kizanzibari natoa wito kwa Wazanzibari wenzangu kuendelea kuikataa CCM na kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa marudio kuwahakikishia kwamba lile pigo la mwanzo halikuwa la bahati mbaya, bali mara hii tuwapige kwa pigo takatifu zaidi. Tuyafanye haya, sio kwa sababu CUF ishinde, bali kwa ajili ya kuokoa uhai na utaifa wa Zanzibar katika ramani ya dunia. Tuweke tofauti ya vyama pembeni na tupiganie nchi yetu ya Zanzibar. Tupiganie utaifa wetu wa Wazanzibari. Tupiganie malengo ya Mapinduzi ya 1964 ambayo ni kuleta usawa, kuondoa ukabila, kuondoa ubaguzi wa aina yoyote na kuleta maendeleo ya kweli kwa watu wa Zanzibar. Tupiganie Muungano ambao utakuwa ni wa nchi mbili zilizo sawa na zenye maamuzi sawa.

Nimalizie kwa kumnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, ambaye Oktoba mwaka jana alisema: “Elections are vitally important, but make no mistake: elections cannot be the only moment for citizens to shape their future. People must be able to engage with their government and with their fellow citizens in political discussion and debate not just on Election Day, but every day.”
“Chaguzi ni nyenzo muhimu sana, na hapana shaka: chaguzi sio tu zinaweza kuwa ni muda kwa raia kutengeneza maisha yao ya baadae. Watu wanatakiwa waweze kufanya maingiliano ya Serikali yao na raia wenzao katika mijadala ya kisiasa na midahalo, sio tu kwa siku ya uchaguzi, bali kila siku.” Haya ndio mawazo yetu na tuna haki ya kuyajadili kwa faida ya taifa letu, huku tukikumbuka kuwa kura yetu ndio sauti ya Zanzibar yetu. Zanzibar kwanza, Zanzibar njema, Zanzibar huru! Hakuna kurudi nyuma!- Zanzibar Daima.

No comments: