Monday, 25 January 2016

MWANASHERIA Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othamn Masoud amtaka Dr Sheni akae Pembeni ili Jaji Mkuu aongoze Nchi



MWANASHERIA Mkuu wa zamani wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ametoa rai mpya ya kuondoa mkwamo wa kisiasa unaoikabili Zanzibar, akisema haiwezekani wananchi kuingizwa katika kinachoitwa “Uchaguzi wa marudio.”Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).  “Kule kwetu Pemba wanasema arudiwae ni mke. Uchaguzi haurudiwi kwa sababu mpaka sasa wananchi tuliopiga kura Oktoba 25 hatujaelezwa kwani kilichotokea ni nini hata uchaguzi ukafutwa. Hivi uliofutwa ni uchaguzi au matokeo ya uchaguzi?”
“Wazanzibari kuambiwa kwamba uchaguzi ulifutwa eti uliharibika ni kudanganyana. Na haifai kudanganya watu. Uchaguzi ulioharibika hauwezi kushuhudia wawakilishi na madiwani waliochaguliwa wakiwa na vyeti vyao mkononi walivyoandikiwa na wasimamizi wa uchaguzi majimboni, ilipofika siku uchaguzi ulipofutwa,” amesema.

Othman ameeleza hayo jana wakati wa kongamano lililoandaliwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kujadili changamoto za kisheria zilizojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar. Kongamano lilifanyika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.  Amesema ufumbuzi wa haki kwa sasa ni Dk. Ali Mohamed Shein anayeng’ang’ania kuwa ni rais halali kukaa pembeni; Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu kushika wadhifa wa urais kama Katiba ya Zanzibar inavyosema, na kuunda Tume ya kumchunguza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Amesema ni muhimu ukafanywa uchunguzi wa kina sasa kuchunguza kama uchaguzi ulifutwa kihalali. Kama ni kihalali kama wanavyoshikilia viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), basi ufanywe uchaguzi mpya kwa taratibu mpya.  “Kama hakukuwa na uhalali wa kuufuta uchaguzi uliokwishafanyika kama tunavyoamini wengi wetu, turudi kwenye Katiba ya Zanzibar kukamilisha kazi iliyoachwa kufanywa na Tume ya Uchaguzi.

Amesema suala la Zanzibar kwa sasa ni sawa na busha ambalo dawa yake ni kulipasua wala sio kulitumbua kama afanyavyo Rais John Magufuli. “Hili la Zanzibar ni busha lipasuliwe tu,” amesema huku akisikitishwa na hali iliopo Zanzibar kwa sasa ya viongozi wachache kutangaza uchaguzi wa marudio sambamba na kujaza vikosi vya ulinzi na usalama nchini kote.
Amesikitishwa pia na kitendo cha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), kushindwa kutoa kauli itakayoonesha uwajibikaji wa kiutawala katika tatizo la mtu mmoja kuhujumu uchaguzi mkuu na kuitia nchi katika matatizo makubwa ya kisiasa, kiusalama na kiuchumi.

“Tunaendelea kuona jinsi Tume za uchaguzi zilivyo sawa na Mkalimani ambaye akikosea tu kutafsiri alichokisikia kikisemwa ameharibu kila kitu. Hapa kuna suala la kasoro ya uadilifu upande wa mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Ameifanya Tume mle ndani kuwa kama Jeshi. Na kwa hapo huwezi kusema kutaendeshwa uchaguzi wa maana,” amesema Othman ambaye alifukuzwa uanasheria mkuu wa serikali mwaka juzi baada ya kukataa ibara za Katiba Inayopendekezwa kwenye Bunge Maalum la Katiba, mjini Dodoma.

Bali Othman pia amesikitika kuona kwamba baadhi ya wanasheria wenye uelewa mpana wa mambo, wanafanya upotoshaji wa vifungu vya sheria na katiba badala ya kuweka wazi kila kitu kwa lengo la kusaidia jamii.

Amezungumzia wanasheria waliotoa maoni kwa kuvizonga vifungu vya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi Na. 11 ya mwaka 1984 ya Zanzibar kwa mtizamo wa kuhalalisha alichoita vurugu za Jecha na waliomtuma kusema uongo.  Amesema Jecha mwenyewe amekiri mbele ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi kuwa alilazimika kusema uongo kwa “vyombo” ambavyo hajavitaja waziwazi. Alitoa kauli hiyo ya kukiri kusema uongo alipokutana na makamishna Novemba mosi, 2015, alipojaribu kutafuta kuhalalisha haramu aliyoitenda siku tatu kabla, tarehe 28 Oktoba 2015, alipojificha na kuibuka kwenye televisheni kutoa tangazo la kufuta uchaguzi mkuu.

No comments: